How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Friday, 17 December 2021

Ushirikina wa ‘Washirika’ Wetu wa Magharibi na Mashariki

Neno mshirika lina nguvu na linavutia kulitumia. Hata hivyo, hugeuka shubiri unapogundua kuwa yule unayeamini na kudhani ni mshirika wako ni adui namba moja kihistoria na katika hali halisi. Leo hii tutagusia mambo mawili yenye kutegemeana. Tutaongelea kile kinachoitwa utaifa wa kinga (Vaccine nationalism) ukaburu wa kinga (Vaccine apartheid) na siasa za kinga (Vaccine politics).
Waliua viongozi wetu, Patrice Lumumba (DRC); Kwame Nkrumah (Ghana); Eduardo Modlane na Samora Machel (Msumbiji); Sylvanus Olympio (Togo), Dr Tafawa Balewa (Nigeria); na pia walipindua wengi sana tu. Waliua tawala, himaya na falme zetu na kuunda vipande vya nchi vya hovyo na ombaomba ili watunyonye kama wanavyofanya sasa nasi tukakubali. Walinyonga wafalme na watemi wetu huku wakiwakweza wao. Ziko wapi himaya za Ghana, Luba-Lunda, Bunyoro-Kitara, Karagwe, Mali, Meroe, Soghai, Kazembe-Maravi, Mwenemutapa na nyingine nyingi nasi tukakubali.
Waliua Dini na Mila zetu za utu na kutuletea mila zao za kinyama na kikoloni walizoziita dini wakati si chochote wala lolote bali mila kama zetu. Hebu jiulize tofauti ya kuabudu na kutambika, watakatifu na mizimu na mengine kama hayo. Hebu jiulize kinachoitwa amri kumi ambazo baadhi yake hata wanyama wetu kama mbwa na paka wanazijua tena bila kufundishwa. Mbwa akiiba nyama au paka maziwa anafanya nini? Jogoo akimkuta mwenzake juu ya jike lake anafanya nini? Waliua majina na utambuliko wetu na kutujaza ujinga uitwao ustaarabu. Leo ukimsikia mchina au mjapani hata kabla ya kumuona unamtambua kwa majina yake na utambuliko wake. Utasiki Hua Guo Wei au Masahiro Nakasone. Mzungu utamsikia Ian Smith na akina Mackenzie. Ukimsikia mwaarabu au mhindi utamtambua haraka kwani utasikia Mugheir al Baghad au Kanjibhai Chavda siyo yule habithi aliyetumiwa na wezi wetu akatoroka na utajiri wetu. Je akiitwa mwafrika utasikia nini zaidi ya Joseph, Simon, John, Mbaraka, Mohamed na majina mengine. Imefika waswahili wenzetu kama vile kule Sudan ya Kaskazini na Somalia wanajiita waarabu wakati ni wamakonde. Tumefikia kupewa majina hata ya mawe na mapaka. Hebu jiulize maana ya Livingstone au Abu Hurreira ni nini kama siyo jiwe lenye uhai na baba wa mapaka? Wengine wanaitwa Seif wakati kwa kibantu ni Jambia tu! Hivi Leon au Lion na Simba wana tofauti gani? 
Akutukanaye hakuchagulii tusi.  Walitutukana kuwa ni makafiri na wapagani nasi tutakubali kiasi cha sasa kutukanana sisi kwa sisi tujikona wajanja wakati majuha. Walitutoza ushuru uitwao sadaka, zaka na fungu la kumi kuendesha himaya zao nasi tukakubali. Leo tunakwenda kwenye makaburi yao kwa majina mbali mbali kuabudu wakati tunayo makaburi yetu. Tumepotezwa na tukapotea bila hata kujitambua. Huu ndiyo ushirikina wa washirika zetu.
Waliua mifumo na utamaduni na kutugeuza tegemezi ili tuwe wa hovyo–––kama tulivyo sasa tangia wakati ule–––ili waendelee kutunyonya na kutudhalilisha kama ambavyo wamekuwa wakifanya. Hebu jiulize. Baba au mama zima tena Rais wa nchi anakwenda kwa baba au mama mwenzake kujidhalilisha kuomba kana kwamba hana akili, mikono wala miguu tena bila kuona aibu. Je nchi zetu haziishi kwa makombo yaw abaya wake? Je, kama binadamu na jamii zenye akili tumejifunza nini? Je tuliwahi kujiuliza ilikuwaje Afrika, kwa mfano, iliishi bila kutegemea wafadhili kwa mamilioni ya miaka hadi ilipovamiwa na kuwekwa chini ya ukoloni?
Je hii inahusiana vipi na yaliyotangulia hapo juu? Uhusiano ni mkubwa tu. Bila kutuharibu kimila wasingeweza kutuharibu kiakili na kiroho. Ndiyo maana hatujitambui na tunaridhika na udhalilishwaji na unyonyaji huku nasi tukivikuza dhidi ya wenzetu. Leo tutaongelea Ukovi-19 na namna unavyotumia kutuumiza ili tujifunze japo hatutaki kufanya hivyo.  Nchi za magharibi na wenzao wa Asia wamejirundikia dozi kibao za kupambana na Ukovi-19 huku wengine wakitushauri watukopeshe kana kwamba sisi ndiyo tuliotengeneza balaa hili ambalo wamekuwa wakituhumiana kulianzisha. Walitengeneza Ukimwi, ushahidi wa kitaalamu upo wakatuambukiza, hatukulalamika wala kuwazodoa. Leo wanajilimbikizia kinga, ujuzi na kila kitu halafu wanaanza kutulaumu kuwa tunaogopa chanjo! Ziko wapi wakati wamezuia wao?  Nini, kwa mfano, mfano wa kuiruhusu India inakiri na kutegeneza chanjo au kutumia viwanda vyake lakini wakashindwa kufanya hivyo kwa Afrika? Siri iko wazi. Hata walipokuja kututawala hapa Afrika walituletea wahindi kununua mazao yetu kwa bei ya kuiba na kutajirika halafu tukaaaminishwa kuwa Waswahili hawajui biashara–––wakati ushahidi wa kihistoria upo kuwa kwenye himaya za Kiswahili za Pwani (Swahili City States) na himaya nilizotaja hapo juu–––tuliweza kufanya biashara hata kabla hawajaja. Kabla ya kumaliza ngoja nitoa mfano kwa taifakama Kanada ninakoishi lenye idadi ya raia ikiwemo akina sie wakazi wa kudumu milioni isiyofika 40. Ajabu ya maajabu, ulipoibuka Ukovi-19 ilinunua chanjo kwa mamilioni kwa ajili ya watu wake jambo ambalo ni haki yake. Hata hivyo, ukiangalia namna wakazi na wananchi wa hapa tunavyohimizwa kuchanjwa na kuongeza booster wakati wenzetu katika nchi maskini hawajapata hata chanjo ya kwanza, unashangaa.
Leo tutamaliza kwa maswali chokonozi na yenye kukera. Je Afrika na Waafrika tutajitambua na kujikubali lini ili tuwajibike kwa mambo yetu zikiwamo afya zetu? Je tutaweza bila kuachana na mila za watu ambazo tunajua fika kuwa ndicho chanzo cha mabalaa na udhalili wetu? Je hawa kweli wanaotudanganya kuwa ni washirika zetu wakati ni washirikina kuna haja ya kuendelea kuwaamini na kuwategemea? Je tumepata faida gani tokana na mifumo na utamaduni wao zaidi ya kuzalisha wapumbavu kibao wanaoamini kwenye kila ujinga ikiwamo miujiza?  Juzi juzi taifa letu lilipoambiwa kuna Ukovi-19 tuvae barakoa, tuliaminishwa kuwa Mungu alikuwa amelikinga na kuondoa Ukovi-19. Ujinga mtupu. Hali ikoje sasa? Tulishindwa hata kusimama na kusema hapa. Badala yake tulihatarisha maisha yetu na wapendwa wetu hadi ukweli ulipodhihirika tena kwa gharama kubwa tu. Tunawalalamikia wakoloni wetu wa jana kana kwamba walipokuja hawajatukuta na watu wenye afya na kuwafanya watumwa baada ya kujaribu wao wagonjwa na kushindwa! Tieni akilini. Naona leo sisemi mengi.
Chanzo: Raia Mwema kesho

No comments: