The Chant of Savant

Tuesday 11 May 2021

Jafo Jitathmini kwa Hili la Takataka

Waziri Seleman Said Jafo (Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira) aliiacha dunia hoi na maswali mengi yasiyo na majibu pale alipokaririwa na vyombo vya habari akitoa siku kumi kwa wanaohusika na kuingiza takataka hatarishi nchini–––kwa kisingizio cha kuingiza shisha–––kuwa wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria. Waziri aliiacha dunia hoi si kwa agizo wala tamko lake bali ile hali ya kuwa na taarifa lakini akaacha kuzifanyia kazi na badala yake akatoa tamko tata tena lenye kuweza kuwastua wahusika wakaishia.Je waziri hakujua wala kuliona hili? Kwanini kama kweli hakuna namna?  Bwana Jafo alisema ana taarifa kuwa mhusika kwenye sakata hili la taka hatalishi alishaingiza makontena 500 yenye uchafu hatarishi? Je kwanini hukutoa taarifa Takukuru na vyombo vingine vya usalama kwanza wakamkamata mhusika ndipo ukatangazia umma? Je waziri alikuwa na haraka ya nini kama siyo kumuonya mtuhumiwa aishie ili mambo yaishe wakati ana taarifa na uwezo wa kufanya hivyo kabla ya kutoa tip inayoweza kuwastua wahusika wakakimbia nchi? Je namna hii tunaweza kukomesha mabaya kama wanaopaswa kuyazuia wanakurupuka na kutoa maagizo na matamko ambayo kimsingi, hayalengi kutusaidia kama taifa bali, kwa kiasi kikubwa kuwa ni kama PR?
        Je  waziri alishauriwa vibaya au kuna namna ya kumstua mhusika aishie na kuwaachia uchafu wenu? Kama taifa, tuna kila sababu na haki ya kuuonyesha ulimwengu kuwa sisi siyo taifa la hovyo kiasi kugeuzwa jalala la kila uchafu tena hatarishi kwa watu wetu na taifa kwa ujumla.
        Maswali nimengi kuliko majibu. Je Tanzania imeharibikiwa kiasi hiki kiasi cha kuhitaji kiasi kikubwa hivi cha shisha? Je shisha nalo ni uwekezaji wakati ni haramu nchini? Hata kama kweli tunahitaji uwekezaji, kweli tumefikia kiwango hiki cha hovyo cha kuhitaji uwekezaji katika shisha bangi na mihadarati?
         Kwanza, hata hao walioingiza uchafu huu, ima hawakutumia akili, au wana namna wamechezea au kudharau vyombo vyetu vya usalama kiasi cha kujiamini hivi. Maana haiingii akilini kuingiza kiasi hiki cha taka bila kuwa na namna ya kufanya hivyo bila kuhofia umakini na weledi wa vyombo husika. Kuna haja ya kuunda tume huru ya kuchunguza kadhia hii ili kujiridhisha kuwa hakuna nyingine kama hizi na kama zipo zimefanyika kwa muda gani na kuleta madhara gani kwa taifa.
        Je hao watumishi wa umma ni nani, wangapi na wametenda jinai hiik wa muda gani? Ikiwezekana kuna haja ya kujua mbinu waliyotumia kutenda jinai hii kwa taifa letu na watu wake. Je ni wanagapi watakimbia nchi baada ya waziri–––ima kwa bahati mbaya hata makusudi, japo hatuamini hivyo–––kuwastua huku akidhani analisaidia taifa wakati anawasaidia wao? Je kwa uzembe huu wa wazi, waziri anajitathmini vipi ili kuitendea haki nchi na ofisi yake? Maana, haiingii akilini umkute ndege anakaribia kunasa kwenye mtego halafu umstue aruke na kupotelea mbali nawe useme ulikuwa na lengo la kumkamata. Je waziri hajui kuwa simba mwenda kimya ndiye mla nyama? Waziri alikuwa na haraka gani hadi anachukua hatua za kinadharia badala za vitendo? Japo siyo mawazo  wala imani yangu, ‘haraka’ ya waziri inaweza kuchukuliwa vibaya kuwa alitaka aonekane mchapakazi bila kuchapa kazi katika kadhia hii au kuna namna. Au ni ile hali ya baadhi ya watendaji kufanya kazi kwa kutumia kamera na kutoa maagizo makali makali wakati hawafuatilii hata hayo maagizo? Tukubaliane. Hapa kuna tatizo tena kubwa tu. Sitaki niseme waziri alikurupuka japo wapo watakaoamini hivyo kulingana na hali inavyojidhihirisha. Hasha. Hata hivyo, hakutendea haki habari au tips alizopata kuhusiana na kadhia tajwa. Hakuwa na haja ya kufanya haraka, kama kweli alidhamiria kukomesha mchezo huu kwa kuhakikisha anakusanya ushahidi wote na kuwashika watuhumiwa ndipo akatangaza.
        Namuomba Mheshimiwa waziri husika ajitathmini. Kama atashindwa, basi mheshimiwa rais aingilie kati ili liwe somo kwa wengine waache ima kukurupuka, kutuchezea shere kama siyo kuwapo namna. Maana mheshimiwa rais aliahidi kwa ukali kuwa ukimzingua mnazinguana. Ukisikia kuzinguana kwenyewe ndiyo huku hata kama ni mtihani mkubwa kwa rais. Tunataka na tunastahili matendo na si matamshi matupu yanayoweza kutoa mwanya kwa wanaotuhujumu kukimbia nchi. Je waziri alishindwa kuliona hili kweli au kuna kitu kimemziba macho asilione jambo jepesi kama hili lisilotaka hata stashahada wala cheti kuling’amua? Je kunani hapa kama tutakuwa wakweli. Maana, haiwezekani waziri akafanya kama alivyofanya asijue madhara ya kufanya hivyo.  Tunaamini waziri anajua kazi yake vizuri kama kiongozi wa umma na raia wa Tanzania. 
        Huwa sipendi kurejea mfano huu. Kwa wanaokumbuka sakata la Chavda wakati wa awamu ya pili watajikumbusha namna alivyoliibia taifa pesa nyingi ambapo badala ya kukamatwa, aliamrishwa aondoke Tanzania ili kuepuka kuwaumbua alioiba na kugawana nao au tuseme waliomtumia kama mbuzi wa kafara.  Je nani wako nyuma ya mchezo huu mchafu ambao waziri anapaswa awajue kwa vile alisema ana taarifa za kila kitu. Je namna alivyojua kuwa mhusika aliingia nchini kama mtalii na kujigeuza mwekezaji wakati ni ‘kanjanja’ kama alivyosema waziri, atashindwa kujua waliowezesha mchezo huu mchafu?
        Tumalizie kwa kumtaka waziri ajitathmini akijua fika kuwa maagizo yake yalitolewa kwa pupa kiasi cha kuweza kuhatarisha harakati za kuwakamata wahusika wa kadhia hii. Si vizuri kurudia makosa kama yale yaliyotajwa kwenye kisa cha Chavda. Kuna mengi tunapaswa kujua toka kwa waziri pia juu ya ni kwanini mchezo huu mchafu umekuwa ukiendelea bila vyombo vyetu vya usalama kustuka na kuchukua hatua stahiki. Mheshimiwa Japo, kuna kila haj ana sababu ya kujitathmini ili haki itendeke na taifa letu liwe salama na siyo kichwa cha mwendawazimu walevi kujifunzia kunyoa. Kama utafanya hivyo, licha ya kutoa soma, kuwajibika na kuonyesha usafi na ‘umakini’ wako, utaliepushia taifa kashfa na hasara visivyo vya lazima.
Chanzo: Raia Mwema kesho.

No comments: