Hivi karibuni
vyombo vya habari vimetoa ripoti ya uchangiaji wa hoja bungeni kwa wabunge. Kwa
ujumla wabunge wa upinzani wameonyesha kutoa michango mingi tofauti na wale wa
chama tawala. Inashangaza kuona mwakilishi wa wananchi anakaa bungeni kwa miaka
mitano bila kutoa mchongo wowote wala kuuliza swali au kuuliza maswali machache
kana kwamba huko atokako hakuna matatizo. Je wabunge wa namna hii mabubu
wanafaa kurejeshwa tena bungeni wakati hawana cha kufanya kule zaidi ya kupata
posho kwa kukaa kimya bungeni? Je wananchi wanapomchagua mtu awawakilishe
anakwenda kule kuwa sanamu au chachu ya maendeleo kupitia hoja na michango
yake?
Katika makala hii hatutataja majina ya
wabunge waliotajwa ima kwa kuchangia sana au kutofanya hivyo kabisa. Cha msingi,
ni kuwataka wapiga kura wawapime wabunge wao wa sasa kutokana na kazi zao
bungeni na majimboni. Kama mnagundua kuwa kumbe mliyemchagua awawakilishe
aliwakilisha tumbo lake kwa kuvuta posho basi msimrejeshe. Maana kufanya hivyo
kutawachelewesha wakati wenzenu wakipaa.
Kwa wanaojua mantiki ya kuwa na bunge
ili kuwakilisha mawazo ya watawaliwa, bungeni si sehemu ya kulala, kukaa kimya
au kuvuta posho. Bungeni ni uwanja wa vita ya kuwakilisha mawazo na matatizo ya
unaowawakilisha. Ni uwanja wa vita ya maendeleo hoja na michango mbalimbali. Ndiyo
maana wabunge wamepewa uhuru kikatiba kuongelea jambo lolote bila kuchelea
kufikishwa mahakamani.
Hata hivyo, kuna haja ya kudurusu ni
kwanini wabunge wengi hawachangii bungeni. Wapo wanaolala kutokana na kutoiweza
kazi ima kwa ugonjwa, uzee hata kutokuwa na sifa za kuwasemea wenzao. Wengine ni
watoro tu kama alivyobainisha spika wa bunge hivi karibuni aliyekaririwa
akisema, “Kuna wabunge wanatoka na kusafiri bila ruhusa, hivi mkipata ajali
huko mtasemaje?” Ni bahati mbaya spika
hakutaja wanakopenda kusafiri. Hata hivyo, inakuwaje mbunge aage jimboni mwaka
anakwenda bungeni aishie kupanga safari nyingine?
Wananchi hasa wapiga kura wanapaswa
kutatua tatizo la wabunge watoro na mabubu kwa vile wanawafahamu. Wengi wanaweza
kutochangia hata kutoroka bungeni bila woga na badala yake wakahangaika na
kutafuta fedha ya kuhonga wapiga kura ukifika wakati wa uchaguzi. Wananchi wanapaswa
kukataa kununuliwa na kuishia kuwa wahanga wa jinai hii. Wakija na fedha
walizozipata kwa kutumia ubunge na kutumia muda wa bunge kufanya biashara
kuleni na wanyimeni kura hasa ikizingatiwa kura ni siri. Vinginevyo, majimbo
yanayoongoza kuwa na wabunge mabubu wasilaumu mabubu hawa watakaposababisha
waachwe nyuma kimaendeleo. Mbunge ni mshenga wa wananchi kwa serikali. Hpaswi kuwa bubu au kwenda kuupiga usingizi
bungeni kama ambavyo wengi wamewahi kupigwa picha wakiuchapa usingizi bungeni
utadhani bungeni ni nyumba ya kulala wageni. Hawa wanaopenda kulala kama
vichanga wasipewe kura ili wakalale vizuri majumbani mwao badala ya kuangusha
wananchi waliowaamini na kuwapa dhamana ya kuwawakilisha wakaifuja.
Nadhani kitu kingine kinachowapa
wabunge mabubu motisha na kiburi ni ile hali ya kuawa katiba kielelezo
iliyokuwa na vipengele vilivyotaka wananchi wawawajibishe wabunge bila kungoja
ukomo wa vipindi vyao. Laiti wananchi wangejua kuwa vipengele hivi vililenga
kuwakomboa wasingeruhusu kikundi cha watu kuua katiba hii ya ukombozi na
kupandikiziwa ya kifisadi wanayoshawishiwa waipigie kura wakati haina maslahi
kwao bali kwa kikundi cha walaji wachache.
Kimsingi, wabunge mabubu ni zao la
mfumo mbovu wa utawala uliojikita nchini ambapo mtu akishapata cheo anakigeuza
kuwa mali binafsi badala kuwa dhamana. Mtu wa namna hii haogopi chochote kwa
vile anajua wale waliofanya kosa wakampa dhamana hawana ubavu wa kumtimua. Hivyo,
sehemu nzuri ya kutimua wabunge mabubu ni kwenye sanduku la kura. Nadhani
sababu ya wabunge wengi tena wa chama tawala kutochangia ni ile hali ya
kujiamini kuwa chama chao kikiwapitisha kitafanya mambo wapiti kama ilivyotokea
kwenye uchaguzi uliopita hata kama wapiga kura watakuwa wamewakataa. Hii maana
yake ni kwamba wananchi wanapoamini kuwa aliyepitishwa siyo waliyemchagua basi
wamgomee asiapishwe kuwawakilisha. Wananchi wanajua mengi. Wanawajua wabunge
waliopandikizwa na chama baada ya kushindwa kwenye sanduku ya kura. Wanajua jinsi
wabunge wengi wa chama tawala wapo bungeni kutokana na jinai ya uchakachuaji
iliyofanyika kwenye uchaguzi uliopita. Mwaka huu wasiruhusu upuuzi huu
kuendelea kuwahujumu wakiachwa nyuma kimaendeleo. Hivyo, uchaguzi ujao uwe ni
uwanja wa kuwauliza wabunge wao walichofanya cha maana kwa muda waliokaa
bungeni wakipiga usingizi, kutoroka na kugeuka mabubu huku wakivuta posho bila
stahiki.
Hata bila kuandikwa magazetini,
wabunge mabubu na vilaza wanafahamika. Kadhalika wabunge machachari na
wahangaikaji wanajulikana. Wabunge wanaokwenda bungeni kupiga dili kama wale
walioshutumiwa kuomba rushwa serikali za mitaa ili kupitisha mahesabu yao
wanafahamika kwa sura na majina. Wahalifu kama hawa hawapaswi kurejeshwa
bungeni. Na hii ikifanyika, itatoa onyo na somo kwa wengine wanaopanga kwenda
bungeni kuchapa usingizi au kupiga madili.
Tumalizie kwa kuhitimisha kuwa wabunge
mabubu na wavivu wa kujenga, kutoa hoja na kuuliza maswali hawapaswi kurejeshwa
kwenye bunge kwenye uchaguzi ujao. Watakaowarejesha wajilaumu badala ya kulaumu
wale waliowachagua wakijua hawafai hata kuwa wawakilishi wa nyumba kumi.
Chanzo: Dira.
No comments:
Post a Comment