The Chant of Savant

Friday 21 May 2021

Wanaomlaumu Wampe Muda Rais Samia

Baada ya kifo cha ghafla cha rais  Dkt John Pombe Magufuli na makamu wake Samia Suluhu Hassan kuapishwa kuchukua nafasi yake, wengi tulidhani lau watu watamwacha Magufuli apumzike kwa amani. Pia tulidhani, baada ya Samia kuvaa viatu vikubwa na vizito alivyoacha Magufuli, naye angeachwa atimize wajibu wake. Lakini hali inavyoonyesha siyo hivyo. Ukipita kwenye mitandao unakutana na maneno ya kikabila, kizushi na kipumbavu kama Sukuma Gang, Mataga na mengine mengi yote yakihusishwa na Hayati Magufuli. Pamoja na kwamba Magufuli hatarudi tena, kuna watu wa ajabu wanaoendelea kumtukana na kumkejeli kana kwamba watamuumiza wakati wanajiumiza na kuonyesha upumbavu wao. Wanashindwa kuwa akili na muda wanaotumia kufanya hivyo, vingetumika kujikomboa ingekuwa faida kwao.
Mbali na Hayati Magufuli, mwingine anayesakamwa wazi wazi kwenye mitandao na kisirisiri na baadhi ya taasisi–––tena nyingine nyeti katika jamii–––ni rais SSH. Tangu ashike ukanda na kuonyesha anavyoumudu kweli kweli, hajakosa maadui ambao kimsingi, wengi ni wale waliiomchukia mtangulizi wake ambao ima walimgwaya au walimlaumu kisirisiri au kujificha nyuma ya unafiki wa kumkweza hadharani wakati wakimponda nyuma ya pazia. Hata siku mia ofisini hajamaliza, wengi wameishaanza kumlaumu hata kumzushia SSH. Rafiki yangu mmoja aliposikia na kusoma baadhi ya mashambulizi kwa SSH aliniandikia ujumbe huu “hata sielewi zaidi ya kuona ni unafiki wa kiwango cha lami. Saa hizi watu wanapinga kila kitu na kukitafutia kasoro. Chanjo wanasema haifai wakati wameambiwa ni hiari kwa raia ila watumishi sekta nyeti hakuna hiari.” Hapa rafiki yangu alikuwa akishangaa namna watu walivyoshupalia chanjo ya corona. Wapo ambao hawajaamini kuwa mwanamke anaweza kuwa rais wa Tanzania na akafaa. Wanasahau kuwa Tanzania siyo Vatican ambayo siku zote hutawaliwa na wanaume na mfumo dume. Sasa SSH ni rais kamili wa Tanzania kwa mujibu wa katiba, kanuni na sheria hadi uchaguzi ujao watake wasitake. Ingawa wanachotaka kufanya ni kumuonyesha kuwa hafai. Wao wanapinga kwa sababu wazijuazo mojawapo ni ile hali ya kutaka tuendelee na msimamo wa kuwa Mungu atatuponya wakati serikali haipingani na hili bali kuongezea kuwa wananchi watakaotaka kuchanjwa, wana hiara ya kufanya hivyo bila kuvunja sheria yoyote. Kwa wanaojua Mungu anavyofanya kazi kiakili, wanawashangaa watu wa namna hii. Mungu anasema kuwa humsaidia anayejisaidia. Hivi kweli uone simba anakuijia ili akutafune, nawe kwa upumbavu wako upige magoti au kusujudu ukitegemea Mungu atamzuia simba asikutafune? Huku ni kumjaribu Mungu. Na Mungu katika mazingira kama haya atafanya kazi moja tu. Kumruhusu simba akutafune ili ulipie upumbavu wako. Hivyo, wanaompinga au kumlaumu rais kuhusiana na corona wanamuonea hasa ikizingatiwa kuwa serikali yake haijamzuia yeyote kuamini aaminivyo au kuchanjwa au kutochanjwa.
Jambo jingine linalotia kichefuchefu ni uongo wa mchana. Huu ni pale alimpomteua CP Salum Rashid Hamdun kuwa mkurugenzi wa Tume ya Kuzuia na Kupambana na  Rushwa (TAKUKURU) makelele yalisikika kuwa kamteua mzanzibari mwenzake wakati maskini Hamdun mwenyewe ni msukuma mwenye damu ya kimanga. Nadhani hapa kilichomponza ni rangi na jina lake vinginevyo, bwana huyu hana nasaba yoyote visiwani. Hata angekuwa mzanzibari, kwani kuna sheria inayomzuia kuwa mkurugenzi wa TAKUKURU? Kesho sitashangaa kusikia kuwa rais SSH anawapendelea akina mama hata wazanzibari hata waislam katika teuzi zake japo wote ni watanzania tena wenye sifa. Huwezi kuwa na watanzania wasio na sifa hizi.
Kama haitoshi, mnamo tarehe 8 Aprili, 2021, rais SSH alimtuma rais wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar, Dkt Hussein Ali Mwinyi kumwakilisha kwenye kikao cha SADC juu ya masuala ya ulinzi kilichofanyika Maputo Msumbiji. Wakosoaji wasiojua kitu wala kuheshimu haki na uhuru wa rais kumtuma amtakaye kumwakilisha walisema walipiga makelele wakiona kama ukiukwaji wakati–––kama tutakuwa wakweli na weledi–––tutakubaliana na ukweli kuwa Dkt Mwinyi ni mzoefu wa masuala ya ulinzi ukimlinganisha na SSH na makamu wake Dkt Philip Mpango. Dkt Mwinyi ni mtanzania aliyeshika wadhifa wa waziri wa ulinzi kwa muda mrefu. Hivyo, rais alimtuma, mbali na kuwa haki ya rais (prerogative) si kwa upendeleo bali kwa kutambua uzoefu na ujuzi wake katika masuala ya ulinzi ya kitaifa na kimataifa. Wapo waliohoji itafaki katika kusafiri wakasahau kuwa Dkt Mwinyi ni namba tatu katika safu ya uongozi wa kitaifa. Mbali na hili, iwapo waziri wa mambo ya nchi za nje anaweza kumwakilisha rais, inakuwaje nongwa rais wa BMZ kumwakilisha rais wakati wote ni marais? Kweli, akutukanaye hakuchagulii tusi. Hivyo, wanaomkosoa rais hapa, wanaonyesha kutokujua kwao mambo haya yanavyokwenda ukiachia mbali ngoa na chuki vya kawaida.
        Jana nilikuwa nawasiliana na rafiki yangu aliyepo Dar es Salaam ambaye ni kati ya wale wasioona zuri lolote serikali ya SSH na CCM inaweza kufanya. Mojawapo ya habari aliyotaka kunijuza ni madai kuwa barabara ya kwenda Mwenge  kutokana na kile alichosema kuwa alikuwa amesikia kuwa rais SSH alikuwa ameshindwa kuwalipa wakandarasi. Hili lililenga kumdhoofisha rais aonekane kutofaa kuongoza nchi na kuendeleza miradi ya mtangulizi wake wakati juzi juzi tu aliliahidi taifa kuwa hakuna kitakachoharibika. Baada ya kumaliza kuongea na huyu rafiki yangu, nilimpigia mwingine ambaye kimsingi, huwa si mhafidhina katika kuidurusu serikali. Alichonijuza huyu rafiki yangu kiliniacha hoi. Kwani alisema kuwa akiwa anakwenda zake nyumbani, alipita barabara tajwa na kuacha mafundi wakiwa kazini. Hivyo, alisema hajui hiyo barabara niliyokuwa nikiongelea. Baada ya kupima taarifa za pande mbili, niliwasiliana na rafiki yangu ambaye ni mwandishi wa habari. Naye alithibitisha kuwa hakuna kitu kama hicho yaani serikali kushindwa kulipa.
        Tumalizie kwa kuwataka wale wote wanaoona kuwa ni haki yao kuzusha na kulaumu wampe rais muda wa kutimiza majukumu yake. Kama wana lolote linalowakera, si kuna uchaguzi ujao. Kwa wanaojua vizuri siasa za Tanzania, watakubaliana nami kuwa kinchoendelea ni siasa za makundi zilizotamalaki nchi ambapo makundi tofauti ya kimaslahi hupingana kutaka kudhoofisha ili kupitisha mtu au watu wao. Makundi haya, hata yanapojikuta hayana namna ya kupenyeza mtu wao, huendelea kuzusha hili na lile ilmradi ima yajiridhishe kuwa yanawadhoofisha wapinzani wao au wale wasiowataka kwa vile hawalindi maslahi yake au wanaandaa mazingira mazuri ya kupata nafasi wakati ukifika. Kwa wanaofuatilia utendaji wake, SSH anafanya vizuri tena ndani ya muda mfupi. Mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni. Mama anajitahidi. Ila mjue kuwa SSH siyo JPM. Na hatakuwa hivyo bali kubaki kuwa alivyo kama binadamu na rais wa Tanzania. Akifanya kama JPM bado atalaumiwa. Na hata anapotenda kama SSH bado atalaumiwa. Hapa cha mno ni kwa SSH kuziba masikio na kufanya yale anayoona yanafaa kwa taifa kwa mujibu wa katiba.
Chanzo: Raia Mwema leo.

No comments: