![]() |
| Picha hii imnechukuliwa toka kwenye blog ya maisha na mafanikio |
The Curse for Salvation
Wednesday, 18 January 2017
Magufuli hana haja ya kutishia vyombo vya habari
Taarifa za vyombo vya habari zilizomnukuu rais John Pombe Magufuli akiyaonya magazeti mawili kutokana na kile anachosema ni kuandika habari za uchochezi si njema kwa taifa tena la kidmokrasia kama Tanzania.
Vyombo vya habari, sawa na Magufuli, vinatekeleza wajibu wake kisheria. Hivyo, hakuna mwenye mamlaka kisheria kuvitisha au kuvilazimisha vifanye anavyotaka. Je Magufuli anaweza kukubali kutenda kazi zake kulingana na matakwa ya vyombo vya habari? Nadhani, Magufuli anahitaji ushauri tena mzuri kuhusiana na namna vyombo vya habari vinavyofanya kazi. Hana haja ya kuviona kama adui kama anatimiza wajibu wake kisheria au pale vyombo vya habari vinapotimiza wajibu wake hata kama hapendi kinachoandikwa.
Uzoefu unaonyesha; hakuna mtawala aliyeshindana na vyombo vya habari akashinda; hasa ikizingatia; wote wapo kwa mujibu wa sheria. Vyombo vya habari vipo kwa ajili ya wananchi na si watawala. Pia vyombo vya habari vinapotokea kukiuka sheria, kanuni na taratibu, kuna utaratibu wa kisheria wa kushughulikia hili; na si kutunishiana misulu na kutishana. Sidhani kama wote tunaweza kuangalia mambo kwa namna moja tukawa salama. Binadamu ni tofauti na wanyama ambao huwa hawabadiliki tokana na kutojaliwa utashi katika maisha yao.
Hata Yesu alisema “kama sehemu zote zingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi?” Wakorintho 12:19. Kama vyombo vyote vitaisifia na kukubaliana na kila inachofanya serikali, mawazo mbadala yatatoka wapi? Jamii isiyokosoana haiwezi kukithi matarajio ya wanajamii wake hasa ikizingatiwa: tuna vionjo na vipaumbele tofauti kama raia wa taifa moja. Kama alivyo na malengo na mipango yake na vyombo vya habari kadhalika. Itakuwa ajabu kuona vyombo vyote vya habari vikisifia kila anachofanya Magufuli. Isitoshe, vipo vyombo vya habari vilivyoanzishwa na kulipwa kwa ajili ya kusifia serikali hata ikifanya mambo tofauti na inavyotakiwa. Pia, vipo vyombo vya habari vinavyojikomba kwa serikali ili vikumbukwe kwenye ulaji. Hivi ni vyombo vya habari uchwara vinavyotumiwa na waganganjaa kupatia kitumbua hata kwa kupinda na kupotosha maadili (ethics) za uandishi . Hivi ni vyombo vya habari vilivyojaa makanjanja wanaotumia kalamu zao kutafuta vyeo na ulaji rahisi. Tuliyaona wakati wa utawala uliopita. Baadhi ya waliodhaniwa kuwa waandishi nguli walijidhalilisha na kujitoa mwili na roho kuandika upuuzi wa kusifia upuuzi ili watupiwe vyeo kama vile ukuu wa Wilaya, Ukatibu katika ofisi za chama tawala na upuuzi mwingine. Pia, vipo vyombo vya habari ambayo hupenda kuviita mbwamwitu vikilinganishwa na vile mbwa wa kufugwa visivyokuwa kujikomba lau vipate tenda, matangazo au wanaovitumia wapewe vyeo hata kama hawana sifa wala stahiki.
Magufuli alikaririwa akisema “hayo magazeti kila ukisema hivi yanapindisha, siyataji kwa sababu yanajifahamu lakini yajue kwamba siku zake zinahesabika. Serikali ninayoiongoza haiwezi kukubali amani kuvurugwa.” Kupindisha ni neno tata. Yanapindisha nini na kwanini? Je amani inaingiaje na upindishaji? Hivi rais akisema uchumi umekua, kwa mfano, magazeti yakasema unadumaa, yanatishia amani? Hapa kinachotakiwa linapotokea jambo kama hili ni kwa wawili kuthibitisha madai yao. Simple. Huwezi kulinganisha Tanzania na Rwanda kuhusiana na kilichotokea mwaka 1994 kwenye mauaji ya kimbari. Kilichosababisha mauaji haya ni mabaki ya ukoloni na utawala mbovu. Vyombo vya habari vinatupiwa lawama kwa vile vilitumiwa na wanasiasa wakabila na wasiotenda haki. Kwa waliosoma historia ya Rwanda, mauaji ya kimbari yaliasisiwa na wakoloni wa Kijerumani pale walipowadanganya Watutsi kuwa ni bora kuliko Wahutu yakaendelezwa na watawala wa Kibelgiji waliochukua nchi ile baada ya vita ya pili ya dunia chini ya kile kilichojulikana kama tutsification (Prunier 2009: 3 aliyekaririwa kwenye Ibreck 2010: 2). Huu ni ukweli (a set of facts). Kuna methali ya kiingereza isemayo Truth is a spectre that scares many (ukweli ni jinamizi linalotisha wengi). Wanaohofia mauaji ya kimbari wanakwenda mbali zaidi ya wanavyopaswa ima kwa kutojua au kwa woga au hila ya kutafuta kisingizio. Kilichosababisha mauaji ya kimbari zaidi ya mabaki ya ukoloni (colonial carryovers) ni ubaguzi na ukosefu wa haki. Huwezi kuwabagua watu tokana na asili au imani yao ukawa salama. Kinachotakiwa nchini si kutishana bali kutenda haki kwa mujibu wa sheria. Huwezi ukabagua magazeti na kutishia kuyakandamiza yakakupenda. Kila binadamu amejaliwa akili na utashi wa kuchagua, kuchuja na kudurusu mambo. Kama vyombo vya habari vitapindisha ukweli vishitakiwe na si kutishiwa kufungiwa wala kufutwa.
Kusema kuwa baadhi ya vyombo vya habari vinaandika habari za kichochezi ni kupindisha na kupotosha ukweli anaodai rais unapotoshwa na vyombo vya habari. Kuna msemo kuwa there are three sides to every story: yours, theirs and the truth. Huwezi kuchochea watu wakakusikiliza kama hawana lao. Kusema kuwa watanzania ni viumbe wa kuchochewa na kutenda ni kuwageuza hamnazo na wasioweza kupembua. Mfano, huwezi kuandika kuwa rais yuko uchi wakati amevaa suti ukasikilizwa au kuaminiwa. Lazima tukiri kuwa kuna tatizo. Mfano, serikali yoyote inayotaka kusifiwa bila kulaumiwa ina matatizo. Kama binadamu ambao tumejaliwa udhaifu (fallibility) tukubali. Kuna sehemu tunakosea; na kuna sehemu tunapatia. Huu ndiyo ukweli na ndiyo majaliwa ya binadamu. Hekima ya kawaida inasema ni heri akukosoaye kwa haki kuliko akusifiaye ujinga.
Tumalizie kwa kumtaka rais Magufuli aangalie upya kitisho chake dhidi ya baadhi ya vyombo vya habari. Tanzania ni mali yetu sote kwa sawa. Pale atakapofanya vizuri ataelezwa. Kadhalika, pale atakapokosea atakosolewa tu. Asiyekosolewa ni Mungu tu.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.
Kijiwe chalaani bakora Rorya
Baada ya kurushwa picha za akina Mura Msama, Magesa, Nyambora, Wambura na Kitamara wakimsulubu mama mmoja kwa utovu wa nidhamu, kujiwe kimeamua kuongeza shinikizo dhidi ya udhalilishaji huu wa kizamani na kinyama. Kama si ukata, kijiwe kilitaka kwenda Kinesi hata Kuruya kuangalia kadhia nzima na kuwasulubu wale waliomsulubu mwenzao bila aibu wala stahiki.
Sofia Lion aka Kanungaembe ameguswa kiasi cha kuanzisha mada kwa mara ya kwanza.
“ Nadhani kila mmoja amejionea udhalilishaji wa akina mama unaoendelea kwenye karne ya 21. Kama mwanakaya na mwakakijiwe naleta hoja ya kutaka tulaani upuuzi huu; na hata ikiwezekana twende kule tutoe adhabu ili liwe somo kwa wengine. Hivi hawa hawajui kuwa anayemdhalilisha mwanamama ni kumdhalilisha mama yao?”
Mpemba anamchomkea Da Sofi na kusema “japo si tabia yangu kuchomekea, wacha leo nkuchomekee dadaangu. Sie tumefunzwa kuwa jicho nkwa jicho. Kwanini hawa wazee nao wasiitwe wakachapwa bakora hadharani lau waonje chungu ya kile walichontendea huyu mama asokuwa na hatia? Maana bila kufanya hivo, wawezaendelea na huu utwahuti wao.”
Mgoshi Machungi anakula mic “kama ingekuwa Ushoto hawa wangeitwa na kuchapwa bakoa ii nao waonje uchungu wa huu ujinga na ujima wao. Kama wanajichukuia sheia mikononi, mahakama zitafanya kazi gani?”
Msomi Mkatatamaa anaamua kula mic “nadhani tunapowalaumu hawa wazee wa jadi peke yao wanaofanya upuuzi chini ya kivuli cha mila tunakosea. Kinachojionyesha hapa ni kwamba tangu tupate uhuru, mamlaka zetu hazikuelimisha wachovu wake juu ya haki za kiraia na haki za binadamu. Hata hivyo, sichangai. Ni matapeli wangapi wamejaa kayani wakiwaibia wachovu chini ya kuhubiri dini wakati ni wizi mtupu? Je hawa wana tofauti gani katika kudhalilisha wachovu na hawa wababu wa kimura walioamua kujifanya sheria? Nadhani tukubali. Kaya yetu ina uoza mwingi wa kimfumo ambao mamlaka yameufumbia macho tokana na kuogopa kuamsha waliolala wakalala wao.”
Mipawa anakula mic “ukweli ni kwamba ukombozi wa mwana mama uko mbali sana. Huoni hata kwenye siasa namna wanavyogawiwa nafasi za nyuma huku wakitumika kama nyenzo ya kusakia kura? Ni bahati mbaya kuwa hata vyama vya upingaji vimeukwaa mkenge huu wa ubaguzi na unyonyaji wa kijinsia.” Anamgeukia Sofia na kusema “hata hapa kijiweni mwana mama uko peke yako. Kwanini? Ni kwamba wenzako wanazuiliwa na waume zao kuja hapa kutoa changamoto zao ili ziwekwe wazi na kushughulikiwa. Au nadanganya?” Sofia anatikisa kichwa kumuunga mkono.
Kapende naye anaamua kung’ata mic “ japo nakubaliana kuna ubaguzi na udhalilishaji wa akina mama wa kimfumo kama wa kuwadai rushwa ya ngono kama mhadhiri wa Chuo cha Usafiri aliyenyekwa juzi, wengine wemezidi. Ukisikia vipigo vya kuua wachovu vimetokea, ni huko huko kwa akina mura. Zikilipuka habari za mapigano ya kikabila kule kule. Hii maana yake ni kwamba lisirikali limelala. Na sasa hawa wababu waliotoa amri ya mama kusulubiwa hadharani wanalistua ili liamke na kufanya mambo kiutuuzima na kisasa badala ya kupiga politiki za kutishia vyombo vya umbea.”
Kanji anaamua kuchumpa na kuzoza “mimi ikolia chozi kuba sana siku naona ile mama sulubiwa. Veve Sofi sema kitu kuba sana. Iko nyonyaji sana ya mama. Kwa jumbani yetu mama yote nanyonya. Kwa dukani yetu bado nanyonya. Kwa taa yetu bado nanyanyasa mama. Mimi taka vatu vote badilika na hesimu mama yote ya kayani.”
Mheshimiwa Bwege aliyekuwa akisikiliza kwa makini anaamua kutia buti na kuzoza “Kanji nakubaliana nawe usemayo. Majumbani hasa kwa magabacholi ambapo dada zetu wengi wanatumikishwa kama watumwa wananyonywa na kubaguliwa kweli kweli. Juzi juzi dada mmoja alisimulia anavyolazimishwa kula mabaki ya magabacholi kila anapowapikia na kuwatengea. Alidai kuwa haruhusiwi kulia mezani bali chini tena jikoni. Kusema ukweli, huu ni uoza wa kimfumo dhidi ya kina mama ambao nao wanaonekana kuushiki hasa ikizingatiwa kuwa hata wasaidizi wengi wa majumbani wananyanyaswa na mabosi wao ambao ni akina mama wenzao.”
Sofia anakula mic tena “kaka Mheshimiwa nakubaliana nawe. Kama alivyosema Msomi, huu ni uoza wa kimfumo uliotambuka nyanja zote za kimaisha. Kama nilivyosema, hawa wazee wa kimura wanapaswa kuwekwa hadharani na kuchapwa bakora. Kama alivyosema kama Mpemba, wanastahili kupewa shubiri ile ile waliyompa mama mwenzetu ambaye sasa amedhalilika zaidi baada ya picha yake kurushwa kwenye mitandao dunia nzima. Ni jana tu kaka yangu aishie Kanada alinitumia picha hiyo kwenye simu yake akilalamika kunani hadi tunajivua nguo hadharani. Kama haitoshi, hata vyombo vya habari vya kimagharibi vimeishaidaka na kuionyesha Afrika kama bara la watu wakatili wasio na kifani.”
Mbwamwitu anaamua kumchokea da Sofi na kusema “hapa dawa ni moja. Just kick their ass. Hawa wadingi ni akina nani hadi watangaze ubabe hadharani? Au hawakujua kuwa miongoni mwao walikuwamo mapaparazzi waliotumia simu zao kuwaanika? Ama kweli ujinga ni mzigo.”
Kabla ya kuendelea si akapita mura Nyambola, acha tumtie kati ili tumpe adhabu! Kama si kujitetea kuwa yeye hakuwako kule wala haungi mkono upuuzi huyu, angeishia kutolewa kafara na kusulubiwa kwa niaba ya wenzake.
Chanzo: Tanzania Daima leo Jumatano.
Monday, 16 January 2017
Sunday, 15 January 2017
Magufuli ataweza kutumikia mabwana wawili?
