How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do
Wednesday, 5 November 2014
Katiba mpya tusingoje wananchi wachome Bunge
MWEZI Oktoba unaingia kwenye historia kama mwezi uliofufua matumaini ya kupata haki kwa nchi za kiafrika kusini mwa Jangwa Sahara. Mapinduzi ya umma yaliyomlazimisha imla wa zamani wa Burkina Faso, Blaise Compaore kuachia ngazi baada ya kuifuja nchi hiyo kwa miaka 27 ni jambo la kujivunia.
Pia mapinduzi haya ya umma yana somo kubwa kwa nchi zinazovujwa na watawala wa muda mrefu iwe ni chini ya udikteta wa mtu mmoja na genge lake la walaji au chama fulani.
Bila shaka watawala wetu watakuwa wametia akilini kuwa janja yao imefichuka. Kimsingi, watawala hasa wababaishaji na mafisadi, ni woga wanaotegemea nguvu za jeshi na hila mbali mbali. Compaore, sawa na maimla wengine, alijidanganya kuwa hawezi kuondolewa madarakani. Alifanya alivyotaka asijue arobaini yake ikifika angeondoka tena kama mbwa!
Kwa yaliyojiri Burkina Faso yanapaswa kuwa somo kubwa kwa Tanzania na nchi nyingine ambazo zimefujwa kwa muda mrefu na magenge ya wezi na maimla. Bila shaka, kwa sasa, wale waliohujumu katiba yetu wamo msambweni wakiomba Mungu Watanzania wasizinduke na kurejesha nchi yao mikononi mwao.
Bila shaka, huko Uganda, Zimbabwe, Rwanda, Equatorial Guinea, Gabon, DRC, Mauritania, Gambia, Lesotho, Swaziland, Msumbiji , Eritrea na Morocco wapo wanaweweseka wasijue la kufanya.
Kwa Tanzania ni wazi kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) sawa na Frelimo, ANC na SWAPO wamo msambweni hasa baada ya vyama tawala kukaa madarakani kwa muda mrefu bila ridhaa ya wananchi na kufanya kila aina ya madudu vikiwekeza kwenye ujinga na woga viliwajaza raia. Ni wazi, hakuna umma wa kondoo wala kuku unaoogopa mchinjaji.
Kwa kuangalia jinsi mchakato wa kuandika Katiba mpya ulivyotekwa na kuvurugwa na CCM, bila shaka, Watanzania wamepata somo kubwa kuwa madaraka ni mali ya umma ambayo ukiamua, mtutu wa bunduki na mabomu ya machozi hayawezi kufua dafu kama ilivyotokea Burkina Faso.
Yalipotokea mapinduzi ya umma Maghreb kwenye nchi za Tunisia, Misri na Libya, watawala wengi walisikika wakisema kuwa hayo hayawezi kuwakuta. Compaore alikuwa miongoni mwao asijue kuwa umma ukiamua hakuna wa kuweza kuuzuia isipokuwa Mwenyezi Mungu pekee.
Yaliyoonekana kutowezekana sasa yamewezekana. Je, watawala wetu wanangoja umma uamshe hasira zake na kuvamia taasisi zinazotumika kuuhujumu? Bila shaka, kama hili litazingatiwa, taasisi ya kwanza kuwa msambweni si nyingine bali Bunge.
Nchini Burkina, Bunge lilitaka kukaa na kubadili katiba ili kumwezesha Compaore kuendelea kuwa madarakani. Haikuwa baada ya umma kuchoshwa na mchezo huu ambao umekuwa ukirudiwa nchini humo na kwingineko barani Afrika.
Waingereza wana msemo kuwa Insanity is doing the same thing over and over again and expecting different results, yaani wendawazimu ni kufanya jambo lile lile tena na tena ukitegemea matokeo tofauti. Watu wa Burkina Faso, sawa na watanzania, walichoshwa na wendawazimu yaani kufanya jambo moja tena na tena ukitegemea matokeo tofauti.
Tanzania, tangu kuingia kwa mfumo wa vyama vingi, imekuwa ikifanya jambo lile lile tena na tena ikitegemea kupata matokea tofauti. Imekuwa ikichachakachua uchaguzi na kufuja raslimali za umma ikitegemea kupata maendeleo na demokrasia.
Compaore kadhalika alifanya hivyo kwa miaka 27 hadi arobaini yake ilipotimu. Watanzania ni zaidi ya Waburkinabe hasa ikizigatiwa kuwa wendawazimu umekuwa ukifayika kwa zaidi ya miaka 50.
Je watajifunza kutoka Burkinabe na kuchukua hatua au kuendelea na wendawazimu wa kufanya jambo lile lile tena na tena yaani kunyamaza wakitegemea miujiza? Nadhani wakati wa kuamka na kurejesha heshima ya umma ni sasa.
Sawa na walivyofanya watu wa Burkina Faso, wahusika wanapaswa kuachana na woga. Kwani wanaowaogopa si chochote wala lolote bali kupe mgongoni mwa ng’ombe. Ng’ombe anakosa nini akimtoa kupe mgongoni mwake na kumsaga saga kwa kwato zake kali?
Je, watanzania hawakabiliwi na hali sawa, na hata saa nyingine zaidi, ya Waburkinabe? Nani anashughulikia ufisadi kwa sasa ambapo pesa ya umma inaibwa kwenye mabenki yetu? Nani anapambana na ufisadi katika mikataba ya uwekezaji uliogeuka uchukuaji na ujambazi wa mchana?
Nani anahangaika kurejesha mabilioni ya shilingi za umma yaliyofichwa ughaibuni? Nani anatoa shinikizo kuwa watuhumiwa wa ufisadi, ujambazi, uvivu, mihadarati na wababaishaji washughulikwe? Je, yote haya yanamuumiza nani zaidi ya umma unaopaswa kujikomboa kwa kuchukua hatua kama walivyofanya wenzao wa Burkina Faso?
Wabunge, hasa wa CCM, wamegeuka mihuri na vijiko vya kuibia mali zetu. Wametumika kupitisha na kubariki kila upuuzi na bado wanaendelea kuitwa waheshimiwa. Wakati wa watanzania kuondokana na woga wa genge tepetevu la walaji umefika.
Badala ya kukaa kwenye vigenge na kujadili kwa mshangao yaliyotokea Burkina, tunapaswa kusimama na kujifunza na kuchukua hatua. Somo kubwa toka Burkina ni kwamba, licha ya umma kuwa wenye madaraka na nchi, una uwezo wa kuamua ni nani atawale na ni katiba gani itumike. Hapa ndipo kitendawili cha katiba mpya kinaweza kuteguliwa tena kwa haraka.
Je, tukisema kuwa watanzania wana kila sababu ya kuingia mitaani na kuhakikisha Bunge halikaliki kupitisha uovu na uhujumu wa katiba tutakuwa tunachochea au kuelekeza ukombozi? Saa ya Ukombozi ni sasa kama ilivyoandikwa kwenye kitabu cha Saa ya Ukombozi ambapo wanakijiji wa Kidhakwa walijikomboa kwa kumtimua mkuu wa mkoa alipokwenda kuuza kijiji chao kwa mwekezaji wa kizungu.
Chanzo: Tanzania Daima leo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
3 comments:
Sisi ni jamii yetu shangaza, hivi karibuni Mzalendo J.S. Warioba kajitokeza kutetea wanyonge kamwe kuungwa mkono siyo na anaowatetea basi hata vyombo vya havikuandika hiyo habari kuna nini hapo!?
Walianza west Africa
Sasa USA kuna tija kwa jamii kwanini uendelee kuongoza
Wabongo ingieni mtaani kwa watatoka tu
Hata kama wamejishika ushoga na wachina
Wachina nao wawekezaji au ni mafisadi , kwao hakuna demokrasi
Anon hapo juu mmnena vyema, tunahitaji kujitambua na kuwashikisha adabu wezi wetu. Hii ya Jaji Warioba ilinisikitisha sana. Natamani nimkamate mhunikama Makonda nimfanyie kitu mbaya hadharani. Wabonge ingieni mitaani. Kwani manyang'au mnaowaogopa si chochote wala lolote bali cowards and con men. Hawawezi kuwaua kwa vile wanajua ICC itamfanyia mtu kitu mbaya. Hivyo hakuna sababu ya kuogopa mambo yamebadilika.
Post a Comment