The Chant of Savant

Friday 24 December 2021

Waliotaka kuingiza sumu za kinyuklia nchini wasakwe na kukamatwa mara moja

Mheshimiwa Rais, nakuamkua kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Leo nakuletea kashfa ya meli ya MV Seago Piraeus Voy iliyokamatwa nchini Kenya ikielekea Tanzania ikiwa na bidhaa zenye sumu za kinyuklia ingawa declaration yake ilisema kuwa ilikuwa imebeba makufuli. Mkurugenzi wa Mamlaka husika nchini Kenya, Robert Njue alikaririwa akisema “hakuna shaka hii ni kuonyesha kuwa kuna utupaji wa vitu hatarishi Afrika Mashariki.”
Mheshimiwa Rais, hili ni jukumu lako kama kiongozi wa nchi mbali na kuwa mwananchi. Wakati tukitafakari nini kifanyike kushughulikia kadhia hii, tujiulize maswali muhimu, yaani: je amieishacheza huu mchezo hatari na mchafu mara ngapi na kusababisha madhara kiasi gani kwa watu wetu? Je ni kwanini? Je wanapata nini hadi wahatarishe maisha ya taifa? Hapa lazima kuna namna. Hii ni biashara haramu tena yenye fedha na ushawishi mkubwa. Je hawa waliotaka kuingiza balaa hili wana mtandao mkubwa kiasi gani nje na ndani ya nchi? Haiwezekani mtu au kikundi wakajiamini kuingiza bidhaa hatari kama hizi bila kuwa na watu wao kwenye maeneo zinakongilia iwe bandarini au mipakani. Kuna haja ya kuchunguza zaidi.
    Mhshimiwa Rais, nashauri tuige mfumo wa Magharibi ambao huwahudumia wananchi kwanza kabla ya wengine. Mfumo huu ni wa kibaguzi wazi wazi. Upo pale kuwahudumia wazungu na si waafrika wala wengine hata kama ni wananchi. Rejea waafrika waliopelekwa utumwani Marekani na kusaidia kujenga taifa lile lakini mfumo ukawatoa nje. 
    Mheshimiwa Rais, ukiachia mbali mfumo wa kimagharibi, hata mifumo ya kiarabu, kichina na kihindi huwahudumia wananchi na si wageni hata kama wameishi kule kwa miaka mingi. Rejea namna waswahili waitwao Jarawa walioko India walivyoachwa kwenye ujima kiasi cha kutumika kama kivutio cha watalii wa ndani na nje na hakuna anayepiga kelele kuhusiana na haki za binadamu. Niseme wazi. Wanavyotenzwa waswahili huko India ingekuwa ni wahindi wanatenzwa hivi Afrika, dunia nzima ingewaka moto. Rejea namna Idi Amin alivyowafukuza tokana na ubaguzi. Dunia nzima ilimlaani kwa vile waliotendwa ni wateule. Je leo, ambapo Ulaya inawafungia mipaka waswahili, wanaokufa majini wakikimbia umaskini iliousababisha nani anahoji? Ajabu na ubovu wa waswahili, tukiguswa, dunia nzima inanyamaza, lakini wakiguswa wengine, nasi tunapiga kelele. Ujinga mtupu na kujibagua wenyewe. Tunadanganywa na udini na ujinga mwingine kuwapigania watesi wetu. Huwa naliona hili kwenye sakata la Palestina. Waswahili wengi huingia hata mitaani kuandamana. Ajabu, waafrika wanaponyima haki zao kama vile kuuzwa utumwani huko Maghreb na Ghuba, hakuna waarabu wala wahindi wanaoandamana lau kuonyesha mshikamano!
    Mhsehimiwa Rais, mfano mwingine ni kutoka Ghuba ambapo wafanyakazi wengi wa kiafrika wamedhalilisha, wamedhulumiwa hata wengine kuuawa na mabingwa wa haki za binadamu wako kimya. Mifano ni mingi. Ulipoibuka ugonjwa wa Ukovi-19 huku China, waswahili walibaguliwa nchini humo hata India ukiachia mbali wachina kubaguliwa kwenye nchi za magharibi kuwa ndio chanzo cha janga hili.
    Mheshimiwa Rais, mie si mbaguzi ila vile vile siyo limbukeni kwa vitu vya ugenini. Kimsingi, mifumo yote ya dunia ni ya kibaguzi dhidi ya mtu mweusi. Hata hawa wenzetu tulio nao wanaojiona kuwa weupe hawatuthamini zaidi ya kutuona mabunga kwa kuwakumbatia wakati wao wanatubagua. Sitaki niseme mengi. Ukienda kwenye mitaa ya Feri na Kariakoo, utauona huu ukweli. Imefikia mahali hata waafrika tunabaguana. Mtutsi anajiona bora kuliko Mhutu, Msomali kuliko Mbantu, Mpemba kuliko Mzanzibari. Kwani hayapo? Imefikia mahali Mhaya anambagua Mnyambo, Mchaga anambagua Mpare, Mkurya anambagua Mkerebe na kadhalika. Wengi wa watu hawa wana tabia ya kuoana wao kwa wao wakiwatenga wale wasio kuwa watu wao. Kwani hayapo haya? Je tufanye nini?
    Mheshimiwa Rais, naomba niunganishe mifumo ya kibaguzi na mada ya kutaka kuingiza sumu za kinyuklia nchini. Nisema wazi. Ukichunguza huyu [hawa] aliyetaka kuziingiza, utakuta anajionyesha kama Mtanzania wa kweli wakati siyo. Hata hivyo, ukichunguza zaidi, utakuta ni kati ya wale wasiowathamini wenzao mbali na kule zilikotoka. Taarifa zinasema sumu hizi zilitokea India. Ina maana India walishindwa kuzitambua na kuchukua hatua? Wangekamata za nini wakati zilikuwa zikitoka kwao kwenda Afrika? Hakuna ugomvi. India, chini ya mfumo wake wa caste, ni taifa baguzi karibu sawa na makaburu wa Afrika Kusini zama za ubaguzi wa rangi. Hivyo, hapa tunapata somo kuwa kila bidhaa zitokazo nje lazima tuzipekue kwa makini kweli kweli vinginevyo tutageuzwa dampo la sumu duniani na kujiangamiza.
    Mheshimiwa Rais, mbali na bidhaa za sumu, siku hizi, nchi za magharibi zimetugeuza dampo kwa bidhaa za kielektroniki na sumu. Tunaletewa mafriji mitumba, kompyuta na zana nyingine kwa nia ya kuzibwaga kwenye dampo ili baadaye tuathirike. Mwaka 2019, kulikuwa na kashfa ya Kanada kutupa uchafu wa plastiki huko Malaysia na Ufilipino. Hawa wenzetu hawatujali wala kutuona kama binadamu sawa na wao. Ndiyo maana wanatubagua, kutunyonya, walitutawala hata kutupeleka utumwani. Hivyo, leo sitaki niseme mengi. 
    Mheshimiwa Rais, nakuomba uingilie kati kwenye kashfa hii ili wote waliohusika wajulikane. Hata India ijulishwe namna tulivyokasirika kuhusiana na jinai hii ya kibaguzi na kimataifa. Niruhusu nirudie kwa hesima na taadhima. Hili ni lako. Iokoe Tanzania toka kwenye ubaguzi, jinai na uchafu huu. 
Chanzo: Raia Mwema kesho.


No comments: