How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Saturday, 28 June 2014

Mnagundua gesi na kuongeza kuomba omba

Mlevi alifurahi sana kabla ya furaha kutumbukia nyongo na kuchukia kusikia kuwa Bongo imegundua kisima kingine cha gesi. 
Nasikia kisima hiki kipya kina gesi ipatayo lita trilioni 85 kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya ulaji huu.
Huu ni ulaji mkubwa si mchezo hasa kama ungeangukia kwenye kaya zenye watawala wenye akili na si Matonya na Wakwapuzi kama niwajuwao ingawa sitawataja majina.
Ni Njaa Kaya tupu! Maana gesi hii kama ingegunduliwa kwenye kaya zenye wasimamizi wenye akili zinazochemka, ilitosha kuongeza gesi kwenye uchumi wa kaya husika tofauti na hii yetu ya akina Matonya.
Wakati wakubwa wakituhadaa kuwa kaya ni kapuku, wajanja wachache wanatafuna na kuhomola njuluku kama hawana akili nzuri.
Hii maana yake ni kwamba huu ulaji uliogunduliwa huko baharini utaongeza ulaji kwa walaji wetu wasio na huruma bali roho mbaya na uroho wa fisi kiasi cha kuitwa mafisi na mafisadi.
Katika kutafakari nini cha kutegemea baada ya kugundulika gesi hii inayopaswa kutuvimbisha kiuchumi na kuondoa umatonya, najikuta nikikata tamaa na kutamani ulaji huu usingeguduliwa.
Taarifa za ugunduzi huu wa ulaji mwingine zilinirejesha nyuma hadi nakumbuka maneno ya mheshimiwa Felix Mkosamali niliyemsikia akisema, “Kamati ya Bajeti inalipwa posho ya Sh. 500,000 kila siku, ni kutafuna fedha tu hapa, hakuna kitu, ni kutengeneza rushwa…wanayaita mashirika kukubaliana nayo.”
Kwa wasiojua anachoongelea Mkosamali, nikwamba Kamati ya Bajeti inayoongozwa na mzee wa vijisenti Endru Chenge a.k.a Bilionea wa Uswazi na Jersey inalipwa njuluku kubwa yaani shilingi nusu milioni moja kwa siku kwa kukaa na kupitisha vitu vya ajabu ajabu. Kwa lugha rahisi ni kwamba kamati husika inalipwa shilingi nusu milioni kama posho ya makalio.
Tunatoa ushahidi wote huu kuonyesha kuwa hata kungegunduliwa machimbo ya dola hapa kayani bado tutaendelea kuomba kwa vile tunapenda sana mchezo huu.
Sijui ni laana ya Matonya au Mchonga! Mimi sijui. Watu wanaoonekana wazima kiakili, wanajigeuza majuha na wehu kienyeji hivi na wakiambiwa ukweli wanasema wametukanwa!
Mwakujua kutukanwa au mnataka mtukanwe?
Mtatukanwa tusi gani wakati ninyi wenyewe matusi na yakiitwa matusi mwaitika tena kwa haraka?
Niliposikia kuwa kisima kingine cha gesi kimegunduliwa si nilikwenda kwenye kanywaji kuwapa taarifa walevi habari njema ya ulaji bila kujua ningeshushuka hadi nikome.
Na kweli, nimekoma na kukomaa kiasi cha kuacha kiranga na kiherehere cha kusifia maangamizi yangu na kaya. Baada ya kutoa nyuzi kuwa tumeongeza ulaji kule baharini, si fyatu mmoja aitwaye Mduanzia akasema eti angetamani kingegeuka kuwa kisima cha kinyesi.
Maana, neema ya gesi, anadai haioni zaidi ya kuwa na kadhia na udhia.
Gesi haijachimbwa, wezi wachache wameshakula chao na kuwa mabilionea ghafla bin vu huku wakiongezea na njuluku za Escrow.
Je! tusiohusika hapa tuna chetu kweli? Anayedhani nazusha au kuchochea awaulize akina Njomba pale Ntwala watamwambia.
Awaulize wawekaji wazawa. Watamwambia jinsi ambavyo muungu-mtu mmoja aitwaye profwesa Sosipita Muongo anavyowawekea mtima nyongo huku akihongwa udoho udoho na upuuzi na wezi wa kigeni wanaokuja kuchukua kwa kisingizio cha kuwekeza.
Muongo huyu alivyo muongo wa kweli utamsikia akijisifu ‘nimefanya hili na lile’ wakati hana lolote bali kusaka ngawira.
Sijui na huo uprofwesa aliupataje!
Maana ukiangalia matendo yake na kusikia maneno yake unashindwa kumtofautisha na wale wahuni wa Mwenge, au alighushi?
Baada ya kutangazwa neema ya gesi, nilipiga picha jinsi waishiwa wapenda kula watakavyoichangamkia.
Nilijikuta nikikumbuka maneno ya Mheshimika mwingine aliyestukia ulaji huu wa bila kunawa wala kuomba, ni Pauline Gekul ambaye alinukuliwa akisema, “Kwa miaka 50 tunakusanya kodi na kula tu…tunanong’oneza, tunaongea, lakini serikali haisikii.Shilingi trilioni 3.7 katika bajeti ya shilingi trilioni 19.8 imetengwa kwa ajili ya kula tu, punguzeni chai, maandazi na posho, tudhibiti matumizi yetu.”
Kwa vile gesi imegunduliwa, bila shaka hawa wapenda vitafunwa wataongezewa gesi mwilini.
Maana hii ni neema yao haswa. Ajabu wakiishamaliza kutafuta hivyo vitafunwa na pesa ya watafunwa, wanakwenda eti kuomba pesa ya kuendeshea sirikali ya watafunwa na waliwa!
Nijuacho wapenda vitafunwa watakaposhiba na kuvimbiwa utawasikia wakitoa gesi kuwa kama mambo yao hayataenda watakavyo basi kaya haitatawalika ukiachia mbali kuingia mwituni au geshi kujazwa gesi na kuchukua kaya.
Hivyo, kugunduliwa kwa gesi zaidi ni pigo kwa mlevi ambaye hana gesi wala hatumii gesi zaidi ya bangi.
Heri ingegunduliwa namna ya kuruhusu na kuhalalisha bangi na gongo kidogo tungefaidi na kupumua.
Maana ulevi wa bangi na gongo hauunguzi kama huu wa gesi.
Kuna mlevi alituacha hoi pale aliposema kuwa anawajua waishiwa wengi walioingia mjengoni wakiwa wembamba kama sindano, lakini muda mfupi waliumuka kama vile wanataka kujaa kwenye ramani ya kaya.
Alisema siri ya kuumuka huku si nyingine bali kutafuna vitafunwa na njuluku huku wakijiongezea gesi hadi wengine kushindwa kuhimili uzito wao. Hivyo, kuvumbuliwa kwa gesi zaidi ni balaa kwa walaji hawa ambao bila shaka wengine watapasuka kama siyo kurejesha namba mapema.
Bila shaka na India nayo inashangilia kugunduliwa gesi kwa vile hospitali zake zitapata wateja wa bei mbaya baada ya kula na kutafuna vitafunwa na fweza ya gesi na kuongeza viribatumbo na gesi, au vipi?
Tuache bangi na utani. Ni aibu kiasi gani kwa kaya kugundua gesi nyingi hivi lakini ikaendelea kutembeza bakuli? Je! Tatizo hapa ni mshiko au ‘problems upstairs?’
Kuna kipindi nakumbuka maneno ya mzee Mchonga aliyesema kuwa, ‘Uchumi wanao lakini wanaukalia.’ Jamani acheni kukalia uchumi huku mkiendelea kuliwa na kulana mbali na kutafunwa na kutafunana. 
CHANZO: NIPASHE 

4 comments:

Anonymous said...

malighafi na madini yote yanayopatikana chini ya ardhi hazijawahi kubadilisha maisha ya wa-waafrika Je tatizo ni nini!?

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon,
Tatizo ni waafrika wenyewe hasa utawala wao na jinsi wanavyouabudia kuuhusudu, kuuogopa hata kushirikiana nao katika kujiangamiza kama jamii.

Anonymous said...

Naanza kuelewa kuwa huu ugonjwa wa akili waliokuwa nao mababu zetu waliokuwa wakimbeba mwaarabu mmoja, na gobole wakiwa wameshika wao hili gobole na babu zetu, huku wakimuogopa...!!!...na baadae kuja kuingizwa mkenge na wazungu ambapo kusainishwa mikataba tata. Sababu walikuwa hawana maarifa haya sasa kuandika na kusoma...Je kizazi chetu nacho wanafanya yale yale hivyo naona kuna-kaugonjwa...tukijadili tuu tunaonekana tunatukana ingawa tunaongelea hali halisi.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon una hoja. Mababu zetu hawakuwa vichaa zaidi ya kuuzana kama tunavyouzana sasa. Kimsingi, ni kwamba, licha ya usomi wetu na usasa, hatukujifunza tokana na historia yetu. Mababu zetu walisalitiana kutokana na hofu ya kuvamiana hata kutumikishana wao kwa wao tofauti na sasa ambapo tunauzana si kwa woga wa hivyo bali roho mbaya uroho ujinga na upogo bila kusahau ubinafsi uliokithiri. Kwa wale tulijitambua ndiyo maana tumeamua kupambana kwa kupitia talanta zetu.