How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Friday, 28 November 2014

Barua ya wazi kwa wabunge wote


Waheshimiwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano,
Bila kujali itikadi au mafungamano yenu, kwanza nawasalimu kwa jina la ukombozi wa taifa hili.
Pili nawasiliana nanyi kwa njia hii ili kuweza kuwashauri mambo mawili matatu kama raia na mzalendo wa taifa hili. Najua ugumu wa hali mnayokabiliana nayo kwa sasa mnapoelekea kwenye uchaguzi mwakani. Kwa wale wa chama tawala, najua fika mko msambweni hasa wakati huu mnapopaswa kuchagua kati ya taifa na chama.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake wamo msambweni. Wanakabiliwa na kashfa ya escrow ambapo inahusiana na wizi wa  takriban shilingi bilioni 200 hadi 300 zilichotwa  na baadhi ya watendaji mafisi na mafisadi toka wkenye akaunti ya escrow Benki Kuu. Hili halikubaliki. Hili ni kosa la jinai linalopaswa kushughulikiwa kwa kuwashughulikia watuhumiwa kwa mujibu wa sheria na kanuni. Pia hili ni dhambi hasa kwa taifa maskini linaloishi kwa kutegemea kuombaomba na kukopa kopa ingawa baadhi ya wakubwa zetu hawaoni hili zaidi ya kuiba kufuja na kutumbua fedha ya umma maskini.
Hivyo, nawaombeni msome barua hii mkitanguliza uzalendo zaidi ya mafungamano ya kisiasa, kujuana, maslahi binafsi au kulindana. Kashfa ya escrow si ya kwanza kwa taifa letu. Zimepita kashfa nyingine nyingi kama vile EPA, Meremeta, SUKITA, uuzaji wa kijambazi wa mashirika ya umma na utoroshaji wa fedha nje. Muhimu niwakumbushe. Hii si mara ya kwanza kwenu, kama wawakilishi wa wananchi, kukumbana na hali kama hii. Nani mara hii anaweza kusahau ujasiri na uzalendo wenu mliposhughulikia kashfa ya Richmond ambapo mlimlazimisha waziri mkuu na mshirika wa rais mwenye ushawishi na nguvu Edward Lowassa kutema madaraka na ulaji akiwa anavitaka? Lowassa aliondoka akilalamika kuwa hakutendewa haki. Aliona kama ametolewa kafara. Hii maana yake ni kwamba watuhumiwa walikuwa ni zaidi ya Lowassa. Watuhumiwa walikuwa serikali nzima ambayo kwa bahati mbaya hamkuigusa. Mlijiridhisha kwa kuangusha mbuyu mkasahau kuwa mlisaza mingine mingi na mikubwa kiasi cha kutoa fursa ya kurudia mchezo ule ule kwa staili ile  ile. Sasa msikubali kufanya kazi nusu nusu wala kuridhishwa na kuangusha mibuyu miwili mitatu. Fyeka shamba zima lililogeuza nchi yetu kuwa shamba la bibi. Tumechoshwa na kashfa na serikali inayozishiriki badala ya kupambana nazo. Msikubali kugeuzwa mihuri ya kubariki na kuhalalisha jinai ya wizi na uhujumu wa taifa. Kuna kesho na kesho kutwa.
Hata hivyo, wapo wanaoona, pamoja na kazi pevu na adhimu, hamkuangalia chanzo cha tatizo. Hivyo, milishughulikia tawi na kuacha shina na mizizi ya tatizo. Sitaki nionekane nawafundisha kazi au kuwalaumu. Huenda hii ilisababishwa na taarifa mlizopewa pamoja na uzoefu. Kwani kashfa ya Richmond ilikuwa ya kwanza na ya aina yake kuwapambanisha na mihimili mingine.
Kutokana na uzoefu wenu hasa mkijikumbusha mapungufu yaliyotokea wakati wa kushughulikia kashfa ya Richmond, naamini kipindi hiki mtakwenda ndani zaidi na kushughulikia majani, matawi, shina mizizi hata mbegu ya tatizo mnalopambana nalo kama wawakilishi wa watanzania maskini wanaowamini na kuwategemea muwatendee haki.
Niseme wazi. Kashfa ya escrow ni zaidi ya watuhumiwa ambao ni mawaziri Profesa Sospiter Mungo na Saada Mkuya, gavana wa Benki Kuu Profesa Benno Ndullu, Mwanasheria mkuu wa serikali jaji Fredrick Werema katibu wa wazira Eliakim Maswi na mkurugunzi wa Tanesco Felchesmi Mramba . Kashfa hii ni kashfa ya serikali nzima. Hivyo, kama mtadhamiria na kutaka kutenda haki, basi serikali nzima iwajibishwe. Tumesikia fununu kuwa kuna mpango wa kumtoa sadaka waziri mkuu Mizengo Pinda. Je Pinda anatolewa kafara kama nani iwapo wenye serikali wapo na wamekuwa kimya bila kutoa angalau tamko hata miongozo ya jinsi ya kulielekea hili?
Tumewasikia baadhi ya wakubwa wa CCM wakihanikiza mtende haki. Hawa wanasema hivyo ima kuwahadaa kuona kama hawahusiki au kwa kutojua ukubwa wa tatizo au kwa kujua lakini wakatumia janja hii waonekana wanakerwa na ufisadi.
Kumekuwapo na malalamiko mengi toka kwa wananchi wakilaumu hata wabunge wa CCM kuwa nao ni mafisadi. Sasa wakati wa kuwaonyesha wale wanaowatuhumu kwa vile ni wanachama wa CCM ni huu. Wakati wa kusafisha nafasi na nafsi zenu (hasa wabunge wa CCM) ni sasa. Itakuwa jambo la ajabu kama mtatishwa au kuwekwa sawa wakati mkijua fika mnayeweza kumuogopa (rais) anamaliza muda wake na haruhusiwi kugombea kisheria. Hivyo, wenye kuwa msambweni hapa si wengine bali nyinyi wabunge.
Mkienda mbali mkaaangalia hata hawa watuhumiwa, nusu yao ni wateuliwa wasio na imani wala kura ya wananchi. Hivyo, huu mtihani na mzigo wa serikali na chama msikubali kutwishwa nyinyi. Wananchi ni zaidi ya serikali na chama. Tanzania ni zaidi ya chama na serikali. Maisha ya kisiasa si karata bali utendaji. Hata kama tukiyaita karata, mnayo karata kipindi hiki. Msiliangushe taifa wala nyinyi binafsi.
Tumalizie kwa kuwaomba na kuwashauri kuwa badala ya kuhangaika na watuhumiwa wachache ambao kimsingi, ni wateule wa rais na washirika wa kundi kubwa la ufisadi zaidi ya hili, shughulikieni serikali nzima ili angalau muweke historia  ya kuleta ukombozi kupitia uwakilishi wenu. Tusingependa lawama mlizopata tokana na mchango wenu kwenye kuandika katiba mpya ambayo inaonekana wazi kutokuwa ya wananchi ziendelee. Wakati wa kuzifuta na kuwaonyesha wananchi kuwa bado mnawafaa na mnafaa kuchaguliwa tena ni sasa. Hata hivyo, si kwamba nawatisha. Mtakavyomaliza kashfa hii ndiko kutakakoamua hatima yenu kwenye uchaguzi ujao.

Niwatakieni kazi njema, afya tele na mafanikio katika mtihani huu wa kuonyesha au vinginevyo uzalendo au usaliti kwa taifa. SAA YA UKOMBOZI WA KWELI NA KAMILI NI SASA. Mungu ibariki Tanzania. Mungu bariki Bunge letu tukufu. Mungu wabariki wabunge na uwape visheni, maono, ujasiri, uzalendo na ukakamavu. AMINA.
Chanzo: Dira ya Mtanzania

No comments: