The Chant of Savant

Sunday 30 May 2021

Mkoa Mpya wa Chato Mtendeeni Haki Hayati Magufuli

Hivi karibuni nimesoma kwenye vyombo vya habari juu ya mapendekezo ya kuunda mkoa mpya wa Chato mahali alipozaliwa shujaa wetu Hayati John Pombe Magufuli rais wa awamu ya tano aliyetutoka ghafla mwezi Machi mwaka huu. Gazeti la Mwananchi Mei 29, 2021 linaandika “Mkoa mpya wa Chato umependekezwa kuwa na wilaya ya Chato, Bukombe zilizopo mkoa wa Geita kwa sasa na wilaya mbili za mkoa wa Kagera ambazo ni Biharamulo na Ngara, huku ikimega kata tatu kutoka wilaya ya Muleba pamoja na baadhi ya maeneo kutoka wilaya ya Kakonko iliyopo mkoani Kigoma.” Kwa wanaomjua Hayati Magufuli, hiki ni kituko cha aina yake ambacho kwake kingekuwa machukizo yasiyo na msamaha. Katika kuunda mkoa husika kwa kumuenzi Magufuli, kuna mambo ambayo wahusika wanapaswa kuyatilia maanani ili wasionekane kama wanamkejeli. Kwa mfano, inakuwaje wanaondoa sehemu kama wilaya ya Karagwe ambako inasemekana alikuwa na makazi ukiachia mbali michango mingine kwa mkoa wa sasa wa Geita kama vile Mbuga ya Burigi-Chato na mambo mengine muhimu?
        Kwanza, tuseme wazi si haki kwa Hayati Magufuli ambaye kimsingi, ndiye aliyeipaisha wilaya ya Chato ukiachia mbali kuanzisha mkoa wa Geita na sasa kuwa kwenye harakati za kuanzisha mkoa mpya wa Chato kama namna ya kumuenzi Hayati Magufuli. Pamoja na uzuri wa wazo hili, hata hivyo, ukiangalia mapendekezo hayo hapo juu, kwanza unashangaa na kusikitika hasa kwa waliomjua Hayati Magufuli na mipango yake ya baadaye kama angeishi hadi kustaafu urais.                             Wanaopendekeza wilaya na kata tajwa hapo juu, hawajaeleza sababu za kuziteua. Hawajatoa sababu na vigezo vya kisayansi na vinavyoingia akilini vya kupendekeza wilaya na kata husika. Sijui kama hawa wamezingatia mambo muhimu katika kufikia hitimisho hili hasa ikizingatiwa kuwa kuna sehemu nyingine ambazo zinafaa kuwa sehemu ya mkoa husika kuliko hizo tajwa kama tutakavyoeleza hapa baadaye. 
        Pili, hata kama hawa wanaoendesha mchakato tajwa wana sababu, haziwezi kuwa na nguvu kama sababu nitakazotoa hapa chini ni kwanini Mkoa mpya wa Chato usiache wilaya ya Karagwe na Ngara na badala yake uache zile za mkoa wa Mwanza wenye ukubwa wa kilometa za mraba 9, 467 ambao tayari ni mdogo ikilinganishwa na mkoa wa Kagera wenye ukubwa wa kilometa za mraba 35,686 yaani karibu mara nne ya mkoa wa Mwanza. Namba huwa hazidanganyi hata kama hatuzipendi. Ukitoa ukubwa wa wilaya ya Karagwe ambao ni kilometa za mraba 7,716 na ule wa wilaya ya Ngara yenye 3,744 bado mkoa wa Kagera utabakia kuwa mkubwa kuliko Mwanza ukiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 24, 226 mbali na ukweli kuwa wilaya mbili tajwa ni kubwa kuliko mkoa wa Mwanza wenyewe. Tuseme wazi kuwa–––kama lengo ni kuanzisha mkoa wa Chato ili kupeleka huduma kwa wananchi, basi wilaya tajwa za Karagwe na Ngara zinafaa kuwa sehemu ya mkoa huu mpya. Kama sababu ni za kisiasa tu na nyingine, basi wilaya husika hazifai.
Tatu, ukweli ni kwamba Hayati Magufuli mwenyewe alikuwa amekwisha kuanzia makazi yake kwenye wilaya ya Karagwe (Sauti Kubwa, Januari 20, 2021) kiasi cha kupafanya nyumbani namba mbili. Japo si wengi wanalijua hili tokana na Hayati Magufuli kutofanya maisha yake binafsi habari, alikuwa na makazi mengine wilayani Karagwe ambako inasemekana alikupenda sana kiasi cha kuanzisha shamba la mifugo. Je hawa wanaotaka kuiweka kando wilaya hii ambayo Sauti kubwa inasema “…. Rais John Pombe Magufuli (JPM) yuko Mkoani Kagera. Alianzia Bukoba na sasa yuko mapumzikoni “nyumbani” kwake kwingine, Karagwe” wanamuenzi kweli au wanamtumia kutimiza matakwa yao binafsi? Je familia ya Magufuli imeombwa mawazo katika mchakato huu?
Tatu, mbali na Hayati Magufuli kuipenda na kuweka makao wilayani Karagwe, pia wilaya hii pamoja na Ngara huchangia sehemu kubwa ya mbuga maarufu ya Burigi Chato. Katika pita pita zangu na kuuliza huku na huku, niliambiwa kuwa hata jina Burigi asili yake ni Karagwe ikitokana na jina la ziwa Burigi lililoko wilayani Karagwe. Hivyo, kwa vigezo hivi na vingine, mkoa mpya wa Chato hauwezi kuiacha nje wilaya ya Karagwe.
Sababu ya nne, ni kwamba––––kwa wanaojua historia ya Ufalme wa Karagwe ambao ulikuwa ni moja ya himaya kubwa kabla ya ukoloni ikishindana na kushirikiana na himaya nyingine kubwa za wakati huo za Bunyoro-Kitara, Buganda na Busoga–––atakubaliana nami kuwa eneo la Chato hadi Sumbawanga liliwahi kuwa chini ya himaya hii kubwa ambayo ilisifika nchini Tanzania ikishindana na Zanzibar kwa umaarufu na kufanyiwa utafiti na wazungu kabla ya kuitawala Afrika. Hata hivyo, himaya hii iliyokuwa na nguvu na maendeleo ya hali ya juu, ilififishwa na hatimaye kufishwa baada ya wakoloni kuanzisha kabila la wahaya ambalo halikuwapo kabla ya kuja ukoloni na kuchukua nafasi yake kiasi cha mkoa wa Kagera kuonekana kama umekaliwa na wahaya wakati una makabila mengine mengi.
Tumalizie kwa kuwataka wanaohusika na mchakato wa kuunda mkoa mpya wa Chato watoe vigezo watakavyotumia kuunda. Pia waeleze kila kigezo kwa ufasaha ili kuepuka kuingiza siasa katika maisha ya watu mbali na kutokumuenzi Hayati Magufuli au kumtumia kufikia malengo yao ya kisiasa. Hivyo, chonde chonde. Mtendeeni haki Hayati Magufuli na kumuenzi kiukweli badala ya kutaka kumtumia kisiasa kwa faida binafsi au tokana na kutojua ukweli wa mambo.
Chanzo: Raia Mwema kesho.

No comments: