Kwanza, nikiri. Mimi ni shabiki
wa mpendwa shujaa, mteule, msifika Ridhiwani Kikwete kufa mtu. Lazima kutangaza
maslahi yangu kwenye mjadala huu. Namshabikia Ridhiwani ajabu. Kuna kipindi
nilitaka kubadili jina langu niitwe Ridhiwani. Kwa kuogopa ngoa ya wavyele
nimeamua kumpa jina hili mtoto wa kiume nitakayempata.
Pia namshabikia Robert Kisena kwa
ujeuri wake hasa kwenye mambo ya connection na mshiko. Hivyo, kuna kipindi
nilitaka nijiite Ridhiwani Kisena lakini sababu ile ile ikanizuia. Hivyo,
kuonyesha ushabiki wangu, nikipata mtoto wa kiume namwita Ridhiwani Kisena na
kama ni wa kike nitamwita Ridhwana Kisenia. Hayo tuyaache.
Leo naandika kuwapasha
wanaowachafua wateule wangu. Huwa sipendi umbea. Huwa roho inaniuma ninaposoma
habari za kuwazushia na kuwachafua wateule wangu hawa.
Juzi katika kusoma kwenye
mitandao nilikuta tuhuma kibao dhidi ya wawili hawa. Mtandao mmoja ulizusha eti Ridhiwani ndiye
anayemtumia Kisena kuendesha kampuni yake ya marehemu Shirika la Usafiri Dar es
salaam (UDA) ambalo sasa linaitwa Simon Group utadhani mtoto si ridhiki. Chochezi jingine lilichangia likisema,
“Inashangaza Ridhiwani bingwa wa kujibu kwenye mitandao amekaa kimya. Je tuhuma
hizi ni mbinu za wabaya wake kumchafua au ni ukweli mtupu? Vyovyote iwavyo,
kuna chembe za ukweli kwenye madai haya hata kama si kwa kiwango kikubwa.
Sipendi kuamini kuwa huu ni ukweli wala uzushi. Ndiyo maana nimejitolea
kuwasaidia wahusika waweke mambo sawa na kusafisha majina yao huku wakifanya
hivyo kwa hoja zinazoingia akilini.”
Baada ya kusoma huo upuuzi hapo
juu nilikaribia kupasuka kwa hasira. Chini yake jingine liliandika, “Huwa
siamini kwenye conspiracy theory ambayo sina tafsiri yake kwa Kiswahili. Hivyo, naanidika waraka huu kutaka kujua ukweli
zaidi. Naandika kwa sababu kuu mbili. Mosi, kutetea mali ya umma ambao nami ni
mmojawapo. Pili, kumpa nafasi Ridhiwani kujitetea angalau hasa ikizingatiwa
kuwa kuna maisha baada ya baba yake kuachia ngazi.” Hili nusu lininyotoe roho
kwa ngoa.
Jingine liliandika, “Kwa
wanaofahamu historia ya Robert Kisena, hawana shaka yoyote aliibuliwa na vigogo
wa CCM hasa waziri Juma Kapuyanga kabla ya kudakwa na Ridhiwani ambaye
anajulikana walivyo marafiki. Ushahidi
wa wazi ni uchaguzi wa mwaka 2010 ambapo Ridhiwani alimpigia kampeni Kisena
lakini akaangushwa na John Shibuda.
Katika kampeni hizi alipigia pia Steven Masele ambaye pamoja na udhaifu
wake sasa ni waziri. Mwingine aliyetumika kama mbuzi wa shughuli ni Salum
Mbuzi.” Liliendelea, “Hata kunyimwa nafasi kwa Shibuda hadi akaihama CCM na
kujinga na CHADEMA na kuiadhibu kwa kuishinda kuna mkono wa Ridhiwani. Laiti
Shibuda angeamua kulisema la moyoni kijana huyu angeumbuka si kawaida.”
Wakati roho ikiendelea kuniuma
jingine liliongezea, “Wapo wanaosema kuwa pamoja na Ridhiwani kujionyesha kama
rafiki wa Kisena, ukweli ni kwamba wote wawili ni wajanja wanaotumiana. Kisena
anajua kuwa Ridhiwani ni mtoto wa rais tena rais mwenyewe asiyejali wala kuwa
mkali kwa familia yake. Hivyo, ni lulu
kutokana na kuwa mtoto wa mwenye nchi kwa sasa. Hivyo, kumnasa Ridhiwani ni
kuunasa utajiri tena wa haraka. Anayebishia hili ambane Kisena aeleze
alivyopata utajiri wake kama hakuna mikono ya watu tena wazito kabla ya
Ridhiwani.” Baada ya kusoma hii nilikwenda kujipumzisha.
Niliporudi nilikuta jingine
limeandika, “Kwa upande wake Ridhiwani anajua kuwa Kisena ni msanii mzuri
anayeweza kufanya madili kirahisi na kwa ufanisi. Pia Kisena, tokana na
historia yake ya kubebwa si rahisi kumuasi bosi wake kwenye biashara ya nyuma
ya pazia. Hivyo, ni kiraka mzuri na mtiifu hasa kwa kuzingatia jinsi anavyotoka
kwenye familia maskini na jinsi kinachoitwa utajiri wake kisivyo kuwa chake
bali wale wanaomtumia.” Nilitamani nilikamate hili na kulinyongelea mbali.
Jingine liliandika, “Kutokana na ukaribu huu
wa Kikwete na Kisena, baadhi ya wachambuzi wanaunganisha mistari na kupata kitu
kizima. Wengi wanahoji. Ni kwanini serikali imekuwa ikijikanganya kuhusiana na
umilki wa UDA kama hakuna wakubwa nyuma ya pazia wakivuta Kamba? Swali ambalo
liliibuka bungeni hivi karibuni ni kwanini serikali imetoa msamaha wa kodi kwa
Kisena kuingiza mabasi 300 wakati ikimkana kuwa si mmiliki wa UDA? Je kama
hakuna wakubwa wezi nyuma ya Kisena inakuwaje apewe msamaha wa kodi kwenye
biashara binafsi hasa ikizingatiwa kuwa biashara anayofanya si ya lazima kama
vile madawa na chakula wakati wa dharura? Je Kisena kama Kisena bila kuwa na
Ridhiwani nyuma ya pazia ana ubavu wa kupata msamaha mkubwa wa kodi bila kuwapo
wakubwa wanaofaidika? Wenye kutaka kujua nani yuko nyuma ya pazia shupalieni
huu msamaha wa kodi wa Kisena mtagundua kuwa yeye ni mtumiwa kama watumiwa
wengine.” Baada ya kusoma hii nilijisikia nikipandisha Usherukamba na kusema
f**ck you.
Jingine lilizidi kunipandisha
presha kwa kuandika, “Wapo wanaounganisha kufutwa kwa kesi ya Idd Simba na
kutochukuliwa hatua Victor Milanzi, mkurugenzi wa UDA aliyemuuzia UDA Kisena
ushahidi wa kuwepo Ridhiwani nyuma ya Kisena. Hata hii jeuri anayoonyesha
Kisena akijuwa wazi kuwa hajawahi kurejesha fedha ya stimulus aliyoipata kwa
mchongo si bure. Kuna Riz nyuma yake.”
Jingine liliongezea, “Kitu
kingine kinachoweza kumuumbua Kisena kama mtu anayetumiwa ni historia yake
ambayo waandishi wengi wameishaianika tangia akiwa sekondari.”
Mtandao mwingine uliandika, “Japo serikali
haitaki kusema ukweli, UDA ilianza kuhujumiwa pale mkurugenzi wake
aliyetimuliwa Milanzi kushirikiana na Simba kuitoa chini ya siasa za kindoto za
uzawa mfu ambao uligeuka kuwa ujambazi wa wazi. Hapa ndipo Kisena alipopiga
bongo kiasi cha kumnasa Simba jambo ambalo baadaye lilimvutia Ridhiwani.”
Kwa kuwazushia wateule wangu
nashauri TCRA ifungie hii mitandao ya kimbea. Wakishindwa sisi wapenzi wao
tutadedisha mtu. Wapendwa endeleeni kula kwani hiyo UDA ni mali ya mtu au umma?
Hakuna haja ya kukanusha wala nini. Pigeni dili kama kawa mwenye wivu ajinyonge.
Tuache umbea. Mkiambiwa Ridhiwani
ni mtoto wa Jakaya Kikwete mtasema ni umbea au uzushi? Heri yasifike ya akina
Saif al Islam Gaddafi. Akili kichwani.
Chanzo: Dira Juni 2014.
2 comments:
Nasikia kutapika
Anon huna haja ya kujihisi kutapika. Badala yake ondoa hicho kinyaa kinachokufanya ujihisi kutapika. Hamasishaneni tuondoe hiki kinyaa.
Post a Comment