The Chant of Savant

Tuesday 20 September 2011

Wafe wangapi tustuke?

Ingawa ajali ya kuzama kwa meli ya Spice Islander huko Nungwi inaweza kuitwa mpango wa Mungu, ukweli si mpango wa Mungu bali uzembe, kutojali, ujinga, woga, roho mbaya na uroho wa binadamu.

Mimi siamini kuwa Mungu alitaka mamia ya watu wateketee. Hivyo basi, badala ya kumlaumu au kumtwisha Mungu mzigo, namlaumu mwanadamu hasa serikali kwa uzembe usio kifani. Mwaka 1996 Tanzania ilikumbwa na msiba mkubwa wa kuzama kwa MV Bukoba. Wengi walidhani hili lingetustua na kutukumbusha kuwa kuna haja ya kufuata taratibu, kanuni na sheria hasa kuzingatia haki ya kuishi ya mwanadamu. Ni ajabu na bahati mbaya kuwa hatukujifunza.

Katika mkasa huu huwezi kulaumu serikali peke yake. Hata raia wa kawaida wanaokubali au kulazimika kujazwa kama dagaa kwenye vyombo vya usafiri nao wana sehemu yao ya lawama. Kwa mujibu wa masimulizi ya manusura ni kwamba hali ya meli na jinsi ilivyokuwa imepakiwa mizigo na watu kupita ujazo vilikuwa wazi kwa kila mtu. Ni bahati mbaya sana kuwa watu wetu wamekubali kutendewa kama wafadhiliwa hata wanapolanguliwa na kukamuliwa na wenye kutoa huduma!

Nchi yetu ina mfumo mbovu wa kubanana karibu katika kila Nyanja za kimaisha. Ukiangalia kwenye nyumba za kupanga, magari ya abiria, bajaj, viwanja, madarasani, hospitalini na hata maofisini, tunasongamana na kuridhika na hali hii. Inatisha na kukatisha tamaa sana. Ukienda mahospitali kwa mfano, unakuta wagonjwa wanalazwa zaidi ya mmoja kwenye kitanda. Magerezani ndiyo usiseme. Ni kwenye nyumba za ibada tu ambamo hatubanani kutokana na kuibuka kwa madhehebu mengi na kupungua kwa waumini. Zaidi ya hapo kila sehemu ni kubanana. Ni ikulu tu ambapo hakuna kubana pakiwakilisha maofisi ya wakubwa yenye kila neema kuanzia viyoyozi, samani aghali na makandokando mengi.

Barabara zimejaa mikangafu na madereva feki huku wanaovunja sheria wakitozwa rushwa. Hali inaachwa iendelee bila kujali madhara yake hasa kukithiri kwa ajali za barabarani. Nani anajali iwapo wakubwa wanasafishiwa barabara wanapotaka kupita? Nani anajali iwapo wakubwa wanatumia ndege na si usafiri wa kawaida? Nani anajali msongamano na mbanano kwenye madaladala iwapo wakubwa wanasafiri kwa magari ya bei mbaya tena kwa kujinafasi? Hii ndiyo roho mbaya na uroho ninavyomaanisha kwenye makala hii.

Ukondoo au woga wa umma kutenzwa kama wasio na haki kwenye nchi yao ni sababu nyingine ya kuwepo kwa maafa kama ya kuzama meli huko Nungwi. Hakuna ubishi. Wasafiri wa meli husika waliona fika kuwa meli ilijazwa sana lakini waliogopa kujitetea kwa kuanzisha hata vurugu kuzuia kupakiwa kama wanyama au watumwa. Hawa kimsingi hawajui haki zao na kama wanazijua wanaogopa kuzidai. Huu ndiyo ukondoo na ujinga. Kondoo hunyenyekea hata kwenye machinjio. Binadamu hapaswi kutenzwa kama kondoo.

Tatizo jingine ni kukithiri kwa rushwa kama alivyokiri rais hivi karibuni kuwa kila sehemu kumetamalaki rushwa. Wenye vyombo vya usafiri na utoaji wa huduma nyingine wanapata pesa kiasi cha kuhonga wamtakaye na kwa kiasi cha fedha watakacho. Kama siyo ilikuwaje mamlaka husika hazikuwa na maafisa wa kuthibiti usalama kwenye bandari? Kimsingi, ni kwamba walikuwa. Lakini hawakuona hatari iliyokuwa inawakabiri wasafari wa meli ya Spice Islander kwa vile rushwa ilikuwa imewapofusha kiasi cha kuwauza wenzao. Sijui kama roho zao haziwasuti kwa dhambi waliyobeba kwa usaliti na uroho. Mara nyingi wanaomilki vyombo kama hivi wana uwezo wa kuvunja sheria bila kukamatwa kutokana na kula na baadhi ya watendaji wa serikali. Hawa wameifanya serikali kuwa mali yao na si mali ya wananchi.

Unafiki ni tatizo jingine hapa. Mwandishi anakumbuka maneno ya Katibu mkuu wa Chama Cha Wafanyakazi wa Kenya (Central Organization of Trade Unions (COTU) Francis Atwoli, aliyekaririwa akiwakemea wanasiasa waliokuwa wakimiminika kutoa salamu za rambi rambi kwa wakenya waliounga kwenye ajali ya moto uliotokana na kulipuka kwa bomba la mafuta kwenye kitongoji cha Sinai jijini Nairobi.

Ajali zinapotokea utawaona wanasiasa wakija na viapo na dua na maneno ya faraja wakijua fika kuwa wao wamechangia kwa kiasi kikubwa ingawa na wananchi kwa tabia yao ya ukondoo hawaikwepi dhambi hii. Atwoli aliwatuhumu watawala kwa uroho na kutokuza uchumi, kuondoa umaskini na kuwa na mipango mizuri kama vyanzo vya maafa kwa jamii inayoendeshwa na njaa na umaskini. Kwanini wanasiasa ambao wamekabidhiwa jukumu la kusimamia sheria hawatimizi wajibu wao? Hili ndilo lilikuwa swali kubwa la Atwoli. Je ni kwa sababu mara nyingi wao kutokana na nyadhifa zao hawakumbani na adha hizi hivyo haziwahusu?

Tatizo jingine ni ubinafsi wa kupindukia. Watu hasa wenye madaraka wanapoteza muda mwingi kwenye kuchuma kiasi cha kuwapuuzia wenzao na haki zao. Kama hili lingetokea kwenye nchi zilizoendelea, waziri wa uchukuzi hakuwa na kazi tena. Lakini nani atawajibika au kuwajibishwa iwapo wote hali ni ile ile? Utamsikia waziri akijitetea kuwa yeye hakuwa nahodha wa meli ile! Lakini iko chini ya wizara yake? Ubinafsi wa kupita kiasi utatumaliza. Hamkushuhudia waandaaji wa mashindano ya Miss Tanzania wakiendelea na sherehe zake ilhali wakijua taifa limekumbwa na msiba mkubwa? Nani anajali?

Mjadala huu hauwezi kuisha bila kugusia uzembe. Maovu yaliyotajwa hapo juu yana mama mmoja yaani uzembe. Nani angetegemea nchi yenye vyombo vyote vya dola, upelelezi na udhibiti kushindwa hata kujua idadi ya abiria waliokuwa wamepanda meli husika? Tunaambiwa 600, 800 na sasa imefikia kulipotiwa 3,00! Ukweli ni upi? Je huyu mwenye mali kama hakuwa na idadi inayojulikana kwa mamlaka zote husika, alikuwa anakatwaje kodi ya mapato? Je alikuwa analipa kiasi alichokuwa akitaka au kuna wakubwa walikuwa na ubia kwenye biashara hii kiasi cha kutolipa mapato? Namna hii kweli tunaweza kujikomboa kiuchumi?

Wafe wangapi tustuke iwapo waliokufa mwaka 1995 kwenye ajali ya MV Bukoba haikutustua? Laiti hada ndege ya rais ingekuwa inajazwa hivi au maisha yake kuwa ya msongamano huenda angeelewa hili. Lakini si hivyo. Yeye anaishi raha mstarehe tena kwa kodi za hawa hawa wanaoteketea kwenye misongamano.

Chanzo: Dira Septemba 2011.

No comments: