Baada ya jamaa mmoja mzalendo mwenye uchungu na kaya kum-SMS muishiwa rahis na kusimamishwa kazi kwa kosa la “kuwasiliana” na rahis wake aliyemchagua kwa kura yake, Mlevi nimeamua kuwasiliana rahis. Kama mbaya mbaya. Kwanza, kwangu si kosa kuwasiliana na rahis. Pili, sijaajiriwa na ngurumbili yeyote. Tatu, ngurumbili tena Songombwingo hawanitishi wala siwajali. Nne, sipendi kujigonga na kujipendekeza kwa ngurumbili awe na madaraka au mchicha. Sana sana huwa napayuka ukweli bila kujali nani ataumia, kununa au kujinyotoa roho. Kwangu, fisadi akijinyotoa au kunyotolewa roho ni sherehe kwenda mbele. Fyatu kama nilivyo, nitajali nini iwapo mafisi na mafisadi yamenifikisha hapa kiasi cha kuishi kwa kutegemea bangi na gongo ili kukwepa kunyotolewa roho na mawazo na hasira za kunyonywa na kugeuzwa asusa huku kaya yangu ikigeuzwa shamba la bibi la mafisi na mafisadi, vinyamkera na songombwingo?
Ngoja nirejee kwenye kisa cha aibu na ghadhabu kilichotekea kule kwa akina Meku ambapo njemba moja iitwayo Poo Mhumbahumba imepewa notisi ya kusimamishwa kazi baada ya ikuu kuichoma kwa kufichua mawasiliano yake ya kuripoti ufisadi kwa big. Kwanza, wanamuonea na kumgwaya. Pili, inaonekana hata mkuu anapenda sana rushwa na ufisadi kiasi cha kushindwa kumpa tafu jamaa huyu asiyependa ufisadi na jinai. Ningekuwa mimi ndiyo big mwenyewe hawa waliomsimamisha kazi mtu mwema kama huyu ningewapiga kalamu na baada ya hapo kuwatupa lupango ili liwe somo kwa wengine wenye viherehere na mawazo mfu na mgando ya kifisadi.
Baada ya Mhumba’ kupigwa chini bila utetezi, nimegundua kuwa kumbe kwenye kaya ya kifisadi ukifichua ufisadi ujue umekwisha! Sasa huyu –kama amepatilizwa kwa kuripoti wizi wa kishenzi wa shilingi mbili –angefichua madude kama escrow angekuwa mgeni wa nani kama siyo kum-Kibanda au kum-Ulimboka? Do you remember these guys and those who tortured them to end up being promoted for that? Wamenikumbusha ushenzi wa wakati wa utawala kidhabi wa Ruxa ambapo mchonga maneno mwenzangu Stan Katabaro alifichua kashfa ya Loliyondo na kunyotelewa roho.
Kwa vile mimi ni kidume kisichoongopa lolote, basi kesho nambeep rahis na baadaye namtweet kisha namtuwangia kumkumbusha aingilie kati kwenye kashfa hii ya Keisiemusii. Haiwezekani mtu mwema aripoti uhalifu halafu afanyiwe kitu mbaya kama kile ambacho mbunge wa Kaagwe ameahidi kumfanyia mkuu wa wilaya hiyo kwa kushirikiana na wahamiaji huku akiwageuza wananchi wahamiaji na wahamiaji wananchi. Tamaa nyingine bwana. Yaani kuu zima la wilaya linajigonga kwa wageni na kuhongwa kiasi cha kusahau kuwa kaya hii ni ya wanakaya. Darling Rwega upo hapa? Kwanini unafwanya mambo ya hovyo hivyo au nawe ni mhamiaji aliyechimbia kayani na kupewa ulaji kama mwenyekiti wa zamani wa mkoa huo aliyegundulika kuwa kumbe ni Mrwanda? Shame on you and all those who are turning a blind eye on you. Hata kama Blunders amefanya blunders zake kama vile kudaiwa kunyang’anya ardhi ya umma na kusimikwa uhishimiwa na Jose Makamba kinyume cha sheria, unadhani anayosema ni urongo? Hivi huyu Rose Kiringini anayekutetea umemtuma au ni shoga yako mnayekula pamoja? Kunani hadi bi huyu atake kuzichapa na Blunders kwa sababu ya blunders zako? Umempa nini huyu Rose hadi anapagawa na kupapatika hivi my friend nshomile Rwega?
Kwa vile nimeamua kumtweet na kumbeep rahis, nasema wazi asipokuwajibisha basi nitawahamasisha walevi wa huko wakushughulikie maana huna maana hadi unawakingia kifua wahamiaji tena haramu. Je wanakupa nini hicho kinachokuchanganya kiasi cha kuwasahau walevi na wachovu wenye kaya dadangu?
Ngoja nimtweet rahis na tweet nyingine. Mheshimiwa rahis, ilikuwaje makamu wako akamteua Eddie Luwasha kumwakilisha kwenye kuchangia masjid halafu akafanya kampeni na kumwaga mifwedha? Je huku si kuanza kampeni kabla ya wakati na kukiuka kifungo cha chama au ilikuwa ni changa la machoni kusema kuwa jamaa yako aliyesema hamjakutana barabarani alisimamishwa wakati watu wake wanaendelea kupeta? Je uliwasikia marafiki wa Luwasha wanavomwaga radhi kila mahali hadi kwenye mlima Kimaranjaro? Hii ni nini kama siyo kampeni? Je hapa mnamdanganya nani na kwanini na hadi lini?
Ngoja nitume tweet nyingine. Nilimsikia juzi jamaa yangu Mwakiwembe akisema kuwa kaya itatuma waangalizi wa uchakachuaji kule Urundi ambako Pyere Nkurumbwiza anataka kung’ang’ania ulaji huku akivunja katiba nanyi mkimgwaya kwa vile nyani wote di dugu moja. Je hamuoni kama mnampa jamaa tafu au ni kwa vile kanchezo anakofanya mmekuwa mkikafanya kwa miaka nenda rudi?
Tweet ya mwisho, nadhani utasoma malalamiko yangu juu ya hekalu lako kufichua jina la jamaa aliyefichua uovu wa KcMc na kusimamishwa kazi ukiachilia mbali kutishwa. Je una lipi la kusema kuhusiana na mzalendo huyu anayedhulumiwa, kutishwa, kuonewa kwa sababu ya uzalendo wake? Nina mpango wa kukupigia na kukuongezea orodha nyingine ya wauza unga. Je utafichua jina langu ukiachia mbali kuiweka kapuni kama zile nyingi za wahalifu ulizosema unazo lakini hutaki kuzifanyia kazi? Kama itakuwa hivyo, naomba unishauri. Twende kwa nani na kwanini usitangaze kuwa ni kuvunja sheria kayani kufichua wizi wa fedha na mali za kaya?
Mheshimiwa sana rahis, naomba nimalizie kwa tweet hii.Tafadhali bin tafadhali mkuu. Chonde chonde ingilia kati mja wako apone na patilizi la mafisadi na washenzi waliomsimamisha kibarua kwa kufichua ujambazi na ufisadi wao. Usipofanya hivyo, walevi tutaingia mitaani na patakuwa hapatoshi ukiachia mbali kujimbika bila jembe. Nashauri uwawajibishe mara moja hawa ngurumbili na songombwingo wanaohujumu walevi na kujifanya wanajua sana sheria hadi kuzipinda na kuwaonea walevi wasio na hatia. Sijawahi kusikia mkuu wa wilaya akitetea wahamiaji haramu badala ya wananchi. Hivi huyu anamwakilisha nani zaidi ya tumbo lake?
Ubarikiwe sana mkuu.
Chanzo: Nipashe Mei 30, 2015.
No comments:
Post a Comment