Hakuna ubishi. Rais John Magufuli ana kibarua kigumu. Hii ni kutokana na mfumo mbovu aliorithi bila kuwa tayari kuufumua na kuufuma upya kisheria zaidi ya kufanya hivyo kisiasa. Juzi akiwa mkoani Simiyu, utata na mparaganyiko wa mfumo umefichua ukweli kuwa Magufuli sasa anao mabwana wawili wa kutumikia yaani utawala wake unaotaka kuwakomboa wananchi, na kuulinda ule utawala mbovu uliowafikisha wananchi anapotaka kuwatoa Magufuli. Moja ya vilio alivyosikia toka kwa wananchi wa Simiyu ni ukosefu wa maji. Katika kutoa majibu mujarabu Magufuli aliamua kuwatoa mbele wahusika ili wawape wananchi majibu stahiki. Mmoja wa watumishi hao alimwambia rais kuwa tatizo la ukosefu wa maji kwa makao makuu ya mkoa yaani mji wa Bariadi ni kutokana na kukwamishwa na mwekezaji ambaye eneo lake ni kilima yanapopaswa kuwekwa matenki ya maji ili yasambazwe.
Baada ya kuelezwa hivyo, rais aliamua kutolea uvivu uwekezaji wa kijambazi ulioingiwa na mtangulizi wake, luteni Kanali Jakaya Kikwete kwa kuamuru matanki yawekwe;na kama mwekezaji atapinga afutiwe leseni ya uwekezaji. Wananchi walishangilia na kupongeza hatua hii bila kufikiri madhara inayoweza kulisababishia taifa huko tuendako.
Kwanza, sijui kama rais alijiridhisha kuwa kuna upenyo wa kisheria wa kufanya aliyoamuru au aliamua kuvunja sheria kwa kutumia madaraka makubwa aliyo nayo.
Pili, sijui kama rais alijipa nafasi ya kumjua mwekezaji husika na angalau kumsikiliza kabla ya kutoa hukumu ya upande mmoja. Tungependa kumjua na kujua namna alivyowekezewa hiyo ardhi na lini.
Tatu, mwekezaji naye ana haki ya kusikilizwa kuliko kutoa amri baada ya kusikiliza upande mmoja. Maana bila kufanya hivyo, Tanzania itaonekana kama kigeugeu inayohubiri uwekezaji na uchumi wa viwanda wakati ikipingana na sera yake yenyewe. Hii inaweza kujenga picha mbaya kiasi cha kuwatisha wawekezaji jambo ambalo litakuwa kikwazo kwa mafanikio ya sera za rais Magufuli.
Nne, kuna haya ya kujua ukweli kama kweli mwekezaji alifuata taratibu zote–au hakufuata utaratibu–na inakuwaje leo rais aamue kutishia kufuta hati yake? Je rais amefuata sheria katika kutoa amri yake; baada ya kushauriwa na wanasheria au ametoa tamko na amri vya kisiasa vinayopingana na sheria kiasi cha kuwa tatizo baadaye?
Tano, tunapaswa kuangalia tatizo ni nini? kuna wakati wengine tunawalaumu wawekezaji wakati matatizo ni yetu. Sioni kama Magufuli anaweza kufikia anakotaka bila kufumua na kuufuma upya mfumo wa hovyo wa sasa aliorithi toka kwa serikali ya mtangulizi wake Luteni Kanali mstaafu Jakaya Kikwete ambayo ililsifika kwa ulegelege na rushwa na matumizi mabaya na ukosefu wa umakini. Sitegemei Magufuli afanikiwe bila kuanzisha mfumo wake mwenyewe unaoendana na dira yake. Hapa la kufanya ni moja; ima Magufuli aanze kujenga misingi ya utawala wake kwa kupambana na maovu na waovu wa awamu zilizopita au anyamaze amalize muda wake kama wenzake. Maana haiwezekani kuwatumikia mabwana wawili yaani kuwakomboa wananchi huku ukiwakingia kifua waliowafikisha kwenye mtego unaotaka kuwakomboa.
Sita, nitatoa mfano mmoja hapa. Uwekezaji mwingi uliofanyika tangia wakati wa serikali ya awamu ya pili hadi ya nne mwingi ni wa kijambazi. Hivyo, utamkwamisha Magufuli kutokana na kuwepo sheria za hovyo zinaoulinda. Wakati ule hapakuwapo na maadili ya uongozi ambayo Magufuli analenga kuyarejesha. Hata ukiangalia wajumbe wa kamati ya Maadili ya Viongozi aliyorithi toka kwa Kikwete ina sura za kifisadi zinazojulikana. Mfano kuna mjumbe mmoja Hilda Gondwe ambaye anadaiwa kujiuzia gari aina ya Toyota Landcruiser la Mkoa wa Kilimanjaro kwa bei ya kutupwa. Sijui kama bado ni mjumbe na kama bado ni mjumbe hili linatosha kuwasha taa nyekundu kwa wahusika kumsimamisha na kumchunguza.
Ukiachia mbali na huyo, ukienda mahakamani ambako wawekezaji watakwenda kufungua kesi za madai ya kuvunjwa mikataba au kufutwa leseni zao na kusababishiwa hasara, wamejaa majaji vihiyo na mafisadi kibao. Watakwenda kule watahonga na kushinda kesi wakiilazimisha serikali kuwalipa mabilioni. Fumua mahakama zote kwanza ili upate watu waadilifu na wenye uchungu na taifa lao wanaojua kazi zao waliosoma vilivyo siyo walioghushi kama alivyowahi kudai mwanasheria Tundu Lissu. Hapa narejea ushauri wangu ambao huwa nikiutoa. Majaji au mahakimu wote wenye tuhuma za ubadhilifu, rushwa na ufisadi wanapaswa kuondolewa ofisini. Marehemu baba wa taifa alikuwa na kisa kimoja ambacho alipenda kukitumia alipokuwa akiongelea usafi wa kimaadili. Alizoea kusema kosa la mke wa Kaisari si kutenda uovu ambao kimsingi ni uzushi bali kushukiwa. Mke wa Kaisari hapaswi kutuhumiwa kwa uchafu achia mbali kuutenda. Sasa inakuwaje tunapokuwa na watu waliotuhumiwa wazi wazi wakaendelea kukalia viti vya kutoa haki wakati wao ni wavunja haki na wachafu?
Tumalize kwa kumshauri Magufuli achague wa kutumikia kati ya mabwana wawili yaani wananchi, na viongozi wastaafu waovu, wateule wao, mfumo wao mbovu na maafisa wengine wa umma wenye kutuhumiwa kutenda uovu na ukosefu wa maadili mbali mbali.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.
Saturday, 14 January 2017
Barua kwa mpendwa na munusurika Escrow
Mpendwa Escrow,
Baada ya kukosa ofa na kanywaji na njuluku za kununulia bangi ka muda mrefu, nimekumbuka mpendwa wangu marehemu Escrow aliyetujaza minjuluku hadi tukasahau kuwa kuna siku kutakuwa na ukapa na ukata baada ya mchezo wa kupiga madili kuuawa na maadili ya Bwana nkubwa Joni Kanywaji wa kutia makufukuli ulaji wetu rahisi.Japo sikupata mgao wa njuluku uliotembezwa baada ya wewe kufanyika moja kwa moja, nilizoea kupata ofa kibao za kanywaji toka kwa wale waliofaidi mabilioni uliyotengeneza. Waingereza huita hii kitu “to trickle down” ambapo majambazi wakubwa kama waliokutengeneza kuwahonga wachovu kama sisi ili kuwa washiriki kwenye jinai ya kuhujumu kaya yao.
Kwa vile sasa miaka inazidi kuyoyoma tangu wakubwa wapya waingie kwenye ulaji, wapo waliojidanganya na kuota mchana wakidhani kuwa angalau wangekufukua huko uliko ili ima njuluku za umma zirejeshwe kwake huku walevi kama sisi tukiendelea kukosa ofa zilizotufanya tuwe na furaha kana kwamba hakuna huzuni. Nilisikia wakosoaji wakitushauri tuache kuwa kama samaki ambao mara nyingi hunaswa kwa nyama ya wenzao kwenye chambo. Kabla ya kusahau, siku hizi napenda kuwasiliana na kuwasilisha kwa njia ya barua tokana na kutunukiwa shahada ya juu ya udaktati katika barua yaani Doctor of Letters kwa kifupi Litt. D. hivyo, usishangae kwanini natumia sana barua badala ya makala. Nataka kuonyesha ugwiji wangu katika nyanja hii ya kisomi japo kilevi.
Mpendwa Escrow, huwezi kuamini kuwa wanywanywa walihanikiza na kuchonga sana eti wale waliokuzaa washughulikiwe. Nakumbuka baba na mama yako Jimmy Rugemalayer na Gabacholi Sethii wa ukoo wa IptL. Walisakamwa wee hadi mkuu akasema hana hamu, nia wala uwezo wa kufukua makaburi ili yasijemuua kwa uoza na harafu. Sijui kama nawe ulikuwa mmojawapo; au ni wengine.
Mpendwa Escrow, wanywanywa na wambea siku zote hawana adabu. Hivi walitaka mkuu atende makufuru ya kuwagusa wasiogusika? Walitaka aumbue wazee wazima tena wazee wenyewe walioridhia uzaliwe nao wapate chao? Mbona hawakutumia akili kushangaa kichanga kama wewe wakati kuna babu yako IptL? Walidhani haya mambo yalianza jana siyo? Mbona walinoa ile mbaya hasa ikizingatiwa kuwa chezo zima lilianza zama zile za ruxa ya kufanya kila mlevi afanyavyo mradi asimuumize mkuu? Mbona walisahau kuwa hata baada ya ruxa kufutika mambo yaliendelea kufanywa kwa uwazi na ukweli kabla ya kuwekwa mikononi mwa maisha bora kwa walevi wote ambapo nawe ulipewa uhai mpendwa? Je hapa utamkamata nani umuache nani? Je hapa akina Rugemalayer na Sethii ndiyo wa kulaumiwa tu au genge zima la wanene? Sijui kwanini walevi hawapendi kusoma historia kuwa wakati babu yako IptL anazaliwa wakunga walikuwa wengi tu tena wakipokezana vijiti baada ya kila mmoja kumaliza ngwe yake? Huu ndiyo ukweli hata kama unakera na kuuma. Hii ndiyo historia. Huwa haiandikwi upya wala kufanyiwa uhariri vinginevyo iwe imeandikwa kwa upendeleo kama ile ya kikoloni.
Mpendwa Escrow, hawa wanywanywa walipenda hata wachungaji wa kondoo wa Bwana waliojazwa minjuluku nao waumbuliwe? Sijui kama akina Father Kigumu aka Kilaini wengependa makaburi yafukuliwe ili nao waumbuke. Sijui kama akina profedheha Anae Kajuamlo wangefurahia ufukuaji wa makaburi. Sijui kama mzee wa Vijisenti angefurahishwa na ufukuaji huu ambao bila shaka ungemuacha uchi yeye na wenzake ingawa wako uchi siku zote.
Mpendwa Escrow, hakuna nilipofurahi na kufarijika kama kuona ulivonusurika hivi juzi pale Shirika la kutoa mimeme lilipotaka kulangua huduma hii. Kwa vile hii haikuwa halali, mkuu aliamua kuwatumbua wanene wa shirika huku akikuacha wewe utanue. Najua hapa wanywanywa watakuwa walichukia sana. Niliwasikia wakisema kuwa hawa jamaa walitolewa kafala. Nilishangaa sana kusikia ujinga huu. Kwani ni Mungu gani asiyetolewa kafala?
Kwa vile sijapata kanywaji na zile zana nyingine vinifanyavyo nichangamke, leo sitasema mengi zaidi ya kuzidi kukuombea maisha marefu mpendwa wangu Escrow. Wala usiwe na shaka. Wajinga ndio waliwao na mwenye nacho huongezewa. Nimalizie kwa kuomba unikumbuke kwa ofa kwa ajili ya kanywaji. Mimi sitaki mabilioni na mamilioni kama wale waroho tena wakubwa wakubwa wenye kufanya mambo ya kitoto na kifisi na kifisadi. Mungu ibariki Escrow. Mungu ibariki IptL.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.
Tuesday, 10 January 2017
Nchemba, wako wapi wauza unga!
Kuna mambo rais John Magufuli amefanikiwa kwa asilimia kubwa tangu aingie madarakani tena kwa muda mfupi na kasi ya ajabu. Magufuli anasifika kwa kutofumbia macho uzembe, matumizi mabaya na kwa kiasi fulani ufisadi. Hata hivyo, pia kuna mambo ambayo rais Magufuli anaonekana kushindwa kabisa kiasi cha kuonyesha ima kuishiwa pumzi au kuyakwepa akilenga kufunika kombe ili mwanaharamu apite.
Leo tutaongelea moja ya mambo yanayoonyesha kumshinda rais Magufuli pamoja na wasaidizi wake ambalo ni kadhia nzima ya biashara ya mihadarati. Si kupiga chuku wala uzushi kukiri kuwa kwa sasa kuna kila dalili kuwa serikali ya awamu ya tano imeshindwa wazi mapambano dhidi ya biashara hii hatari na haramu.
Maneno ya hivi karibuni ya msaidizi mkuu kuhusiana na mapambano dhidi ya mihadarati, Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi, Lameck Mwigulu Nchemba yanaonyesha na kuunga mkono dhana hii kuwa serikali imeshindwa mapambano dhidi ya biashara ya mihadarati. Nchemba alikaririwa na vyombo vya habari hivi karibuni akisema “inasikitisha na haivumiliki kuona nguvu kazi ya Taifa inapotea huku wauzaji wakinufaika kwa pesa haramu, ifahamike wazi vita ya Serikali dhidi ya wauzaji ni kubwa kuliko wanavyofikiria.” Ukiyafanyia uchambuzi maneno ya Nchemba, licha ya kuwa maneno ya kukata tamaa ni maneno ya mtu aliyeshindwa kabisa kiasi cha kuishia kulalamika kana kwamba hana uwezo wala nyenzo za kupambana na kadhia na jinai husika. Sasa kama Waziri mwenye kila aina ya zana za kupambana na uovu analalamika, hawa wa chini hasa wahanga nao wasemeje? Kwa vile Waziri ni msaidizi mkuu wa rais, maneno yake ni ya bosi wake pia. Je kweli tumeshindwa kwa sababu hatuna uwezo au ni kwa sababu ya kuendekeza ufisadi na woga wa kawaida tu? Niliwahi kuonya kuwa tusipoangalia, biashara ya mihadarati itageuka balaa kubwa kuliko hata ukimwi kutokana na wanaopaswa kupambana nayo ima kuogopa au kuwa wanufaika wa jinai yenyewe. Nilizidi kupata wasi wasi pale rais Magufuli aliposema kuwa hana mpango wa kufukua makaburi kwa vile anaweza kushindwa kuyafukia asijue kufanya hivyo ni kuonyesha udhaifu wa serikali yake dhidi ya majanga mengine kama mihadarati. Nilihoji; kama rais anashindwa makaburi, je angeweza mihadarati? Maneno ya Waziri wake sasa yamethibitisha hofu yangu.
Tukiachia mbali woga na ukosefu wa ithibati ya kupambana na mihadarati kama janga la kitaifa na kimataifa, tuangalia upande wa pili ambao ni urahisi wa kupambana na kadhia husika. Nasema wazi kukwa ni rahisi ya kukomesha dawa za kulevya kama serikali itafanya yafuatayo:
Mosi, ihakikishe wale wote wanaoshukiwa wanachunguzwa bila kujali hadhi zao kisiasa na kimaisha hata wawe ni marais.
Pili, ifahamike kuwa ni rahisi kuwajua wauza mihadarati au wanufaika na makuwadi wao. Kwanza, wana mali nyingi zisizoweza kutolewa maelezo sahihi ya upatikanaji wake. Pili, wengine wamejificha nyuma ya shuguli nyingi halali kama vile dini, biashara na hata siasa.
Tatu, ukiachia mbali dalili zitokanazo na wauzaji, makuwadi au washitili wao wa kisiasa, kuna namna nyingine rahisi ya kuwabaini wauza unga. Ukitaka kuwabaini basi kamata watumiaji ilil wakuonyeshe wapi wanapata unga na nani anawauzia. Changamoto ambayo akina Nchemba wanapaswa kushughulikia ni kwanini watumiaji wajulikane, wauzaji wasijulikane? Ukitaka kujua ni wapi kuna paka wengi, angalia palipo na panya. Haiwezekani tushindwe kuwabaini na kuwashughulikia wauza mihadarati wakati tunao vijana wengi watumiaji waliotamalaki mitaani kwetu. Tunamdanganya nani na kwanini wakati kila kitu kiko wazi na rahisi? Je hapa tatizo ni kuwabaini wauza unga au ukosefu wa ujasiri na utayari kuwakabili? Tukubaliane kuwa kinachogomba si kuwabaini wauza unga bali utayari wa kufanya hivyo. Wapo na wanawahonga viongozi. Rejea kashfa ya shisha. Yameishia wapi baada ya kuwekana sawa? Mnamdanganya nani? heri mhalalishe hiyo haramu ili kijulikane kuliko kula huku na kule.
Turejee kwa Nchemba, kulalamika hakutoshi. Kamateni wala na wabwia unga mtawapata wauzaji kirahisi ukiachia mbali kuwa kuna vigezo vingi vya kuwabaini ingawa wanajulikana. Pia ifahamike kuwa suala la mihadarati si suala la Wizara ya Mambo ya Ndani pekee. Linapaswa kuhusisha wizara karibia zote muhimu na za mbele zikiwa ni zile za Afya, Fedha, Katiba na Sheria, Vijana na Usalama. Wizara ya Afya inaweza kusaidia kubaini watumiaji ambao wanaweza kuielekeza Wizara ya Mambo ya Ndani kuwakamata. Wizara ya Fedha kupitia mabanki inaweza kutoa taarifa za watu wanaowekeza fedha nyingi bila maelezo au wenye kutia shaka. Wizara ya Vijana inaweza kuainisha ni vijana wangapi wameathirika, kiasi gani na walipo ili kubaini maeneo sugu. Na wizara ya Usalama inaweza kutumia taarifa zilizokusanywa kwenye asasi na wizara nyingine na kuzifanyia uchunguzi kubaini chanzo na ukubwa wa tatizo. Wizara ya Katiba na Sheria ina wajibu wa kuhakikisha majaji na mahakimu wanaopatikana na makosa ya kuhongwa na wafanyabiashara ya mihadarati wanafukuzwa kazi mara moja na kufikishwa mahakamani.
Kwa ufupi, kupambana mihadarati ni rahisi. Hakuna sababu ya Waziri kulalamika. Kama ameshindwa kazi aachie ngazi wenye uwezo wachape kazi.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano kesho.
Kijiwe na Mikakati ya Mwaka Mpya
Baaada ya kufanikiwa kumaliza mwaka 2016, Kijiwe kimejiandaa kuleta mapinduzi kwa kupambana na changamoto mbali mbali kama vile kupambana na ufisadi na ufisi; kuhimiza matumizi bora ya mali za umma;kuwapayukia viongozi wazembe; na kuondoa ubabe wa kisiasa.
Msomi Mkatatamaa anaingia, kama kawaida yake, ana jarida moja maarufu la kimataifa la Uongozi liitwalo Global Leader. Analiweka mezani baada ya kuamkua huku akijiweka vizuri kwenye benchi tayari kulianzisha. Anakohoa kidogo na kuangalia huku na kule na kusema “herini ya mwaka mpya wapendwani wote. Nashukuru kuwaona wote mkiwa timamu na tayari kuukabili mwaka mpya kwa nguvu na akili mpya ila si kwa ari, kasi na nguvu mpya vilivyoishia kuwa usaliti na uzandiki kwa kaya yetu tukufu.” Anakohoa tena na kuendelea “hebu jamani leteni mipango yenu ya mwaka mpya kama wana kijiwe ili lau tuidurusu na kuitafakari pamoja na kuamua nini tufanye kwenye mwaka huu tuliouanza.”
Kabla ya kuendelea, Kapende anamchomekea “kwangu mwaka huu ningependa uwe wa kuleta uwajibikaji wa kweli na sawa kwa walevi wote bila kulindana wala kuwekana sawa kama ilivyo sasa ambapo kashfa na makaburi maarufu yanaendelea kupeta huku wakubwa wakituweka sawa kuwa mambo ni sawa wakati si kweli.”
Kabla ya kuendelea, Mbwamwitu anachomkea “una aya za kuunga mkono madai yako au ni rongorongo na politiki?”
“Mijitu mingi kwa kushindwa kubadilika, unadai aya kwenye mambo ya siasa au ni usugu wako wa kwenye mihadhara ya vihiyo wasiojua kitu chochote wajifanyao kujua dini za wenzao wakati zao zinawashinda? Omba ushahidi upewe lakini si aya. Hakuna aya hapa na hatuzitaki.” Anajibu Mipawa akionyesha wazi kuwa na hasira na kutopendezwa na masuala ya dini kwenye siasa.
Msomi anarejea “sameheaneni ili msamehewe. Si vibaya kuonyesha hisia za mchovu hata kama hazikubaliki. Basi ili kuokoa mjadala, Kapende omba ushahidi na si aya.”
Kapende anakula mic huku akitabasamu “nilifanya makusudi ili kuzuia wachovu kuleta dini kwenye mjadala huu adhimu ndugu zanguni. Ninchotoka kuongelea hapa ni uwajibikaji wa pamoja tena kwa usawa kwa ajili ya mustakabali wa kaya yetu.”
Kabla ya kuendelea Mpemba ananchomekea “wamaanishani wakati twaaambwa wote tuwajibike wakati wakubwa wakiwajibika pia? Hebu tupeni maelezo lau tuelewe unichomaanisha shehe Kapende.”
“Ninapoongelea uwajibikaji namaanisha uwajibika wa kweli. Kwa mfano, hadi sasa hatujui madingi wetu wote watatu wana utajiri kiasi gani, wameupataje, wanautumiaje na wana mpango gani kutumegea nasi ili kutuonyesha mapenzi na uwajibikaji wao.” Kapende anajibu huku akitabasamu.
Kanji anakula mic “veve Pende iko chokozi sana dugu yangu. Sasa nataka tajiri ya bana kuba na bi kuba uende kuiba tajiri yao? Veve mbona hapa nataja tajiri yako dugu yangu?’
Mipawa anakula mic “utajiri wa mheshimiwa Kapende unafahamika. Hivyo hana haja ya kuutaja hasa ikizingatiwa kuwa yeye si kiongozi.”
Mgoshi Machungu anakatua mic “wagoshi mimi sihitaji hata kujua utajii wa rahis na makamu wake hasa ikizingatiwa kuwa ni watendaji wema wenye historia safi. Ningependa kujua utajii wa watanguizi wao ambao wameiingiza kaya yetu kwenye umaskini na kuwa shamba la chizi visivyo na kifani. Cha mno ningependa kujua utajii wa vitegemezi na vitegemezi vya Njaa kai ii kuwawajibisha bia kuindana kama iivyo.”
Msomi anarejea “hapa ndugu yangu Mgoshi unataka kufukua makaburi na ushindwe kuyafukia kama jamaa. Kama tungekuwa tunawajibishana vilivyo na kwa haki, Njaa Kaya na ukoo wake wangekuwa Segerea wakinonihino kwenye debe wakingojea Pilato awafunge maisha au kuwanyonga na kunawa maji kuwa dhambi zao hadaiwi. Hata hivyo, nani amvishe paka kengele wakati tuliowategemea wameonekana kugwaya na kujifanya hawaoni wala hayawahusu wakati wanaona na yanawahusu?”
Sofia Lion aka Kanungaembe anakula mic “mie msinikumbushe yule mama mwalimu mwenzangu tena kihiyo kutengeneza njuluku hadi akamiliki shule yake binafsi. Hamkusikia walivyozuia mizigo yake bandarini na kuanza kubadili lugha kuwa hakuwa na mizigo wakati tunajua kuwa biashara yake maiaka yote imekuwa ni kuhujumu kaya na kutumia ofisi ya dingi kujineemesha kama mama Anayo Tamaa Makapi? Mimi nmependa ya Dokta Kanywaji kumzuia bi mkubwa wake kujiingiza kwenye uchuuzi wa kipuuzi kwa mgongo wa kukuu hata kama ana madhaifu yake kama kuwalinda majambazi na vibaka hawa wakubwa.”
Mheshimiwa Bwege anaamua kutia guu “mie naona tudhamirie mwaka huu kufukua makaburi lau hawa wezi tunaowajua tuwawajibishe ili kutoa somo la uwajibikaji kwa wachovu wote badala ya kuhubiri maji na kunywa mvinyo kama ilivyo. Tunataka uwajibikaji hasa kurejesha nyumba za wachovu zilizoibiwa na kutwaliwa na Dugong Denjaman Makapi ambaye naona siku hizi hasikiki baada ya kuadhirika kiasi cha kutegemea hisani ya dingi ambaye ni dogo kwake. Ama kweli hujafa hujaumbika! Nani alitegemea mjivuni kama Denjaman kuufyata hivi tena kirahisi. Angejua kila lenye mwanzo lina mwisho wala asingepoteza muda kujidai asijue ni dalili za uvivu wa kifikiri.”
Kijiwe kikiwa kinanoga si akapita Njaa Kaya akitoka kuzurura! Sauti zilisikaka, msulubishe huyo Vasco da Gama!
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano kesho.
Sunday, 8 January 2017
Kikwete hakustahili kuwa Mkuu wa UDSM
Baada ya rais John Magufuli kumteua rais mstaafu Luteni Kanali mstaafu, Jakaya Kikwete kuwa mkuu wa chuo kikuu cha Dar Es Salaam (UDSM) wanaojua namna Kikwete alivyokacha nafasi hiyo walishangaa sana. Inakuwaje mtu aliyekacha nafasi husika akiwa na madaraka afae kwenye nafasi aliyoikacha mwenyewe? Je nini maana ya kustaafu? Je hakuna watu wengine, tena wenye sifa, ambao wangeweza kuteuliwa? Mie naona kuteuliwa kwa Kikwete ni tatizo. Kwanza, kama nilivyosema hapo juu, hana sifa za kuwa mkuu wa chuo kikuu nje ya urais. Uzoefu wake wa kuacha nafasi hiyo unaweza kusema mengi. Pia anapopewa kazi kama hiyo, ina maana anapokea mishahara miwili yaani marupurupu na stahiki za rais mstaafu na mkuu wa chuo. Ukitaka kuona tunachomaanisha kuhusu kutofaa kwa Kikwete kuwa mkuu wa chuo, juzi alifanya kama alivyofanyiwa kwa kumpa mkataba wa mwaka mmoja rafiki yake Profesa Lwekaza Mkandala alipotimiza umri wa kustaafu. Je hapakuwapo na maprofesa wengine wenye siha ya kuweza kushikilia wadhifa huo au ni yale yale ya kutumia ofisi na nafasi za umma kufadhiliana? Kwani lazima Kikwete au Mkandala? Hii si haki. Inakuwa kituko kwenye taasisi ya kisomi kama UDSM kuendeshwa kisiasa kiasi cha watu binafsi kuigeuza kama taasisi isiyo ya kisomi. Nadhani, kwa aina ya taasisi, haikupaswa ku-recycle watu au kuwa na watu ambao ni recycled. Taasisi inayozalishwa wasomi kila siku haiwezi kukosa mtu wa kufaa kuwa mkuu wake hadi aliyestaafu awe-recycled. Kwa maana hiyo, rais afikirie kufuta huu mkataba wa nyongeza aliopewa Mkandala na rafiki yake Kikwete. Pia kwanini Magufuli asiige mfano wa Mwl Julius Nyerere wa kuwa mkuu wa chuo kikuu hiki muhimu na cha kwanza yeye mwenyewe badala ya kuendeleza utamaduni ulioanzishwa na watu waliokuwa wakiogopa kwenda kule kukalishwa kitimoto kushiriki midaharo? Magufuli ni msomi.
Tokana na mfumo wa chama kimoja, tulizoea, na kusimikwa ufisadi na ubinafsi baadaye, kupeana kazi kwa kujuana na kulindana. Hivi karibuni rais John Magufuli alisikika akisema hakuna mtu atakeruhusiwa kuwa na vyeo viwili kwa wakati mmoja. Hii maana yake ni kwamba mtu anaposhikilia nafasi mbili, licha ya kupokea mishahara zaidi ya mmoja, anawanyima wengine fursa ya kuajiriwa. Hili moja, je hali inakuwaje anapoteuliwa mtu aliyekwisha kufanya kazi na kustaafu huku wakiachwa wale ambao hawajawahi hata kupata fursa hii?
Tangu aingie madarakani, rais Magufuli amefanya mambo mengi mapya na makubwa. Hata hivyo, inaonekana anaanza kukwamishwa na mazoea kiasi cha kuanza kujipinga kuhusiana na haki za ajira kwa watanzania. Kwani akiwa rais ameishawateua watu waliostaafu tena wasiofaa kuwa wenyeviti au wajumbe wa bodi. Chukulia Anna Abdallah kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa bodi ya Makumbusho. Huyu alishashika kila wadhifa kuanzia ubunge hadi uwaziri. Kama ni kuchuma ameishachuma vya kutosha. Mwingine ni spika wa bunge mstaafu, Anna Makinda ambaye aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa bodi ya NHIF. Huyu kama si tamaa, ameishachuma vya kutosha. Kama Abdallah alishakuwa mbunge, waziri hadi spika. Hata umri wake si wa kuutumikia umma bali kulea wajukuu. Mwingine ni Augustine Mrema aliyeteuliwa kuwa mwenyekiti wa Parole wakati ima wahusika walishastaafu au wana nafasi nyingine kama Mrema kama siyo kuendeleza ukale na ubinafsi wa chama kimoja ni nini? Je uenyekiti na ujumbe wa bodi upo kuhifadhiana kwa wanasiasa au kwa minajili ya utendaji bora kwenye mashirika.
Ukiachia mbali bodi za mashirika, uchochoro mwingine ambao umekuwa ukitumiwa na serikali kufadhiliana ni ofisi za balozi zetu nje. Unashangaa kuona mtu anastaafu mfano jeshini hapohapo hata kabla ya kufika nyumbani anateuliwa balozi. Unajiuliza; kwani hizi nafasi ni za rais binafsi kiasi cha kuacha vijana wengi waliojaa wizarani na mitaani wenye ujuzi wa kuweza kuwakilisha nchi? Tunao mabalozi wangapi wazee waliokwishastaafu jeshini au kwingineko lakini wakateuliwa kwenye nafasi kama hiyo inayohitaji watu wenye kuchemka na wenye nguvu? Mfano mwanajeshi na ubalozi wapi na wapi kama tutatukuwa wakweli? Wengine wanastaafu na kuteuliwa wakuu wa mikoa au wilaya. Je hii si kuwanyima kazi watanzania wengine wenye haki na uwezo wa kushika nyadhifa hizi? Kwanini tusibadili sheria na kuweka vipengele vilivyo wazi kuwa watu ambao wameishafanya kazi na kustaafu wasiruhusiwe kuteuliwa kwenye nafasi zozote? Tokana na serikali ya hovyo na goigoi iliyopita, tumejaza watu wa hovyo kwenye ofisi zetu za ubalozi nje. Walioteuliwa kutokana na kujuana. Hawa nao wanapaswa kutumbuliwa tu ili kuepusha hasara kwa taifa. Kwani, walipewa mamlaka wasiyo na sifa wala uwezo nayo.
Tumalizie kwa kuwataka rais na wananchi kuhakikisha unapangwa utaratibu wa kuepuka ajira na uteuzi ambao si chochote bali recycled, sina neno la Kiswahili.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.
What a shame from Ghanaian new President!
What sort of academic incidence and laziness for the head of state and his government to blindly and shamelessly plagiarise somebody's speech! I didn't know that we still have leaders who are such crazy and lazy so to speak. The new president of Ghana did exactly this. Listen to his speech. It speaks volume visa-a-vis such blatant plagiarism committed by the head of state. The year 2016 saw two new president committing this offence. The wife of the US's president-elect, Donald Trump, Melanie did exactly the same by plagiarising Michelle Obama's speech. Shame on you all!
Saturday, 7 January 2017
Barua ya Faru Toto kwa faru John (Baba)
Baba Faru John,
Naandika waraka huu ili ukufikie huko kuzimu japo ambao bado wanaamini kuwa uko hai. Wanasema eti ulibadilishwa jina na kuitwa Ole Sokoine. Vyovyote iwavyo, nitakuhabarisha. Hii ni kutokana na kutaka kukujulisha kinachoendelea baada ya kifo chako chenye kuzua kila aina ya utata kwa wanyama na wanadamu. Pamoja na kwamba hauko nasi kimwili, wanao tunaamini uko nasi kiroho. Pia, nichukua fursa hii kukufahamisha kuwa kwa sasa wakubwa wa taifa letu wameamua kulinda legacy yako kwa kuwawajibisha wote walioshiriki mauaji yako ya kibinadamu kwa namna moja au nyingine. Ninapoandika, wazito wapo wanahangaishana huku watu wazima wakitoa maelezo ya kitoto kiasi cha kumfanya bosi agomee utetezi wao.
Vyombo vyote makini vya habari, si vya uchafu aka udaku, vimesheheni habari zako. Picha yako sasa inajulikana sawa na ya wajina wako John mwenye jina jingine lenye maana ya maji yanayochanganya wanayokunywa binadamu. Kwa vile John si jina la kutania, tunapanga kubadili majina yetu watoto wako wote tuitwe Toto John na Toto Joanna, Janet au Mary kama shukrani ya wakubwa hawa wanaotupigania.
Baba, baada ya kifo chako nasi tumekuwa maarufu ghafla bin vu. Kama mambo hayatabadilika, baba umejitoa kafala kwa ajili yetu. Maana, hakuna mkubwa anayelala bila kwenda kwa bosi kutoa maelezo ya kufa kwako hata kama hayaingii akilini. Ilmradi kila mkubwa na vimbwanga na vibwengo vyake.
Waziri mkubwa, kwa alivyokupenda na kukuthamini, ameitisha uchunguzi ambapo vinasaba vyako (DNA) vitachukuliwa toka kwetu watoto wako, pembe zako (kama kweli zile alizopelekewa kwake ni zako), kaburi lako (kama kweli lipo na ni lako) na popote vinapoweza kupatikana ili kuhakikisha kweli ni wewe uliyekufa bila kuugua tena ghafla.
Baba, tumefarijika kusikia bosi akiuliza maswali ambayo nasi tuliuliza ila kwa vile tu wanyama, hakuna aliyetuelewa. Kati ya mengi, bosi aliuliza maswali, tena yanaoingia akili, mia kidogo. Baadhi yake ni:
Mosi, ilikuwaje ulikufa bila kuugua? Sisi wanao tunajua ulivyokuwa mzima wa afya huku ukifyatua wadogo zetu wengine ili kuondoa hali ya sisi kuwa viumbe walioko kwenye hatari ya kutoweka.
Pili, je daktari wetu alikuwa wapi; ni nani na ana taarifa gani kuhusiana na mauti yako? Tunamshauri mkubwa na mkubwa wake wajina wako wahakikishe daktari huyu anatoa maelezo yanayoingia akilini.
Tatu, je baba zima na jabari kama wewe ulitokaje Ngorongoro crater hadi huko Grumetti, sijui guruneti, ulikofia ghafla au ulikanyaga guruneti likakulipua? Je hicho kitufe walichokuwa wamekufunga kikiwasiliana na setalite kilikuwa kinafanya kazi gani na kina taarifa zipi? Nne, je kuna mchezo mchafu hasa baada ya pembe zetu kupata soko kuliko hata dhahabu huko kwenye bara la washirikina wanaopenda kututumia kwa upuuzi wao? Tano, je ukweli ni upi na nani anao na kama hajautoa anadhani atafanikiwa kuua au utamuua yeye?
Baba Faru John, watoto wako tunakukumbuka kila siku kiasi cha kushindwa hata kula majani na kuchezacheza kama tulivyozoea. Tunahofia kuwa nasi tukikua tunaweza kupotea kama ulivyopotezwa, kuswagwa au kupakiwa kwenye malori na kwenda kuuawa kwingine ili ushahidi upotee. Kama si bosi kusukuti, ulikuwa ndiyo hivyo, umemalizwa wakati sisi tukingoja kwenye mstari.
Baba yetu faru John, kwa heshima yako na upendo wetu kwako, sisi watoto wako tunapanga kuandamana hadi ikulu kuomba kuonana na rais ili tuulize maswali yetu kuhusiana na kifo chako na mustakabali wetu kama wanyama wa nchi hii. Umefika wanyama kutendewa haki. Pia tukifika kule, tutamuomba rais awape kipaumbele wenye ulemavu wa ngozi ambao, sawa nasi, viungo vyao vinatumika kishirikina kiasi cha kuhatarisha mustakabali wetu kama viumbe wa muumba.
Baba, sijui kwanini wanadamu wanakuwa hamnazo kiasi hiki. Wanatuua wasijue wanaua kesho yao na vizazi vijavyo. Au wao hawajali juu ya vizazi vyao kama sisi wanyama ambao kwa sasa tunaonekana kuwa na akili kuliko baadhi yao. Tutashindwaje wakati sisi hutuuani sisi kwa sisi wala kuwaua wao ili kuuza viungo vyao kama wanavyotufanyia?
Wako faru Toto.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.
Thursday, 5 January 2017
Magufuli nawe timua wamachinga wa kisiasa
Katibu Mkuu wa Tucta, Nicolaus Mgaya, alipokuwa akisoma risala katika mkutano mkuu wa sita wa shirikisho hilo mbele ya Waziri Mkuu Majaliwa alikaririwa na vyombo vya habari akisema“Sisi kama viongozi wa vyama vya wafanyakazi, hatukubali jinsi viongozi hao pamoja na wanasiasa wengine, wanavyowafukuza kazi watumishi kwa kutaka mambo yao yaende vizuri.” Je kama wafanyakazi wenye kujua mambo wananyanyaswa, hao wananchi kawaida wa vijijini wanavumilia maonevu kiasi gani? huu ni mfano tu. Rejea juzi baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya walivyokuwa wakiwatimua wamachinga tena bila kuwaandalia mazingira ya kufanyia biashara stahiki kabla ya rais kuwapiga stop.
Unyanyasaji uonatendwa na baadhi ya wateule wa rais ni tatizo kitaifa. Hata hivyo, nani wa kulaumiwa. Nadhani kama tutarejea historia ya utawala wa kikale wa chama kimoja, tunaweza kujua ni kwanini Tanzania imekuwa na wakuu wa mikoa na wilaya tena wasiochaguliwa na wale wanaopelekewa kuwaongoza. Wanateuliwa na mtu mmoja yaani rais. Hii nadhani ilifanyika wakati wa utawala wa chama kimoja tokana na ile hali ya chama kuwa na nguvu kuliko serikali. Hivyo, chama kilitafuta namna ya kuibana na kuisimamia serikali kwa njia ya kuhakikisha mwenyekiti wake anakuwa rais. Hivyo, aliamua kutumia nafasi hii kuwateua wanachama wenzake kwenye nafasi za kiserikali ili kuweza kumsaidia kutumia kofia cha chama kufanya kazi za kiserikali na kukifaidi chama.
Sasa ni miaka mingi tangu tuachane na utawala wa chama kimoja. Hata hivyo, pamoja na kuanzisha mfumo wa vyama vingi kinadharia, kivitendo, Tanzania bado ina mabaki na makovu mengi ya utawala wa chama kimoja. Hapa ndipo mgongano unaoanza kujitokeza baina ya wakuu wa mikoa na wilaya na wanachi unapoibua chimbuko lake.
Kwa vile mambo yanaendelea kubadilika, ili kuwa na viongozi wenye kuweza kuleta ufanisi bila migongano na wananchi, tunapaswa kubadili mfumo wetu. Kwanini kwa mfano rais wa nchi ambaye ndiye mwenye mamlaka makubwa achaguliwe na wananchi lakini si wakuu wa mikoa au wilaya? Tokana na kwamba Tanzania si nchi ya majimbo, wengi watasema kuwa kuruhusu kuchaguliwa kwa wakuu hawa kutakuwa kinyume na mfumo wetu. Kwanini tusiwe ha hybrid system yaani mfumo kizalia au mchanganyiko ambapo tutakuwa na viongozi wote waliochaguliwa na wale wanaowaongoza ili kuleta uwajibikaji wa kweli badala ya wahusika tulio nao sasa kuwajibika kwa mtu mmoja aliyewateua kiasi cha kuwadharau na kuwanyanyasa wananchi? Kama rais ni mwenyekiti wa chama tawala na anaongoza nchi, kwanini wenyeviti wa mkoa wasichukue nafasi za wakuu wa mikoa na wilaya ambao wanaonekana kama wakoloni kwenye maeneo yao? Hii itasaidia kuondoa unafiki wa sasa ambapo makada wa chama tawala wanapewa nafasi za kiserikali na kujifanya hawapendelei wakati wanapendelea wazi wazi? Pia kuruhusu wakuu wa mikoa na wilaya utasaidia kufanya mambo yafuatayo:
Utaondoa ukale wa rais kuwateua marafiki au watu wake wa karibu kama sehemu ya kupeana ulaji hata kama wahusika wanaweza wasifae kwenye nafasi husika.
Pili, kutaondoa kiburi na dharau kwa watawaliwa tokana na ukweli kuwa wahusika watakuwa wamepitia kwenye mikikimiki ya kufikia walipo. Nakumbuka juzi rais John Magufuli alipositisha zoezi la kufukuza wamanchinga mijini alisema kuwa wakuu wa mikoa na wilaya wanafanya hivyo kutokana na kutojua ugumu wa kusaka kura. Kwa vile ni wateule wa rais, wengi wanajiona miungu watu wasiokosea na wasioguswa. Rejea hivi karibuni mkuu wa mkoa wa Dar Es Salaam kumuita afisa wa wilaya kichaa wakati si kichaa ukiachia mbali kuwahi kumweka ndani mbunge wa Ubungo Saidi Kubenea na baadhi ya watendaji wa Halmashauri ya Kinondoni alipokuwa mkuu wa wilaya.
Tatu, kutaondoa dhana kuwa wakuu husika ni wakoloni waliopelekwa na rais kwenye mikoa na wilaya kutawala na si kuongoza. Na hili lina ukweli usiopingika kuwa wengi wa wakuu wa mikoa na wilaya hawajui shida, tamaduni na mahitaji ya mikoa wanakopachikwa na kuishia kufanya kazi kumridhisha aliyewateua au kuwadharau hata kuwadhalilisha wananchi.
Naweza kutumia mfano wa Magufuli wa kuwakaripia baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya waliokuwa wakiwabughudhi na kuwafukuza wamachinga nao kuwa wamachinga wa kisiasa. Hivyo, naweza kumshauri Magufuli kuanza kuwafukuza wamachinga hawa wa kisiasa ambao wameanza kuonyesha udhaifu wa mfumo wetu.
Tumalizie kwa kumhimiza rais na serikali yake waangalie namna ya kubadili sheria ili kuondoa manyanyaso na migongano isiyo na ulazima. Kwani inachelewesha taifa letu licha ya kuwaumiza watu wetu. Wakati wa kufadhiliana kisiasa umepitwa na wakati hasa wakati huu wa “Hapa Kazi Tu”.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.
Subscribe to:
Posts (Atom)
