Tunaandika makala
hii kujaribu kutoa ufafanuzi, kama si majibu, kwa makala ya ndugu George Maziku
ya tarehe 18 Juni 2014 kwenye gazeti la Tanzania Daima la Jumatano akijibu
makala ya Mwanakijiji ya tarehe 11 Juni 2004 katika gazeti lile lile. Kutokana
na ufinyu wa nafasi, tutadurusu na kuonyesha udhaifu wa makala ya Maziku japo
kwa ufupi ili kutoa nafasi na kwa wengine watakaotaka kufanya hivyo wafanye
hivyo.
Japo Maziku
anadai alifanya utafiti bila
kuunyesha, alitoa tuhuma za jumla na reja reja bila hata chembe ya ushahidi
unaoingia kichwani dhidi ya, kwanza, watanzania wote, pili, wabunge wa Dar Es
Salaam wote na tatu, Mwanakijiji. Kutokana na makala husika kuwa nyepesi na
yenye kujaa mapofu, dhambi ambayo mwandishi aliwatuhumu wenzake, akairudia,
hatutajibu neno kwa neno (verbatim) zaidi ya kuonyesha baadhi ya mapungufu na
si yote. Maana, kama ni kuijibu makala nzima ipasavyo, unaweza kuandika hata
kitabu. Tutatumia lugha nyepesi ili wahusika wajue wanachofanya siyo na
hawajafanikiwa.
Kwanza, hoja za
Mwanakijiji bado zina mashiko kwa watu wenye utashi na utambuzi wa mambo katika
uhalisia wake. UDA imeuzwa kifisadi na haina tija kwa wakazi wa Dar. Hili liko
wazi tu. Ushahidi? Mosi, rejea maneno ya
mwenyekiti wa Kamati ya
Mashirika ya Umma (POAC) Zitto Kabwe, aliyekaririwa akisema, “Kama kuna watu
ambao wameuziwa chochote wameingia choo cha kike (maana ni batili maana hawana
kibali cha CHC).” Hili halihitaji ufafanuzi. Liko wazi.
Pili, rejea ripoti
ya Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa fedha za serikali (CAG) iliyotolewa hivi
karibuni inasomeka, “Bodi ya
wakurugenzi wa UDA iliendelea na uuzaji wa hisa bila kupata kibali cha Serikali
na hata CHC.” Tatu, rejea tamko la Mei14, 2014 la waziri mdogo wa Fedha na
Uchumi, Adam Malima, aliyeliambia bunge kuwa UDA haijauzwa. Je hawa wote
wanatetea mkate wao na maslahi binafsi? Kama ni hivyo, tungemwomba Maziku na
yeyote m wenye ushahidi atoe.
Pia Maziku,
bila mafanikio amejitahidi kutetea kampuni ya Simon Group na wazawa.Bila hata
tahadhari, Maziku alianza kwa tuhuma dhidi ya watanzania akisema, “Watanzania
ni watu ajabu sana. Mara nyingi wanaweza kutumia nguvu nyingi na muda mwingi
kupigania jambo ambalo hata hawana faida nalo.” Hii si kweli. Watanzania sawa
na watu wengine popote pale duniani ni watu wa kawaida wenye akili na si
mapenzi kibubusa wala kutetea upuuzi hata kama wapo baadhi wanaotetea upuuzi.
Madai kama haya ni mazito. Ni vigumu kuyathibitisha kisomi. Laiti Maziku
angeonyesha “uajabu” wa watanzania tena wote, angeeleweka na hata kuheshimika
ukiachia mbali hoja yake kuleta tija na kuwa na mashiko. Pamoja na Maziku kutoa
tuhuma za ajabu bado hawezi kuitwa mtu wa ajabu zaidi ya mtu asiyejua
anachotetea tokana na kushindwa kuleta ushahidi wenye ithibati na ushawishi
kiakili. Sana sana alichobainisha Maziku kwenye mwanzo wa makala yake ni
kuonyesha hisia za ukabila na unasaba pale na hata kutumiwa anaposema, “wanufaika ni watu
wengine ambao hata hawana nasaba nao.” Kwa mantiki ya haraka ni kwamba Maziku
anajifichua kuwa ana nasaba na Simon Group. Hii haikubaliki. Huwezi kumtetea
mtu kwa sababu ni Msukuma au Mtumbuka mwenzako. Huu ni unepi na ufisadi wa
kiakili.
Ukiachia mbali
na watanzania wote aliowazushia uajabu na hata ulimbukeni wa kutetea wasicho
nacho faida, Maziku amewatuhumu wabunge wa Dar akisema kuwa wanatetea maslahi
binafsi na si taifa bila kutoa ushahidi pale alipoandika, “Bali wanafanya
(baadhi ya watu na wabunge wa Dar) hivyo kwa kusukumwa na maslahi binafsi,
wanatetea mkate wao.” Dai hili ni tata. Huwezi kusema mtu anatetea maslahi
binafsi au mkate wake bila kutaja hayo maslahi ili wasomaji wayajue na
kupitisha hukumu yao kama watu wenye akili na maarifa.
Kimsingi, hoja
anayotaka kujenga Maziku ni kwamba wanaopinga ufisadi katika uuzaji wa UDA wanatetea
maslahi binafsi na ni watumwa wanaotumiwa na wenye kutaka kunyakua UDA. Je yeye
anatetea maslahi ya nani kama si binafsi baada ya kutumiwa? Huu unaweza kutumika kama ushahidi
kimazingira (circumstantial evidence)
wa kujifunga (incupatory evidence)
dhidi ya Maziku kuwa anatumiwa na Simon Group.
Katika kutaka
ku-justify hoja yake nyepesi, Maziku
anaweka mbele uzawa bila kujali haki na kanuni. Je kila mzawa ni wa kuungwa
mkono hata kama anafanya madudu? Kwanini
Maziku hahoji madai kuwa Idd Simba, meya wa Dar Es Salaam, Didace Massaburi na
Victor Milanzi, aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa UDA waligawa shirika la umma kwa
faida binafsi?Sijui kama kweli Maziku anajua jinsi UDA ilivyouzwa kifisadi
chini ya ushawishi wa Simba ambaye anadaiwa kuhongwa shilingi milioni 400? Je Maziku huwa hasomi magazeti
au anafanya makusudi? Mbona wizi na ufisadi uliozunguka uuzaji wa UDA
unajulikana hata kwa wasioishi Tanzania?
Tunachoweza
kusema ni kwamba Simon Group inaendelea kupigiwa kifua na baadhi ya vigogo wa
CCM kama alivyodai mbunge wa Ubungo John Mnyika bila wahusika kukanusha au kutoa
utetezi. Mnyika alikaririwa akiliambia bunge ifuatavyo, “Ni kwa nini watuhumiwa
wameachiwa? Mheshimiwa Spika, haya yasipojibiwa tutaamini kuwa jambo hili
linawahusu vigogo wa CCM na mnawalinda katika ufisadi huu.” Mnyika alikuwa
akishangaa ni kwanini serikali hasa DPP haikuchukua hatua ilhali ripoti ya CAG
ilibaini ufisadi. Si serikali, CCM wala DPP aliyejitokeza kujibu hoja ya
Mnyika. Hii maana yake ni kwamba wahusika wanakiri ukweli wa madai husika.
Kwa vile nafasi
haitoshi, tunaishia hapa tukimshauri Maziku ajitahidi kufanya lau utafiti
kidogo anapojibu hoja nzito kama ya Mwanakijiji. UDA imeuzwa kifisadi atake
asitake. Anayepinga hili aje na ushahidi wenye mashiko badala ya jazba na
kuzulia watu katika kutetea uoza. Huwezi ukatetea uoza eti kwa vile anayeufanya
ni mzawa. Mwandishi makini ni yule anayetetea haki ya wasio na haki na kuwa
sauti ya wasio na sauti (Voice of the voiceless). Kinyume na hili huku nako ni
kutumika kwa aina fulani ambako hakufai kuwa sifa ya mwandishi au mchambuzi.
Mwenyekiti Mao Tse-Tung wa China alizoea kusema, No investigation (research), no right to talk. Kama huna ushahidi
tafitishi huna haki ya kusema.
Chanzo: Dira Juni 2014.
2 comments:
Kama iwapo Simon Group siyo Kampuni ya ubabaishaji. Je kwa nini wasingeanzisha kampuni yao mabasi Dar from the start.
Uzoefu ukiona viongozi wa C.C.M wanatetea sana jambo basi fahamu fika kuwa kuna uozo mkubwa umefanyika katika kuiba mali ya umma.
Huyu Maziku hana tofauti na hao walevi wengine wanaotetea huu wizi na ujambazi unaofanyika kukiwa bado mchana kweupe.
Maziku kumbuka Ulimwengu unabadilika na iwapo njaa ndiyo inayokusababisha kutetea uozo basi elewa hilo suluhisho lako ni kwa ajilia muda mfudpi. Mwanakijiji anazungumzia suluhisho la muda mfupi na mrefu pia.
Watu wote wenye uelewa tosha wanafikiri leo, kesho na keshokutwa siyo kama wewe unafikiri maisha ni leo...husiwe kama wanyama porini, hawalimi lakini wanaishi.
Binadamu tumeumbwa kutatau matatizo na siyo kuleta matatatizo hapa duniani.
Anon umesema vyema. Asante sana naamini ujumbe wako utawafikia walengwa ili waache kufikiri kwa usawa wa pua.
Post a Comment