The Chant of Savant

Thursday 29 September 2011

Ukitaka utajiri saidia ukwepaji kodi TRA

NIMEANZISHA Kampuni ya Twalakodi kwa Raha Account au Taint Revenue Ashaming (TRA) baada ya kugundua kuwa kumbe kusaidia watu kukwepa kodi ni utajiri wa haraka kwa baadhi ya waroho na wezi.

Mpayukaji nimeanzisha kampuni ya TRA ili kusaidia serikali ya Bongolalaland kukusanya kodi vilivyo kwa njia ya kuruhusu watu binafsi kuweka kodi mifukoni mwao kwa niaba ya serikali.

Kwanza nikuonye. Ili kufanya hii biashara ya kula kodi ama uwe kigogo serikalini au unajuana na kigogo. Maana rafiki, mke, mtoto au mramba viatu wa kigogo naye ni kigogo. Upo hapo? Ukiona dogo watoto wa wakubwa nao wanakuwa wakubwa, usianze kutafuta mchawi au miujiza kwa matapeli wa Jangwani, Mwenge, Mikocheni na kwingineko.

Hayo ya makando kando ya vigogo tuachane nayo na kuzama kwenye kampuni yangu mpya.

Kampuni yangu itakuwa ikifanya upelelezi na kuuliza maswali. Kwa kuanzia, tuko tunafanya uchunguzi kutokana na ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa na waziri mkubwa mwenye Mizengwe ya Kupinda pinda ni kwanini makampuni kwa mfano ya madini yanalipa kodi kidogo kuliko hata yale ya pombe za kienyeji kama Chibuku? Hili ni swali muhimu la kuuliza na kujiuliza.

Je, nyuma ya pazia kuna wezi wenye ushawishi wanaolipwa kodi kwenye akaunti zao za siri kule Jersey na Island of Man? Je, maofisa wetu wadogowadogo nao wanapata kitu chochote kuwasaidia hawa wachukuaji wanaoitwa wawekezaji kuchukua chao kilicho chetu kinachoitwa chao na makahaba wao wenye ulaji?

Kuna uwezekano na hili likawa ni ukweli kutokana na uchunguzi uliofanywa na Dk. Msomi Mkatatamaa (si daktari wa kughushi kama wale washenzi wenye ulaji) na kugundua kuwa kumbe maofisa wengi wa Twalakodi kwa Raha Account pamoja na udogo wa nyadhifa zao ni matajiri wa kutupwa. Kama si mchezo huu, utajiri na ukwasi huu wanaupata wapi?

Tumegundua kuwa wafanyakazi wa TRA hata wawe wadogo kiasi gani ni walaji wazuri wa kodi ya wabongolalaland ya Danganyika. Wana mimali kama hawana akili nzuri. Wengine hawajui hata jinsi ya kutumia hiyo pesa wanayoipata kirahisi. Wengine hata ukisikiliza maongezi yao ni rushwa tupu. Anayebishia hili aende kwenye kampuni za simu na kuchukua nakala za maongezi ya viumbe hawa wenye akili ndogo lakini wanaofanya kazi kwenye ofisi yenye jeuri ya mshiko.

Hatutaishia kuhoji utajiri wa vijizi vidogovidogo vya TRA. Tutahoji hata wakubwa zao. Je, wao hawaoni mchezo huu? Kama wanauona na kuupuuzia wanafanya nini kwenye ofisi za umma? Je, wananufaika vipi na mchezo huu? Jibu lililoibuliwa na uchunguzi wa kisomi wa Mkatatamaa ni kwamba wengi wa waajiriwa wa TRA ni watoto au ndugu wa wazito waliomo sirikalini. Anayebishia hili aende mwenyewe kwenye ofisi za ulaji kama vile TRA, benki kubwa, mipakani, mita za kusoma mafuta, uhamiaji ambayo kwa sasa ni uhamishaji, atajionea mwenyewe.

Watajwa hapo juu kwa mujibu wa taarifa ya uchunguzi nilioamuru na kuwa chini ya mwenyekiti Msomi Mkatatamaa au Kamati Maalumu ya Kijiwe ya Mkatatamaa (KMKM), imebainisha kuwa wafanyakazi wenyewe wa TRA wanamiliki mali nyingi kama vile mahekalu, magari ya kifahari, mashamba na akaunti zilizoshiba kuliko walevi wengine.

Swali ambalo liliisumbua kamati ni kwanini sirikali haiwachunguzi hata kuwastukia? Jibu lilijitokeza kuwa katika nchi ya majizi, watoto na marafiki au jamaa za wakubwa huwa hawachunguzwi wala kushughulikiwa hata kama wanajulikana. Wapo wanaouza bwimbwi achia mbali kukwepa kodi. Wapo wanaokula kodi bila kujali wanaoilipa. Wapo wanaofanya vitu kama vichaa wasijue balaa wanalotengeneza.

Kijiwe kimeamua kuchunguza ili kuwasaidia pia kuusaidia umma kuepusha machafuko huko tuendako. Hivyo basi, wahusika wasidhani tunafanya hivi kuwachukia au kuwatibulia. Tunafanya hivyo kuepusha kaya na maafa yatokanayo na watu kukata tamaa baada ya kuibiwa na kunyonywa sana. Niliyashuhudia kule Masri, Libya na Tunisia. Hivyo, kinachofanyika ni uzalendo uliotukuka.

KMKM ilishangaa kukuta vijana wadogo walioingia kazini chini ya miaka kumi kuwa na mimali ya kutisha huku sirikali ikisema hakuna fedha. Fedha za kufanyia mambo ya maana kama kuwatoa walevi kwenye umaskini hakuna. Ila pesa ya wezi wachache kutumbua ipo tena kwa sana. Tazama yale madini na wanyama vinavyovushwa kila siku huku walevi wakiendelea kusota.

Tazama ajira zinazokwenda kwa wabangaizaji wenye uhusiano na wakubwa. Tazama uchukuaji unaoitwa uwekezaji. Tangu lini mtu akawekeza kwa kuchukua au kujenga kwa kubomoa? Kama wao ni vipofu na matahaira kiasi hiki, kiasi cha kutoona balaa hili, kijiwe kimeliona.

Pamoja na kamati kuchunguza ukwepaji wa kodi, nimeiamuru iwachunguze wafanyabiashara hasara ya siasa na biashara. Ingawa mkuu aliwahi kusema kuwa wahusika wachague moja, kumbe ulikuwa usanii. Tangu aseme hivyo amefanya nini kulikomesha hili wakati tunaona wafanyabiashara wengi tena wa bwimbwi wakizidi kuvamia siasa? Kuna siku nitaamuru yeye na familia yake wachunguzwe. Sitajali kuwa tarumbeta lake, Rweyependekeza atatutukana kuwa tu wambea na wenye husuda. Ikifika siku ya siku nitamchunguza potelea mbali liwalo na liwe.

Leo sichongi sana. You know what? Nawahi aepoti ya uwanja wa ndege kwenda kutanua Nuyoko na shosti wangu. Ukitaka kujua miujiza nenda TRA.

Chanzo: Tanzania Daima Septemba 28, 2011.

No comments: