BAADA ya kijiwe kunyaka taarifa kuwa kuna mpango wa kununua rada nyingine, kimekaa kama Kamati ya Ukombozi wa Umma kulaani na kupinga ujambazi huu.
Mipawa anaingia akiwa analalamika. “Kusema ule ukweli hali inatisha. Sijui tufanye nini kuondokana na ujambazi huu wa mchana kweupe na kugeuzwa mabunga na mabwege kama yule mhishimiwa aliyejitangaza kuwa bwege?”
Kabla ya kuendelea mzee Maneno anauliza; “Kwani unaongelea ujambazi gani katika kaya ya kijambazi ambapo ripoti za ujambazi ni suala la kawaida?”
“Naongelea huu ujambazi mpya ambapo eti kaya ina mpango wa kununua rada nyingine wakati ile iliyotukwangua mabilioni haijawahi kufanya kazi hata ya kunasa mawimbi ya njiwa.”
Mgosi Machungi aliyekuwa akisoma gazeti la Danganyika as usual anajibu; “Nadhani wangenunua tungui badala ya hiyo mikangafu ya rada. Shamba la baba yangu mzee Shemweta haingii mtu na kuiba hata makakaa, mapaachichi, mafyokisi hata kuchuma bwache, nk’hoko au maeze kwa sababu kumezindikwa na tungui. Hivyo, nashaui na kaya inunue tungui ili kuzindika kaya yetu.”
“Hee Mgosi hizi ndude za kisambachi ni dawa za kienyeji au matunguli yenyewe?” Anadakia Mbwa Mwitu aliyetoka kumpiga bomu Msomi Mkatatamaa.
Mpemba naye hajivungi. Anakwanyua mic. “Yakhe shamba la babako si la bibi au la chizi kama hii kaya. Twaliwa twajiona na hatufurukuti wallahi! Kwanini haya mauzauza na ujambazi hutokea karibu na uchakachuaji uitwao uchaguzi?”
“Yakhe unauliza jibu au swali? Ulitegemea washinde vipi wakati wameharibu kila kitu? Hapa lazima wapige njuluku za kuhonga wale watakaowawezesha kuchakachua na kutuletea mabwege na balaa jingine.” Anajibu Mipawa huku akifunua gazeti.
Kabla ya Mpemba kujibu Mijjinga anachomekea; “Kwanini sirikali imeendelea kulala kitanda kimoja na majambazi waliotuletea mfu rada au mkangafu?”
Kapende aliyekuwa akimaliza kutoa oda ya kahawa kwa wote anakwanyua mic. “Kwanini tusiwakamate Endru Chengee, Iddy Rashidi na ponjoro Vithilani na kuwanyonga halafu tukawachinja na kuwapa simba mwituni wakamalizia uchafu huu?”
Kanji hataki kuachwa nyuma. Anaramba mic. “Hapana. Mimi kataa. Chinja wunja haki binadamu. Kama nashitaki yeye shitaki, lakini hapana nyonga na chinja na tawanya kwa simba kula yeye.”
Mipawa hakubali, anasema; “Kanji haki za binadamu ni kwa binadamu si kwa wauaji na majambazi kama hawa. Hawa wangekuwa China wangetundikwa shaba tu. Tuache uvivu wa kufikiri kama Tunituni Benny aliyetutukana asijue naye yumo.”
Msomi anaamua kutia guu. “Kama alivyosema Ami pale sisi tunaliwa tukijiona. Huwezi kupoteza dola milioni 40 kwa kaya ambayo mkuu wake hana tofauti na Matonya wengine isipokuwa kuvaa suti kali kali na kupanda pipa kutumia kiasi hiki kwa kununua uchafu unaoendelea kutuozea na asiwajibishwe mtu. It is impossible for sane society. It is possible only for zombies and gawks. Samahani naongea Kikameruni tokana na kuchukia. Maana huu ujambazi unachefua Mungu ajua.”
Msomi anakunywa kahawa yake na kuendelea; “Usishangae kusikia mwaka kesho baada ya uchakachuaji kuambiwa kuwa kuna mpango wa kununua ndege ya rahisi. Kama haitoshi lazima ikulu nayo itafanyiwa ukarabati kwa mabilioni. Hakika Mkapu alituachia legacy chafu ya kijambazi!”
Kabla ya kuendelea, Mchunguliaji anachomekea; “Yote tisa. Kumi nangoja kusikia NGO ya first lady ajaye itaitwaje. Wote huu kweli urithi wa Ben na Ana wa AN&BEN iliyoiba mgodi wetu wa Kiwila.”
Msomi anaendelea huku akiweka ki-Android chake mezani. “Hii kaya imerogwa na aliyeiroga aliishajifia. Maana ukifanya hesabu za haraka utagundua kuwa hatupaswi kuombaomba wala kukopa kopa. Tunafanya hivyo kwa vile tuna akili za kukopa na kuomba bila ulazima. Hebu fikiria ujambazi wa Dola milioni 581 za kununua eti virutubisho na dawa feki, EpA dola milioni 150, Misamaha na utoroshaji wa kodi bilioni mbili, EpA ya juzi milioni 122, rada mkangafu milioni 40, kukarabati ikulu dola kama milioni 20, kashfa ya ndata milioni zaidi 100, uzururaji ughaibuni weka bilioni mbili…” Kabla ya kumaliza Mijjinga anaongeza; “Kaka imetosha sitaki kufa kwa shinikizo la damu.”
Leo Bi Sofi katuletea mgeni kijiweni ambaye jinale ni Bwege. Wala hajivungi anatuonyesha alivyo bwege, anakatua mic. “Acheni chuku. Mnajifanya mabingwa wa kukosoa wenzenu. Acheni ubingwa wa kusema kana kwamba mmeishawahi kuongoza au kukoa kitu chochote. Mambo ya sirikali si rahisi kama mnavyodhani.”
Anajibu Msomi huku akionyesha kudharau mawazo ya Bwege; “Hakuna mambo rahisi kama ya sirikali, hasa kwenye kaya ya mataahira kama hii. Yangekuwa magumu wasanii wangekaa kwenye ulaji miaka kumi? Kama alivyosema Mgosi heri wanunue tunguli ili kuonyesha uhovyo wao na kushindwa.”
Kanji leo kaamua kuwa mbishi kweli kweli. Anakatua mic huku akitabasamu akimuangalia Kanungaembe na kusema; “Mimi hapana unga kono tunguli. Tunguli iko mambo ya zamani dugu zangu.”
Mijjinga hamkawizi. “Kanji hujakosea. Huu mchongo ukipita utasikia gabacholi na kibaka mzaliwa wamepiga njuluku na kuwaacha walevi solemba kama kwenye mkangafu wa rada na dege lenye mafua la rahisi ombaomba. Hukusikia waliokamatwa juzi uwanja wa ndege wakivusha mamilioni ya dola kana kwamba kaya haina mwenyewe?”
“Yote tisa. Hakuna kilichoniacha hoi kama yule bi kizee wa Kinigeria aliyedakwa na bwimbwi hivi karibuni.” Anachomekea Mchunguliaji.
“Nadhani alikamatwa kwa vile hakuwa ima amewahonga njuluku au kwa vile si soap soap vinginevyo hata ngono ingetosha kuacha apitishe zali lake.” Anazoza Mbwa Mwitu.
Mgosi aliyekuwa akisinzia sinzia aliamua kula mic. “Tungui muhimu jamani. Basi kama hawataki kununua tungui wapeekwe kwa mganga wakapepewe ili ubwege na roho ya wizi viwatoke. Hatiwezi kuendeea kuwa mashahidi wa maangamizi yetu. Kia mwaka tunachezewa mahepe kana kwamba hatina akii!”
“Wizi wizi wizi wizi mtupu. Hakuna cha rada wala nini. Heri waagize tunguli toka Mashindei au vipi?” Anatania Mipawa huku akimkata jicho Mgosi.
Kijiwe kikiwa ndiyo kinanoga si likapita shangingi la Andru Chengee. Tokana na msongamano wa mikangafu tulimnyofoa kwenye shangingi na kumshushia kipigo. Kama si ndata kuwahi tungemfanyia kitu mbaya sana jambazi huyu.
Chanzo: Tanzania Daima June 4, 2014.
2 comments:
Lazima inunuliwe mwaka huu kwani hujui Mwakani uchaguzi mkuu
Anon nimekupata usemayo ni kweli. Kwa hiyo tutanunua rada kwa maneno na vitendo ni kuchakachua.
Post a Comment