The Chant of Savant

Sunday 19 December 2021

Ndoa za vibabu/bibi na vijana wa kiafrika ukoloni na utumwa mpya


Kisa cha bibi wa kizungu na kijana wa kiafrika nilichoshuhudia uwanja wa ndege mmoja–––sitautaja–––wakibusiana kimenisukuma kuandika haya. Kuna ukoloni na utumwa kimapenzi vimezuka ambapo waafrika ndiyo wahanga–––tokana na maingiliano ya kimtandao––– hata maisha. Mabalaa haya yamejikita kwenye mapenzi ya bandia ambapo mmoja wa ‘wapendanao’ humtumia mwenzake kulingana na hadhi yake kijamii mbali na rangi yake. Si suala jipya tena kuona vibabu/bibi vya kizungu vikifunga ndoa na wavulana/wasichana wa kiafrika mtawalia. Bila kupoteza muda–––hapa kuna tamaa, ujinga na umaskini–––kama vyanzo vya ukoloni na utumwa huu wa kimapenzi.
Katika mila za kiafrika, mwanaume hutegemewa kuoa mtu ima wa umri wake au anayemzidi umri japo si kwa mbali sana. Hivyo, inapotokea mwanaume, tena kijana, akaoa mwanamke mwenye umri au zaidi ya mama yake, jamii iliyomzunguka hustuka, kuhuzunika na kushangaa, kuchukuia hata kulaani. Inapotokea binti akaolewa na kibabu, hali huwa hivyo. Kwani, kwa waafrika, hakuna kitu muhimu katika ndoa kama tegemeo la kuzaa watoto ambao, mara nyingi, ndilo malipo kwa jamii na wazazi. Ndoa bila mtoto, kwa muafrika, ni janga. Sasa tujiulize. Inakuwaje kitu hiki muhimu kwa maisha ya jamii ya kiafrika kinawekwa kando na wahusika? Je ni zaidi ya hili? Inakuwaje kijana wa kiafrika wa kike au kiume kukubali kufunga ndoa na zee lisiloweza kumzalia au kumzalisha watoto–––likimzalisha–––humuachia ujane? Je hapa tatizo ni tamaa, ujinga au umaskini ukiachia mbali ibada za rangi ambapo mtu mweupe, hasa mzungu, anaonekana mali hata kama si mali kitu?
Katika mahusiano haya, waafrika hutumiwa na wazungu. Kwani, sijawahi kuona mzee wa kiafrika akioa msichana wa kizungu au bibi wa kiafrika akiolewa na kijana wa kizungu. Kwanini? Hapa kuna tatizo; si rahisi kupata majibu sahihi bila kudurusu. Kwa akili ya kawaida na mazoea, hili si jambo la kawaida, hasa kwa waswahili. Kimsingi, katika ndoa hizi, mwenye mamlaka ni mweupe na asiye na madaraka ni mswahili. Hivyo, ni rahisi kusema kuwa mswahili anaolewa katika mahusiano haya.
Kiafrika, mwanaume humuoa mwanamke na mwanamke huolewa na mwanaume. Ila katika uhusiano tunaojadili hapa, mwanamke na mwanaume wa kiafrika huolewa na mzungu na mzungu humuoa muafrika bila kujali kama ni mwanaume au mwanamke. Mbali na ukoloni hu una utumwa wa mapenzi, jambo ambalo limezoeleka ni kuona vibabu matajiri vya kiafrika vikioa mabinti wabichi wanaofuata ulaji kwao.  Kadhalika, hata katika ukoloni na utumwa huu wa mapenzi, mswahili huwa na mategemeo kuwa akiolewa na mzungu ataukata kwa kuweza kwenda majuu au kutumiwa madola.  Hapa thamani ya maisha ya binadamu, ambayo kawaida, thamani yake ni kubwa kuliko chochote, huishia kuwekwa kwenye vitu vya hovyo tokana na ima ujinga au umaskini kama masalia ya ukoloni wa kimila ambapo mtu mweupe ni mkombozi wa mtu mweusi–––hata kama dhana hii ni hovyo na ushahidi wa utumwa wa kiakili, kimaadili na kimila.
Hebu tuwe wakweli wapendwa wasomaji. Hivi kuna mapenzi kati ya kizee cha miaka–––tuseme miaka 60,70 au zaidi kuoa kijana wa miaka 30,35 hata 40 au msichana kigoli kuolewa na babu yake? Hapa tunapata dhana ya ubaguzi wa kujitakia ambapo muathirika hujiona dhaifu mbele ya mkoloni wake bila kujali jinsia. Hapa kuna maswali. Je kuolewa na mzungu ni kuukata au kupatikana mbali ya kudhihirisha ujinga, umaskini na tamaa ya wahusika? Nimeishi na wazungu kitambo si haba. Kama kuna kitu wanacho si kingine bali umimi. Mila iitwayo kwa kiingereza individualistic humtengeneza mtu kujiona kama huru na asiyejali wengine isipokuwa yeye. Hapa ndipo chanzo cha kwanza cha balaa hili kilipo mbali na ukoloni ambapo waafrika wameaminishwa na wakaamini–––iwe ni kwa kupitia dini au siasa–––kuwa wazungu ni wakombozi wakati ni waangamizaji. Utamuona Yesu mweupe wakati hakuwa mzungu. Mitume wote siyo waafrika. Maandiko matakatifu yote ni ya kigeni na lugha zinazotumika kuyaeneza. Huu ndiyo mzizi wa kila kitu. Mfano, wazungu wameweza kuzizuia nchi za kiafrika kuwapa fidia na mafao wakulima wao wakati wao wakifanya hivyo kwa wakulima na watu wao. Sababu? Waligundua, kutengeneza, kutangaza na kueneza ‘weupe’ kuwa ukombozi na wengine wenye dhambi. Unashawishikaji kuwa kila mtu anazaliwa na dhambi wakati mtoto mdogo ni malaika; usihoji kama hakuna tatizo hapa?
Ukoloni na utumwa kwa waafrika ulianza tulipohujumiwa na kurubuniwa kuacha mila zetu na tukakumbatia mila hatari za kigeni ziitwazo dini na ustaarabu japo si chochote wala lolote bali maafa kwetu. Mzazi unajisikiaje kijana wako wa kike/kiume anapoolewa na bi kizee kuliko hata baba au mama yake kwa kisingizio cha ‘mapenzi hayana macho.’ Mapenzi yana macho. Ndiyo maana, hayaishi bila kuwa na uhuru na utashi wa kuchagua, ambao katika balaa hili jipya haupo. Binadamu anapotumia njaa, tamaa, ujinga na umaskini kama nyenzo za kufikiri, anaweza kufanya jambo ambalo hata mnyama hawezi kufanya.
Tumalize kwa kuwashauri vijana wa kiafrika kuacha kuuza utu wao eti kwa tamaa na ujinga wa kwenda majuu. Wakishafikishwa ‘majuu’, huumizwa na kuwa watumwa zaidi wakaishia kujuta kama mmoja niliyekutana naye kwenye mji jirani aliyenyofolewa Arusha na kuishia kwenye utumwa. Kimsingi, haya si mapenzi bali ujinga, ukoloni na utumwa wa kujitakia. Akili inapoingia tumboni na kuukimbia ubongo, matokeo yake ni maafa ambayo sasa yanalinyemelea bara letu. Serikali zetu zinapaswa kuingilia kati kuhakikisha vijana wetu wana elimu safi ili kuepuka kutumiwa kwa kujiingiza kwenye utumwa tuliojadili hapa. Nini mawazo yenu vijana kabla hamjaangamia mkijiona kwa tamaa, ujinga na upogo?
Chanzo: Raia Mwema kesho.


No comments: