The Chant of Savant

Friday 11 June 2021

Rais Samia Anajua Anachofanya Hababaishi

Hivi karibuni, rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha makucha yake sawa na mtangulizi wake Hayati John Pombe Magufuli. Alipoapishwa, wengi walidhani kwa vile ni mwanamama atakuwa legelege wasijue hakuteuliwa na kuweza kwenda na spidi ya Magufuli kwa makosa. Katika kuonyesha kuwa ana msimamo na anajua analofanya, alipoingia madarakani, alimtema aliyekuwa Katibu Kiongozi, balozi Bashiri Ally Kakurwa tena bila kupepesa jicho. Kwa kumuondoa Ally aliyekuwa amepanda vyeo haraka haraka–––tena akiwa ni mgeni kwenye chama na serikali–––kulimwonyesha kama mtu aliyependwa na kuaminiwa san ana Hayati Magufuli. Hata hivyo, hii haikumzuia rais SSH kumweka pembeni na kuanza kusuka timu ya kuchapa kazi.
Hatua ya pili iliyomwonyesha SSH kama mtu mwenye kujiamini na kujua anachofanya ni pale alipobadili baraza la mawaziri huku akiwapangua hata ambao usingetegemea mbali na kuwaingiza kwenye baraza ambao pia usingewategemea. Hii si kazi ya mtu anayebabaisha bali anayejua anachofanya. Hii si kazi ya mtu anayejaribu. Ni kazi ya mtu anayefanya kweli.
Kabla ya zege kupoa, rais SSH alimdondosha aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa. Hili nalo lilitoa onyo kwa wale waliodhani kuwa rais angekuwa mtu wa kutegemea kila alichofanya mtangulizi wake wasijue kuwa alishaandaliwa vilivyo. Hivyo, hakusita hata kidogo kufanya vitu vyake. Kama haitoshi, kabla ya Byakanwa kupoa, mara aliyekua mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya akaweka pembeni kupisha uchunguzi ambao mwisho wake ulimwacha na pingu mikononi huku akitumia muda wake wa kuwa nje ya ulaji korokoroni hadi kitakapojulikana. Kwa wanaojua mambo ya utawala na mabadiliko ya uongozi, walianza kutoa tahadhali kwa wengine wanaofanana na wale waliokwishanyolewa bila maji.
Baada ya rais SSH kufanya vitu vyake, wasiomtakia mema wala kumwelewa walianza kudhani hii ilikuwa nguvu ya soda kumbe siyo. Kwani, sakata la Sabaya likiwa bado moto si amemtumbua aliyekuwa mkuu wa Mwanza ambaye alikuwa amehamisha toka Mbeya. Nadhani alipoonya kuwa ukinizingua tunazingua, si wengi waliomwelewa. Kwa wale waliomwelewa, rais alimaanisha kuwa watu wachape kazi na kuhakikisha wanawahudumiwa wananchi tena wanyonge. Ni bahati mbaya kuwa rais SSH huwa haongei kwa ukali na amri ila kwa Kiswahili laini cha visiwani, jambo linalowafanya wachache waelewe hata pale anapokuwa amechukizwa na jambo au kuwa mkali. Kwa waliofanya kazi naye hasa wakati wa Bunge la Katiba watakwambia kuwa rais si mtu wa kutikisika wala kuonyesha hasira. Hii ikichanganywa na ile hulka ya makamu wake Dk Philip Mpango, inakuwa vigumu sana kwa walio chini yao kuelewa somo.
Ukiachia mbali kuwa vigumu kujua ni wakati gani rais amechukia, ni mtu anayejiamini  ambaye akiamua, hakuna atakayeweza kumyumbisha. Hivyo, mtu wa namna hii anahitaji watu makini na si wababaishaji au wenye kujipendekeza ili waendelee kwenye ulaji hata kama hawana sifa. Badala ya wao kuwa mtihani kwake, yeye ndiye mtihani kwao kama ilivyotokea kwa watumbuliwa hapo juu.
Mbali na kutoonyesha hisia zake wazi wazi, baadhi ya maamuzi ya SSH yanamwonyesha kama mtu anayetumia vitendo kutoa maonyo mbali na kuwaacha watu wasijue nini kitafuata. Kwa wasiojua ugumu wa kuongoza nchi ambazo zilishaoza kwa ubadhilifu na uoza, watasema rais anateua watu bila kujiridhisha wala kufanya vetting. Si kweli. Anachofanya hapa rais ni kuwaweka wateule kwenye tension ili watimize wajibu wao badala ya kuridhika na kuanza kupiga siasa na usanii. Nadhani hii inatokana na uzoefu wa muda mrefu ndani ya serikali. Kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake, SSH anawajua watu waliomzunguka mbali na kujifunza toka kwa mtangulizi wake kuwa siyo wote wasemao bwana bwana wanamaanisha. Wengine ni wachumia tumbo na wasaka tonge ambao wako tayari kumsifia yeyote ili mradi tonge liingie kinywani. 
Kutokana na kuwa mzoefu na mtu anayewajua wateule wake, rais haoni aibu wala sababu ya kutumbua wala kupangua kama kufanya hivyo kutaleta tija. Pia hii humuonyesha kama mtu anayekubali kufanya makosa na akasimamia kile anachokiamini. Bila hii nadhani SSH asingekuwa hapo alipo leo. Kwani, haikuwa kazi rahisi kuenenda na spidi ya Hayati Magufuli. Kama alivyohimili spidi na mikiki ya mtangulizi wake, nadhani watakaotaka kudumu naye lazima wahimili spidi yake na mikiki yake kadhalika. Inanikumbusha utani mmoja aliowahi kuutolewa na wasanii wa kikundi cha Redykyulass wakimuigiza aliyekuwa rais wa awamu ya pili wa Kenya Hayati Daniel arap Moi ambaye naye aliingia madarakani kama alivyoingia SSH baada ya kuwa makamu wa rais mwenye nguvu sana Hayati mzee Jomo Kenyatta aliyefariki madarakani mwaka 1978 na Moi kuchukua usukani na kuongoza taifa hilo kwa miaka 24. Alisema kuwa alipokuwa akiambiwa simama, aliruka. Hivyo, haikuwa vibaya naye kuwarusharusha waliokuwa chini yake baada ya kuwa rais. Hata Hayati Magufuli aliwahi kusema kuwa mkiaminiwa madaraka basi tawaleni.
Mwisho, tumalizie kwa kumpongeza rais SSH kwa kujiamini na kufanya maamuzi magumu bila kujali malalamiko wala manung’uniko au kuwaangalia watu usoni. Namna hii, kweli ‘KAZI IENDELEE’ kama ilivyokuwa kwa ‘HAPA KAZI TU.’ Ndugu rais, pale utakapoona panalegalega piga chini ili kazi iendelee na Tanzania isonge mbele.  Nakusalimieni kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jibuni. Kazi iendelee.
Chanzo: Raia Mwema Kesho.


No comments: