The Chant of Savant

Tuesday 13 September 2011

Rutabanzibwa anangoja nini ofisini?


Baada ya katibu mkuu wa wizara ya ardhi Patrick Rutabanzibwa kupatikana na hatia ya kuidharau mahakama na kuhukumiwa, wengi wanaamini wakati wake wa kuachia ngazi umefika. Maana, hata kama ni vigumu kujisuta kutokana na ulaji uliomzunguka na usugu wa kupenda kula uliowajaa watendaji wetu, sifa na jina lake vimeishachafuka vilivyo. Hivyo, Rutabanzibwa hana haja ya kungoja apigiwe makelele na kutungiwa mashairi na nyimbo au kuandaliwa maandamano ndipo ajiwajibishe. Pia angefanya haraka kuachia madaraka ili kumpunguzia mzigo rais aliyemteua kutokana na kuwa mengi ya kufanya. Swali linaloulizwa ni je atawezaje kukaa kwenye ofisi ya umma wakati aheshimu sheria za nchi anazopaswa kuzilinda na kusimamia? Je rais anayehimiza uwajibikaji kila siku atamfumbia jicho?

Jina la Rutabanzibwa lilianza kusifika kwa wanahabari kutokana na kuhusishwa na kashfa mbali mbali kuanzia IPTL hadi ya hivi karibuni ya uuzaji viwanja. Hata hivyo, pamoja na Rutabanzibwa kutajwa kwenye kashfa nyingi, aliendelea kubakizwa madarakani. Hakuhangaika kukanusha wala kujitetea. Hata anapojaribu kujitetea kama alivyofanya kwenye kashfa ya sasa, anafanya hivyo kujionyesha kama mjanja anayeongea na watu wasio na akili wala uelewa wa lolote isipokuwa atakalo yeye. Hii laweza kutafsiriwa kama kiburi cha hali ya juu. Na pili hii inaweza kuchukuliwa kuwa shutuma zilizotolewa dhidi ya Rutabanzibwa ni za kweli ndiyo maana hakuhangaika kuzikanusha wala kujitetea. Hili, kimsingi, limekuwa likiwaudhi na kuwasumbua watanzania wengi hasa wapenda haki ambao wanashangaa ni kwanini mhusika hachukuliwi hatua hata kuwajibishwa.

Nani mara hii kasahau au kusamehe kashfa aliyotuhumiwa kwayo Rutabanzibwa ya kusaini mkataba wa hatari kwa taifa wa IPTL ambao umegeuka donda ndugu kwa taifa? Nadhani bado watanzania wanakumbuka yaliyofanyika mjini London wakati wa kashfa hii.

Kwa kosa alilopatikana nalo hatia Rutabanzibwa, anapaswa kuwa mfano kwa watendaji wengine wanaodhani mahakama za Tanzania zipo kuwaadhibu watu wadogo na kuwakingia kifua na kuwaogopa wanaojiona wakubwa. Rutabanzibwa ameonyesha mfano mchafu hakuna mfano. Naamini hata rais aliyemteua hataweza kumvumilia tena kutokana na aina ya kosa alilotenda hasa akiwa mtumishi wa umma wa ngazi ya juu. Kudharau mahakama si kosa dogo. Hata hivyo, mahakama imekuwa na huruma sana kwa kumpa adhabu yenye uchaguzi kati ya kifungo au kulipa faini. Vinginevyo alipaswa apewa adhabu zote ili liwe somo kwa wengine wanaodhani mahakama ni chombo cha kudharau na kuchezea.

Kadhalika kutokuwajibishwa au kuwajibishwa kwa Rutabanzibwa kutatoa fursa kwa watanzania kutathmini upya msimamo na maagizo ya rais ambaye amekuwa akijitahidi kuwaaaminisha kuwa yuko kulinda maslahi kanuni na sheria za nchi kwa mujibu wa kiapo chake cha utumishi. Hii ni fursa adimu ambayo inaweza kutumiwa na rais kurejesha heshima yake kuhusiana na ambavyo amekuwa akiwashughulikia watuhumiwa wa kashfa mbali mbali.

Ukiachia kupatikana na hatia ya kudharau mahakama, Rutabanzibwa ni mmoja wa maafisa wa juu wa serikali wanaotuhumiwa na kashfa nyingi kuanzia kipindi cha awamu ya tatu. Ingawa wengi wanaona kama Rutabanzibwa analindwa, kipindi hiki hakuna sababu yoyote ya msingi inayoweza kutolewa ni kwanini asiachie ngazi. Kwa msingi huo, rais ambaye kikatiba ndiye aliyemteua, anapaswa kuzingatia kuwa kuendelea kuwa na mtu asiyetii sheria wala kuheshimu mahakama kutamshushia hadhi na kufanya umma uwe na shaka naye. Hivyo, jambo la maana na la haraka kwa rais kufanya ni kumwajibisha ingawa hatuna utamaduni huu kutokana na mifano mingi ya ambao wameishatuhumiwa bila kuwajibishwa.

Rutabanzibwa anapaswa kuwa mfano. Na si mfano tu. Anapaswa kuwajibishwa haraka ili kuonyesha jinsi rais anavyochukia kuwa na watu wasioheshimu sheria na mahakama. Maana hatuwezi kuwahimiza wananchi wetu wafuate na kuheshimu sheria wakati sisi tunaowahimiza ni mabingwa wa kuzivunja na kudharau taasisi halali za umma.

Kuna haja ya watu kama Rutabanzibwa kuadhibiwa vikali kutokana na kuanza kujengeka mazoea kwa baadhi ya walevi wa madaraka kudharua taasisi za umma. Hivi karibuni, katibu mkuu kiongozi Philemon Ruhanjo, alionyesha dharau ya wazi kwa bunge na rais wa nchi kwa kumrejesha kazini mtuhumiwa wa ufisadi, katibu mkuu wa wizara ya Nishati na Madini David Jairo katika mazingira yanayoonyesha wazi kupindwa sheria.

Kwa kumshikisha adabu Rutabanzibwa, litakuwa onyo kwa wengi wanaodhani kuwa wao hawaguswi.
Chanzo: Dira Septemba 2011.

No comments: