How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do
Thursday, 26 June 2014
Tunataka uongozi kwa Kinana si uongo – 2
KATIKA makala ya “Tunataka uongozi kwa Kinana si uongo”, niliahidi kumdurusu zaidi Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahaman Kinana, hasa kutokana na matamshi yake yaliyozua utata na kukanganya.
Leo najaribu kumuonyesha kama mpinzani ndani ya CCM aliyemo ndani.
Matamshi mengi ya Kinana, licha ya kutokisaidia chama chake wala yeye, yanaonyesha wazi jinsi anavyofanya kazi ya upinzani ima kwa kujua au kwa kutojua.
Wanaojua mikakati haramu ya siku hizi ya kuusaka urais nchini, wanasema kuwa Kinana anajua anachosema. Wapo wanaokwenda mbali na kumuona kama mtu anayetumikia mabwana wawili kwa makusudi ili litakapoangukia naye awemo. Kwa wajuzi wa mambo wanaojua dhamira fichi ya Kinana hawashangai zaidi ya kushuku kama atafanikiwa.
Wanachoweza kufanya ni kutahadharisha wananchi kuwa waangalifu kwa aina hii ya viongozi wenye sura na ndimi nyingi.
Kinana alikaririwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ayamango, Kata ya Mamire wilayani Babati, mkoani Manyara, akisema; “Lipo tatizo kubwa la serikali kuchukua muda mrefu sana kushughulikia matatizo ya wananchi, jambo hili linasemwa miaka yote, kila siku wananchi wanalalamika, viongozi wapo, watendaji wapo, serikali ipo, lakini hatua hazichukuliwi, naahidi kulifikisha suala hili kwa rais ili tuone tutalitatua vipi.”
Maneno ya Kinana ni ukweli mtupu. Kweli lipo tatizo la serikali, si kuchukua muda mrefu kutatua matatizo ya wananchi, bali kuwa sehemu ya tatizo.
Wananchi wanalalamika, lakini serikali yao haina masikio wala nia ya kuwasikiliza. Kwa kuliona hili, tunampongeza Kinana ingawa ukiangalia sababu na udhati wa kulisema, hastahili pongezi.
Kuonyesha Kinana anavyofanya kazi ya upinzani na hapo hapo ukada wa CCM, hebu angalia maneno yake aliyotamka akiwa Ayamango. Alikaririwa akisema; “Naahidi kulifikisha suala hili kwa rais tuone tutalitatua vipi.” Ya kweli haya?
Haiwezekani serikali hiyo hiyo anayosema Kinana inachukua muda mrefu kutatua matatizo ya wananchi, ipelekewe matatizo yale yale ambayo imeshindwa kuyatatua kwa muda mrefu kama anavyokiri Kinana.
Je, hapa Kinana amesahau au anataka kuwadanganya wananchi? Inashangaza sana kuona Kinana akitaka kumpelekea rais matatizo ambayo serikali yake imeshindwa kuyatatua kwa muda mrefu. Huku ni kujichanganya hata kuchanganyikiwa.
Anachotaka kufanya Kinana ni sawa na kumpelekea mbwa mfupa ule ule uliomshinda hadi ukamng’oa meno. Tumsaidie Kinana, Kikwete hana historia wala tabia ya kusikiliza wala kutatua matatizo ya watu.
Rejea alivyopelekewa majina ya wauza unga, majambazi na majangili lakini asiwakamate kama alivyokiri mara nyingi kuwa ana majina yao.
Je, Kinana atatenda miujiza gani kumbadilisha mtu wa namna hii? Tunaweza kusema kuwa Kinana amejitahidi kupiga siasa ili aonekane ana uchungu na wananchi, hasa ikizingatiwa kuwa uchaguzi wa rais umekaribia na kila mwenye kuutaka utajiri wa haraka na kulinda maslahi yake anaweza kuuotea hata kama hana sifa, ajenda wala hafai.
Inashangaza kwa Kinana kukiri na kutambua kuwa serikali haitatui matatizo ya wananchi wakati ina kila kitu kuanzia viongozi, watendaji na nyenzo zote halafu ukaipelekea serikali hiyo hiyo matatizo hayo hayo ambayo imeshindwa kuyatatua kwa miaka mingi kama unavyokiri ukaeleweka au kuleta maana zaidi ya kujichanganya hata kuwachanganya wale unaowaambia.
Kufanya hivyo, licha ya kujichanganya ni kudanganya wazi wazi. Huku ni kujipinga ambako ni ushahidi kuwa ima msemaji hajui anachosema au anajua, lakini anaamua kudanganya kwa kuwafanya anaowaambia kama hawana akili sawa sawa.
Maana haiwezekani shetani na malaika wakafanya kazi moja. Serikali imeshindwa kutatua matatizo ya wananchi. Je, dawa yake ni kuipelekea hayo matatizo au kuitimua ili wenye uwezo wa kuyatatua wachukue nafasi yake na kufaya hivyo?
Kinana anajua jibu hata kama anajifanya halioni. Ni mwehu pekee anayeweza kupeleka mtoto kwa mchawi aliyemuua ili amfufue wakati aliishamuua. Je, kuna haja ya kufanya hivyo ili kuendelea kuthibitisha ujuha na wehu wa mhusika au kuchukua hatua mujarabu zenye kuingia akilini na kuwezekana?
Kwa ushauri wa Kinana, kimsingi, ni kwamba anawahimiza wananchi waendelee kutendewa ndivyo sivyo. Anachofanya Kinana ni kutaka “kuwaweka sawa” wananchi ili awatwishe mkenge mwingine kama ambavyo yeye na chama chake wamekuwa wakifanya.
Kuonyesha uhalisia wa utapatapaji wa Kinana na jinsi anavyotumikia mabwana wawili, alikaririwa akisema; “Hii serikali ni ya wananchi, ni lazima iwatumikie wananchi.”
Je, kama kweli serikali ni ya wananchi, kwanini imeshindwa kutatua matatizo yao ilhali ina nyenzo zote kama alivyobainisha Kinana? Jibu la swali hili analo Kinana mwenyewe aliyekaririwa kwenye mkutano huo huo akijipiga mtama kwa kusema; “Nimepita mahali nikaambiwa kuna mgogoro wa ardhi zaidi ya miaka 20 sasa, na mara ya kwanza walikuja mawaziri wanne.”
Hii maana yake ni kwamba wananchi wamemwonyesha wazi wazi Kinana jinsi serikali anayoongelea isivyo ya watu wala yenye uwezo wa kutatua matatizo yao kama anavyokiri kwenye nukuu hii sema hataki kukubali ukweli.
Je, serikali anayoongelea Kinana ni ya wananchi au ya kundi fulani la watu lisilojali hao wananchi kiasi cha kupuuza matatizo yao kwa miaka mingi tu?
Kama kweli hii serikali ni ya wananchi kwa vitendo na si kwa maneno ya majukwaani, kwanini Kinana hataki kujipa kazi kidogo ya kufikiri akajiuliza ilikuwaje ichukue miaka zaidi ya 20 bila kutatua tatizo la wananchi anaowahadaa kuwa ni yao?
Je, hawa wahusika wangekuwa ni kina Kinana wanaowahadaa wananchi, serikali ingewapuuza kwa miaka zaidi ya 20?
Tumalizie kwa nukuu ya Kinana inayosema; “Wakafika wengine nane (mawaziri) na hivi karibuni walikuja 11, lakini hakuna walichokifanya, sasa wanang’ang’ania uongozi wa nini kama hawawezi kutatua kero za wananchi?” Ajabu ya maajabu, Kinana anataka kumpelekea rais aliyewateua na kuwalinda mawaziri hao hao ili atatue matatizo yao yaliyoishinda serikali yake! Ya kweli haya shehe? Tunataka uongozi kwa Kinana si uongo.
Chanzo: Tanzania Daima Juni 25, 2014.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
2 comments:
Huyo mwana porojo hawezi kuacha porojo, hapo tatizo ni hao wasikiliza porojo na kuamini ni maneno yenye ukweli.
Inaonekana walevi wanapenda sana porojo hasa kusifiwa ujinga na kuonyeshwa machozi ya mamba.
Post a Comment