The Chant of Savant

Tuesday 5 May 2015

Kijiwe chamkumbusha rahisi ahadi zake

 Rahisi Jey Kiquette ameanza kuaga wachovu. Kwani mwakani saa kama hizi atakuwa nje ya ikuu akitazama wenzake wanavyofanya vitu vyao. Ni wakati mgumu. Maana hujui atakayechukua ngoma atakutenza vipi hasa ikizingatiwa kuwa unaacha madudu na uoza kibao nyuma.
Leo kijiwe kimekaa kama kamati kumkumbusha mheshimiwa rahisi baadhi ya ahadi zake ili lau atoe maelezo kabla ya kuishia.
Leo Mpemba ndiye anaanzisha mada. Anakatua mic, “Jamani miaka haikawiii wallahi. Naona ni kama jana tulipokwenda kwenye uchakachuaji tukaishia kupata zali.”
Mipawa anakula mic, “Ni kweli muda haukawii sema kuna wakati unaganda hasa ukiangalia mauzauza yanayoendelea.”
Mgosi Machungi anapoka mic, “Tikubaiane. Miaka kumi iiyopita imekuwa ya hasaa kwa kaya yetu hasa tokana na mkuu kushindwa kutekeeza ahadi zake.”
Msomi anatia buti kwa kasi ya ajabu, “Msemayo ni kweli japo sikubaliani na hoja kuwa mkuu hakufanikisha kitu. Kama mnakumbuka, aliingia kwenye ulaji na kauli ya ANGUKA. Na kweli alihakikisha tunapata anguko hasa wale tulioamini ahadi zake. Kwa hili amefanikiwa kiasi cha kustahiki nishani ya maanguko.”
Sofia Lion aka Kanungaembe anamchomekea Msomi huku akimkazia macho, “Sasa usomi wako unakupelekea kubaya. Ni lini mheshimiwa rahisi alisema kuwa sera yake ni anguka kama siyo uongo wa mchana. Unadhani hatuna akili kiasi cha kutuletea vitu vya kuzua namna hii?
Msomi anakatua mic huku akitabasamu, “Sofi dadangu niseme mara ngapi kuwa kuna kitu kimekuingilia?”
Kabla ya kuendelea Sofi anajihami, “Sasa kaka Msomi haya matusi. Nataka ujibu swali badala ya kurusharusha.”
“Usikonde dadangu nimejiandaa kukutosheleza kwa dozi ya uhakika. Ninaposema ANGUKA sizui. Namaanisha kauli mbiu ya Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya ambayo ukiiuganisha unapata ANGUKA. Mbona ni jambo rahisi dadangu!”
“Kumbe unamaanisha muunganisho wa kauli mbinu!” Sofi anajibu akionyesha wazi kuzidiwa kete.
Kabla ya kuendelea, Kapende anamchomekea, “Sofi huna haja ya kubisha. Kama hili unaona lina shaka basi nakupa dozi nyingine tofauti. Unakumbuka jamaa aliahidi kutaja majina ya wauza unga majambazi, mafwisadi, majambazi hata vidokozi bandarini aliyesema ana orodha zake?”
Kabla ya Sofia kujibu Mbwamwitu anaongezea, “Pia akumbuke kuwa jamaa yake aliahidi maisha bora kwa wote. Yako wapi iwapo kwa  miaka kumi tumeendelea kuwa hapa kijiweni bila ajira ukiachilia mbali shilingi yetu kuendelea kuporomoka kama ina ugonjwa wa kuharisha?”
Msomi ananyakua mic, “We Mbwamwitu, unaongea kama umesoma nilichokuwa nataka kusema. Nadhani dadaangu hapa atatosheka na ajinyamazie kimya.”
Sofia anaonyesha hana la kijibu zaidi ya kutoa macho kama panya aliyenaswa mtegoni.
Kanji anakamua mic, “Jamani dugu zangu sema kweli. Mimi ona jamaa fanya mambo kuba sana. Najenga barabara. Nasatangaza jina ya taifa kwa dunia sana sana.”
Mheshimiwa Bwege hangoji. Anakula mic, “Kama utaangalia mambo kwa uoni wa karibu unaweza kuona jamaa kafanya maajabu. Ila kama utatuliza akili utagundua kuwa mengi ni sanaa. Barabara unazomsifia zinafikia kiwango cha ubora wakati zinasifika kwa kunyotoa wachovu roho tokana na kujengwa chini ya kiwango? Hizo ziara za kutangaza kaya nje ndiyo sitaki niziongelee hasa ikizingatiwa kuwa kaya yetu inafahamika hata kabla ya kupata uhuru.”
Mchunguliaji anaamua kuchomekea, “Kwani tulinchagua akazurure au atawale kwa kutatua kero zetu badala ya kuzizidisha kwa kupenda kutanua huku akitumia mabilioni ya kodi zetu?
“Mie nakubaliana na Msomi mia kwa mia kuwa alichofanya ni kufanikisha anguko la kaya. Hivi mnajua deni la kaya limeumka kiasi gani? Je mnajua ni kiasi gani mafisadi wameshika kani? Laiti angesema alikuwa akienda ughaibuni kudai mabilioni yaliyofichwa na washikaji zake lau angeeleweka. Mengine naona sanaa tu.” Kapende anazidi kusiliba.
Mgosi anarejea, “ Kapende tafadhai usitiize. Maana ukiangaia madudu na uoza viivyotamaaki unatamani ulie tate nane tate nane aondoka huenda wakaja watu wenye udhu na akii waekebishe huu uoza.”
Kabla ya kuendelea Kanji anamchomekea, “Dugu yangu Gosi hap alia. Kama nalia vatu nacheka veve.”
Msomi anaamua kutia daruga tena, “Wazee, kama tutakuwa wakweli ni kwamba hii miaka kumi inayoisha imekuwa ya hasara na nakma. Tuombe Mungu jamaa atimue lau tuanze arifu na ujiti. Maana mambo yalivyokaa hasa uchumi na uwajibikaji, tuendako twaweza kuchenchiana hasa kama Tume ya NEC ya uchakachuaji itampa ushindi fisadi mwingine. Who wants the same mess once again?”
Sofi haridhiki. Anakula mic, “Jamani mfanyiwe nini ndipo mshukuru? Juzi nilisikia kwenye hotuba ya mheshimiwa kuwa amekuza elimu hasa kujenga shule nyingi za upili kayani. Je haya si mafanikio.”
Mzee Maneno anakula mic, “Umemaliza? Hizo shule ni shule kweli au mijengo ya kuongeza ujinga? Shule gani zinatoa wahitimu wasiojua kusoma na kuandika kama ambavyo utafiti wa hivi karibuni umebaini? Ulitegemea alisemee hili wakati anajua alivyovurunda?”
Mpemba anajerejea, “Wallahi umenikumbusha haya maafa ya kuua ilmu. Kweli, usemayo, wategemea watu kama docta Shukuruni Kawa-mbwa wakuze ilmu wakati wako pale kuiua? Hebu jikumbushe tukio la hivi karibuni ambapo waliazimia eti ilmu kayani itatolewa kwa kimakonde. Haya nayo maendeleo au ndiyo hiyo hiyo ANGUKA anoogelea Nsomi?”
Kijiwe kikiwa kinanoga ndata walianza kufunga barabara kupisha msafara wa rahisi.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 6, 2015.

No comments: