How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 4 June 2014

Namlilia mama yangu nchi yangu!


 
          Nayaandika haya kwa uchugu wa namna yake. Kila uchao hali mama yangu nchi yangu inazidi kuwa mbaya. Watoto wake wasio na hatia wanazidi kuangamizwa na wenzao waliogeuka majambazi na mafisi na mafisadi waliojazana kwenye ofisi za umma wakiuma kila kilicho mbele yao. Kila siku tunapata taarifa za misiba na majanga kana kwamba tumelaaniwa.
Vyombo vya habari siku hizi vimegeuka chanzo cha mauti ya walio wengi hasa wanaokufa kutokana na shinikizo la damu lisababishwalo na wanayosikia juu ya jinsi nchi yao inavyodhulumiwa na kuhujumiwa. Tunapata habari za wizi wa mabilioni kila uchao ukiachia mbali kushamiri kwa jinai kama vile ujambazi, uzembe, mihadarati na mengine mengi.
Tumejikuta tukilia kama wasi kwao ndani ya nchi yetu wenyewe. Tumefikia mahali tumekata tamaa. Hatuna wa kututetea wala wa kutusemea. Tuliowaamini na kuwachagua wabunge watuwakilishe kwenye mabunge ya Katiba na la kawaida wamegeuka waimba mipasho na mabingwa wa kejeli matusi na uzushi. Wanavuana nguo mchana kweupe tena mbele ya watoto. Tumeshikwa mateka na wale tuliodhani ni wenzetu. Tunalia na kusaga meno tukiomba mkono wa Mungu ushuke na kutuokoa lakini wapi. Mungu alishatupa akili, maarifa, mikono na juu ya yote nchi yenye raslimali lukuki. Je tatizo ni nini?
Tuanze na elimu. Wakubwa zetu wameamua kutujaza ujinga ili waendelee kutuangamiza wao na mawakala wao toka nje. Wakati wakidhoofisha elimu yetu, wanapeleka watoto wao kusoma nje kwenye elimu bora na ya maana tena kwa kodi zetu. Utawajua wanaporejea na kupendelewa katika ajira na nafasi nono za kisiasa za ulaji. Kwa wale wasiojulikana utajua walivyobobea tokana na kusoma nje usomwapo wasifu wao kwenye siku ya harusi au misiba yao. Kama walivyofichua baadhi ya wabunge wenye uchungu na nchi yetu, elimu yetu iko chumba cha mahututi wenye kuhitaji uangalizi maalum yaani Intensive Care Unit (ICU). Wakati janga hili likiendelea, baadhi ya wakubwa waliokabidhiwa idara na wizara husika wanatukoga hata tunapogundua madudu yao. Mfano, waziri wa Elimu Shukuru Kawambwa alipobainika kuwa ndiye chanzo cha kifo cha elimu yetu, na kutakiwa kuachia ngazi, alisimama tena kwa nyodo na kusema asingejiuzulu. Na kweli, hakujiuzulu zaidi ya kuendelea kufanya madudu.
Baada ya Kawambwa kugoma kujiuzulu, wengi walikosea wakidhani rais aliyemteua angemwajibisha. Rais hakufanya hivyo. Wapo wanaosema ni kwa sababu ni marafiki tena wanaotoka jimbo moja. Rais hakukanusha. Hii inaonyesha kuwa madai haya yana ukweli.
Baada ya kugundua kuwa kuua elimu hakutoshi, waliamua kuua viuana wetu kwa kuwaletea mihadarati ili iwamalize kabisa. Tunasikia nje ya nchi shehena za unga zikikamatwa zikitokea Tanzania tena kwa kilo mamia na si vijiko. Hakuna anayejali. Watajali nini wakati unga unasaidia kutengeneza mataahira wengi ambao hawawezi kuhoji uchafu unaotendeka kila uchao. Watajali nini iwapo biashara hii haramu inawaingizia mabilioni kwa haraka? Hatuzushi wala kuzua. Muulize rais amekamata wangapi tangu apewe orodha ya wauza unga miaka nane iliyopita? Imefikia mahali viwanja vyetu vya ndege vimegeuka njia rahisi ya kupitisha unga hata wanyama hai. Na hakuna anayejali zaidi ya kuendelea kutupumbaza kuwa hayo ndiyo maisha bora kwa wote yaliyoahidiwa na wakubwa zetu wakati wakituingiza mkenge kuwapa ulaji.
Kama bwimbi halitoshi, wameamua kuiba raslimali zetu na kuzifuja kana kwamba hakuna kesho. Kila uchao wachukuaji waitwao wawekezaji wanakuja maskini na kuondoka matajiri wa kutupwa. Wakubwa wanaangalia baada ya kupewa chao. Tumegeuka taifa la hovyo Mungu anajua. Nani mara hii kasahau sakala la juzi ambapo serikali ilipoteza bilioni 83 za kodi ya mafuta? Nani amesahau afisa aliyeitwa na bunge akaeleza aliyoeleza alivyouawa kwa kunyongwa hotelini baada ya kurejea toka Dodoma? Hili ndilo taifa letu la mafia.
Wanyama wetu hasa tembo wanazidi kumalizwa na majangili ambao mchungaji Peter Msigwa mbunge wa Iringa Mjini (CHADEMA) amesema wazi kuwa ni marafiki wa rais Jakaya Kikwete ambaye kwa kuona ukweli mbichi wala hakujibu tuhuma hizi. Je kama hakuna ukweli ni kwanini rais au wasemaji wake hawakujibu tuhuma tena kwa majibu yanayoingia akilini?
Nchi yetu imegeuka chanzo kizuri cha wakwepa kodi tena wenye biashara kubwa tu. Rais wetu anakesha kwenye ndege kiguu na njia akienda ughaibuni kuomba pesa tena kidogo kulinganisha na ile anayoacha iibwe kana kwamba nchi yetu ni shamba la bibi. Tokana na tabia hii ya kwenda kusaka misaada huku akiacha pesa kubwa kuliko anayopewa kwa dharau na kejeli kumesababisha kujengeka dhana mbali mbali kama vile kuitwa Vasco da Gama yule jambazi wa kireno aliyezunguka dunia akifanya uporaji. Pia imejengeka dhana kuwa anafanya hivyo ili kujilisha pepo na kulipwa per diem. Kama kawaida yake, rais hakanushi wala kutoa ufafanuzi zaidi ya kuendelea na business as usual. Ajabu wakati tukiombaomba tuna jeuri ya kutumia mabilioni eti kuadhimisha kumbukumbu ya Muungano usio na kichwa wala miguu! Hilo moja. Jingine ni kwamba pamoja na rais wetu kufanya safari nyingi kuliko wote waliomtangulia, kama ilivyofichuliwa na Mthibiti na Mkaguzi wa Fedha za serikali kwa kimombo Controller and Auditor General (CAG) kumbe hata tiketi za kusafiria tunalanguliwa mara kumi na sita ya bei halali! Wizi ndani ya wizi!
Maskini wa Danganyika ameendelea kuwa kitowewo cha wanyama mwitu wa ndani nan je. Anatozwa kodi kubwa wakati wageni watukufu wa watukufu wanafanya biashara bila kulipa kodi. Kila mwenye meno anamla maskini wetu ambaye naye amegeuka kondoo ambaye humtii mchinjaji wake. Analiwa kila uchao na kila ajaye kutokana ima na woga na kujifanya hayamhusu wakati yanamsulubu! Je kulialia kunatosha kutuondoa kwenye janga hili la kujitakia na kutengenezewa na wale tunaowalipa?
Kuna maafa na maangamizi mengi yanafanyika. Kwa uchache tokana na nafasi kutotosha, leo nina kila haki ya kuililia Danganyika yangu na watu wake waathirika. Hakika, naililia nchi yangu iliyogeuzwa  Danganyika.
Chanzo: Dira Juni 2014.

2 comments:

Anonymous said...

Pole Mwalimu, sisi tunahitaji siyo unachotaka wewe, tambua hilo!

Sisi tunapenda wajinga ili tuendelee kuwapoteza hivyo tunajitahidi kwa kila hali kuweka mazingira mazuri yasikowa ya kizalendo ili kupata majuha wakutosha kwa aliji ya kutupigia kura na kutusujudi

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon,
Du! Eti mnahitaji wajinga ili waweze kuwapa kura ya kula siyo? Namna hii nitachelewa kurejea Danganyika ili angalau vitegemezi vyangu vigraduate vinginevyo ni msiba. Wenzenu wanawekeza kwenye elimu ili kuendelea nyinyi mnaendelea kuwekeza kwenye ujuha na ujinga!