Taarifa kuwa wabunge wamekuwa
wakiombaomba fedha kwenye mashirika kukidhi shida mbali mbali binafsi na za
kisiasa zinawafanya waonekane kama wabuge badala ya wabunge. Kwanini mbunge
ategemee kuomba wakati ana jimbo kubwa ambalo lina raslimali nyingi kuanzia
watu hadi maliasili? Je nao wameathiriwa na mdudu wa kuombaomba kama serikali
yao?
Aliyefichua
uombaomba wa wabunge si mwingine bali mwenzao Tundu Lissu aliyekaririwa
akiliambia bunge, “Sifa hizi zina sababu yake. Kuna nyaraka na barua
zinazoonyesha wabunge mbalimbali waliochukua fedha za mifuko hii kwa sababu
mbalimbali.” Baada ya Lissu kulipua bomu hili alishambuliwa na wahusika hata
kwa matusi ya nguoni badala ya kupinga madai aliyotoa.
Lissu
aliongeza, “Unaweza ukajiuliza maswali mengi. Wizara inaomba fedha katika mfuko
wa jamii ili kununua kompyuta na vifaa vingine vya ofisi wakati ina bajeti ya
ununuaji wa vifaa hivyo.
Inatisha.
Wabunge waliotuhumiwa kuombaomba toka kwenye Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF)
ambao waliusifia kwenye michango yao bungeni kama kulipa fadhili.
Waliotajwa ni pamoja na Mbunge wa Kongwa
ambaye pia ni Naibu Spika, Job Ndugai; Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi; Naibu Waziri wa Katiba na Sheria,
Angela Kairuki na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Pindi
Chana na wabunge Betty Machangu (Viti Maalumu), Livingstone Lusinde (Mtera),
John Komba (Mbinga Magharibi), Eugen Mwaiposa (Ukonga) na Gudluck Ole Medeye
(Arumeru Magharibi).
Hapa
tunaongelea wabunge wanaoomba pesa kwenye mashirika. Je ni wangapi wanaomba
pesa kwa wawekezaji kiasi cha wawekezaji kugeuka miungu kama ilivyotokea kule
Mara ambapo mgodi wa dhahabu unaendelea kuwaumiza wananchi wa kule bila
serikali kuchukua hatua?
Hivi waziri
anapogeuka ombaomba unategemea atatenda haki pale anapojikuta akipambana na
shirika linalomfadhili? Jibu analo Lissu aliyekaririwa akisema, Hali hii
inaweza kusababisha Bunge likashindwa kutimiza wajibu wake wa kikatiba wa kuisimamia
Serikali na taasisi zake.” Haya mashirika si wajinga. Wanatoa fedha kwa wabunge
wakitegemea kuwatumia. Maana hakuna cha bure duniani tunapongea kiuchumi. Ukitaka
kuona huu ukweli hebu jiulize: Inakuwaje shirika kama NSSF kutoa pesa kwa
wanasiasa wakati wanaochangia mfuko huo wakizungushwa kupata mafao na michango
yao kama hakuna biashara nyuma ya pazia? Kuonyesha baadhi ya wabunge wetu
walivyogeuka wabuge, mmojawapo, Machangu alikaririwa akijitetea kwa kutoa
majibu ya kibugebuge aliposema, “Ni muongo kabisa (Lissu) yeye inamhusu nini
hiyo?” Huyu hata kama ameingia kwa
tiketi ya kupendelewa hafai. Anauliza eti yanamhusu nini Lissu wakati
akishuhudia heshima ya bunge ikishuka tokana na upogo na uroho? Yanamhusuje wakati
kazi yake kama mbunge wa upinzani ni kuisaidia serikali kurejea kwenye mstari? Huyu
kweli ni mbunge au mbuge asiyejua hata mambo mepesi kama haya wala wajibu wake?
Mwingine aliyethibitisha
waheshimiwa hawa walivyogeuka wabuge ni Lusinde aliyekaririwa akisema, “Fedha hizo tumeshapata na
pia tuliomba nyingine katika Kiwanda cha Saruji cha Wazo bado hatujapata.” Mbunge
kama huyu anayetegemea kufadhiliwa na kiwanda kama Wazo Hill anaweza kusimamia
haki za wananchi wa maeneo hayo wanalalamikia kiwanda husika kuchukua maeneo
yao ya ardhi au kuchafua mazingira wakati alishalishwa ubuge?
Trumegeuka taifa
la hovyo sana. Taifa la ajabu la maombaomba wakati mali tunayo ila tumeikalia. Rais
anakesha kwenye ndege akienda ughaibuni kuomba huku akishindwa kurejesha fedha
zilizofichwa Uswizi. Waziri naye anaomba bila kumsahau mbunge. Je namna hii
tutafika? Tunakuwa kama hayawani kuomba kile ambacho tuna uwezo wa kuzalisha
kama tutaamua kutumia akili sawa sawa!
Ni bahati mbaya
sana kuwa baadhi ya watuhumiwa wamejitahidi kugeuza tuhuma za uombaomba kuwa za
kisiasa wakati kimsingi ni za kimaadili. Huu ni ushahidi kuwa madili yamechukua
nafasi ya maadili kiasi cha wabunge wetu kugeuka wapiga madili badala ya
kusimamia maadili ambayo kimsingi, ndiyo yangewawezesha kuwanufaisha wale
waliowachagua. Hatuwezi kufika kwa mfumo huu wa kila mtu kujihudumia kwa njia
safi na chafu. Hatuwezi hata kidogo. Tukiweza tutaangamia kama jamii na taifa
kutokana na upogo na uroho wa baadhi yetu wanaotaka kuhalalisha haramu. Uombaomba
si kitu kizuri hata kama kinafanywa na watu wenye madaraka makubwa kama rais
wabunge na mawaziri. Kinachopaswa kufanyika si kuupenda bali kupambana nao kwa
njia ya kujitegemea na kupambana na ufisadi na sera za kibabaishaji.
Ombaomba ni
ombaomba hata akivaa suti au kuitwa mheshimiwa au rais na makorokoro mengine. Uomba
omba ni udhalilishaji na ukorokocho.
Leo hatusemi
mengi. Badala ya wabunge wetu kujigeuza wabuge na kuchukia kila anayewakosoa au
kupinga udhalili huu wa kujitakia, wabadilike na kuwa wabunifu kwenye majimbo
yao kiasi cha kuweza kujijengea heshima. Kuomba hakuwezi kutatua matatizo ya
wahusika zaidi ya kuwadhalilisha na kuwafanya watumwa wa wale wanaowafadhili. Kimsingi,
wabunge wetu wachukie na kuepuka kuwa wabuge yaani wapenda udoho udoho au vitu
visivyolingana na hadhi yao.
Chanzo: DIRA
2 comments:
Sijawahi ona wala sikia nchi omba omba na misaada kama Tanzania
Kila kukicha kampuni za simu kutoa misaada je ni kweli ni misaada au 10% ya misamaha ya kodi
Dunia nzima huendeshwa kwa kodi bila kodi hakuna maendeleo
Anon hujakosea. Heri wangekuwa ombaomba wanaokula pamoja na si mibaka inayopewa na kuficha huko huko nje. Hivi ulitegemea nini makampuni ya simu kuendeshwa na matapeli wa kigabacholi? Ni bahati mbaya hata wadanganyika wamezoesha ufadhili kiasi cha kuacha kufikiri wakifikiri juu ya nani atawafadhili hata kwa kuwapa mabaki ya alichowaibia.
Post a Comment