The Chant of Savant

Sunday 5 December 2021

Rais Samia Mulika Taasisi Zote za Umma

Mheshimiwa Rais, kama ada salamu kwa JMT. Sema, kazi iendelee. Na kweli, kwa moto uliouwasha juzi, naona kazi inaendelea kweli kweli. Kwani, wapo walioanza kuuliza, kunani mbona huyu hatumbui? Kwa kitendo cha juzi cha kuwatumbua bodi ya Mamlaka ya Bandari na Bandari, waingereza husema, umepiga risasi ya onyo. Je watakuelewa bila kutumbua na kutumbua na kutumbua?
    Mheshimiwa Rais, barua ya leo itaongelea kutumbua na kutumbua na kutumbua na kutumbua hadi ikukere utumbue kweli kweli tena kwa marefu na mapana. Nadhani unanielewa. Kwani, bila kutumbua, utalaumiwa na kulaumiwa na kulaumiwa tena na wale wale wanaofanya huo uchafu wanaokulaumu kwao.  Hao ndiyo wanadamu. Unakumbuka kisa cha Yesu alipokwenda Yerusalem akaponya wagonjwa? Alipokelewa kwa hoihoi, nderemo, shangwe na vigeregere hadi kutandikiwa miswala akanyage. Aliwaponya na kuwanywesha wengi. Ila siku alipokamatwa, ni wale wale waliompokea kwa shangwe walikuwa wa kwanza kupaza sauti na kusema “asulubiwe, asulubiwe asulubiwe” kama ambavyo watu tena wa ndani ya serikali yako wameanza kusema “ulaumiwe, ulaumiwe na ulaumiwe” ili wao wanusurike.
        Mheshimiwa Rais, baada ya kukupa ninachodhamiria kuwasilisha, ngoja nizame zaidi ndani. Kwanza, nakupongeza, kwa kuazima maneno ya rafiki na rais wangu Benjamin Mkapa, uwazi na ukweli wako katika kueleza madudu yanayofanyika kwenye taasisi za umma tena yakifanywa na watu wetu walioaminiwa dhamana wakati wako watu wengi wenye uzalendo na ujuzi lakini hawana dhamana wala kazi. Kwa kuzingatia wingi wa wasomi tulio nao, nakwambia tumbua, tumbua na tumbua tu. Kata mti na panda mti mbegu zipo nyingi. Hire and fire.  Tunao wasomi wa kutosha.
    Leo sina jipya zaidi ya mapya. Nagusia Kampuni ya ujenzi wa meli ya kituruki uliyosema kuwa ilipata tenda wakati haina uwezo. Je hawa walioipa hiyo tenda hawakufanya utafiti? Kama. Hawakufanya, kwanini? Kama walifanya, ni kwanini hawakugundua yaliyogundulika tokana na juhudi za serikali yako? Je kuna kitu walipewa kiasi cha kupofuka na kutoiona haki hata kwa kutumia common sense na badala yake wakatumia uncommon sense?  Je wameishatuingizia hasara kiasi gani na kwa muda gani? Je hawa ni akina nani na wanangoja nini kwenye ofisi za umma? Je hata Takukuru nalo hili linangoja amri yako? Kwani kazi ya Takukuru nini na kwanini wamepewa kila aina ya wataalamu na fedha ili wafanye nini kama hawawezi kunusa madudu kama haya? Je Takukuru nawauliza, hamna wachunguzi wenu? Je nyinyi na hawa wezi mnalipwa kwa nini wakati mnaliangusha taifa kwa maslahi uchwara binafsi?
    Mheshimiwa Rais, kwanza, naomba nitoe ushauri. Lazima wahusika washughulikiwe haraka sana iwezekanavyo kuweka wazi majina ya wezi hawa, kuwachukulia hatua za haraka mojawapo ikiwa ni kuwasimamisha kazi ili uchunguzi wa haraka ufanyike na matokeo yake kutolewa kwako nawe uyatoe kwa umma. 
    Pili, makampuni matapeli kama hili la kituruki lipigwe marufuku kufanya biashara Tanzania. Chunga. Huwa wakipigwa marufuku, huenda kwao na kubadilisha majina na kurejea kufanya uchafu ule ule. Hapa la kwanza, ni kuwabana makuwadi wao. Pili ni kuujua mtandao wao na kuuvuruga. Na nne ni kuhakikisha mnaimarisha makampuni ya ndani yanayoweza kufanya kazi kama hizo. Je serikali–––baada ya kufariki kwa mzee Salehe Songolo–––imefanya nini kuwatafuta na kuwaandaa watanzania wengine wanaoweza kujenga meli?  Je hawa mainjinia tunaosomesha na kuhitimu kila mwaka ni wa nini na wanaweza kufanyia nini kama taifa? Wataishia kuwa vibarua wa wageni tu kana kwamba vyuo vyetu havina sifa au bongo zetu zimejaa matope?
    Tatu, wakamatwe haraka wale wote walioshiriki mchezo huu mchafu warejeshe fedha za umma bila kusahau kuwawajibisha kuanzia kuwafukuza na kuwasimamisha kazi na kuwapeleka mahakamani baada ya kuwafilisi haraka.
    Nne, kamata mali zao haraka sana wakati uchunguzi ukifanyika. Hapa lazima tuwabane watoe maelezo ya namna walivyozipata mali husika. Tena hizi hazihitaji utaalamu kuzijua. Angalia namna wanavyoishi ikilinganishwa na vipato vyao halali.
    Mheshimiwa Rais naomba nimalize kwa kukueleza kuwa wananchi wanataka kuona matendo siyo malalamiko wala manung’uniko. Kama yatakuwapo, yawe ni yale yatokanayo na kibano kwa wahalifu hawa. Kama ulivyosema, ajabu ya maajabu ni kuwa wale wale wanaofanya ufisadi ndiyo hao hao wanalalamika kuwa ufisadi umerejea wakati umekuwapo siku zote mchwa hawa walipopewa dhamana ya umma.
    Mheshimwa Rais, jicho kali ulilopiga kwenye bandari na uchafu wao litumie hilo hilo kumlika sehemu nyingine nyeti kama vile viwanja vya ndege, mipakani, madini, utalii, usafirishaji kwa ujumla, viwanda, biashara, uwekezaji, uhamiaji, TRA, mahakama na polisi ambako mishiko inapigwa kila uchao huku watanzania wakiendelea kuumia.
Chanzo: Raia Mwema kesho.

No comments: