The Chant of Savant

Tuesday 12 May 2015

Kumbe wagombea CCM ni mabilionea!



Hivi karibuni watanzania walishuhudia mashindano ya kuonyesha ukwasi na “upendo” wa wanaopigiwa upata kutoa mgombea wa chama tawala CCM. Mafahari wa tatu kati ya wengine wanaopigiwa upata kuutaka urais kupitia CCM, Mizengo Pinda waziri mkuu wa sasa, Bernard Membe waziri wa mbo ya nchi za nje na Edward Lowassa waziri kuu aliyetimliwa na kashfa ya Richmond walikutana Zanzibar na kuonyesha utajiri wao wakati wa hafla ya kuchangia mfuko wa maendeleo wa mkoa mpya wa CCM wa Magharibi huko Zanzibar
 Hata hivyo, wengi wanashangaa jamaa walivyopata huu utajiri ambao si wa kawaida kwa viwango vya kitanzania ukiachia huu moyo wa kutoa. Kwanini wawe na upendo na moyo wa kutoa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu kama siyo hongo kwa chama ili kiwapitishe? Na kwanini CCM haiwatakishi maelezo ya jinsi walivyochuma huu utajiri? Kweli CCM hii inayopokea na kushabikia fedha zenye kila dalili ya shaka inaweza kuongoza mapambano dhidi ya ufisadi na rushwa? Je watu wenye jeuri ya fedha hii wanatumia, kuweka benki, kuwekeza kiasi gani? Je wana wafadhili wasiotaka kujulikana walioificha nyuma ya “marafiki” wanaowatumia kulinda maslahi yao ya kibiashara au kifedha? Swali muhimu na kubwa linalowasumbua wengi ni uhalali wa fedha husika. Je kama kwenye tukio dogo na moja kama hili wanatoa mamilioni kiasi hiki, kwenye uchaguzi watamwaga mabilioni kiasi gani ili wayarejesheje bila kuiuza nchi? Je tunahitaji rais mwenye jeuri ya fedha au mwenye uchungu na maisha ya wenzake? Nadhani wakati wa wagombea kutaja vyanzo na ukubwa wa utajiri wao umefika ili kuepuka kuendelea kuweka wezi, mafisadi na wasaka tonge ikulu ili waendelee kuichezea na kuiuza nchi yetu.
 Vyombo habari viliripoti kuwa Pinda na marafiki zake kuchangia jumla ya Sh203 milioni. Huku Lowassa, Membe na marafiki zao walichangia jumla ya Sh101.5 milioni. Wengi wanaendelea kushangaa utajiri wa hawa jamaa ambao wanaweza kuunguza mamilioni ya shilingi huku wakijua wazi kuwa atateuliwa mtu mmoja tu kati ya wote wanaotaka kugombea urais. Kimsingi, wanachofanya ni kama kununua tiketi ya bahati nasibu kwa mamilioni bila kuchelea kukosa. Mtu wa namna hii lazima atakuwa na ukwasi si wa kawaida. Je ameupataje? Je hawa wanaotwa marafiki wa vigogo hawa wakisiasa ni akina nani? Wahusika hawataki kutaja wala kuweka mambo wazi.
Wamefanya vizuri kuuonyesha umma wa watanzania ni mafisadi kiasi gani hawa walivyo. Haya mamilioni wanayochanga bila shaka waliyaiba toka kwa watanzania kama siyo kuhongwa wakifanya kazi ya watanzania. Hawafai. Nadhani huu ni ushahidi kuwa kwa sasa CCM haina tena aliye msafi wala mwenye kufaa kuongoza nchi kama tutakuwa wakweli kwa nafsi zetu.
Kwa vile msimu wa kugeuzana mabunga na wasahaulifu umewadia, watanzania wategee vimbwanga kibao ambapo pesa chafu itokanayo na rushwa, mihadarati na ujambazi mwingine itaingizwa kwenye mzunguko kwa njia ya takrima kama hizi tunazoongelea. Wasafishaji hawa wa fedha haramu ima wao au mawakala na wafadhili wao watatumia fursa hii kusafisha fedha yao chafu huku wakijenga mazingira ya kujiweka karibu na watakaopitishwa na kushinda uchaguzi tayari kwa kutengeneza fedha zaidi.
Wanaodhani huu ni uzushi wajiulize swali moja kuu: Kwanini sarafu ya Tanzania huporomoka sana kila unapokaribia na baada ya uchaguzi? Jibu ni simpo. Watawala huamuru ichapishwe fedha nyingi na kuingizwa kwenye mzunguko kinyemela kiasi cha thamani ya shilingi kuporomoka kama inaharisha kama ilivyo sasa. Kwa ushauri tu, wanaotaka kununua au kuuza mali wafanye hivyo kwa sasa. Maana baada ya uchaguzi shilingi itakuwa hoi. Kwa anayetaka kuona mkururo (trajectory) ya sarafu ya Tanzania na namna ambayo imekuwa ikishuka, aangalie thamani yake kila unapokaribia uchaguzi.  Angalieni kuanzia 1985 alipong’atuka Mwalimu Julius Nyerere, 1990, 1995, 2000, 2005 , 2010 na sasa 2015 mtakuta kuwa kila baada ya miaka mitano ima karibu au baada ya uchaguzi sarafu yetu huporomoka ikilinganishwa na dola ya kimarekani.
Hawa wanaomwaga mamilioni ukiwauliza wameyapata wapi hawatakupa jibu. Wapo wanaosema kuwa mishahara yao ya ubunge inawatosha kutoa kiasi kikubwa kama hiki. Si kweli. Kwa watu wanaopenda kupata kuliko kutoa, kama si uchaguzi kuwalazimisha wasingefanya hivyo. Kimsingi, ni kwamba watawala wetu hawako tayari kugusa fedha yao zaidi ya kutaka iongezeke. Hapa tunachoweza kusema ni kwamba wapo watu wachafu hasa wafanya biashara iwe halali au haramu wameishawanunua watu wao ambao nao sasa wanataka kuwanunua watanzania. Kusema eti wanatoa mifukoni mwao hili haliingii akilini. Kama watu wako tayari kutumia magari ya umma huku yao wakiyafungia nyumbani, sijui kama watu wa namna hii wanaweza kutoa hata senti kwenye fedha itokanayo na mishahara yao vinginevyo mishahara yenyewe iwe ile fichi.
Tumalizie kwa kuwataka watanzania hasa wapiga kura kula fedha ya hawa wanaojionyesha wanazo na kisha wasiwapigie kura. Maana wakiwapigia kura watakuwa wamewapa fursa ya kuwauza na kurejesha fedha wanayowahonga sasa maradufu huku wananchi wakiendelea kuteseka kwa umaskini na ukosefu wa huduma bora zaidi zaidi kwa miaka mitano ijayo. Kama watoa fedha chafu hawa wanavyowageuza majuha kwa kutaka kuwatapeli, basi kuleni fedha yao lakini kura yenu msiwape ili wengi wafe kwa ugonjwa wa moyo baada ya uchaguzi.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 13, 2015.

3 comments:

Anonymous said...

Salaam Mwalimu Mhango,
Mwalimu Mhango,wewe na mimi tunakumbuka vizuri sana kwamba wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere kulikua na maadili na miiko ya uongozi kwa viongozi wote wa uma ambao wanalitumikia taifa lao,kwa maadili na miiko ile iliyowekwa na chama cha TANU kupitia Azimio la Arusha ilionekana kama ni kikwazo kikubwa kwa viongozi wenye ubinasi na uroho wa utajiri kwa kupitia kila njia za wizi na ufisadi,matokeo yake vionggozi hao baada ya kuondoka Nyerere madarakani wakaliua Azimio la Arusha. Na kwa kinyemela na kisirisiri bila ya hata wananchi kujua nini kinachoendelea wakaibuka na Azimio la Zanzibar ambalo ndio chanzo cha kuporomoka maadili na miiko yote ya uongozi na ndio mwazo wa nchi yetu kufanywa ni shamba la bibi na viongozi hao wapo madarakani hadi hii leo.Mzee wa RUKHSA bila ya kuona haya akaja na machozi ya mamba kwa kudai eti Azimio la Arusha halijakufa!!!je ni unafiki wa kisiasa au dhamira zao zinawasuta kila wakilisoma Azimio la Arusha?Na kama ni kweli Azimio la Arusha halijakufa kwa nini viongozi hao wa CCM ambao ni chimbuka la TANU, ambao wengi wao ni wezi,mafisadi na wanaoshirikiana na mapepari wa kimagharibi au hata wa kichina kujitajirisha wao familia zao na marafiki zao wamelitupilia mbali Azimio la Arusha na kulikumbatia kwa nguvu zao zote Azimio la Zanzibar?Na hata kudiriki kuyatupilia mbali maoni ya wananchi ya rasimu ya katiba mpya ya maadili na miiko ya uongozi ambayo inaelewana na ile ya Azimio la Arusha?
Kwa nini Mwalimu Mhango machango wa wananchi kama huu utupiliwe mbali katika rasimu ya katiba yetu?Ebu na tusome maoni hayo ya wananchi kama yafuatavyo katika rasimu hiyo:
"kiongozi wa umma hatopaswa kutoa au kupokea rushwa, kiongozi wa umma hatopaswa kujilimbikizia mali kinyume cha sheria, na pia kwamba kiongozi wa umma hatopaswa kutumia wadhifa, nafasi au cheo chake kwa manufaa yake binafsi, familia yake, ndugu, jamaa au marafiki zake au mtu yeyote aliye na uhusiano naye wa karibu."
Mwalimu Mhango,kutupiliwa mbali kwa maoni haya ya wananchi ni wazi kabisa kwamba viongozi wa CCM wanataka kutueleza kwamba nchi ni mali yao binafsi na hawategemei kwamba wataondoka madarakani kamwe, kwa hiyo katiba ni lazima iwalinde wao na iende kwa masilahi yao wao,familia zao,marafiki wao na mabepari wa nje!!!!

Anonymous said...

Mwalimu Mhango,-naendelea- kama tunavyojua wazi kwamba nchi zote zilikomaa kidemokrasia zina maadili na miiko ya uongozi na ukiukwaji wa maadili na miiko hiyo ni lazima uachie ofisi hata kama ulivuta bangi ulipokuwa shule ya msingi au sekondari!!!.Na tunaelewa wazi kwamba kwa viongozi wanaotaka kuja madarakani au wanasiasa ambao wanagombea nafasi ya juu ikiwa urais au wakuu wa mikoa kama vile nchi ya Marekani ni lazima kwa mwanasiasa huyo au kiongoozi huyo awe tajiri na kuwa tajiri sio tatizo isipokuwa watu wanataka kujua chanzo cha asili ya utajiri wako kinatoka na nini na wapi.Hili linakuwa halina mjadala na hata kueleweka kwa kiongozi huyo au mwanasiasa huyo kama analipa kodi yake kama inavyopaswa kwa serikali na kufeli kulipa kodi kwa serikali ni moja ya kosa kubwa ambalo linaweza kumpeleka mwanasiasa huyo jela na kupoteza nafasi yake ya kisiasa nchini.
Katika siasa tunaelewa wazi kwamba kuna makundi mbali mbali ya mibing'inyo,manufaa na masilahi ambayo yanawaunga mkono wanasiasa hao wanaopigania ngazi ya juu na michango yao inajulikana wazi na wala hakuna kinachojificha kwa kuwaunga kwao mkono kwa pesa na kwa kujitolea kwa ushiriki wa watu katika kupiga kampeni zao.Hili linajulikana pia,
sasa kwa hii hali ambayo inayotokea katika nchi yetu ya wanasiasa wetu kutojulikana chanzo cha utajiri wao na kutojulikana kwa wafadhili wao na mambo kwenda kimya kimya na kienyejienyeji kwa kututanulia misuli ya kutuonyesha utajiri wa halali na haramu kana kwamba wanachangia harusi au maulidi ni kutuona na kutuchukulia sisi wananchi kama watoto wadogo wa kupewa peremende tu na tutawachekelea tu kila baada ya miaka mitano.Lilokuwa wazi kwa wakati wetu huu wa sasa wa UBEPARI kuwa utajiri au ubilionea sio dhambi,isipokuwa dhambi kubwa ni kwa watu kutojua wapi umeupatia utajiri wako au ubilionea wako .Hali hii inatakiwa ikabiliwe kwa umakini sana kwa nguvu zote za wananchi hususa vyama vya upinzani vikifanikiwa kuja madarakani tunataka mtusafishie nchi yetu.
Mwalimu Mhango,ushauri wako na nasaha yako kwa wananchi hapa ni mahala pake kabisa katika kupambana na majambazikama haya ya kisiasa katika nchi yetu pale ulipomalizia makala yako kwa kusema.........Tumalizie kwa kuwataka watanzania hasa wapiga kura kula fedha ya hawa wanaojionyesha wanazo na kisha wasiwapigie kura. Maana wakiwapigia kura watakuwa wamewapa fursa ya kuwauza na kurejesha fedha wanayowahonga sasa maradufu huku wananchi wakiendelea kuteseka kwa umaskini na ukosefu wa huduma bora zaidi zaidi kwa miaka mitano ijayo."

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon usemacho ni kweli kuwa Azimio la Arusha lilliuawa na Azimio la Kijambazi la Zanzibar jambo ambalo lilimuudhi mwalimu Nyerere hadi akamwita John Malecela mhuni. Wengi walishangaa ni kwanini Nyerere alimshambulia Malecela na si Mwinyi. Ukweli ni kwamba Mwalimu alijua kuwa uwezo wa Mwinyi wa kufikiri ni mdogo ikilinganishwa na Malecela. Hivyo, baada ya kuua miiko ya maadili walianzisha madili badala yake. Wanaiba wanavyotaka na kufuja wapendavyo kwa vile hakuna sheria ya kuwabana.
Nchi za kidemokrasia zina miiko ya maadili lakini si nchi za kifisadi. Hata hizo nchi ni wanafiki kwani ndio wanaoziwezesha serikali zetu za kishenzi na kiwizi kuwa madarakani kwa kuwapa mikopo ambayo huishia kufichwa kwenye mabenki yao na kutengeneza ajira kwa watu wao. Ili kujiondoa na kadhia hii wananchi wanapaswa kkuacha kuibiana au kutapeliana bali wawakabili viongozi. Kuna kipindi naona kama majambazi wanajitahidi kuleta mapinduzi kwa njia ya kuwaibia walio nazo ambao wengi wamezipata kiharamu. Hata hivyo hii si njia sahihi. Njia sahihi ni wananchi kuidai nchi yao tena kwa nguvu hata kama ni kwa kumwaga damu. Naona muda umeniishia kwa vile naandaa makala za wiki ijayo. Kwa machache hayo naamini nimegusia japo hoja yako ya msingi ya maadili ya madili na unafiki wa watawala wetu. Juzi ulimsikia Kikwee akisema kuwa akistaafu atajishughulisha na utunzaji wa wanyama wakati ndiye huyo huyo aliyewauza wakiwa hai kwenda Uarabuni sawa na mwinyi alivyouza Loliondo akishirikiana na jambazi Ndolanga.