BAADA ya Kijiwe kugundua kuwa Chama Cha Mafisi na Mafisadi (CCMM)
kimezima harakati za kuzuia kuchunguza ujambazi wa SCLOW aka Screw wa
madafu bilioni 200, Kijiwe kimekaa kama kamati kulaani ujambazi huu.
Pia Kijiwe kinalaani danadana na sanaa zilizoonyeshwa katika ujambazi
wa UdAr ambapo majambazi waliofanya hivyo wanafahamika kuwa ni Juma
Kapuyanga, Dida Masaburiz, Idd Lion, Riz Kiqueet, Bob Kisenha na
wengine waliojificha nyuma ya pazia. Msishangae kuona Kijiwe kimeingia
full masnonda kwenye politiki.
Ni kutokana na kuwepo ombwe hasa tangu Njaa Kaya aanze kufuja kaya
kwa uongo badala ya uongozi, sanaa badala ya sera na ufisi na ufisadi
badala ya usafi na uzalendo.
Mgosi Machungi siku hizi amegeuka mwanasiasa. Anasoma magazeti kama
hana akili nzuri. Anaingia na kulianzisha. “Wagosi mmesoma hii habai ya
wizi wa mabiioni kupitia kampuni la kijambazi la IpIITL na hii danadana
kuhusiana na UdAR mjengoni? Watu wazima hovyo. Wanafanya mambo kama
hawana akii! Kia siku sanaa sanaa wanadhani hatina akii? Shame on them
all!”
“Unaongelea hii EPAA mpya kuelekea kwenye uchakachuaji? Nilijua.
Wataiba. Wamezoea. Usishangae kutokea ujambazi mwingine. Hata ujambazi
huu wa UdAR si bure.
“Hamkuona waishiwa walivyovuana nguo juzi mjengoni huku wale wa genge
la uchakachuaji wakichekelea bila kuchukua hatua?” Anadakia Msomi huku
akituma SMS kwenye mtandao wake wa kiganjani.
“Hakuna waliponikuna kama kuanza kukamata uchawi hata mabalozi. Hivi
huyu kihiyo Maselee aliyepata ulaji tokana na kujuana na mwana wa
mteule Riz anaongeaje wakati madarasa hayapandi? Mnaona alivyoharibu
hadi mabosi wake kumkana na kumwangukia mama wa Kikameruni asiwanyime
njuluku na viza wanapokwenda kuzurura na kukagua akaunti zao kule?”
Anachomekea Mijjinga.
“Hawajamuangukia mtu. Hayo ni mambo ya kidiplomasia.” Anachomekea Bi. Sofi Lion aka Kanungaembe.
Mbwa Mwitu anadakia. “Wamemwangukia ili wamfanyeje? Waangalie
asiwakameruni. Maana hawa jamaa kwa kupenda kamchezo haka hakuna
mfano.”
Mchunguliaji anajibu. “Wakameruniwe mara ngapi iwapo bajeti
zinategemea wafadhili kila mwaka? Bila shaka walishawekewa masharti
ambayo wengine hatuyajui.”
Kanji hajivungi. “Kameruni nini? Hapana jua hii Kameruni bwana.”
Muishiwa Bwege naye analonga. “Kwani kukameruniwa vibaya? Wakitaka kuliwa acha waliwe maana ni mali yao au vipi?”
Msomi anagundua kuwa wakianza mambo ya kukameruniana wataharibu mada.
Anakula mic. “Hawa jamaa kweli wameishiwa. Kila mwaka wanarudia madudu
yale yale. Maana yake ni kwamba ni wavivu wa kufikiri kiasi cha
kukalia wimbo ule ule wa jogoo. Jamaa ameingia kwa kutumia EPAA na sasa
ataka kuondoka na EPAA ya kumwezesha kujilipa na kutafuta kibaraka
wake amrithi na kumlinda kama alivofanya kwa Tunituni Ben Makapu
aloasisi na kutekeleza EPAA. Nasikia amuandaa Abduli Al Somali
Kinamna.”
Mpemba anakula mic. “Yakhe hujakosea. Hawa weshaishiwa siku nyingi.
Wemelewa ulaji kiasi cha kufanya mambo kama hayawani. Mie siku zote
nalaumu wachovu waniojifanya hayawahusu wakati waliwa kila uchao. Hivi
kweli huu ujambazi wa IpIITL Srew na UdAR wahitaji elimishwa ndiyo
waandamane au nao wana uvivu wa kuamua? Utaona hata hili zengwe la
Mizengwe Pinder kupinga kuundwa kamati ya kuchunguza litapita bila
kupingwa ati.”
“Mgosi tiheshimiane. Unawezaje kusema kuwa tinaliwa wakati tikiwa
tinaona na kusikia kama si uchokozi? Hemu tiombe msamaha haaka kabla
sijapiga mtu zongo.” Mgosi Machungi analalamika huku akimkazia macho
Mpemba.
“Yakhe simaanishi wote japo ni wote kwani hata wao waliwa japo watula
sie. Huoni wanivolindana? Wasingekuwa wote waliwa wangewachukulia
hatua akina Saada Mkuyati, Freddie Wereema, A liar Kim Maswii, Dida
Masaburiz Makalio, Ben Ndururu, Sossie Mwongo, Juma Kapuyanga, Idd
Lion, Vikta Milaanzi na majambazi wengine waniojulikana kufanya huu
ujambazi wa nchana. Nani ankamate nani wakati wote wevi?” Anajitetea
Mpemba kiasi cha kukivunja mbavu Kijiwe.
Mipawa aliyekuwa ndiyo anamkabidhi mzee Maneno gazeti anakwamua mic.
“Hakuna kituko kilichoniacha hoi kama wapingaji kupendekeza eti buge
liunde kamati ya kuchunguza EPAA hii iitwayo Screw kwa Kisukuma. Nani
aunde kamati wakati yaliyomkuta mwenzao Eddie Ewassa mwana wa Luwasha
hayajasahaulika? Siku hizi amenywea kiasi cha mbio zake za kutaka ukuu
kufifia huku al Shabuub Kinamna eti naye akiutaka. Si aende akatawale
kwao Mogadisho.”
“Usinitajie huyu Kinamna. Hamjui kuwa ni mmojawapo wa waliochonga
EPAA hasa ikizingatiwa kuwa ndiye alikuwa kiongozi wa propaganda wa
Njaa Kaya? Kama jamaa huyu atapitishwa tumekwisha! Mie nitahama kaya.
Maana itakuwa ni aibu iliyoje?” Analalamika Kapende.
“Mie sisikitishwi na wachovu kwa vile kama wataamua kujihujumu kwa
kuruhusu hata majangili kukaa ikuu hiyo shauri yao. Mie nasikitikia
tembo wetu na faru. Kama waliweza kumsimika balaa huyu Njaa Kaya hata
huyo al shabuub wanaweza kumsimika na wachovu wasifanye kitu kama
kawaida yao.” Anazoza Mijjinga huku akiwa amekula ndita ile mbaya.
“Kipindi hiki hakubali mtu upuuzi tena. Hebu wajaribu watuletee hao
mafisadi wao waone tutakavyowafanyia kitu mbaya,” anatishia Mipawa.
Msomi hamkawizi. “Kama mmeletewa hili balaa kama alivyosema Mijjinga
na hamkufanya kitu, mtakifanyaje sasa? Kama mmeshindwa kuwachoma moto
majambazi wa Screw ya IpIITL na hawa wa UdAR mtafanya nini kukwepa
kutawaliwa na TX? Mtatawaliwa na hata mkewe Njaa Kaya kama ataamua
kumuachia maulaji.”
Kapende anachomekea hata bila kungoja Msomi amalize. “Usemayo kaka ni
kweli mtupu. Mna habari hili kampuni la bandarini la Ticks ni mali ya
Niziro Kadamage na hakuna anayehoji wakati alilipata alipokuwa waziri?
Ulize ili kashfa ya Tunituni Ben na Ana Tamaa kujitwalia Kiwila
limeishia wapi? Ulizia mabilioni ya Uswizi yameishia wapi? Jamani, hii
kaya ni shamba la chizi mtake msitake. Kila mwana kaya analiwa kivyake
vyake hata kama haipendezi.”
Kijiwe kikiwa ndiyo kinanoga yalipita mashangingi ya akina Kapuyanga,
Ndururu, Mkuyati, Were-ma, Idd Lion na Masaburiz. Acha tuyakimbize ili
tuue mtu! Kama si madereva wao kuongeza kasi tungewachoma kama vibaka
wallahi.
Chanzo: Tanzania Daima Juni 11, 2014.
No comments:
Post a Comment