Katika mifumo mingi ya elimu duniani, vijana wengi hubarehe au kuvunja ungo wakiwa kwenye ngazi ya sekondari. Kisaikolojia hii kipindi hiki huitwa foolish age na mambo mengi yanayofanyika hapa yanaweza kuwa foolish things au mambo ya kiwanagezi kama kuitana majina kama njuka, nyuka na mengine mengi kulingana na mahali aliposomea mtu. Kimsingi, njuka au nyuka ni mwanafunzi mgeni wa kidato cha kwanza katika vipindi viwili vya awali. Kwani afikapo muhula wa mwisho, hujiandaa kuwa mzee yaani kidato cha pili ambaye kazi yake ni kuwachangamsha kwa njia ya adhabu na vitisho kidato cha kwanza watakaomfuatia.
Kwa uchache, nataka nijikite kwenye neno njuka au nyuka na namna lilivyotumika ili tuone kama lifaa kutumiwa na waheshimiwa wabunge. Nakumbuka nilipokuwa njuka nilivyokuwa nahitaji mzee anilinde ili wasinihenyeshe. Hiki huwa kipindi kigumu ambapo woga na mateso hutawala. Nakumbuka mwenzangu alivishwa khanga na mzee akimwimbia na kutaka aitikie kama mkewe. Pia nakumbuka walimu walivyokuwa wakiwawinda wazee uchwara ili waache kufanya uonevu. Nakumbuka pia tulipojaribu kumchangamsha njuka wakati ndo tumeingia kidato cha pili. Huyu jamaa alikuwa mkubwa kwetu akaamua kutushushia kipigo pamoja na kushirikiana tukaamua kutoka mkuku au unyayo kama tulivyozea kusema. Yalikuwa na maisha na mambo ya kitoto ambayo hayana umuhimu wala sababu za kuyakumbuka kiasi cha waheshimiwa wabunge kuyaendekeza. Mara nyingi, tokana na vipigo vya hawa njuka, wapo waliowaumiza hata wengine kuua wenzao huku wengine wakipata suspension na wengine kufukuzwa moja kwa moja tokana na upumbvu wa foolish age. Hii haiwezi kuwa sifa wala lugha ya wabunge waheshimiwa hata kidogo. Kuna tatizo tena kubwa tu hata kama wahusika hawalioni. Waheshimiwa wana mambo mengi ya msingi ya kufanya na siyo kuitana majina ya ajabu ajabu na aibu kama njuka, mswaki na mengine kama hayo. Nampongeza mbunge Jerry Slaa (Ukonga-CCM) aliyekerwa na kukemea matusi haya ya wazi kabisa.
Katika kikao cha bunge kinachoendelea, nilimsikia mbunge wa viti maalum akimuita mbunge mwenzake, tena wa kuchaguliwa njuka. Mwanzoni nilishangaa. Ila pale mbunge mwenzake alipotaka kujua maana ya njuka, ndiposa nikaelewa na kuendelea kushangaa na kusikitika. Swali la kwanza lililonijia ni kwanini wabunge wetu ambao hupenda kuitwa waheshimiwa wanatumia lugha ya kihuni kama vile ambayo tuliitumia tukiwa kwenye foolish age kana kwamba nao wako kwenye foolish age? Kama mimi, mbunge aliposikia neno njuka alitaja ajulishwe maana yake. Ndipo alipojibiwa “si unajua umeishia darasa la saba mwanangu… huwezi kuijua” alisema Mbunge wa kuteuliwa (CHADEMA), Halima Mdee akimjibu mbunge wa Joseph Kasheku (Geita Vijijini-CCM). Ajabu ya maajabu, badala ya mbunge kuona aibu, alimjibu kimasihara huku mheshimiwa spika naye akicheka kwa majibu ambayo kimsingi yalipaswa kumhuzunisha mtu yeyote aliyekomaa na mwenye heshima.
Tokana na mapungufu haya, kwanza najiuliza: Kwanini wabunge wajilinganishe na vijana ambao wako kwenye umri wa kupevuka (puberty stage)? Kwanini wanajilinganisha na watu ambao wako kwenye foolish age na siyo wanachuo hata wanajeshi kama wana shida ya kujilinganisha. Je hawa njuka nao wanapigwa na kulowanishiwa viti vyao ukiachia mbali hata wengine kunyang’anywa masurufu yao kama inavyofanyika kwenye unjuka kweli ambao kalinye ya kule asikwambie mtu. Je nao wanatembezeana undava na makandokando mengine?
Kwa wanaojua jukumu la mbunge, watakubaliana nasi kuwa mbunge ni mbunge bila kujali ana miaka mingapi amehudumu bungeni. Kwanza, mbunge huwawakilisha wapiga kura na wananchi wake wakati njuka anawakilisha tumbo lake na familia yake iliyomtuma kwenda shule.
Pili, wabunge ni watu waliokomaa kiakili n ahata wengine kitaaluma. Hivyo, kujilinganisha na watoto wa sekondari ni kujidhalilisha na kulidhalilisha bunge na kazi zake kwa umma bila kusahau hadhi yake.
Tatu, hata lugha ya huyu kamalizia la saba na mwanangu ni lugha za kihuni ambazo hazifai kutumiwa na wawakilishi wa wananchi wa Tanzania. Sasa kama hawa wenye shahada moja au mbili wanawadharau walioishia la saba, na madaktari na maprofesa nao wawafanye nini hawa?
Nne, je neno hili la utani tena wa kumdhalilisha anayeitwa ni la kibunge? Je linastahiki kutumika kwenye ukumbi wa bunge tena wakati mheshimiwa akichangia? Je bunge la namna hili linawafundisha nini vijana wetu ambao wangetaka kuwa wabunge kesho? Haya ni baadhi ya maswali tunayopaswa kujiuliza na ikibidi kuyajibu kwa usahihi ili kesho tusije kusikia wawakilisha wa wananchi wakiitana majina ya aibu zaidi ya haya. Hivi mtu anayemwita mheshiwa mwanangu atashindwa kumtupia matusi ya nguoni kama vile msexxxyz ambalo kwa wahuni wa mjini ni neno la kawaida? Je tukifikia hapa bunge letu litaweza kuendelea kuwa na hadhi na sifa ya kuitwa tukufu? Chonde chonde jamani. Tanianeni lakini msifanya bunge letu tukufu lianze kuonekana kama tukutu. Kwa faida gani na ya nani?
Naomba kumalizia makala haya kwa kuwaomba wabunge kwanza waelewe nimesukumwa na uchungu na uzalendo kuyaona yale ambayo tulioko nje ya uwanja tunayaona kuliko wachezaji. Pia kwa wivu wa hadhi ya chombo hiki, nimejikuta siwezi kuangalia hizo clips za matusi haya na kujinyamazia kama mtanzania anayelipenda na kulithamini taifa lake. Kwa ufupi ni kwamba huu ni ushauri wa bure kwa waheshimiwa wabunge. Tafadhalini, chukueni tahadhari kabla ya kutumia maneno mkizingatia kuwa nyiny–––kama viongozi na wawakilishi wa wananchi–––ni kioo cha jamii. Wengi tunawangalia na kuwasikiliza kwa makini kujua na kuona kama kweli mnatuwakilisha au mnajiwakilisha.
Chanzo: Raia Mwema Aprili 28, 2021.
No comments:
Post a Comment