How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Saturday, 14 June 2014

Mlevi apanga kuikopesha sirikali

Baada ya mlevi kunyaka nyeti kuwa sirikali imewamba ile mbaya, kwa vile yeye ni mzalendo wa kupigiwa mfano, anapanga kuipa tafu kwa kuikopesha kiasi cha pesa ambacho huwa anatumia kujikimu kama vile kununua ulabu na mibangi.
Haiwezekani kaya yenye mamilioni ya walevi, rasilimali, mali na kila utajiri kuendelea kusota hivi.
Nani aliwaroga enyi walevi ambao kila kitu kiliwekwa wazi mwaka ule wa 2005?
Ajabu ya maajabu pamoja na mabalaa yanayokumba kaya hadi kuishiwa na kutegemea wahisani, walevi wanaendelea kudunda kana kwamba kesho hawatachenjiana kama hawatabadilika.
Kwa vile mlevi ni mtu mwema na mwenye mishemishe nyingi, licha ya kuipa tafu sirikali, anapanga kutangaza hadharani kuwa wamchague akamate wote waliofilisi kaya hii bila huruma. Mlevi haoti wala kuongea mambo ya politiki. Amedhamiria kuikomboa kaya hii ili nayo irejeshe heshima yake na kusonga mbele badala ya kuendelea kuserereka ikielekea kuzimu.
Ifuatayo ni mipango ya mlevi kuhakikisha kaya inarejesha utajiri na heshima yake tena kwa haraka.
Mosi, nitahakikisha kwanza nakamata wezi, mafisadi, wauza bwimbwi, majambazi, wanaotorosha njuluku kwenda ughaibuni haraka na kwa kustukiza.
Nitaanzia operesheni tokomeza umaskini, wizi, ufisadi na jinai. Hapa sina cha msalie Mtume wala nini bali kuweka watu lupango kama sina akili nzuri.
Pili, nitahakikisha nafuatilia dili zote kuanzia ulipoanzia ujambazi unaoitwa uwekezaji ili kuhakikisha narejesha mali moja baada ya nyingine huku nikifunga wote walioingia mikataba ya kijambazi na kipuuzi kwa kuangalia matumbo yao badala ya mustakabali wa kaya.
Hivyo, wote wenye biashara na akaunti fichi wakae mkao wa kuliwa naja mkombozi wa kaya aliyetabiriwa na mitume akina Mchonga, Kinjekitile, Mkwawa, Milambo, Nyungu ya Mawe na wengine.
Lazima kuanzisha utaratibu wa kutumia kompyuta kwenye kila kitu ili kukwepa kuibiana. Lazima kila mlevi awe na kitambulisho na taarifa zake zitunzwe kwenye kompyuta kuu.
Tatu, nitahakikisha narejesha maadili na kuondoa madili.
Bila maadili madili yataendelea hasa ikizingatiwa kuwa kutokuwapo maadili ndicho kichocheo kikubwa cha madili. Hapa lazima kurejesha siasa ya Uadilifu, Uwajibikaji na Maendeleo (UUM).
Natamani kurejea Ujamaa na Kujitegemea ili kupambana na Uhujumaa na Kujimegea vinavyoendelea. Lakini kwa vile mfumo huu ulishazikwa na mabepari, sitaki wanicheke na kupata sababu ya kunifurusha toka kwenye maulaji.
Tatu, nitachapisha orodha ya majina ya wale wote watakaokamatwa na kiasi cha fedha na mali watakazokamatwa nazo bila kuficha wala kuzungusha.
Hii itasaidia, kwanza, wahusika kujulikana, pili umma kujua kiasi gani cha mali ulikuwa umeibiwa na tatu, hii itasaidia umma kujua umerejesha mali kiasi gani na kila mwezi nitakuwa natoa taarifa juu ya maendeleo ya zoezi zima.
Nne, nitafuta misamaha ya kijambazi ya kodi hasa kwa wachukuaji ambao wamekuwa wakifaidi na kubadili majina ya biashara zao kila baada ya miaka mitano.
Tano, nitahakikisha bidhaa zinazouzwa na kuagizwa toka nje zinakaguliwa kuhakikisha hakuna ‘mis-invoicing’ au kushusha thamani halisi ya bidhaa husika ambako kimsingi kumekuwa chanzo kikubwa cha kuibiwa mabilioni kaya yetu kila uchao.
Sita, nitafuta Takokuru na kuanzisha asasi huru ya kupambana na jinai zihusianazo na uchumi yaani ‘Special Team Instituted to Combat Krimes (STICK).’
STICK itakuwa huru na haitaripoti kwa rais wala nani isipokuwa kwa wananchi wenyewe.
Saba, nitaunda ‘ANTI-STICK’ yaani ‘Authorized Network Tasked With Inspecting STICK.’
Hii itasaidia kufanya kile waluguru huita ‘check and balance’.
Sambamba na ‘Anti-Stick’, kutakuwa na taasisi nyingine ya siri itakayochuguza ‘Anti-Stick na Stick’ huku nazo zikiwa na mamlaka ya kuichunguza hii taasisi ili kuepuka kuchezeana kama ilivyo kwa sasa.
Nane, wana kaya watawajibika kisheria kutangaza mali na umaskini wao bila kujali cheo cha mtu wala ukoo na mtandao wake.
Mlevi hataruhusiwa kutumia zaidi na anavyopata wala kupata zaidi ya anavyostahiki.
Tisa, nitapunguza ukubwa wa sirikali nikihakikisha kuwa kila mwana kaya anachapa kazi kwa kadri ya uwezo wake na kulipwa kwa kadri ya kazi aliyofanya.
Kumi, nitapunguza mishahara na marupurupu ya wanasiasa hasa wale wa mjengoni.
Kila mtu atalipwa kwa kadri ya elimu yake. Lazima nisisitize. Ninaposema elimu namaanisha elimu halali na inayowekwa kwenye vitendo. Kwa mfano, kama mlevi atasema ana PhD halafu utendaji wake ni kijanja kijanja kama akina Juma Kapuyanga, J4 Majembe, Ben Ndururu, Saada Mkuyati, Adam Milima ya Kigoma,Shcool Kawadog, Sossie Muongo na wengine lazima warejeshwe shule na kusomea shahada yake upya tena kwa kujilipia ukiachia mbali kudaiwa arejeshe njuluku zote alizolipwa akiwa anafanya usanii.
Kumi na moja, kuhujumu uchumi, kughushi, ufisadi, kuuza bwimbwi ni makosa kati ya mengi ambayo adhabu yake itakuwa ni moja tu, kunyongwa hadi kufa.
Hapa ifahamike kuwa wale wote ambao kwa sasa wanatuhumiwa kwa makosa haya na kukingiwa kifua na wahalifu wenzao lazima wawe wa kwanza kuhukumiwa na adhabu zao kutekelezwa ili uwe mfano, onyo na somo kwa wengine.
Kumi na mbili, nitafumua, kuvunja na kusuka upya mageshi yote ili kuhakikisha yanaleta ufanisi na kuwatumikia walevi badala ya vyama na wanasiasa mfu na uchwara. Nitapiga marufuku wakubwa wa mageshi kushiriki au kushirikishwa siasa.
Mfano, hawataruhusiwa kuteuliwa mabalozi, wakuu wa wilaya au mikoa, wenyeviti wa bodi za wizi na ulaji wala kutumikia chama chochote hata kama kinatawala au kula. Hapa nitaweka mfumo kama wa kaya zilizoendelea na kuhakikisha mfumo huu hauchezewi.
Leo nitaongelea hatua za kiutawala. Bado za kiutendaji kama vile kupambana na ukwepaji kodi, magendo, uzembe, ubabaishaji na maovu mengine kama hayo ambayo yamehalalishwa kwa mlango wa nyuma. Kwa leo sitasema mengi zaidi ya kuwaonyesha walevi nitakavyoikopesha kaya na kuisimamia na kurejesha njuluku zangu.
Leo salamu ni kwa washikaji wangu wa pale Horohoro. Pokea salamu toka kwa mwana wa Adam. 
CHANZO: NIPASHE Juni 14, 2014.

No comments: