How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 12 May 2015

Kijiwe chatabiri maafa baada ya uchakachuaji

 
          Baada ya kijiwe kushuhudia wajivuni na wasaka tonge wanavyoshindana kuonyesha ubabe katika kutapanya ukwasi wao wa kutisha shaka jinsi ulivyopatikana, kimeamua kutoa onyo na angalizo kwa yatakayojiri baada ya uchakachuaji uitwao uchaguzi hapo Oktoba mwaka huu ambapo ngoma itaamuriwa rasmi kumrithi Njaa Kaya.
Mgosi Machungi ndiye anayelianzisha kwa kujifanya mtabiri. Analonga, “Jamani mimeona hawa wajivuni wasaka tonge kupita kua ya kupatia wanavyomwaga fedha kwa mabiioni? Je mnadhani wanayapata wapi haya mabiiioni?”
“Rushwa, ufisadi na kununuliwa,” anajibu Mbwamwitu kwa ufupi.
Kapende naye anachomekea, “Wengi mnaowaona wakijifanya mabingwa wa kutoa wamenunuliwa nao wananunua wachovu ili baadaye waiuze kaya zaidi ya ilivyouzwa sasa huku waathirika wakiwa wapiga kura wenyewe kama hawatakuwa makini.”
 “Si kwamba nawawangia wala kuzua. Ukweli ni kwamba wengi watakufa kwa ugonjwa wa moyo baada ya kutoka kapa baada ya kuunguza mabilioni yao ya kutia shaka,” anajibu Mipawa huku akisigina kipisi cha sigara kali.
Sofia Lion aka Kunungaembe anamtazama kwa jicho la ukali Mipawa na kulonga, “Kwani wewe ni Mungu au mtabiri? Kwani wewe huwezi kufa kama wengine? Kwanini watu mmekuwa maskini hadi mnakuwa na roho mbaya hivi?”
Msomi naye hataki aachwe nyuma. Anatia buti, “Msemayo yana mashiko. Wengi watakufa au kupata matatizo ya kiafya japo dadangu Sofi hataki kukubaliana na ukweli huu.” Anaweka vizuri tai yake na kuendelea, “Maana hii jeuri ya fedha inayoonyeshwa unashangaa kuwa hawa hawa ndiyo waliokuwa wakijifanya wanafunzi mahiri wa mzee Mchonga. Laana yake lazima iwakumbe waadhirike hapa hapa duniani wote tukishuhudia.
Kabla ya kuendelea kijiwe kinajibu, “Aaaamina na iwe hivyo mkuu.”
Msomi anaendelea huku akitabasamu, “Wamemsaliti, wamemgeuka na kuwageuka wana kaya kiasi cha kuwaibia na sasa kuwatambia na kuwanunua kwa bei ya karanga. Tuombe Mungu waadhirike ili angalau wezi na mafisadi wakubwa wakubwa wapungue.”
Kabla ya kuendele Mpemba anakatua mic, “Yakhe unosema kweli tupu. Wemetugeuka na kutugeuza asusa hivi hivi twaona. Wallahi mie wakinipa nshiko wao nakula na kuwanyima kura yangu.”
Kanji anakwanyua mic, “Pawa tafadhali hapana tabiri baya kwa wenzako. Kama nakupa shiko veve kula lakini sio ombea vao baya bwana.”
Sofia anarejea kutoa usongo, “Hata wewe unayewatabiria mabaya yanaweza kukukuta tu.”
Mzee Kidevu anamchomekea Sofi akisema, “Unadhani Mgosi anaweza kufa kama yule tapeli kidhabi aliyezoea kutoa utabiri wa kuwatisha wapingaji. Naona na kitegemezi chake kimeanza utapeli ule ule. Kweli mtoto wa nyoka ni nyoka!”
Mbwamwitu anarusha kimondo, “Kweli huyu jamaa alikuwa tapeli akiwatapeli matapeli wa kisiasa  ili kupata ulaji wake. Kama kweli alikuwa mtabiri wa kweli mbona hakutabii kuwa jamaa atapata gonjwa a mshipa na apasuiwe?”
“Thubutu, angemtabiria maafa haya mbona angemnyima ulaji na kufarakana naye. Kimsingi alichokuwa akifanya ni kumgeuza bunga mwenzake na kupata ulaji wake haramu kitu ambacho kimerithiwa na kitegemezi chake.” Anajibu mzee Maneno huku akimpa kikombe muuza kahawa.
Mbwamwitu anasema, “Mmwangie hadi azimie.”
Mzee Maneno anamkata jicho na kusema, “Bwana mdogo uwe na adabu. Wewe ni wa kunipa ofa za matusi kama hii? Basi kama kumwagiwa waona dili kamawambie ammwagie baba yako.” Mzee anaonyesha kukereka wazi wazi.
Msomi anaamua kuokoa jahazi. Analonga, “Mzee mwenzangu achana na utani wa Mbwamwitu tujadili mada ya kuhonga fedha chafu walizohongwa na kununuliwa kwazo hawa wajivuni.”
Mipawa anarejea, “Umesikia mtoto wa farmer alivyomwaga mabilioni? “
Kabla ya kuendelea mheshimiwa Bwege anakatua mic, “Alikuwa mtoto wa mkulima zama zile kabla hajaula. Kwa sasa si mtoto wa mkulima zaidi ya fisadi mkubwa tu anayeweza kumwaga mamilioni bila aibu. Sijui mzee Mchonga aliyemchonga angefufuka angepatwa kihoro kiasi gani?” anakohoa kidogo na kuendelea, “Siku zote nikiwaonya kuwa tuna mfumo wa kijambazi na kifisadi, wapo wanaonuna na kuona ninazusha. Sasa mmeona. Hakuna anayeuliza walivyochuma haya mabilioni na kwa muda gani, wanayatoa ili kupata nini. Ni bahati mbaya kuwa hata chata lao limeamua kulala nao kitanda kimoja.”
Mgosi anakula mic, “Tikubaiane jamani. Kama na sisi titakaa na kuangaia tu bia kuchukua hatua, hawa wajalaana watakuja kutiuza tifanyiwe kitu mbaya siku za usoni. Maana tinakaa na kuangaia tu kana kwamba hatihusiki na kaya yetu.”
Mpemba hangoji. Anatia timu, “Yakhe unkuna kwa pwenti zako Mgosi wallahi. Twapaswa kuungana na kuwatolea uvivu kwa kuhimizana kuwanyima kura wale wote tutaoona wahonga fedha. Maana huu ushahidi kuwa watugeuza biashara sie ati.”
“Ami naungana nawe mia kwa mia. Kila mwaka tunalalamika ufisadi ufisadi ufisadi bila kuchukua hatua. Je sisi si washiriki wa dhambi hii inayoangamiza jamii ambapo madaraka yamegeukwa nyenzo ya kuibia umma?”
Msomi anarejea tena, “Hakika, umma unashiriki kikamilifu kuhalalisha haramu hii. Ila nina uhakika kwa jinsi wachovu walivyopigika, mwaka huu wanaweza kubadili upepo na sura ya mambo.”
Sofi naye leo kaamua kuwa mbishi. Anarejea na kusema, “Hilo dua la kuku kakaangu. Mambo ya upinzani yako mijini. Vijijini watazoa kura na kupeta mtake misitake.”
“Hapa nakuunga mkono Sofi hata kama sipendi mawazo yako mgando. Wajinga ndiyo waliwao wakitoa waache waliwe. Sisi tutajiridhisha kuwa hatukujirahisi kama unavyoshabikia.”
Kijiwe kikiwa kinanoga si likapita shumbwengu la mwana wa mkulima bilionea. Acha tulimwagie kahawa na kulirushia kashata na kutimka ili ndata wasitutembezee kichapo tukawaumiza!
Chanzo: Tanzania Daima Mei 13, 2015

No comments: