The Chant of Savant

Tuesday 14 December 2021

Kuna Haja ya Kuepuka Ugaidi wa Kimataifa

Hivi majuzi wenzetu nchini Uganda walishambuliwa kigaidi ambapo watu walipoteza maisha na wengine kujerehiwa. Tokana na kadhia hii, Uganda sasa iko nchini DRC ‘ikiwasaka’ magaidai wa kundi la ADF. Tukumbuke. Ni Uganda hii iliwahi kuivamia DRC baada ya kumweka madarakani na hatimaye kukosana na Laurent Desire Kabila. Baada ya kelele nyingi kimataifa, Uganda na wavamizi wenzake waliondoka nchini DRC ambako wanashutumiwa kuiba mali nyingi hasa madini, mbao na mali nyingine. Je tutajuaje kuwa Uganda–––kwa kutumia kisingizio cha mashambulizi ya ADF–––inarudia mchezo wake? Nini tofauti ya uvamizi wa sasa na ule wa awali? Na je hii ndiyo njia pekee ya kutatua mgogoro huu?
        Kwa sasa dunia imejaa ugaidi wa kitaifa na kimataifa tena ukitendwa na magaidi wakubwa kuliko hata hao wadogo wanaowasaka. Unatendwa na nchi zinazojifanya vinara wa vita dhidi ya ugaidi na madhara yake ni makubwa kuliko yale ya ugaidi wa makundi. Wataalamu wa ugaidi wanakubaliana kuwa ugaidi unaotendwa na mataifa ni mkubwa na hata madhara yake ikilinganishwa na ule wa vikundi. Hasara na idadi ya vifo ambavyo vimewahi kusababishwa na ugaidi wa vikundi haifikii hata aslimia kumi ya ule unaotendwa na nchi ima dhidi ya watu wake, makundi au mataifa mengine. Mfano, tangu lianze kutenda Ugaidi, hakuna ugaidi ambao umewahi kutendwa duniani kulingana na ule uliokwishatendwa na taifa la Marekani au Ufaransa. Mataifa haya yameishaua na kupindua viongozi wengi wa kiafrika ukiachia mbali kudhoofisha nchi nyingi.
 Sina haja ya kutetea kundi la ADF ambalo limeishaua watu wengine nchini DRC. Vile vile suingi mkono taifa moja kulivamia jingine kisa eti ni kusaka magaidi. Lindeni mipaka yenu au kaa mzungumze na wapinzani wenu. Kilichotokea nchini Iraki baada ya kupinduliwa imla Saddam Hussein au Libya kilipaswa kuwa somo kwa nchi moja kuingilia nyingine kwa kisingizio cha kusaka magaidi. Tangu wakati ule Iraki na Libya zilijifia kiasi cha kugeuka chaka la uhalifu na mapigano huku mali zao zikisombwa mchana kutwa na magaidi wa kubwa wa kimagharibi waliozivuruga tena bila aibu wala huruma. Kuna nini cha maana kimebakia pale Libya ikilinganishwa na kabla? 
Ni bahati mbaya kuwa baadhi ya nchi nyemelezi za kiafrika zimeanza kuiga ughaidi huu wa kimataifa. Kwa sasa Kenya imekwama nchini Somalia. Afadhali hata ya Kenya. Kwani, Somalia ilijifia zamani na pia Somalia haina raslimali za maana za kuibiwa. Kuna nchi ima zinatumiwa na maghaidi ya kimagharibi kuibia nchi nyingine ili kulisha soko huru la magharibi. Na hiki ndicho chanzo kikubwa cha vita ya DRC, taifa lenye kujaliwa utajiri wa raslimali kuliko zote Afrika ambazo madini yake mengi ndiyo roho ya viwanda vingi vya nchi za magharibi hata na mataifa yanayoibukia kama vile China na India.
        Inashangaza kuwa DRC imejiunga kwenye Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) na umoja huu unakaa kimya wakati mambo kama haya yakiendelea. Kwanini EAC isikae na kuona namna ya kusaidiana na wananchama wake kupambana na makundi ya kigaidi kama ADF? Je kuruhusu kila nchi itumie agenda zake za siri na misuli yake ndilo jibu zaidi ya kuhatarisha amani kwenye ukanda huu? Tanzania ilipoingia Uganda kumtoa Idi Amin, ilikuwa imechokozwa na Uganda na siyo kundi la wapinzani. Hata kabla ya kuingia vitani, ilikwenda ilitaka ushauri toka kwenye mafungamano yake ya kimataifa. Je Uganda imefikia kuingia DRC baada ya kushauriana na nani? Je itaendesha operesheni zake kwa muda gani? Tunavyojua uchumi wa nchi za kiafrika zinazotegemea misaada, mikopo na kuomba omba, hakuna nchi yenye misuli kifedha kuisaidia nyingine zaidi ya kuwa na wafadhili nyuma ya pazia ambao nao hufadhili nchi husika kulinda maslahi yake kwa kuhofia kujiingiza kichwa kichwa na kuwaudhi wakubwa wenzake au kuumia.
        Hata hizi nchi zinazofadhiliwa nyuma ya pazia kupigana vita ya kulinda maslahi ya wakubwa zake ni sehemu ya ugaidi tena wenye madhara kuliko ule wa vikundi nyemelezi kama ADF ambalo–––kama Uganda ingependa kuliangamiza na si kulitumia kama sababu ya kuingilia DRC¬¬¬–––ingeishaliteketeza siku nyingi. Uganda iliwezaje kumshinda Joseph Kony lakini ikashindwa kuteketeza kundi hohehahe kama ADF kama kweli ina nia ya dhati ya kufanya hivyo? Je kuna mchezo kati ya Uganda na ADF? 
        Leo Uganda imeingia DRC kuwawinda ADF. Kesho Rwanda itaingia DRC kuwasaka wahalifu waliotekeleze mauaji ya halaiki ya 1994. Je DRC, kama mwanachama wa EAC atakuwa na faida gani ya kujiunga na jumuia ambayo hata haiwezi kuitetea ukiachia mbali kuona wanachama wenzake wakiivamia na kujichukulia watakacho? Je huu ndiyo umoja Afrika iliopigania ambao, hata hivyo, watawala wetu wameshindwa kuuleta?
        Hatuna ubishi kuwa kilichotokea Uganda hivi karibuni ni mashambulizi ya kigaidi. Je hii ndiyo njia sahihi ya kupambana nao? Tunajua ugaidi upo na kila nchi inayokumbana nao ina haki ya kujilinda. Je nchi husika inapata wapi haki ya kuvamia nchi nyingine kana kwamba maslahi yake ni ya maana kuliko ya nchi inayoivamia? Je suluhu kwa ugaidi kama huu wa ADF ni kuvamia DRC au kuhakikisha DRC inatumia uanachama wa EAC kujiimarisha kisiasa ili kuweza kulinda mipaka yake? Laiti nchi za EAC zingekuwa zinaona mbali, huu ndiyo ulikuwa wakati mwafaka wa kuunganisha nchi hizi na kufagilia mbali makundi kama haya na kutenda haki kwa wananchi wake
        Tumalizie kwa kusisitiza kuwa siku hizi ugaidi umekuwa kisingizio cha nchi za magharibi na nchi za kiafrika ambazo hazina raslimali za kutosha kuvamia na kuibia nchi zenye utajiri wa raslimali. Kwa kuzingatia mtindo huu mpya, magaidi wanaosakwa mara nyingi si binadamu bali raslimali. Hivyo, huu ni ukoloni mpya kwa Afrika ambao unaendeshwa na waafrika wenyewe dhidi ya waafrika wenzao. Ni wizi mpya unaofanywa na waafrika dhidi ya wenzao huku wanaonufaika wakiwa ni mabwana zao wa magharibi au mataifa yanayoibuka.
Chanzo: Raia Mwema kesho.

No comments: