The Chant of Savant

Wednesday 12 May 2021

‘Wazee wa Dar’ ‘Uwakilishi Maalum’ Ni Ujima na Ukoloni Mamboleo


Hivi karibuni rais Samia Suluhu Hassan (SSH) alikuwa na mkutano na wazee wa Dar es Salaam. Waandaaji wa mkutano huo na mheshimiwa rais ndiyo wanaojua mantiki na sababu ya kuchagua wazee wa Dar na si wazee wa eneo jingine kama vile Dodoma ambapo ndiyo makao makuu ya nchi. Sina ugomvi na wazo wala mkutano wa mheshimwa rais kukutana na wazee wa Dar wakati wowote na kwa sababu yoyote ikimpendeza. Hata hivyo, nina maswali. Kwanini wazee na wazee wa Dar na si wa Dodoma au mkoa mwingine? Je ni sababu na vigezo gani vilivyotumika kuteua wazee wa Dar mbali na wao kujifanya wawakilishi wa wazee wote nchini? Je hao wanaodai kuwawakilisha waliwachagua? Na kama waliwachagua,wamechauguliwa vipi? Je kweli wazee wa Dar waliwakilisha wazee wote nchini? Tungefurahi kama maswali haya yangejibiwa au kufikiriwa wakati mwingine mheshimiwa rais atakapoamua kukutana na wazee. Pia afanye mpango wa kukutana na vijana ambao ndiyo injini inayotekeleza busara na ushauri wa wazee kama vipo katika utawala wa haki na sheria.
        Kubwa lililojitokeza kwenye mkutano tajwa ni kwa rais SSH kutoa onyo kwa wanaotaka kurejea jinai ya zamani. Alikaririwa akiwaaminisha wananchi akisema “leo nimesoma mtandaoni, Dar es salaam kuna watu wanajaribu kupima kima cha maji, vijiujambazi ujambazi na uporaji vimeanza kuja juu, naomba nitoe meseji wasijaribu kupima kina cha maji, IGP upo hapa, mitandaoni wanamtaja afande mmoja kuwa alikomesha ujambazi, wanasema mama turudishie, IGP kaliangalie hilo vizuri.” Nampongeza rais kwa kulisemea hili. Hata hivyo, kulisemea na jambo moja na kutekeleza ni jambo jingine.
         Jambo jingine ni ile hali ya wazee wa Dar kutaka nao wapewe nafasi za upendeleo kwenye taasisi za maamuzi kama vile mabaraza ya miji, bunge na megineyo. Hili halina tija zaidi ya kuturudisha kwenye ujima na kutoendelea ukiachia mbali kupendeleana na kubaguana. Litaongeza mzigo kwa walipa kodi ukiachia mbali kutokuwa na umuhimu wowote. Wakati tunapendekeza kubana matumizi na wengine wakitaka ianzishwe kodi ya uzalendo, inabidi tuangalie kubana matumizi na siyo kupanua na kuzidi kumuumiza mlipa kodi maskini. 
         Tunachopaswa kufanya ni kujiuliza. Kwanini viti maalum, umaalumu upi wakati wote wana changamoto? Leo tuna viti maalumu vya vijana, wazee, wasomi walemavu ambao hawamwakilishi yeyote zaidi ya matumbo yao. Kwani, wizara husika zitafanya kazi gani? Je tutabaguana na kupendeleana ili iweje na kwenda wapi? Tuweke mfumo wa haki wa kushindania fursa badala ya kutegemea hisani. Maana, kila jimbo lina kila aina ya watu hawa wanaopewa uwakilishi wa kupendelewa. Kila jimbo lina wazee, wanawake, walemavu na vijana ambao wanawakilishwa na mbunge wa jimbo ukiachia mbali kuwa na wizara maalum kwa ajili ya watu hawa. Je hawa wabunge¬¬¬–––kama siyo kuendelea kuwagawanya watu wetu na kuendelea kuwafanya tegemezi ili wasione matatizo yao na kuyatatua–––wanamwakilisha nani kama hawa wanahitaji wawakilishi maalum.
        Kesho tutaambiwa vinahitaji viti vya uwakilishi vya watoto, wanajeshi, madaktari, waandishi wa habari, wasomi, wakunga, wagonjwa, wazururaji hata makahaba. Hivi viti havina tija na vinatuchelewesha na kutufanya tuwe wavivu wa kufikiri. Rejea vinavyoliaibisha bunge kwa sasa ambapo wabunge waliotimuliwa na chama chao wameng’ang’aniwa na bunge wakati hakuna wanayemwakilisha ukiachia mbali kuwa pale kinyume cha sheria. Rejea walivyopewa majina mabaya kama vile Covid-19. Hii yote inaonyesha kutohitajika kwao katika mfumo wetu wa kiutawala. Tunahitaji kujikomboa pamoja na taasisi zetu.kama hivi viti ni dili, kwanini wale tunaoona wameendelea hawana hivi viti? Rejea ukweli kuwa nchi za magharibi zimeendelea kwa kuweka mazingira ya haki na mfumo wa kupigania fursa za uongozi bila kuangalia jinsia au hali maalumu. Huku hakuna viti maalum vya aina yoyote. Kwani, watu hawataki wala kutegemea upendeleo au umaalum. Hata kuteuliwa kwa rais SSH kuwa makamu wa rais na hatimaye rais si kwa sababu ni mwanamke. Hapana, ni kwa sababu ni binadamu, mtanzania na mwenye sifa zinazofaa. Angekuwa hana uwezo angechaguliwa eti kwa vile ni mwanamke? Hata haya maneno ya ni rais mwanamke ni upuuzi. Huyu ni rais wa Tanzania basi. Naye anapaswa kujisikia na kujichukulia hivyo. Hakuna mwenye haja na jinsi ya mtu. Hata sheria inapokuwa ikifanya kazi yake, haiangalii jinsia wala umri wa mtu ukiondoa ule wa watoto. Ukifanya makosa unashughulikiwa kama rais basi.
Wazee waliutumia uzee kutaka waonewe hisani ili kuboresha maisha yao. Kwani hawakujiandaa? Je viinua mgongo walivyopewa baada ya kustaafu vitafanya kazi gani? Kama kuna changamoto basi wanayo vijana na walemavu kuliko mtu yeyote. Andaeni mazingira safi badala ya kupeana upendeleo usio lazima
Hakuna haja ya kukamuana na wapiga simu au wengine kutafuta kodi ya uzalendo zaidi ya kubadili mfumo wetu wa kikoloni na tegemezi. Nini kifanyike? Andaeni mfumo bora wa haki na huru unahimiza ushindani wenye tija.Mfano hapa Kanada, kila mtu ana bima. Hivyo, hakuna mawazo tegemezi ya kutegemea upendeleo au umaalum bali ithibati. Mzee, mtoto, mtu mzima, kijana, na wengine wote wana bima ya Afya. Hawahitaji upendeleo na hakuna upendeleo. Kuna haki badala yake. Hakuna anayetaka kupendelewa bali kutendewa haki bila kujali jinsia wala nini isipokuwa wanaobaguliwa na kunyonywa kimfumo kama wananchi wa asili ya hapa, wageni na wengine ambao mfumo huwahimiza na kuwafanya wawe tegemezi na mzigo kwa hasara yao huku wanaowatawala wakiendelea kuwaibia wakitajirika na hawa wakizidi kuwa maskini. Huu ni mfumo wa kikaburu ambao umefumbiwa macho hapa nchini. 
Kimsingi, haya mambo ya upendeleo, licha ya kukinzana na uhalisia na sheria na usawa wa binadamu, ni aina fulani ya ukoloni. Hakuna nyenzo na zana zinalisha na kunufaisha mfumo wa kikoloni kama utegemezi. Rejea viinchi vidogo kama Ufaransa, Uholanzi na Uswisi vinavyosaidia Afrika wakati imejaliwa raslimali zenye thamani lukuki. Mfumo huu umejengeka kimataifa kwenye dhana ya ufadhili na ufadhiliwaji ambapo mwenye kufadhili ana nguvu juu ya yule anayemfadhili. Japo Hayati rais John Pombe Magufuli hakuliona na kulielezea kama nifanyavyo, aliweza kupiga vikali dhana ya umaskini na utegemezi wakati tumejaliwa raslima zenye thamani lakini tukashindwa kuzitumia kiakili na vilivyo.
Tumalize kwa kumshauri rais SSH asiingie mtego wala kufanya huruma ya hata kufikiria kutoa upendeleo kwa wazee. Hata hivi viti maalum vya sasa vinavyoanza kuumbua chama chake, angeviondolea mbali na kujenga mfumo wa haki wa ushindani ambapo wanaume na wanawake watashindana kwa haki ili kukomesha mfumo dume na wa kikoloni. Hili linawezekana. Rejea wanawake wawili wanaowakilisha vyama upinzani bungeni walivyochaguliwa bila kupendelewa na kuwabwaga wanaume. Rejea hata SSH alivyowabwaga wanaume na kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Hayati Magufuli. Si kwa sababu ni mwanamke. Ni kwa sababu ana sifa zilizokamilika za kuongoza basi. Hivyo, basi, wazee wa Dar na wale wanaolilia au kutegemea viti vya uwakilishi nisameheni. Fikiria juu ya kuunda mfumo wa haki utakaoleta maisha bora kwa wote badala ya kila kundi kutaka upendeleo. Hivi viti havitatua matatizo yenu sana sana vitaendelea kuwagawanya na kuwadhoofisha. Ni ushauri tu wa bure.
Chanzo: Raia Mwema leo.


No comments: