How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday 20 May 2015

Kijiwe chamshangaa mzee Pinda


Baada ya Mzee Mizengwe iliyoPinda kuja na mizengwe yake akisema kuwa kaya ilipata mafanikio ndani ya miaka kumi ya jamaa yetu, wanakijiwe wameamua kumpa vipande vyake kuwa asemeyo ni sisasa na usanii tu.
Mpemba anaingia akiwana gazeti la Danganyika Daima lenye kichwa cha habari, “Mzee Mizengwe aainisha mafanikio ya lisirikali na Njaa Kaya.”
Baada ya kuamkua anasema, “Jamani mwaona haya matusi ya wazi ya nguoni ya huyu nzee mwenye Mizengwe ilo-Pinda? Eti asema kuwa kaya imefanikiwa ndani ya miaka kumi ya ufisadi wa kunuka? Huu uongo nkubwa Wallahi.”
Kapende anakwanyua mic, “Ulitegemea aeleze ubovu wa bosi wake? Athubutu aone atakavyopiga kalamu na kuishia hata kupoteza ndoto zake za kuwania urahisi. Kwa sasa kila mtaka urahisi lazima ajigonge kwa jamaa akitegemea aungwe mkono japo jamaa mwenyewe anafahamika alivyo kidhabu si kawaida.”
Msomi Mkatatamaa anaingia kwa fosi na kusema, “Sioni makosa ya spindoctor kama huyu hasa ikizingatiwa kuwa akina Rweyependekeza wameshindwa kiasi cha kumtwisha zigo la kashfa mzee huyu anayeonekana kutumiwa kama nepi.” Anakohoa tokana moshi wa sigara kali anayovuta mzee Maneno kumsumbua na kuendelea, “Nilidhani angeongelea maisha bora kwa wote tuliyoahadiwa zama zile za usanii na utapeli chini ya dhana ya ANGUKA ambayo imemuangusha jamaa kweli kweli.” Anachukua gazeti na kusema, “Tazama rongorongo ya mchana ambapo jamaa anasema eti wachukuaji wameongezeka na kutoa ajira kwa wachovu wapatao laki nane na ushei. Mbona haelezi aina za kazi na kipato chake ukiachia mbali idadi ya wageni walioingizwa chini ya kisingizio cha uwekezaji ambao kimsingi ni uchukuaji?”
Mgosi Machungi aliyekuwa akisoma gazeti anampasia Mchunguliaji na kuguguna mic akisema, “Jamani tikubaiane. Kama kuna maendeeo ambayo huyu Mizengwe anasifia nadhani ni yae ya kuuhusu mafisadi kama wae wa escroo kutawaa kaya kwa muango wa nyuma. Kaya itaendeeaje wakati inaibiwa na kia njuuku inayoingia inapeekwa Uswizi na kwenye fuko la uchakachuaji wa mwezi wa kumi? Wanadhani hatijui uchafu wao hawa?”
Mijjinga aliyekuwa akitikisa kichwa anaamua kula mic, “Mzee Mizengwe aliniacha hoi alipoongelea barabara ambazo si chochote wala lolote bali makaburi ya kuzikia wachovu hata kabla ya wakati wao. Kwa tunaojua jinsi barabara zilivyofinywa ili wakubwa wapate mgao, tunashangaa kuona huu ufisadi nao ukiitwa maendeleo. Laiti angetaja kiasi cha fedha kilichotumika tukalinganisha na ubora wa barabara zenyewe ambazo hazina tofauti na njia za panya ukilinganisha na za majuu. Urongo mwingine ni wa kitoto sana.”
Mipawa anaamua kukwanyua mic hata kabla ya Mijjinga kumaliza pwenti yake, “Nilidhani ataongelea maendeleo ya kukua deni la kaya na kuongezeka wa idadi ya safari alizofanya Vasco da Gama ughaibuni akitangaza kaya.”
Sofia Lion aka Kanungaembe anaamua kukatua mic, “Hivi nyinyi mfanyiwe nini ndiyo mridhike? Hivi haya maendeleo yote kama vile kujenga shule za kata, kujenga barabara ya magari yaendayo kasi jijini na mambo mengine mengi hamuoni kuwa ni maendeleo au lazima mpinge kila kitu?”
Msomi anarejea, “Sofi dadang go tell it to the birds. Mbona hugusii mahospitali ambapo sasa imegeuka fasheni kwa wenye nazo kutibiwa India wakati wasio nazo wakitapeliwa na matapeli wajiitao waganga wa kienyeji ukiachia mbali wachunaji wanaowaahidi miujiza wakati ni upuuzi? Mbona huongelei kutokuwapo usalama na haki za binadamu hasa tokana na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi? Mbona hugusii ufisadi ambapo mafisadi sasa wana lisirikali ndani ya lisirikali la jamaa?”
Kabla ya Msomi kuendelea Kanji anakwapua mic na kusema, “Veve Somi sindilia sana Sofi kwanini hapana ona huruma. Veve nasindilia nasindilia tena kwa guvu yako yote kwanini dugu yangu?”
Kijiwe hakina mbavu hasa kutokana na tafsiri ya kushindilia tena kwa nguvu zake zote. Msomi anajitetea kwa kuigiza lafudhi ya kigabacholi akisema, “Kanji dugu yangu hapana mimi sindilia dada yako. Iko nasindiliwa na ile natetea si mimi dugu yangu. Mimi hapana penda sindilia mtu na kama nasindilia basi nafanya hivyo nyumbani yangu.” Kijiwe hakina mbavu jinsi kigabacholi kinavyobukanywa na waswahili.
Mheshimiwa Bwege anaonekana kutopenda kigabacholi. Hivyo, anakula mic, “Jamani hebu turejee kwenye mada. Mzee Mizengwe ameamua kutuzengua ili wapika kura ya kula wachague genge lake liendelee kuwabamiza mkenge. Cha msingi hapa ni kupanga maandamano ya kupinga kuambiwa urongo mchana kweupe ili kuweka sumu kwenye kitumbua chao.”
Kijiwe kikiwa kinanoga si vijana wa kihuni wakajambishana kiasi cha kumsua mzee Maneno aliyeamka kwenda kuwakabili na kukivuruga!
Chanzo: Tanzania Daima Mei 20, 2015.

No comments: