The Chant of Savant

Friday 28 May 2021

Kuna Haja ya Mataifa ya Afrika Kuachana na Unafiki Kuhusiana na Israel


Kwa waliokua miaka ya nyuma hadi miaka ya 80 watakumbuka namna mataifa mengi ya Afrika yalivyosusia utawala wa kikaburu na kibaguzi wa Afrika ya Kusini ya wakati ule. Msimamo huu dhidi ya ubaguzi na ukaburu haukutokana na kuichukia Afrika ya Kusini kama taifa bali sera zake za kibaguzi na kikaburu ambazo ziliwabagua, kuwanyonya, kuwatesa na kuwanyang’anya utu Weusi wa Afrika ya Kusini. Hivyo, kuuadhibu na hatimaye kuutokomeza, mataifa mengi ya Kiafrika yaliutenga na kuuwekea vikwazo vya kiuchumi na ushirikiano utawala wa Afrika ya Kusini na hatimaye kuutokomeza toka kwenye uso wa ardhi. Kimsingi, kilichokuwa kikiendelea nchini Afrika Kusini ilikuwa ni jinai ambayo kila binadamu mwenye akili alipaswa kupiga vita na hatimaye kushinda kama ilivyotokea mwaka 1997 baada ya kutokomezwa kwa utawala huu habithi.
        Leo tutaongelea namna hasira na namna ya kupambana na ukaburu unaoendelea nchini Israel ambako wapalestina wanatenzwa hata zaidi ya makaburu walivyowatenza Weusi wakishirikiana na mataifa ya Ulaya. Katika kupambana na ukaburu na ubaguzi wa rangi, Tanzania iliongoza mataifa ya mstari wa mbele hadi ukaburu na ubaguzi wa rangi vilipoteketezwa na kuondolewa kwenye uso wa dunia pamoja na kuungwa mkono na kusaidiwa na mataifa ya magharibi. Kwa sasa, kadhia ya ubaguzi na unyama tulivyoshuhudia nchini Afrika Kusini vimehamia nchini Israel, taifa ambalo liliundwa na mataifa ya magharibi ili kuzitisha na kuzinyonya nchi za mashariki ya kati zenye utajiri wa gesi na mafuta. Tangu taifa hili liundwe, limekuwa likiwanyanyasa wapalestina ambao dhambi yao ni kuwa na ardhi iliyomegwa na kuundwa taifa la kibaguzi la kizayuni.  Kinachofanyika nchini mashariki ya kati kinapaswa kulaaniwa na kupigwa vita kwa nguvu zote. Hivi karibuni, dunia ilishuhudia mauaji na uharibifu wa mali vya kutisha. Unyama huu ni mkubwa kuliko hata ule wa Septemba 11 wakati taifa la Marekani lilioposhambuliwa na kikundi cha kigaidi cha al Qaida ambapo majengo yaliyokuwa alama ya ushufaa wa taifa hili yalishambuliwa na kubomolewa sawa na majengo ya Palestina yaliyoangushwa hivi karibuni ukiachia mbali vifo vya watu wengi wasio na hatia. Kwa mujibu wa Al Jazeera (Mei 26, 2021) ikikariri ripoti ya umoja wa mataifa, majengo zaidi ya 1,000 yaliharibiwa katika mashambulizi ya siku 11 huku watu 243 wakiwamo watoto waliuawa ambapo Israel ilipoteza watu 12 tu (BBC, Mei 26, 2021)
        Wakati haya yakiendelea, kuna baadhi ya mataifa ya kiafrika ikiwemo Tanzania yameimarisha uhusiano na taifa hili la kibaguzi na kigaidi. Je kwa kufanya hivyo, hatujirahisishi na kuwa sehemu ya jinai dhidi ya watu wasio na hatia? Je huu si unafiki unaofanywa na watu waliokuwa mstari wa mbele kupambana na kuangamiza utawala uliofanana na huu wa Israel wakati wakifumbia macho jinai hii inayoendelea? Tunamkomoa nani? Ajabu na unafiki wa ajabu, hata mataifa ya kiarabu ambao ndiyo waathirika na walengwa wakubwa nayo yamegwaya kwa kuogopa viongozi wao wasipoteze ulaji wao binafsi hata kama wanajua uovu wanaolinda au kugwaya.
        Mbali na kushinikiza kuwa kuna haja ya kuitenga Israel kwa kuwaonea wapalestina, tuchukue fursa hii kuwataka waafrika waanze kujithamini na kuwathamini wenzao ili nao wathaminiwe kama watu sawa na wengine. Kwa mfano, wakati tunapohanikiza kuwalaani makaburu wa Israel, tunakaa kimya kuhusiana na wenzetu wanaouana kwenye nchi kama vile the Central African Republic ambapo waswahili wanauana kwa misingi ya imani za kigeni. Tunakaa kimya wakati waswahili wanapoendelea kudhalilishwa, kubaguliwa hata kuuana mashariki ya kati walipokwenda kusaka vibarua kama vile kufanya kazi za ndani, ulinzi na nyingine nyingi. Tunakaa kimya ambapo waswahili wenzetu wa kwenye nchi za maghreb yaani Algeria, Libya, Moroko, Tunisia, Mauritania, Misri na Jamhuri ya watu wa Saharawi wakiwauza waswahili wenzao utumwani. Tunakaa kimya pale waswahili wenzetu tena Weusi nchini Sudan ya Kaskazini wanapoukana uafrika na kujiita waarabu. Ni aibu kiasi gani?
Kadhia ya mashariki ya kati juu ya ukaburu na ubaguzi wa Israel imetugawa waswahili baina ya wakristo na waislam. Waislam walio wengi wanailaani Israel si kwa sababu inawatesa wanadamu bali kwa vile inawatesa waarabu na waislam ilhali wakristo wakiunga mkono Israel chini ya dhana hafifu na feki ya taifa teule. Wanadhani waisrael ni wakristo wenzao wakati siyo. 
        Tunapaswa kulaani kinachoendelea kwa misingi ya ubinadamu lakini siyo misingi ya udini.  Jinai, ubaguzi na ukaburu havina dini na kama vinayo basi ni dini ya shetani. Israel inayowahadaa waswahili kuwa inaweza kusaidia nchi zao nayo inaishi kwa misaada toka Marekani na mataifa ya magharibi. Isitoshe, Israel inawabugua hata watu Weusi. Waulize waethiopia waitwao mafalasha waliodanganywa wakahama nchi yao na kwenda kuishi Israel wanakobaguliwa kwa kisingizio kuwa wao ni waisrael Weusi. Hakuna kitu kama hicho zaidi ya ujinga na ubabaishaji wa kawaida ambao unatokana na ujinga, roho mbaya na uroho. Al Jazeera (Machi 28, 2018) licha ya kuripoti maandamano ya mafalasha kupinga ubaguzi linasema kuwa kiongozi mmoja wa kiyahudi rabbi Yitzhak Yozef aliwaita watu weusi nyani kwenye kwenye mahubiri yake mnano tarehe 17 Machi, 2018.
        Mbali na mafalasha, wakimbizi wa kiafrika walioko Israel wanateswa na kubaguliwa sawa na walivyofanyiwa wenzao wa Afrika ya Kusini chini ya ukaburu. Mwaka 2013, mkimbizi  Hatftom Zarhum toka Eritrea aliuawa na kundi la wayahudi na hakuna alichukuliwa hatua. Badala yake watu wanne waliohusika na mauaji haya walipewa adhabu ya kifungo cha nje na kutoa huduma za kijamii kana kwamba aliyeuawa alikuwa mbuzi. Kwa mujibu wa Al Jazeera, mwaka 2014 vijana wawili wa kiyahudi walimuua msudan  Bbikir Ali Adham-Abdo (40)  na hawakufungwa kwani walipatikana na hatia ya kuua bila kukusudia pamoja na kufanya mauaji ya dhahiri.
        Tumalizie kwa kushauri kuwa kinachofanywa na nchi za kiafrika tokana na ujinga zijue kinachoendelea dhidi ya waafrika nchini Israel na kuchukua hatua. Kama wanachofanya ni tokana na roho mbaya, ubinafsi na ujinga, hatuna cha kufanya bali kuwakumbusha kuwa wanashiriki jinai na ni unafiki wa kunuka tena kujidhalilisha na kuwadhalilisha na kuwachuuza waafrika wote.
Chanzo: Raia Mwema leo.

No comments: