The Chant of Savant

Tuesday 1 June 2021

Tunamtaka Mchwa Anayetafuna Fedha Serikalini

Japo sina uhakika kama kuna pattern katika upigaji ulioibuliwa na waziri mkuu Mheshimiwa Majaliwa K. Majaliwa hivi karibuni, kuna uwezekano kukawa na mchezo huu katika wizara nyingine kama siyo zote. Kwanza, kabla ya kuzama kwenye kadhia hii, niipongeze serikali kwa kuwa macho hasa baada ya kuondoka simba wa vita dhidi ya ufisadi. Nasema hivi kwa kuzingatia kuwa wizi ulioibuliwa hivi karibuni kwenye hazina, ulifanyika nchi ikiwa kwenye maombolezo ya kifo cha Dk John Pombe Magufuli (RIP). Hii licha ya kuonyesha roho mbaya na ubinafsi vya kutisha, wahusika ni kama wanasherehekea kuondoka kwa mwamba huu. Hili halina shaka. Kwani, tangu kilipotangazwa kifo cha gwiji huyu–––tumeona kwenye mitandao ya kijamii–––namna mafisadi au vibaraka wao walivyoshangilia wasijue kuwa kuondoka kwa shujaa mmoja ni ujio wa mwingine. Nani alijua kuwa hili lingeibuka na kufichuliwa haraka na kisayansi hivi? Hata hivyo, kwa namna serikali ya awamu ya sita inavyopambana na kuendeleza vita ya ufisadi kwa makini na weledi mkubwa, wale walioamini kuwa kila kitu kilitegemea juhudi na nguvu binafsi vya Hayati Magufuli wamezodolewa na wanakosea kuendelea kudhani hivyo. 
Wanaodhani kuwa kifo cha Magufuli ni mwisho wa vita ya ufisadi wanakosea sana. Wanashindwa kuelewa kuwa Magufuli hakuwa akipiga vita uoza kwa ajili yake binafsi bali kwa ajili ya taifa. Wanashindwa kuelewa kuwa serikali ni taasisi na siyo mtu mmoja yaani rais. Wanashindwa kuelewa kuwa somo ambalo ameliacha Magufuli litawafanya watanzania kuwa wakali kama pilipili wanapogundua uoza kama huu. 
Kama nilivyosema hapo juu kwenye kichwa cha makala, kuna haja ya kufanya uchunguzi kwenye idara, wizara hata mikoa, wilaya na halmashauri zote nchini ili kujiridhisha kuwa huu mchezo haukufanywa tokana na timming na ukubwa wa tukio lililohangaisha taifa zima tokana na kazi ya Hayati Magufuli ilivyotukuka kiasi cha kumgusa kila mtanzania mwenye mapenzi mema na nchi yake. Kwa wanaojua  namna Hayati Magufuli alivyokuwa amewabana na kuwatetemesha waovu nchini, hawatashangaa kuwa kifo chake kiliwadanganya wengi na kudhani wakati wa kurejea mazoea ya kuuibia na kuhujumu umma yalikuwa yamerejea.  Hata hivyo, matukio kama haya, licha ya kuizindua serikali, yaihimize kuongeza bidii katika kupambana nayo. Hapa lazima kazi ya kutumbua na kuibua waovu iendelee kama ilivyokuwa kwa hapa kazi tu na lazima kuendelea kutumua iwe ni hapa kazi tu.
Pia, itoshe kusema kuwa wale wote waliokuwa wanadhani kuwa kifo cha Magufuli ni kifo cha vita dhidi ya ufisadi wajue kifo chake kinaweza kuwa mwanzo wa vita kubwa kuliko hata aliyowahi kupigana dhidi ya janga hili. Maana, Hayati Magufuli alipoingia madarakani, alikuta nchi yetu imegeuzwa shamba la bibi ambako nyani hujifanyia watakavyo lakini akakomesha mchezo huu tena kwa muda mfupi na kwa kiwango kikubwa. Hii licha ya kuwa urathi wake, ni changamoto kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake kwa ujumla kuwa awamu ya sita, pamoja na mambo mengine, itapimwa kwa namna itakavyoendelea kuzuia taifa kuwa shamba la bibi.
Tunashauri uchunguzi wa kina ufanyike tena kwa utuo ili kubaini walioko nyuma ya kadhai nzima na mbinu walizotumia na kujua lini walianza mchezo huu ili kujua kama ni endelevu au ndiyo umeanza. Hii itasaidia kupambana na kadhia nyingine kama hizi hata kujua viashiria vya uwepo wa uchafu kama huu kwenye wizara ya fedha na wizara nyingine hata idara za umma.
Pia ifahamike kuwa kilichofanyika siyo ubadhirifu wala wizi wa kawaida bali uhujumu uchumi ambao kesi zake zinafahamika zisivyo na dhamana. Hii itasaidia kuwapa onyo wengine wanaodhani serikali ya awamu ya sita siyo makini kutia akilini kuwa kasi ni ile ile na saa nyingine ikawa zaidi hasa ikizingatiwa kuwa kurudi kwake kwenye uchaguzi ujao kutategemea na namna ilivyofanya kazi za kuuletea maendeleo umma wa watanzania. Hizi zinaoibiwa ni kodi za wananchi maskini ambao wakisikia mabilioni haya licha ya kusikitishwa ni kama wanatiwa madole machoni. Huu ni uchokozi kwao. Na unapaswa kukomeshwa mara moja ili kuweza, si kuwaletea maendeleo ya pamoja tu bali hata kupunguza ugumu wa maisha kwa watu na kaya binafsi.
        Tuhitimishe kwa kushauri Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kushikia kashfa husika kama mwewe ashukiavyo vifaranga ili kuwapa ukweli watanzania wawajue hawa walioshindwa kubadilika wakataka kuendekeza mazoea ya wizi. Wakati wa kifanya hivyo, wahakikishe wanashirikiana na polisi ili kuhakikisha zinapelekwa mahakamani kesi ambazo hazijabemendwa ili kuepuka kutoa mwanya wa wahusika kuchomoka kwenye kesi ya wazi wazi ya uhujumu uchumi. Tunawatakieni kila heri katika kuhakikisha ukweli unajulikana na pia haki inatendeka kwa pande zote.
Chanzo: Raia Mwema Kesho.


No comments: