The Chant of Savant

Tuesday 13 September 2011

Leo nafikiri kama mbuzi na si mlevi

Sithi Hosana, hosana, hosana,
Kuwe Nkosi yamakhosi.
Hosana, hosana, hosana.
Hosana, hosana, hosana, hosana.
Siyaguqa phambi kwakho, sizinikela lamuhla.
Thumel’uMoya oNgcwele, uzasikhanyisela, Sithi...
Sicel’uthando, lomusa enhliziyweni zethu.
Ibizo lakho, lidunyiswe, emhlabeni lasezulwini, Sithi...
Siyabonga, Baba wethu ngokusithanda
kwakho konke, Sithi...

Naomba nisitafsiri bali niende kwenye yaliyonikuta.

Juzi mwenzenu nilifaidi sana. Nikiwa zangu kwa Mama Betty nikipata kanywaji si akajitokeza fisadi mmoja toka chama fulani cha mafisadi anayegombea ulaji kule Igungaa lilikodondoka gamba la Kagoda. Jamaa alinipiga kwa makulaji ya nyama ya mbuzi sina mfano! Niliagiziwa mbavu, salala na figo nikajichana kama sina akili nzuri. Jamaa alitaka eti anipeleke Igungaa nimpigie debe. Hakujua mie japo mlevi bonge la mjanja. Nani afanye unepi kama wale waandishi makanjanja wanaotumikia mitumbo yao zaidi ya nchi? Sorry nimesahau. Alitaka eti niandike makala safi kwa wanywa gongo kumpamba ili anunue magazeti yote na kuyasambaza kule Igungaa asijue wengi wa wapiga kura hawajui kusoma wala kuandika!

Kwa wanasiasia uongo hili si tatizo hata kidogo. Ingekuwa nchi za wenzetu hiki ni kile wanachokiita bull’s eye. Hivyo, wange-barnstorm kuhakikisha watu wanapata angalau elimu ngumbaru.

Turejee kwa mpuuzi huyu. Hakujua mie ni msomi wa kupigiwa mfano ingawa PhD yangu nimeipata kwenye chuo kikuu cha Gongo! PhD yangu ya gongo ni kali kuliko zile za vyoo vikuu ambazo husababisha wenye nazo kuuibia umma kama mbuzi avamiavyo shamba. PhD ya gongo haigushiwi na kila juha ili aitwe daktari wakati ni kihiyo kama Msampuri anayefikiri kwa makalio. PhD ya gongo haigushiwi. Iga ufe kwa supu ya mawe si kanywaji ka kudandiwa na kila juha sawa na PhD yake.

Baada ya kujichana nyama mulua ya mbuzi nilianza kufikiri ni kwanini wanadamu humfuga na kumla mbuzi. Jibu rahisi nililopata ni kwamba wanadamu huwala mbuzi, kondoo, kuku na hata chamanki nchanga kwa vile wanawazidi akili. Je nyama ya mbuzi haiwakomeshi kwa uchoyo wao kwa kuwasababishia kuvimba miguu. Je nyie mliwao hamounekani na kufikiri kama mbuzi? Msiseme nawatukana kuwalinganisha na mbuzi ingawa ni hivyo. Kwanini mnaliwa? Hili ndilo swali langu la leo.

Mbuzi hawauawi kwa risasi kama swala na mbarapi. Lakini bado hufa tena kifo cha taratibu cha visu na manyanyaso. Je si bora kuishi kama swala kuliko mbuzi? Mbuzi hupigwa kwa mijeledi na kufungwa kamba. Swala wake mkuki au risasi lakini baada ya shughuli. Mbuzi na kondoo ni viumbe wa hovyo wasio na kumbukumbu. Ukimfokea mbuzi wakati anakula mahindi shambani mwako anadhani ni miaka mingi iliyopita. Ukirudia kumfokea anadhani ni jana. Hadi atie akilini hadi jiwe litu kichwani mwake hata kumvunja ubavu. Hiyo ndiyo akili na kumbukumbu ya mbuzi. Mbuzi hana kumbukumbu, na kama anayo basi ni ya muda mfupi sawa na wadanganyika ambao kila uchapo uchafuzi hukirimiwa gongo na mapupu kama jamaa alivyonifanyia akidhani nami ni mbuzi. Mie nilivibukanya vilaji vyake na sasa namtolea nyodo. Kama yu mjanja basi aje anipasue tumbo achukue uchafu wake. Mie hata kama mlevi ni mjanja tena bonge la mjanja niishie kwa gongo kuliko takrima za kipuuzi na ufisadi kama wa Ewassa.

Nazidi kujiuliza. Je hawa ndata wanaokuja hapa kwa Mfuga Hyena na kuwatoa wauza gongo na wala bwimbwi mitaa ya Mnazi Mmoja Lumumba uchache kwa vile wanavunja sheria si mbuzi? Watashindwaje kuwa mbuzi iwapo nao wanatenda jinai kwa kutumia jinai wakijua fika wakidakwa kibarua kinaota nyasi? Hawa nao ni mbuzi. Maana mbuzi huwa hafikiri wala kuwa na kumbukumbu zaidi ya kulialia meeee. Unampiga mtu bao ukimatwa unalia meeee! Meee ndio muziki wa mbuzi. Ndiyo maana mbuzi hula majani bila kufikiri kubadili sawa na hawa watenda jinai waishio kwa jinai wasibadilike. Je hawa si mbuzi binadamu? Je hawa wanaojilimbikizia mimali wakijua wakati waja wa kuwanyang’anya hiyo mimali na kuwatupa lupango umekaribia siyo mbuzi? Unafanya ufisadi halafu ukivuliwa gamba unaanza kulia meeee! Ndugu zangu wa magamba mpo hapo? Unachangisha pesa ya kuwahonga waishiwa ukimatwa unalia meeeee! Mbuzi mkubwa hata kama una cheo.



Nazidi kuwaza. Kwanini mbuzi hunya na kulala humo anyamo? Jibu rahisi ni kwamba ni kwa sababu yu mbuzi. Je hawa wanaochezea ofisi za umma wakijua fika si za urithi wana tofauti gani na mbuzi au kuku anyae na kulala pale aliponyea? Maskini mbuzi hana kesho ns kama ipo ni mashaka mtupu. Yake ni leo leo maana hajui kama kesho atapona kisu hata kama karidhika na kamba! Mbuzi ni mbuzi hata akae kwa bilionea bado atakula majani na kuitwa mbuzi. Mbuzi ni mbuzi hata awe tajiri miongoni mwa mbuzi wenzake. Mbuzi si mjanja mbele ya majani hata kama anayala. Huenda majani yangekuwa na miguu yangemkimbia.

Ingawa nami naweza kuitwa mbuzi hata kuwekwa kwenye kundi la mbuzi kutokana na kuwa mtumwa wa gongo. Je mtumwa wa gongo na mtumwa wa ufisadi nani mbaya zaidi kwa taifa? Hakika naona mbuzi kila mahali. Naona mbuzi wanono na waliokonda. Naona mbuzi wakilia lia meee kwenye kiza na umaskini wasijue la kufanya kwa vile wao ni mbuzi. Jamani, mbuzi ulimkosea nini wadudi hadi ukaridhika na umbuzi?

Leo siongei na wanywa gongo kama kawa. Naongea na mbuzi wangu. Nyie mbuzi, mtaacha lini umbuzi wa kuliwa mkijiona? Nanyi mbuzi muwalao mbuzi wenzenu mwadhani ni ujanja? Mbuzi ni mnyama mwenye kumbukumbu kidogo. Hata ukimletea demokrasia badala ya kuchagua mbuzi mwenyewe amuongoze atamchagua fisi! Je wawachaguao wawalao wana tofauti gani na mbuzi? Mbuzi ana nafuu kwa vile ni hayawani na hajihangaishi na kubadili mwelekeo wa maisha yake. Mawazo yake yameganda kama ya yule mama wa mjengoni ambaye bado hajui kuwa mambo yalishabadilika na ibada za sanamu zilishaondolewa! Hamumuoni akicheza Makidamakida? Yule naye ni mbuzi wa aina yake tena wa shughuli kama waliwao. Hamkumuona juzi akimteua fisi Ewassa kuwachunguza mbwamwitu wakati yeye ni fisi?
Chanzo: Dira Septemba 2011.

No comments: