BAADA ya udaktari na uprofesa kugawiwa kama njugu hasa kwa matepeli
na wasaka sifa wanaotapeliana na kugeuzana mabunga, wana kijiwe kwa vile
wana sifa kuliko wengi wa wanaopewa vitu hivi, nao wameamua kujipa
uprofesa. Baada ya kusukuti na kukubaliana, uprofesa utagawiwa kama
ifuatavyo:
Profesa Emeritus wamepewa Alhaj, Mtukufu, Luteni Kanali, ndugu,
Mheshimiwa, Field Marshal Dk. Mpayukaji Msemahovyo na Dk. Msomi Mkata
Tamaa. Full Profesa imekwanda kwa Dk. Mijjinga wa Shedi, Dk. Kapende wa
na Dk. Mgosi Machungi.
Associate profesa ni Dk. Mpemba Ami, Dk. Maneno, Dk. Mchunguliaji na
Dk. Mbwa Mwitu Dk. Mheshimiwa Bwege.Wakati Kanji na bi Sofi Lion aka
Kanungaembe wamepewa vyeti vya ushiriki wa kijiwe.
Yote haya yameanza baada ya Mchunguliaji kuingia na kulianzisha akisema, “Wazee mmesikia uprofesa wa kugawiwa kama njugu?”
Kapende anajibu huku akibeua midomo, “Unaongelea huu utapeli wa mchana
kwa wapenda sifa wanaochuuza watu wao kwa zawadi za kipuuzi siyo?”
Mijjinga hangoji Kapende aendelee. Anakula mic, “Mie nimesikia.
Nangoja waramba makalio yake kwenye mitandao waanze kujikomba kwa
kumuita jamaa yangu mchunga mbuzi profesa Njaa Kaya Kiwewe.”
“Pilipili usokula yakuhusu nini kama si wivu na umbea? Hata wakimuita
mtume wewe yakuhusu nini? Mwenye wivu si ajinyonge? Mtake msitake mkuu
ni Profesa hata mkimuita mchunga mbuzi hata mchuna ngozi. Halo halo!” Bi
Sofi Lion aka Kunungaembe anaamua kuwapa vipande vyao wanaomkejeli
muungu wake.
Msomi Mkata Tamaa kutaka kumkatisha tamaa Sofi anang’aka kwa umombo,
“When professorship is offered to wank instead of wonk there is a
problem.”
“Mie hili la waramba viatu wala halinipi taabu. Najiuliza hawa walotoa
huu uprofea alopewa atatoa nini? Maana maisha ya kisasa kula na kulipa
ati.” Mpemba anaamua kukamua mic.
Mbwa Mwitu anajibu haraka, “Vya kuwapa anavyo vingi. Wametoa vya ubongoni kwanini asitoe vya mwilini?”
“Mbwa mitu acha tusi hovyo. Hiyo ya mwili nini? Kwanini tukana vatu bure bwana?” Anachomekea Kanji huku akicheka.
Msomi anarejea, “Mie wapeane vyovyote wapeanavyo mradi viwe vyao
hainihusu. Kasheshe ni pale tutakapoona hawa watoa upuuzi kama uprofesa
kwa wachunga mbuzi na wauza karanga kuja hapa na kuanza kupewa upendeleo
kwenye mambo ya biashara. Hapa patakuwa hapatoshi.”
Mgosi Machungi anatia timu huku akibwia kahawa yake, “Usemayo kwei.
Mambo ya kuhongana upuuzi kama shahada suti au michango kwenye kampuni
ya bi mkubwa yanapaswa kukomeshwa.”
Mzee Maneno anakwanyua mic, “Mtayakomeshaje wakati mmeruhusu katiba mpya kuchakachuliwa?”
Kapende anachomekea,“Nadhani kuchakachua katiba si jibu. Ndiyo maana
kijiwe tulipanga kususia hii kiini macho tunayoambiwa eti ni kura ya
kupitisha au kutopitisha katiba feki.”
Mheshimiwa Bwege anatia timu, “Uprofesa mwingine choo kweli kweli.
Tangu lini mchunga mbuzi na muuza mananasi tena aliyeshirikiana na fisi
kuwararua kondoo anaowachunga akapewa uprofesa?”
Msomi anaongezea,“Kila nikiwaambiwa kuwa shule si kitu ya kuchezea
huwa mnadhani najipa ujiko. Angalia vihiyo wanavyouzimikia hadi wengine
kuwa tayari hata kuwatoa sadaka watu wao ili waonekane wasomi hata kama
ni vihiyo? Anabwia kahawa yake na kuendelea.“Ubaya ni kwamba imefikia
mahali hata watu waliohujumu na kuzika elimu kwenye kaya zao wanapewa
uprofesa. Hii haikubaliki.”
Mzee Kidevu ambaye siku nyingi hakuhudhuria kijiwe anatia timu, “Hebu
tuwe wakweli. Unategemea nini kutoka China. Huoni visimu vyao
vinavyozimika. Nasikia hata vitoto vinavyozaliwa na dada zetu wanaozaa
na wachina vinazimia hovyo hovyo kama vijisimu vya mchina.”
Mpemba anauliza, “Hivi huyo rais wa Uchina akija hapa aweza pewa
ujinga kama huu akaukubali au wapewa hawa wanaodhaniwa hamnazo?”
Mgosi Machungi anapoka mic huku akicheka, “Umetikumbusha kisa cha juzi
pale Kaiakoo nilipoona mchina akichoma mahindi. Eti huyu naye ni
mwekezaji wakati ni mchukuaji na mganga njaa. Hivi mswahili anaweza
kuuza mahindi china wakati wachina hawana ajira wasimnyotoe roho na
walivyo wabaguzi!”
Mheshimiwa Bwege anaamua kurejea tena, “Washangaa wachina kufanya
umachinga kama kuuza mahindi na kusukuma mikokoteni? Kwanini wasifanye
hivo iwapo wachunga mbuzi wanakwenda kule na kufanywa wasomi hata kama
utapeli? Hapa nadhani wahusika wanatapeliana. Huyu anampa mwenzie
dhahabu feki na yule analipa kwa fedha feki. Ngoma droo. Tangulini
uprofesa ukatolewa kama njugu?”
Mpemba ananyaka mic,“Yakhe naona kama uprofesa waanzagawiwa kama njugu
basi nasi wana kijiwe tutambue usomi wetu kwa kuwa maprofesa tokana na
nchango wetu kwenye kupambana na utwahuti kayani mwetu. Mnaonaje hili?”
Mgosi anapokea ngoma na kuweka kifuani na kusema,“Ami tinakubaiana
nawe. Kama wachunga mbuzi wanapewa upoofesa kwanini sisi mapoofesa wa
kwei tisiotambuika tikatambuika japo kidogo?”
“Unashangaa hili? Hukusikia juzi nchini Zimba za Mabwe ambapo bi
mkubwa yaani mke wa jongwe Bob Mugabie alitunukiwa shahada ya uzamizi
baada ya kufanyiwa mtihani na wengine wakati hata shahda ya kwanza hana?
Unadhani kulala kitanda kimoja na bwana mkubwa mchezo? Wengine
wanaondoka na NGO na wengine wanataka warithi hata urais!”
Kijiwe kikiwa kinanoga si msafara wa Prof mchunga goat ukapita. Acha
tumzomee kwa kututia aibu kwa kuhongwa upuuzi mtupu. Muhimu muelewe kuwa
tangia sasa wanakijiwe wote ni maprofesa isipokuwa wale vibaraka na
vidhabi.
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 5, 2014.
No comments:
Post a Comment