The Chant of Savant

Thursday 30 December 2021

Kwanini wahubiri wengi wa kisasa wamejigeuza wanasiasa?


Wakati maovu kama vile wizi wa mali za umma, uzembe, ujambazi, upofu, upogo, uzinzi, utapeli, uongo,  uroho, roho mbaya, utoaji mimba, ubabaishaji na mengine kama na haya vikiongezea, wahubiri wengi–––hasa wa kujipachika–––wamegeuka wanasiasa kiasi cha kutelekeza uhubiri na neno la Bwana. Baada ya kuongezeka kwa matumizi ya mitandao na uhuru usio na mipaka, ukiachia mbali kutafuta umaarufu wa haraka hata kwa njia za hovyo, tunashuhudia utitiri wa clip mitandaoni zinazorushwa na wahubiri wanaojifanya wajuzi wa kila kitu. Je inakuwaje neno la Mungu linatelekezwa na siasa inachukua kani? Kuna sababu nyingi mojawapo zikiwa:
Mosi, baada ya wenzao wa kujipachika kupenya kwenye vyama na kupata vyeo vya kisiasa hasa ubunge, wengi sasa wanatumia majukwaa yao ya kidini hata kwa kujipachika kutafuta namna ya kuingia kwenye siasa ili wapige fedha tokana na wanasiasa kulipwa vizuri na bila kulazimishwa kuwa wasomi. Rejea akina Getrude Rwakatare, na sasa, Josephat Gwajima kutumia umaarufu kwa kidini kukwaa ubunge. Mfano, Gwajima aliwahi kusema kuwa hawezi kugombea cheo cha kisiasa hata kama ni urais kwa sababu ni kazi dhaifu kuliko kazi ya Bwana. Punde, aliramba matapishi yake tena akapitishwa kugombea kwa mizengwe. Sasa amenogewa kiasi cha kuanza kutaka kuukata mkono unaomlisha. Je ni wangapi wanaomkumbusha Gwajima maneno yake? Je ni wangapi waliyakumbuka wakati wakimpitisha kinyume na matakwa ya wale anaodai kuwawakilisha? Je Gwajima anasemaj? Je mamlaka zina fanya au kusemaje? Wewe msomaji unafanya au kusemaje? Uzuri wa mitandao, inatunza kumbukumbu–––na inauma huku na kule––––hasa kama tataidurusu kwa makini na kuimaizi ili kuwakaanga vidhabi hawa kwa mafuta yao.
Pili, wengi wamegundua udhaifu wa kimfumo, kisheria na kiutawala ambao uruhusu watu wasio na sifa kujipachika vyeo vikubwa kama vile unabii, uaskofu na vingine vingi na kujipatia mali na umaarufu ima kwa kuwanyonya waumini wajinga na waliokata tamaa au kutumia asasi za dini kufanya biashara kama kuingiza magari bila kulipa sheria. Nadhani hii ndiyo siri ya wengi walioingia bila kuwa na baiskeli wala nyumba kutokea kuwa matajiri wa kutupwa tokana na kuvuna wasikopanda huku mamlala zikiangalia tu. Unashangaa namna mtu wa kujipachika anapata wapi jeuri, kwa mfano, kusema eti ikulu imekaliwa na mwana au binti wa shetani! Kweli? Tunaelekea au kuelekezwa wapi?  Kwani lazima tuwategemee vidhabi hawa wasio na dini wala utu zaidi ya fedha na utajiri?
Tatu, mfumo wetu wa kifisadi umetoa mwanya kwa watu kutajirika na kuishi kitajiri bila kulazimika kueleza walipo na walivyochuma utajiri wao. Kwa nchi nyingi za kiafrika, ni rahisi kulala maskini na kuamka tajiri mamlaka zisiulize miujiza uliyofanya kufika hapo. Hii inanikumbusha visa vya kukamatwa matapeli wa kinigeria ambao wengi wao ni wachungaji wakiwa na shehena za madawa ya kulevya. Je ni wangapi hawajakamatwa, kustukiwa wala kufichuliwa iwapo mifumo yetu ni ya hovyo na kipofu? 
Nne, ukosefu wa maadili kijamii. Watu wetu wengi wanaabudia na kushobokea vitu kiasi cha kuibiwa wakijiona wasilalamike wala kushuku. Tumejigeuza jamii ya kuabudia utajiri na vitu bila kujipa nafasi ya kuhoji namna vinvyopatikana. Je ina maana mamlaka hazijui kuwa kuna michezo michafu inafanyika kiasi cha kuvutia matapeli wengi kujivika vyeo vitukufu ili kuwaibia vipofu? Nani hajui kuwa Yesu aliwahi kuliona hili akaonya “jihadharini na manabii wa uongo wanaowajia wakiwa wamevaa ngozi ya kondoo, kumbe ndani ni mbwa mwitu wakali” (Matayo 7: 15). Mtume Petro anaukubaliana na Yesu akisema “manabii hawa wa uongo wanachotaka ni pesa zenu tu. Hivyo watawatumia ninyi kwa kuwaambia mambo yasiyo ya kweli” (2 Petro 2: 3) na “na watatokea manabii wengi wa uongo ambao watawapotosha watu” (Matayo 24:11). Je hatunao mingoni mwetu manabii hawa wa uongo na wapenda fedha? Wanamfuata na kumhubiri nani iwapo Yesu alikuwa maskini akikiri wazi kuwa “ Mbweha wana mashimo yao, na ndege wa angani wana viota vyao, lakini mimi Mwana wa Adamu sina mahali pa kulaza kichwa changu.” (Matayo 8: 20). Je hawa wahubiri, maaskofu, mitume, manabii, wachungaji (ambao sie huwaita wachunaji) bado wanamhubiri Yesu huyu huyu maskini ambaye alishindwa hata kuwa na sarafu mfukoni hadi akakopa kwa samaki?
Tano, wanatumia ujinga wao wa kutojua madhara ya kile wanachofanya kupumbazwa na tamaa na uovu kiasi cha kuendelea kujipa motisha wa kuendelea kufanya “ubatili mtupu; mambo yote ni ubatili” (Mhubiri 12:8) wasijue watatokea watu wenye mawazo makubwa na wakweli kuwafichua kama tunavyojaribu kufanya hapa ili waathirika na wahanga ambao ni jamii na hata mamlaka kuwachukulia hatua kabla hatujaangamia pamoja.
Mwisho, sasa nini kifanyike? Nadhani jibu ni rahisi. Tuwabane na kuwanyima pumzi kwa kuwataka wathibitishe madai yao. Tuzidurusu, kuzitafsiri kisheria na kisomi dhana za kufunuliwa ili kuepuka matapeli wachache kuzitumia kuendelea kutuibia na kuhatarisha hata usalama wa jamii na taifa kama inavyoanza kujitokeza. Kila anayeibuka anajifanya mtaalamu wa kuwajua wanawake, miujiza, maisha na uzima wa milele wakati hana hoja wala lengo lolote zaidi ya njaa, tamaa na ujinga wake. Wanatumia roho mtakatifu wakati wamejaa roho mtakakitu na roho mtaka chafu. Tieni akilini. Wale wanaoshangaa ni kwanini wahubiri wengi wamegeuka wahubiri wa siasa badala ya neno, wamepata jawabu mujarabu hapa. Nawatakieni Heri ya Mwaka Mpya.
Chanzo: Raia Mwema kesho.

No comments: