How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do
Wednesday, 19 November 2014
Visa vya marais wetu kutibiwa na kufia nje
TAARIFA kuwa Rais Jakaya Kikwete amefanyiwa upasuaji wa tezi dume au busha (Prostate) bila shaka zilistua wengi kama si wote. Wengi hawakujua, ama walifichwa ukweli kuwa Rais anaumwa.
Hawajui ukubwa wa tatizo wala lilipoanza. Wanashangaa Rais kufanyiwa upasuaji. Kwani inaonyesha alishachekiwa na kugundulika ana tatizo. Hivyo, kufanya ahadi na mtaalamu wake aliyetajwa kama Dk. Edward Shaefer wa John Hopkins University, Maryland, Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa zilitolewa na ofisi yake, ni kwamba Rais anasumbuliwa na kinachoonekana kuwa kansa ya kizazi. Kwa jinsi taarifa zilivyotolewa kwa uchache, uwezekano wa mengi kusemwa ni mkubwa. Hata hivyo, sitashangaa kusikia mengi hasa ikizingatiwa kuwa viongozi wetu huficha maradhi kana kwamba wao si binadamu wanaougua hata kufa.
Kuumwa ni kitu cha kawaida kwa mwanadamu ila kwa watawala wetu ambao wanajiona si wanadamu hii si saizi yao hadi yawakute ya kuwakuta. Tulidhani wangejifunza tokana na kifo cha baba wa taifa, Mwl Julius Nyerere ambaye wasaidizi wake waliufanya ugonjwa wake na kuufanya siri kubwa bila sababu zozote za msingi. Je watawala wetu na wapambe na waramba viatu wao watajifunza lini kuwa wawazi na wakweli?
Hivi karibuni taifa jirani la Zambia lilimpoteza Rais wake, marehemu Michael Chilufya Sata baada ya kuficha ugonjwa wake kwa muda mrefu hata kufikia kutishia kuwafunga wale walioonyesha shaka juu ya afya yake.
Mficha maradhi kilio humfichua. Kwani muda haukupita mauti yakafichua walichokuwa wakificha wenzetu wa Zambia. Kuhusu taarifa za Kikwete kufanyiwa upasuaji ni ukweli kuwa inashangaza kuwa watanzania hadi sasa hawajui ungonjwa anaoumwa ni upi na ulianza au kugundulika lini na wapi.
Kwanini wanatuficha hivi wakati mhusika ni kiongozi wetu anayetibiwa kwa kodi zetu? Kukoleza mambo taarifa zenyewe zimetolewa kwa lugha nyepesi bila kueleza hata historia ya masahibu yake.
Hata hivyo, tunamtakia siha njema. Apone haraka ila tunawalaumu wasaidizi wake kuficha ugonjwa. Tusingeomba haya yaikute Tanzania. Maana, kwa wanaojua historia ya ziara za mara kwa mara za Kikwete nje, inaaweza kujengeka dhana kuwa alikuwa anaumwa kwa muda mrefu. Wapo wanaoamini kuwa ziara za Kikwete huku na kule ni kupambana na gonjwa ambalo hataki kuliweka wazi.
Pamoja na kuwa stahiki yake kutibiwa popote, wengi wanahoji ni lini watawala wetu wataimarisha huduma za afya nchini ili watibiwe hata kufia nyumbani? Wamehujumu na kuvuruga huduma za jamii.
Wanapougua, hata kutaka kupima mafua, hukimbilia Ulaya. Huu ni ubinafsi hata kama unatendwa na wakubwa. Tunapoandika Muhimbili ni nusu kaputi kihuduma. Nani mara hii kasahau kashfa ya hivi karibuni ambayo nayo imefutikwa chini ya busati ya chuo cha International Medical and Technology University (IMTU) kutupa mabaki ya miili ya binadamu kwenye mashimo ya kuchimba mchanga baada ya incinerator ya Muhimbili kuharibika kwa muda mrefu?
Nani hajui kuwa baadhi ya viongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wametuhumiwa kusambaza na kuuza madawa feki kama alivyofichuliwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida?
Je, amechukuliwa hatua gani zaidi ya kukingiwa kifua na wenzake wanaokimbilia Ulaya kupima mafua na kuacha watanzania waendelee kuteketea kwa magonjwa yanayoweza kuzuilika na kutibiwa nyumbani?
Je, Kikwete aligunduliwa lini na tatizo lake la tezi dume? Je, ahadi ya kukutana na mtaalamu (daktari wake) iliwekwa lini? Je, tatizo la Kikwete lina ukubwa gani? Haya ni maswali yanayojirudia sana.
Kuna haja ya kuweka wazi historia ya tatizo la Kikwete ili wananchi wajue. Kwanini walipie gharama zote za matibabu ya Rais wakati wamefichwa kinachomsibu? Rais si mtu binafsi kiasi cha kuficha hali yake ya kiafya. Kuendelea kuficha maradhi ya Rais si kumtendea haki wala watu wake.
Tunadhani wakati wa watawala wetu kubadilika na kututendea haki kama watu wenye akili sawa sawa umefika. Kitendo cha kuendelea kukimbilia kutibiwa na kuangaliwa afya zao nje tena wakifanya siri kinawafichua kama watu wasiofaa kuwa viongozi. Kinaonyesha walivyoshindwa vibaya sana na wapo madarakani kwa manufaa binafsi. Haiwezekani kila mwaka viongozi wa Afrika waletwe maiti toka nje. Je, Afrika itajitegemea lini?
Hata hivyo, nchi ya Afrika Kusini imeonyesha mfano mzuri. Rejea jinsi baba wa taifa lile, Mzee Nelson Mandela alivyofia nchini mwake. Huu ni mfano wa kuigwa na ni suto kubwa tu kwa watawala wetu wanaojiangalia wao wenyewe na familia na marafiki zao huku umma ukiendelea kuteketea. Haya ndiyo maisha bora aliyowaahidi watanzania Kikwete? Kwanini roho zao haziwasuti kwa tabia hii ya mauaji ya halaiki barani Afrika?
Kuna haja ya watanzania kushinikiza walioficha maradhi ya Rais wawajibishwe mara moja ili liwe somo kwa wengine watakaofuata. Maana tumechoshwa na tabia hii ya kutawaliwa na miungu watu isiyougua wala kustahiki kutibiwa nyumbani.
Wanachofanya ni sawa na mama ntilie mmoja aliyepika chakula akawauzia wateja huku akiagiza chakula chake hotelini. Mama ntilie wa namna hii ni wa kususwa na kusitishwa kutoa huduma kwa umma. Maana hana udhu wala utu wa kuweza kufanya hivyo.
Chanzo: Tanzania Daima leo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment