The Chant of Savant

Saturday 3 September 2011

Aliyeiroga Tanzania sasa marehemu





Mkuu wa mkoa wa Rukwa Daniel Ole Njoolay akikabidhi ambulansi ya "kisasa" aina ya bajaj kwa mkuu wa wilaya ya Mpanda, Dk Rajab Rutengwe (kushoto). Ambulansi za miguu mitatu zimesambazwa na serikali kusaidia kutoa huduma za afya vijijini ambapo mkoa wa Rukwa utapokea miguu hii mitatu 20. Picha na Hamza Temba

Bila aibu wala wasi wasi serikali yenye kusifika kwa kununua mashangingi kwa ajili ya viongozi na watumishi wake hata wa chini eti imesambaza utitiri wa ambulansi za miguu mitatu nchi nzima katika karne ya 21. Jamani, kwanini wao wanapata pesa ya kununua mashangingi hata kutoa misamaha ya kodi na kuwatesa watanzania hivi? Pamoja na matusi yote haya ya nguoni bado watanzania wanaendelea kuichagua Chama Cha Mafisadi! Je hapa mgonjwa tena wa akili zaidi ya wananchi ni nani? Je watawala nao wanaowavua nguo wananchi hivi bado nao ni wazima? Je aliyewaroga watanzania ni nani? Hakika kama yupo mi marehemu na hakuna wa kuwazindua toka kwenye 'ufu" huu.

Hivi mabilioni ya EPA, Meremeta, Buzwagi, SUKITA, ATCL, THA,NBC na mengine mengi yaliyoibiwa na watawala wakishirikiana na majambazi wa kihindi yangeweza kununua magari mangapi ya kusafirishia wagonjwa?

Ukiangalia na ukweli kuwa watawala watu huangalia cha mbele kabla ya kinachokusudiwa, kuna uwezekano hii ni biashara ya kigogo mmoja akishirikiana na makuwadi wa kihindi. Kuna haja ya kuchunguza sana wizi na udhalilishaji huu wa mchana. Maana waliofanya hivi hawana uchungu wala heshima kwa nchi na watu wake na si waaminifu hata kidogo. Karne ya 21 ambapo wenzetu wanatumia Air ambulance, sisi tunaletewa kituko kiitwacho bajaj! Nahisi kupasuka.

Bado hapa Jakaya Kikwete anajisifia kuwa ameleta maendeleo ya kurudi nyuma kwa watanzania nao bado wanaendelea kumvumilia. Hivi uchafu huu wangefanyiwa walibya hata wamisri wangemfanya nini rais wao? Maana ukiangalia viwango vya maisha katika nchi za Maghreb ambazo zimejikomboa hivi karibuni na kulinganisha na marehemu Tanzania ni kifo na usingizi.

Hizi bajaj zinachekesha licha ya kusikitisha. Hivi huyo anayemhudumia mgonjwa atakaa wapi? Maana ambulansi si kusafirisha mgonjwa haraka tu bali hata kumhudumia. Je hilo vumbi na jua havitammaliza huyo mgonjwa kabla ya kufikishwa huko Hospitali kuandikiwa dawa na kuambiwa akanunue? Hapa bado hatujaangalia barabara zilizojaa misongamano na madereva feki ambao bila shaka watakigonga hiki kibajaj na kumuua dereva na mgonjwa wake. Tuache utani. Hivi aliyebuni upuuzi huu ana akili nzima kweli?

Kuna haja ya kutafakari na kubadilika haraka kabla hawa watu hawajatuzika hai. Je hawa wanaoogopa kuingia mitaani kudai haki zao hawafi kwenye huduma mbovu za jamii ukiachia mbali kufa kwa ugonjwa moyo wakifikiri jinsi ya kubangaizi na kufisidi ndiyo waishi?

4 comments:

Unknown said...

Thanks for honestly relating your experiences and opinions and good luck to you.
Chevy W-Series Turbo

Anonymous said...

A truly amazing phenomenon like Halley's comet.

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Oh Boy !!!

Rik Kilasi said...

Hii kali ya mwaka!