The Chant of Savant

Tuesday 4 May 2021

Mama Samia, Kitabu cha Magufuli ni Kitabu Chako


Mama nakusalimia na kukutakia ramadhani njema. Kwanza, naomba nitumie fursa hii ya mfungo kuongea nawe japo kidogo kuhusiana na masuala muhimu kwa taifa letu nawe ukiwa mkuu wa nchi. Hivyo, mlengwa na mhusika mkuu.  Pia ufahamu. Si mara yangu ya kwanza wala ya mwisho kuwasiliana nawe wala kukushauri. Mama usinichoke tafadhali.  Baada ya kuvunja rekodi nchini kwa mara ya tatu mfululizo ukiwa ni mwanamke wa kwanza kuwa makamu wa Bunge la Katiba, makamu wa rais na hatimaye rais wa nchi, kumekuwapo matamko mbali mbali kuhusiana nawe bila kusahau mtangulizi wako Hayati John Magufuli (Mungu Ipumzishe Roho Yake kwa Amani (MIRYA). Mojawapo ya jambo nililosikia ilikuwa ni mjadala juu ya kwanini awamu yako inaitwa ya sita na si ya tano. Hili ulishalijibu vilivyo. Hivyo, halitanishughulisha leo.
Leo naandika rasmi kuhusiana na nukuu ninayoisikia mara kwa mara kuwa ya “Kila zama na kitabu chake “ ambayo bila shaka alitoa rais mtaafu Ali Hassan Mwinyi wakati fulani kwa lengo tofauti na inavyoanza kuharibiwa na kutumiwa vibaya. Tokana na dhana hii, wapo watu wanaokushinikiza uachane na yale yaliyotendwa na mtangulizi wako kana kwamba hamkuwa pamoja katika kuyapanga na kuyatenda ukiachia mbali kuwa sera za chama kilichowapa tiketi yake mgombee urais. 
        Kwanza, niseme wazi kuhusiana na falsafa ya kila zama na kitabu chake. Si kweli na si lazima kila zama iwe na kitabu chake. Kwanini vurugu hivi kana kwamba kitabu ni muhimu kuliko taifa, malengo na matarajio yake? Tutakuwa na vitabu vingapi?  Mbona Biblia na Quran zimekuwapo zama zote. Je mwili wote kama utakuwa sikio, jicho litakuwa wapi? Falsafa hii siyo stahiki kwenye uongozi wa nchi hasa wakati huu ambapo awamu ya sita ni muendelezo wa ya tano kama tutazingatia kuwa ndiyo wananchi walichagua na yakatokea yaliyotokea. Wewe na Hayati Magufuli mliutafuta uongozi pamoja kwa malengo ya pamoja kama mlivyoaminiwa na chama chenu na watanzania. Sasa inakuwaje watu waje na mambo ya kila zama na kitabu chake kana kwamba nyinyi ni tofauti? Nimependa kauli mbiu na salamu yako ya “Kazi Iendelee.” Laiti ungeongeza na kusema “Hapa Kazi Tu Indelee.” Kwanini napingana na kila zama kuwa na kitabu chake? Ukiangalia kuwa ulichukua madaraka kwenye ngwe ya pili ya awamu ya tano, mambo mengi mliyoanzisha hayakuwa yamekamilika. Sasa tuseme yote haya yanawekwa kando ili nawe uje na kitabu chako? Cha nini wakati nchi unayolenga kuijenga ni ile ile?
         Pili, katika kukinzana na dhana ya kila wakati na kitabu chake, rais mstaafu marehemu Benjamin William Mkapa alisema kuwa tunakosa continuation, yaani muendelezo pale tunapobadili uongozi wa nchi. Na hii si nzuri kwa taifa. Alikuwa sahihi. Tunajenga nchi. Hivyo, badala ya kuangalia mtu na ndoto zake tuangalia malengo, matarajio na ndoto za taifa siyo fikra na utashi wa mtu tunayempa dhamana ya kuongoza taifa. Mhusika afuate matakwa yetu kama waajiri wake badala ya kila mtu kuja na yake kana kwamba kazi anayofanya ni yake binafsi na si ya watanzania.
        Tatu, hivyo, kimsingi, kitabu cha Magufuli ni cha Samia, cha Tanzania na cha CCM. Haiingii akilini kuwa mema aliyoanzisha Hayati Magufuli yawekwe pembeni na kuanzisha mengine eti kwa vile kila rais ana utashi wake wakati utashi ni wananchi waliomuajiri. Hatuwezi kuwa na vitabu vingi vya ujenzi wakati tunajenga nchi au nyumba moja. Ujenzi wa daraja au nyumba hauwezi kuwa na vitabu tofauti ukawa ujenzi wenye maana zaidi ya vurugu. Hatuwezi kukaribisha vurugu kwenye ujenzi wa nyumba ambapo huyu anataka ghorafa. Huyu anataka ajenge tembe. Huyu anataka daraja la kuning’inia, yule la nguzo moja au mtambaa. Je hapa  tutaangalia namna ya kupitisha fasheni zetu au ukweli kuwa wote tuna lengo moja na wajibu mmoja kwa watu wamoja.
        Kama nilivyosema hapo juu, miradi aliyoanzisha Hayati Magufuli hakuanzisha kwa ajili yake binafsi bali kwa ajili ya Tanzania. Alianzisha miradi mikubwa iliyolifanya taifa si kuendelea tu bali kuheshimika. Mfano, kama tutafuata falsafa ya kila mtu na kitabu chake, ni tija gani miradi yote hii ikipigwa kalamu na kuanzisha mingine au mambo mengine? Tujifunze. Nasikia wasaliti wakitaka tuendelee na mradi kichaa alioukataa Hayati Magufuli na kutoa sababu wa Bagamoyo. Tuurekebishe ili kukidhi mahitaji ya taifa na kuondoa mapungufu huku tukijikita kuujenga kwa fedha yetu badala ya kukopa hata kama itatuchukua miaka mia.  Hata atakayoanzisha Samia vile vile si kwa ajili yake bali taifa. Hivyo, hakuna haja ya kuhangaika na kubadili michoro ya nyumba au daraja bali kufanya maboresho na kuhakikisha miradi husika inakamilishwa. Niseme kabla ya kusahau. Hayati Magufuli alikataa kuidhinisha mradi wa ujenzi wa bandari Bagamoyo tokana na kutokuwa na maslahi kitaifa. Nitashangaa, chini ya dhana ya kila zama na kitabu chake, kama mradi huu utafufuliwa bila kulieleza taifa mapungufu na maslahi yake kwa taifa. Nasema hivi bila wasi wasi kuwa mawazo yangu na yale yanayofanana nayo yatasikilizwa. Kwani, tunawaajiri marais watutumikie kwa malengo tuliyojiwekea bali si kwa ajili ya kufanya watakavyo. Wapishi wengi huharibu mchuzi.
        Nne, kama taifa tufahamu kuwa hatufanyii nchi majaribio wala kuonyeshana umwamba wa namna tunavyoweza kushindana katika kubomoana badala ya kuendeleza. Urais ni kama mbio za kupokezana kijiti. Kila mwenye kubahatika kushiriki, hufanya anapoweza na kumkabidhi anayefuata kwa kuhakikisha kuwa lengo lao wote ni moja, kumaliza mbio kwa ushindi. Hivyo, dhana ya kila zama na kitabu chake hapa haina mashiko vinginevyo kama inalenga kwenye kuboresha lakini siyo kutoa utetezi wa kuvuruga au kuhujumu.
        Tano, kwanini nasema kitabu cha SSH ni cha JPM? Jiulize. Je Magufuli asingempendekezea, kumteua na kumwamini Samia, angekuwa hapa alipo sasa? Hata kama waswahili husema asiyekuwepo na lake halipo, kwenye hili, la Magufuli haliwezi kuondolewa na SSH. Ikiwa hivyo, basi tujue tunakaribisha vurugu katika ujenzi wa nyumba au kushona nguo yetu. Hatuna haja ya kufikiri hivyo hasa ikizingatiwa kuwa wote tunatumikia taifa la Watanzania na si mapenzi yetu binafsi bali ya umma.
  Sita, tukiangalia mifano toka nje, utagundua kuwa nchi za wenzetu zimeendelea kutokana na kuwa na mifumo inayofuatwa na viongozi bila kujali itikadi zao. Rejea vurugu za Donald Trump ambazo tokana na kujengeka kwa mfumo unaojitegemea alishindwa kulisambaratisha taifa la Marekani. Marekani ingekuwa nchi ya kiafrika ingesambaratika chini ya Trump na uhafidhina na ujinga wake.  Hivyo, hao wanaendekeza dhana ya kila zama na kitabu chake wajiulize: Tunashindana na nani na kwanini na ili iweje? Tuanendekeza kila zama na kitabu chake kuwahi nini wakati Tanzania itakuwapo siku zote? Tujifunze toka Sri Lanka na Zambia juu ya wachina wanavyowaingiza mkenge tokana nan chi hizi kupwakia miradi kwa kuangalia maslahi uchwara binafsi na ya karibu.
Mwisho, kitabu cha Magufuli ni cha Samia na cha Samia ni cha Magufuli nani cha Tanzania basi. Kama alivyosema Hayati Mkapa, kuna haja ya kuwapo na continuity badala ya discontinuity chini ya dhana ya kila zama na kitabu chake.
Chanzo: Raia Mwema kesho.


No comments: