Kutokana na
urafiki na udugu wa Mlevi na marehemu Thomas Isidore Sankara, Rais wa
zamani wa Burkina Faso wiki iliyopita
Mlevi aliamuru kwenda kutia timu kule Burkina ili kutia shime mapinduzi
matakatifu ambapo ‘muimla’ wa muda mrefu wa kaya hii Blaise Compaore aka
‘Ebola’ aliangushwa.
Mbuyu huu ulipigwa chini fasta kwa nguvu ya walevi
kayani humo.Walevi wa Burkina hawana mchezo na mafisi na mafisadi. Walimtimua
Compaore na kuwagomea ndata kuchukua ulaji wao.
Hivyo, ninapoandika nafanya hivyo toka Ouaga kama
wanavyopenda kuita mji wao mkuu Ouagadougou ukikosekana Wagadugu.
Nimefikia mitaa ya Avenue de Capitaine Thomas
Sankara karibu na Lycee Phillipe Zinda Kabore kwenye mtaa maarufu wa Rue
Nongremasson yaliko makutano na Ave de la Liberte kwenye hoteli ya Le Pavillon
Vert. Naona yule anacheka akidhani hizi ni kamba.
Si kamba
hata kama sitanui na bi mkubwa wangu kwa kodi za walevi, bado ninao uchache wa
kusafiria kwenda kufanya mapinduzi ili liwe somo kwa walevi wa kaya yetu.
Kwa vile
kilichokuwa kikiwakumba walevi wa taifa hili wanaoitwa “Burkinabe” kama ambavyo
sisi tunaitwa Watanzania ni kile kile kinachowasibu walevi wa kayani mwetu.
Mlevi
amekwenda kule kupiga shule na siyo kupewa uprofesa wa kuchunga mbuzi kama wale
wengine walioogopa umande wakaua elimu na kutukuza ufisadi. Mlevi licha ya kuwa
msomi wa kweli, husaka elimu kila inapopatikana huku akichangia kwa kutoa elimu
aliyo nayo kuhusiana na suala zima la ukombozi.
Pili mlevi alikwenda kwa Wa-Burkinabe kuwafariji
ndugu wa marehemu Sankara na kuwapongeza kwa kuishinda Ebola ya kisiasa
iliyokuwa ikiwatafuna kwa miaka 27.
Nina mpango wa kuonana na Mariam Sankara (mjane wa
marehemu) vitegemezi vyake Phillipe na Auguste kule Ufaransa baada ya kuzuru
makaburi ya Thomas mwenyewe hapa Ouaga na baadaye makaburi ya Margueriete
Sankara na Sambo Joseph Sankara huko Yako kijiji alikozaliwa Sankara.
Katika ziara yangu ya Burkina niligundua yafuatayo:
Mosi, ukweli kuwa madaraka siku zote ni mali ya
walevi sema walevi wenyewe huwa hawalitambui hili na kama wakilitambua
wanajificha kwenye woga. Jamani, msiogope tena.
Kwani kiboko ya wakandamizaji na wauawaji wa waandamanaji kwa sasa yaani
International Criminal Court (ICC) hailali ikiwatazama na kuwasaka wanaojaribu kuwaua
waandamanaji.
Mnadhani Compaore alivyokuwa na roho mbaya
alishindwa kuamrisha mbwa wake kuwasagasaga waandamanaji? Alitaka sana. Ila
alipokumbuka hili dude liitwalo ICC alinywea na kuamua kutoka baruti kama mbwa
aliyeiba mafuta.
Pili niligudua kuwa watawala hasa vidhabi wezi na
mafisadi, licha ya kuwa wababaishaji na wenye kutishatisha hawajiamini. Ni woga kuliko hata kichanga. Rejea Compaore
na genge lake la majambazi walivyotoka nduki wasijue hata waendako bado
wanaweza kunyofolewa na kuishia lupango kule the Hague.
Baada ya kuongea na upinzani nchini Burkina,
niliwashauri wamshitaki kwa mauaji ya Sankara na wengine wengi aliowaua kama vile mwandishi na rafiki yangu
Norbet Zongo aliyefichua mauaji na utoaji wa kafara wa mazeruzeru aliofanya
akimtumia ndugu yake Fancois Compaore aliyekuwa mshauri wake wa uchumi wakati
ni kihiyo. Tatu, niligundua kuwa walevi wakichoka husema, “Sasa imetosha na
liwalo na liwe.” Wakifikia hapa, hakuna risasi, mabomu ya machozi wala vipigo
vinaweza kuwanyamazisha.
Nne, niligundua kuwa hata Bongolalaland aka
Danganyika wana haja ya kulianzisha hasa wakati huu ambapo wamepokwa katiba yao
na manyang’au yanayotetea uoza na ufisadi. Hivyo, jamani nasisitiza msiogope
njia iko wazi kujiletea mabadiliko na mapinduzi ya kweli.
Saa ya ukombozi ni sasa. Tano, niligundua kuwa
watawala siku zote wanatumia hila, longolongo na gilba, ukiwashupalia wanatoka
nduki na kuacha kitu kwa walevi. Ila hapa kuna tahadhari. Mnapoamua kuwapiga
chini wezi na watesi wenu, msiruhusu ndata kudandia na kupora ulaji kama
ilivyotokea Masri ambapo ndata walichukua ulaji na kuandaa uchaguzi feki na
kutwaa maulaji. Burkina walilikataa hili wazi wazi. Nanyi msikubali hili
litokee.
Power is for boozers not ndatas or ndutus.
Tumeelewana?
Katika uchunguzi upembuzi wangu wa kilevi,
niligundua kuwa Compaore alifanya makosa yafuatayo:
Kwanza, kama wasaliti wetu walivyomsaliti mzee
Mchonga, alisaliti mapinduzi matakatifu yaliyoongozwa na kamanda Thomas Sankara
(Mungu aiweke mahali pema peponi roho yake).
Pili, alimuua Sankara mkombozi na nabii aliyekuwa
ameahidiwa kuwakomboa Wabukinabe.Tatu, alikaa madarakani muda mrefu akiifuja
kaya ya Burkina bila kujua kuwa mwisho wake ungefika.
Nne, hakusoma alama za nyakati sawa na wezi na
mafisi na mafisadi wetu ambao hutumia madaraka kama kijiko kikubwa cha kuchotea
utajiri wa walevi maskini asijue siku wakikengeuka wataipatapata fresh.
Tano, Compaore alijisahau na kujiona muungu mtu
sawa na miungu wetu wanaofuja ulaji wetu wakigawana na kula kwa miguu na mikono
bila kuomba wala kunawa.
Hata kama Compaore alibahatika kupewa upenyo na
waramba makalio yake na kutimkia Cote d’ Ivoire, kuna siku watamtia nguvuni ili
alipie madhambi yake hapa hapa duniani.
Wengi tulitamani yamkute yaliyomkuta Muamar Gaddafi
ila aliponea chupu chupu. Kutokana na nilichoshuhudia Burkina, naweza kutabiti
kwa kinywa kipana kuwa akina Compaore aka Ebola waliosalia barani kwetu watie
maji baada ya mwenzao kunyolewa.
Wale ving’ang’anizi wawe wetu au magenge yaitwayo
vyama waliong’ang’ania ulaji huku wakiwaibia na kuwahujumu walevi wakae mkao wa
kuliwa na si kula. Hatuwezi kuendelea kutenzwa kama mataahira na hayawani.
Tuna akili na nguvu ya kujitambua na kuwatambua na
kuwafurusha wezi wetu wanaotutapeli kwa kujionyesha wana nguvu wakati si
chochote si lolote. Akina EPA, Kagodam, Richmonduli, Escrew na majambazi
wengine wakae mkao wa kuliwa tu watake wasitake.
Mwisho, kwa uchambuzi huu mfupi wa safari yangu ya
Burkina naamini walevi watatia akilini na kuona mwanga kuwa wakiamua wanaweza
hata leo kuondoa wale wanaowaibia na kuwatenza kama mabunga na mataahira. Kwa
ufupi hiyo ndiyo ilikuwa safari yangu ya kujifunza na kufundisha ukombozi kwa
walevi. SAA YA UKOMBOZI NI SASA. Haya shime walevi amkeni mjikomboe kweli
kweli. Bye bye from Ouaga Burkina.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment