The Chant of Savant

Tuesday 14 December 2021

Si Lazima Wote Kuitwa Dokta

Shahada za heshima honoris causa zina heshima zinapotolewa na mamlaka stahiki na kwa watu wanaostahiki kwa njia, sababu na sifa stahiki.  Kwani, ni ushahidi kuwa anayetunukiwa ametoa mchango usio wa kawaida katika jamii ima kitaaluma au nyanja yoyote iwe ya jamii au sayansi kiasi cha kutambuliwa na kustahiki heshima hii. Hata hivyo, shahada hizi huwa za hovyo na hata kashfa na hukosa heshima tokana na yafuatayo:
        Mosi, zinapotolewa na taasisi feki.  Kwani, kwanza ni feki na pili hazina mamlaka wala uhalali wa kutoa shahada yoyote hata ikiwa ni ya kwanza. Hivyo, wanaoingizwa mkenge na kuibiwa fedha zao na kupewa upuuzi huu wanaonyesha ujinga na ushamba vya hali ya juu. Kimsingi, kwa wale wenye angalau sifa kiasi fulani, kukubali kufanyiwa ujinga huu ni kujichafua badala ya kupata  hizo sifa wanazosaka kwa udi na uvumba.  Wanachofanya hapa, ni kufichua ukihiyo na usaka sifa wao na namna ambavyo hawana sifa zozote. Wanataka sifa bila stahiki.  
        Pili, zinapopatikana kwa kutoa fedha kwa vyuo feki na si mchango kwa jamii. Mbali na kuibiwa na kugeuzwa mabunga, wahanga wa sifa hizi za kisomi wasizokuwa nazo, wanaibiwa fedha, wanachafuliwa na kutenda kosa la jinai kama kungekuwa na mamlaka zinazofuatilia vitu kama hivi. Kwani, kinachofanyika, wanalipia kashfa na uchafu kwa wale wenye sifa na kwa wasio na sifa, wanalipia sifa feki ambazo hawana na wala hawatawahi kuwa nazo vinginevyo waende shule au watoa michango isiyo ya kawaida kwa jamii. Mwandishi wa makala hii inao watu wake wa karibu waliopewa shahada za heshima tokana na michango yao isiyo ya kawaida kwa jamii.  Mmojawapo ni rafiki yangu na mzee wangu Spika Mstaafu Pius Msekwa. Alipopewa shahada yake ya heshima, nilimuandikia ujumbe wa kumpongeza bila kuwa na wasi wasi wowote. Kwanza, alipata shahada yake ya kwanza kabla hata sijazaliwa na ya pili kabla sijawa msomi. Kimsingi, ni mtu anayestahiki shahada ya heshima. Kwani, licha ya kutoa mchango mkubwa kwa jamii hasa kushiriki utumishi bora, kuwa msomi wa kweli, ameandika vitabu vingi juu ya historia ya nchi yetu.
        Tatu, vyuo feki au diploma mills, hutoa uchafu wao kwa watu wasio na sifa sawa na vyuo vyenyewe. Kimsingi, hutoa kwa watu wa hovyo. Kwa sababu watu wa heshima wanavikataa kwa kuogopa kuipoteza. Navyo, vinawasaka ili kujihalalishia biashara hii feki na haramu. Hakuna mtu mwenye usomi wake wa kweli au heshima yake anaweza kukubali uchafu huu achilia mbali kuutolea fedha kama inavyosemekana vihiyo wengi wanaotapeliwa hufanya. Kimsingi, kinachofanyika–––unapokubali kupokea uchafu huu–––licha ya kujichafua, unaonyesha ulivyo kihiyo na usiye makini kiasi cha kutapeliwa kirahisi. Pia, inakuonyesha kama mtu asiye na heshima wala maadili ambaye yuko tayari kutafuta sifa kwa njia haramu. Hii siyo sifa ya kiongozi. Mtu yeyote kwenye nafasi ya uongozi anayekubali kujirahisisha na kudhalilishwa hivi, hafai kuendelea kuwa kwenye wadhifa wa umma.
Kwa wale walioingizwa mkenge huu na kutapeliwa kama wana heshima, basi wajue hawajatapeliwa fedha tu bali hata heshima. Wanachofanya kufanya mara moja ni kurudisha huu uchafu kwa matapeli waliowapa hata kama hawatawarudishia fedha zao.  Kurudisha huu uchafu na kuukana, pamoja na kuonyesha kuwa hawakufanya utafiti uzuri na walipenda vya dezo au njia za mkato, lau kunaweza kuwarejesha heshima hata kama siyo kwa kiwango kikubwa. Badala ya kuonea fahari usomi huu uchwara, ambao, kwa wanaozijua au kuzisotea hizo PhD, ni uchafu ambao wahikila mtu mwenye akili na heshima anafaa kuuonea aibu kiasi cha kuulaani na kuukana kama kweli nao si matapeli wenzao waliopokea shahada hizi wakati wanajua kila kitu.
        Kwa watu wenye dhamana za umma waliopewa shahada feki nao wakazikubali na kujiona wamepata sifa stahiki, basi, kama ni watu wa kuteuliwa, uteuzi wao utenguliwe na kama ni watu wa kuchaguliwa, wananchi wasiwachague; kwani watakuwa wanachagua matapeli na watu wa kutia aibu wasio na heshima wala wasio wakweli kwao na kwa wenzao. Wanaaibisha ofisi zao na wale waliowachagua au kuwateua.
Tumalize kwa kushauri yafuatayo:
        Mosi, watu wetu watafute sifa za kisomi kwa kuzihenyekea; na kama hawana uwezo, wakubaliane na majaliwa yao.
        Pili, watu wetu waepuka kujiingiza kwenye jinai na utapeli kama huu. Kwani, taasisi feki hazina sura. Haziumii kisifa kama wanavyokuwa wahanga wake. 
Tatu, wahusika wajielimishe japo kidogo ili waweze kujua vitu vinavyowezekana na visiovyowezekana. Kwa wale wanaoona lazima waitwe madaktari lakini hawana uwezo wa kuusomea basi wafanye mambo yasiyo ya kawaida kwa jamii kama vile kuihudumia vilivyo. Na hata inapotokea wakafanya hivyo, wanapokaribishwa kupewa shahada za heshima, wachunguze uhalali na sifa za vyuo vinavyofanya hivyo. Vinginevyo, wanapokuwa wamepakwa kinyesi hivi, inakuwa vigumu kutofautisha kati yao na washirika wao katika jinai hii ya kishamba na kilimbukeni. Kwani, lazima wote tuwe madaktari?
Chanzo: Raia Mwema kesho.

No comments: