The Chant of Savant

Saturday 21 June 2014

Mlevi kuanzisha Waishiwa Boxing Club (WBC)

Baada ya wiki iliyopita kushangaa jinsi walevi wanavyoweza kuibiwa huku dingi akiwa kinara wa kubomu, wiki hii tunaangalia namna ya kuwakwamua wahishimiwa toka kwenye wingu zito lililozunguka utendaji wao na tabia zao.
Mlevi ameamua kuingilia kati ili kuokoa hadhi ya wahishimiwa ambao kwa sasa wanaonekana zaidi waishiwa na si wahishimiwa japo si wote. Kwa upendo mkubwa na taadhima, Mlevi amekuja na mbinu mpya ya kurejesha heshima ya waishiwa wahishimiwa.
Baaada ya kugundua kuwa kumbe waishiwa wa mjengoni wanajua kuyachapa makonde, mlevi anapanga kuanzisha kampuni ‘special’ kwa ajili ya kupromoti masumbwi Waishiwa Boxing Club (WBC). Kampuni hii itaepusha wahishiwa kupata hasara kwa kuzichapa bila kiingilio.
Yaani nakuwa promota. Tofauti ni kwamba sitapromoti wachovu au ngurumbili wa kawaida, bali waishiwa wahishimiwa.
Hivi utajisikiaje kuona mbunge wako akimgaragaza mtu kwa mangumi kuthibitisha mlivyo ‘tough?’ Kwa wale ambao wabunge wao watatolewa ‘knockout’ nisameheni.
Kimsingi, WBC inalenga kuwaondelea waishiwa hatari na kuonekana wa hovyo sawa na wapiga debe wa daladala wanaopigana hata kwa kugombea karanga.  Haiwezekani wahishimiwa wetu waendelee kutopea kwenye uishiwa hadi kutaka kushikana mashati tena hadharani, wenye akili na hishima tusifanye kitu.
Hivyo, WBC licha ya kuwa klabu ya burdani, inalenga kurejesha heshima za waishiwa wapenda kuchapana makonde ukiachia mbali kurushiana mitusi ya nguoni.
Nadhani jamaa yangu Pita Sherukamba upo na unanielewa sana na wale jamaa zangu toka Zenj na ndugu yangu Ali Kesi. Jioni Komba, Stivu Wahasira, Jiwelinaloishi Lusindi na wengine ambao ni mabingwa wa mitusi na mipasho mnanipata.
Bila shaka, mtaunga mkono huu ukombozi wenu.
Napanga kutoa burudani ambayo haijawahi kushuhudiwa popote duniani. Licha ya kutoa burudani na kuongeza kipato cha waishiwa, ndondi zitapunguza majungu, mipasho na mitusi.
Pia ndodi zitawasaidia waishiwa kupunguza viribatumbo vitokanavyo na kuvimbiwa ulaji na hishima. Naamini ndondi licha ya kuwaburudisha waishiwa na watazamaji, pia zitaondoa tabia uchwara ya woga fulani kutishatisha walevi kuwa watakwenda porini kama mambo yao hayatapita.
‘Simple’, kama unayaweza ingia uringoni badili ya msituni au kukimbilia kututishia geshi.
Sitanii. Kwa vile Bongo inaruhusu mtu yeyote kuanzisha kitu chochote kuanzia EpA, madhehebu ya dini, ESCROW aka.. screw na mambo mengine, nina hakika nitapata leseni hii inayolenga kutunisha mshiko wa wahishimiwa.
Waishiwa wakipata posho ya kuzichapa, makalio, usingizi, mipasho, taarabu na mambo mengine bila shaka watakuwa wenye furaha.
Pia njuluku watakazozoa baada ya kushiriki pambano zitawaepushia kwenye kubomubomu kwenye mashirika binafsi kama ilivyofichuliwa hivi karibuni kiasi cha waishiwa kuumbuka na kuumbuana kabla ya kulianzisha segere lililotaka kuishia kwenye ndondi kiasi cha mlevi kupata wazo la kutengeza njuluku.
Pia waishiwa wakishazoea kuzichapa hawatakuwa tayari kuburuzwa na chama kama kamati.
Maana kutokana na kujua kuzichapa, kama atatokea mtu au kikundi cha watu hata chama kuwatisha, wataamua kurusha ngumi haraka na kumaliza udhia hapo hapo bila kuhitaji kupoteza muda na njuluku za umma wala kutoa burudani kwa vyombo vya umbea.
Baada ya kuanzisha WBC nataka nihakikishe kwenye ule ukumbi wa mjengoni nako kunakuwa na ukumbi wa ndondi.Pia, nitapendekeza sheria zibadilishwe.
Kama ikitokea waishiwa wawili kushindwa kuelewana, sheria zizuie matusi na kuruhusu wazichape.Kuzichapa kutaondoa nongwa ngoa na kukata ngebe kiasi cha kuokoa njuluku na muda wa umma ukiachia mbali kupata pesa na ujiko.
Kwa sasa naangalia uwezekano wa kupanga mechi baina ya Daud Kafulia na Sossie Muongo ili kuondoa shaka juu ya ukwapuaji wa njuluku zipatazo madafu bilioni 200 kwenye fuko la ‘screw’ hivi karibuni.
Nataka wahishimiwa hawa watwangana mangumi hadi ukweli ujulikane juu ya ni nani alikwapua njuluku za walevi. Badala ya Muongo kutujaza uongo na umbea, tunamtaka ulingoni apambane na David aliyemchapa Golliati.
Mechi nyingine bila shaka itakuwa baina ya Annae Kajuamlo Tiba- Ijuka vs Khalima Mundee ili tujue madai ya ukwapuzi wa ardhi yataisha vipi. 
Naamini huu mtanange utavuta wengi hasa ikizingatiwa kuwa unahusisha akina dada ambao siku hizi wamekuja juu karibu kwenye kila kitu.
Baada ya mechi ya Tiba na Mundee, napanga ifuatie ile ya Bill Lukuvie na Pita Msigwani ili tuone nani kijogoo wa wanyalukolo.
Hii nayo lazima itakuwa mechi ya kusisimua hasa ikizingatiwa kuwa wana masumbwi husika wanasifika kwa mihasira yao. Ila natoa onyo, hakuna haja ya mtu kujinyonga eti kwa sababu ametolewa ‘knockout’.
Hivyo, badala ya kutumia ‘knck-on’ itokanayo na ‘knockout’, wahusika wanashauriwa kuwa watulivu na wenye kukubali kuwa ulingoni ndiko msema kweli.
Kuna kipindi nilipanga kupanga mechi baina ya Jioni Komba na Kangi Lugo-la, lakini kwa kujua kuwa Jioni anaonyesha kuwa na afya yenye mgogoro hasa kiribatumbo, bado nawasiliana na daktari wa mchezo huu ili anipe ushauri.
Kwa vile lengo na WBC ni kurejesha heshima ya mjengo, nawashaurini waishiwa wote waliokuwa wamewekeza kwenye matusi na ngumi za mitaani waachane nayo na kuja kujiunga na ngumi za kulipwa ambazo bila shaka zitawaongezea mashabiki na wapiga kura ya kula mwakani.
Kwa vile walevi wamepigika hasa baada yakugundua kuwa kuna mafisadi wengi kuliko wanavyoweza kufuga na kulisha, ubabe unaweza kuwa mtaji mzuri wa kisiasa hasa utakapokuwa umeonyeshwa ulingoni badala ya ngumi za mitaani au kwenye viwanja vya mjengoni.
Baada ya kufanya majaribio ya mechi tangulizi za waishiwa, nitapanga mechi moja ya kufa mtu baina ya Sam Sixx na Annae Makidamakida ili kuamua nani anapaswa kuwa kipaza sauti wa mjengo kihalali. 
CHANZO: NIPASHE 

No comments: