The Chant of Savant

Sunday 30 May 2021

Malipo ya Wabunge Hawa Ni Ufisadi Mwingine

Hivi karibuni rais Samia Suluhu Hassan aliwahakikisha na kuwaaminisha watanzania kuwa mapambano dhidi ya matumizi mabaya ya fedha na raslimali za umma yaliyoanzishwa na Hayati Dkt John Pombe Magufuli yanaendelea. Bila hiyo, hata chini ya kauli mbiu yake Kazi Iendelee, wengi waliamini kuwa watanzania na taasisi zote walimwelewa. Mbali na rais kutoa hakikisho, kumekuwapo na sauti za kutaka iwepo kodi ya uzalendo ambayo haitalenga kuwaumiza maskini bali vigogo katika ngazi za juu serikalini. 
        Leo tutaongelea kadhia ambayo–––licha kuwagombanisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)–––inaonekana kuikichafua Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake kama hawatabadili msimamo wao juu ya wabunge hawa. Tunajiuliza maswali mengi kuhusiana na kadhia hii. CHADEMA kilisema wazi kuwa wahusika walifukuzwa uanachama tokana na kwenda kinyume na maagizo ya vyombo husika kwenye chama. Kimsingi, chanzo cha mgogoro mzima ni pale CCM iliposhinda viti vyote vilivyokuwa vimeshikiliwa na CHADEMA hadi kwenye uchaguzi wa mwaka jana. Baada ya pigo hili, wanawake waliobwagwa, wakiongozwa na Halima Mdee, waliamua kupindisha kanuni–––kwa mujibu wa CHADEMA–––na kuendesha uchaguzi wa viti maalum na kujipatia ulaji. Hapa kimsingi, wahusika walionyesha namna walivyokuwa wakisaka madaraka bila kujali kama walikuwa wakifuata au kuvunja taratibu za chama chao hadi wakafukuzwa. Baada ya kufukuzwa, wahusika walikimbilia bungeni ambako waliapishwa bila hata kusikiliza malalamiko toka kwenye chama chao. Hii si haki na wala haiisaidii CCM, serikali yake wala nchi hasa ikizingatiwa kuwa fedha na marupurupu wanavyolipwa si mali ya CCM, serikali wala bunge bali ni kodi ya mwananchi. Bila kufuata utaratibu na kujulikana sababu za msingi za wabunge hawa wasiomwakilisha yeyote wala chama chochote kuendelea kuwa bungeni na kulipa ni matumizi mabaya ya fedha za umma. Kimsingi, ni ufisadi wa kimfumo ambapo faida za kisiasa za kundi moja zinawekwa mbele hata kwa maumivu ya wananchi maskini ambao fedha yao inatumika kuwatunza watu hawa wasio na chama wala uhalali wa kuwa bungeni ukiachia mbali kutomwakilisha yeyote bali matumbo yao.
        Baada ya mgogoro kunyunyuta, spika wa bunge Mheshimiwa Job Ndugai alisikika akiwatetea tena ka kuita barua ya CHADEMA ya kumtaka awawajibishe kipeperushi jambo ambalo lilifanya wengi wakune vichwa na kujiuliza kunani? Kama haitoshi, Ndugai aligeuka wakili wa wabunge hawa 19 ambao wamepewa jina la Covid-19 bila kueleza alianza lini kufanya jukumu hili na ili iwe nini. Japo ni haki yake kumtetea au kumshabikia hata kumkingia kifua amtakaye, si haki ya spika kutoa maamuzi ambayo yanayonyesha wazi yanavyowatwisha mzigo walipa kodi kama ilivyo kwenye kadhia hii.  Je ni fedha kiasi gani taifa linapoteza kwa kuwalipa wabunge waliokwisha kufukuzwa na chama chao? 
        Siju mshahara na marupurupu ya mbunge. Hata hivyo, tuchukulie kuwa kila mbunge analipwa shilingi 10,000,000 kwa mwezi. Hii maana yake tunapoteza karibu shilingi milioni 200,000,000 bila kuhusisha matumizi mengine kama vile posho ya kila siku, pesa ya mafuta, nyumba na mengine mengi. Kama wabunge hawa bandia wataendelea kuwa bungeni, ina maana kwa mwaka watakuwa wanakula si chini ya shilingi bilioni 2.4 kwa nwaka. Na kama wahusika wataendela kuwang’ang’ania hadi uchaguzi ujao, taifa litakuwa limepoteza jumla ya shilingi bilioni 12. Je pesa hii–––kama ingetumika kwa busara–––ingeweza kufanya mambo mangapi ya maana kwa watu wetu maskini. Kama sikosei hesabu, pesa hii inaweza kujenga si chini ya kilomita 60 za reli ya kisasa ya Standard Gauge. Niruhusu nitoke nje kidogo ya mada. Kama tukifutilia mbali ubunge wa viti maalum, tunaweza kwa miaka mitano, tuna uwezo wa kujenga barabara ya lami toka Dar es Salaam hadi Tabora hata Mwanza bila kukopa.  Je tunafanya hivi kwa faida gani na kwa utajiri au ulazima upi? Je, kama tutaachana tabia ya kuhudumiana, wanabariki jinai hii kweli hawaoni kuwa wanawaumiza wananchi na wanachofanya si haki? Je hata hawa wanufaikaji hawaonyeshi walivyo wabinafsi ambao wako tayari kupinda na kuvunja sheria ilmradi wapate wao? Je mamlaka za juu hazioni ufisadi huu wa kimfumo? Je kwa kuendelea kunyamazia jinai si ushahidi kuwa ima viongozi wetu si makini au wana sura mbili?
        Juzi rais SSH alimtumbua aliyekuwa mkurugenzi wa TPA, Deusdedit Kakoko ambaye niliandika barua ya kuunga mkono kadhia hii kabla ya kufanya utafiti wa kina, jambo ambalo nalijutia kwa kusikiliza upande mmoja, kwa upotevu wa shilingi bilioni tatu na ushei pale Bandarini. Je rais ambaye alionyesha ukali kwa fedha ndogo kama hii ikilinganishwa na wabunge hawa watakayofuja, yuko wapi aone haya mabilioni?
        Tumalize kwa kuwaomba wakubwa wetu wanaowang’ang’ania wabunge tajwa au kuwafumbia macho na madhara wanayosababisha kwa fedha za walipa kodi waachane nao wamalizane kwenye chama chao. Kama wanawaona ni mali sana basi wawashawishi wahamie CCM kama wengine ambao walishafanya hivyo. Na kama ni vyeo, wawape vyeo vingine badala ya kutujazia mkanganyiko kwenye bunge tukufu la wananchi ambalo linapaswa kuwa na wawakilishi wa umma na siyo wa matumbo yao. Pia hawa wanaowakingia kifua wajue kuwa pesa wanayolipwa watu wao si pesa toka mifukoni mwao. Kuna kesho pale wahusika watakapokuwa nje ya mamlaka waliyo nayo wakilipa kodi au kuulizwa walifanya nini wakati walipokuwa na mamlaka. Pia na wabunge husika wajitathmni wakijua kuna kesho.
Chanzo: Raia Mwema kesho.

No comments: