The Chant of Savant

Monday 13 December 2021

Wasanii wetu watofautishe usanii na ubabaishaji


Huwa sipendi kuongelea mambo madogo hasa yanayowahusu watu binafsi. Huwa napenda kuongelea mambo makubwa na muhimu kwa taifa. Nikiri. Ni mara ya kwanza kuandika makala inayoongelea watu wa kada ya sanaa. Pamoja na kuandika makala ambayo hata idadi yake siijui japo naweza kusema zinaweza kufikia maelfu kwa uchache tu. Ni leo tu, kwa mara ya kwanza naandika makala juu ya wasanii na sanaa.
        Katika kuangalia maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika, nilichukia. Ni pale nilipopata ambacho sikutegemea mtanzania aishie nje. Baada ya kufaidi gwaride, na mambo mengine ya kuvutia kama vile utenzi, na nyimbo, kitumbua kiliingia mchanga kiasi cha kuacha kumalizia masaa manne ambayo nilitenga usiku kuangalia sherehe husika. Ni pale alipoitwa msanii wa vichekesho (standing comedian) aitwaye Masanga Mbanagaizaji (hili si jina lake). Akiwa amevaa mavazi ya hovyo ambayo hayaendani na sherehe husika alianza kubwabwaja huku akiwaacha hadhira vinywa wazi badala ya kucheka na kumshangilia kama angekuwa amekidhi lengo. Alisema alisema “Mheshimiwa Rais, nashukuru leo pia mkuu wa majeshi yup oleo. Tunaendelea kununua mavifaru na haivitumiki. Zungumza hapo na honourable Kagame hapo kidogo tutest vyombo. Mavyombo yanakaa tu.” Baada ya kutamka maneno haya, hata jukwaa kuu lilionekana kustuka, sijui kuudhika.  Kwani, hakuna vicheko wala makofi kama tulivyozoea pale msanii anapowasilisha vilivyo ujumbe wake. Naamini Mheshimiwa Rais, licha ya kustuka, aliudhika. Pia, naamini waliomwalika huyu msanii lazima wataonywa au kutomwalika tena ukiachia mbali kubadili utaratibu wa kualika wachekeshaji kwa mazoea badala ya kuzipitia kazi zao kabla ya kuzirusha kwa jamii.  Sijui Kagame alijisikiaje hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania si nchi ya kuweza kulinganishwa na nchi kama Rwanda kijeshi na kimkakati.  Hivi kweli mtu mjuzi anaweza kutaka nchi ifanyie majaribio silaha zake kwa kuua watu? Kuna vitu  havipaswi kufanyiwa ucheshi wala utani. Mfano, huwezi kwenda mahali patakatifu ukiwa uchi wala kushauri wanaokwenda pale wafanye hivyo eti unachekesha au kutania. Utani una namna na mafunzo yake kwa jamii. Je kwa huyu mbangaizaji kutaka tutest silaha zetu kwa Rwanda, alilenga kuwasilisha; na alimaanisha nini? 
         Kwa mtu anayejua diplomasia na mahusiano ya kimataifa, kwanza, hawezi kuamini kuwa kitu hiki kimetamkwa tena kwenye hafla muhimu kama hi. Pia, kwa mtu anayejua maana ya neno uchonganishi kimataifa, haamini. Hata msemaji angejua madhara na ukubwa wa alichobwabwaja wala asingekubali hata hiyo tenda ya kujaribu kuchekesha kwenye hadhira hii akaishia kujidhalilisha na kuhatarisha hata usalama wake.
Kwanza, si kweli kuwa tangu tupate uhuru silaha tunazonunua zimekaa tu. Mwaka 1978 tulikwenda Uganda kumchakaza Idi Amin na kuwakomboa waganda toka kwenye utawala wa kiimla na kijinga wa Amin. Hatukuishia hapo, baada na kabla ya hapo, Tanzania ilitoa msaada wa hali na mali kwa nchi za Kusini mwa Afrika chini ya kile kilichojulikana kama Nchi Zilizokuwa Mstari wa Mbele wa Ukombozi wa Kusini mwa Afrika (Frontline States––FLS) ambazo zilichangia pakubwa kukomboa nchi za Kusini mwa Afrika.  Mbali na hiyo, Tanzania imetuma majeshi yake kwenye nchi mbali mbali kama vile Comoros, DRC na nyingine pale zilipokumbwa na vurugu.
        Inaonekana, huyu msanii haijui hata historia ya nchi yake. Huu ni ushahidi kuwa anahitaji japo elimu kidogo lau juu ya historia ya nchi yake na namna mataifa yanavyohusiana. Ni bahati mbaya kuwa hata wale waliompa tenda ya kuchekesha kwenye sikuku muhimu kama hii, ima nao hawakuwa wajuzi wa mambo au hawakuona kazi za mhusika kabla ya kuruhusu kuwekwa hadharani.
Huu ni mfano na ushahidi mdogo kuwa wasanii wetu wengi hawana elimu wala hawataki kujielimisha. Wengi wanaamini katika vipaji bila kuvinoa. Vipaji pekee haviwezi kukidhi haya ya jambo lolote. Vinahitaji kunolewa kwa njia ya kujisomea na kujiendeleza kwa kila namna. Wengi wanasukumwa na dhiki kuingia kwenye sanaa na wakishapata majina hawajiendelezi bali kuridhika.         Pia, wasanii wetu wengi, hawatafuti msaada wa wajuzi. Na matokeo yake, wengi hawatoi kazi zinazoridhisha. Mfano, wanamuziki wetu wa kizazi hiki, wanapenda kuimba mapenzi na matusi kana kwamba hakuna mambo mengine muhimu. Ukiondoa magwiji kama akina Marijani Rajab, Muhdin Ngurumo, Hassan Rehani Bitchuka, na wengine waliotangulia, muziki wa sasa ni mapenzi na matusi, basi. Hata kwa upande wa wachekeshaji, ukondoa mzee Jangala na mzee Majuto kwa mbali, hakuna mchekeshaji mwenye kuonyesha kipaji kinachoridhisha. 
Wasanii wetu wafanye yafuatayo:
        Kwanza, wawe na tabia ya kujiendeleza kwa kusaka maarifa iwe kwa kujisomea au kwenda shule ili waweze kufanya vitu wavavyoelewa na vinavyoeleweka na kukubalika. Lazima wajifunze kutofauti hadhira.  Kuchekesha harusi siyo sawa na kuchekesha taifa. Mbona chuo cha Sanaa Bagamoyo kipo na kwanini hawakitumii kujinoa?
        Pili, wahakikishe kazi zao ziwe zinapitiwa na wataalamu wa fani kabla ya kuziweka dharana. Kama huyu Masanga Mbangaizaji angekuwa amekwenda kwa mtaalamu na kumwonyesha kazi yake, basi asingejiaibisha na kuabisha taifa. 
        Tatu, waache kufanya sanaa ima kwa kusukumwa na mazoea au njaa au kutafuta umaarufu. Watafute ujuzi wa sanaa ili kuweza kuimudu vilivyo.
        Nne, watofautishe sanaa na ubangaizaji ambao watoto wa mjini huita usanii. Kama wameamua kuwa wasanii basi wafanye sanaa na siyo usanii kwa maana ya ubabaishaji na ubangaizaji kama ilivyojionyesha. Wenye busara wanasema kuwa ni vizuri kuonyesha ujuzi wako na kuficha ujinga wako.
        Tano, hata wale wanaowaalika wasanii, wawe wanapitia kazi zao kabla ya kuziruhusu kutumika. Kama wakifanya hivyo, wataepusha aibu niliyoina kwenye maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika.
Chanzo: Raia Mwema leo.

No comments: