How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Monday, 7 June 2021

Tuwanyonge au Kuwafunga Maisha Wanaohujumu Nchi Yetu


China, wizi, uhujumu uchumi na makosa mengine kama haya hupewa adhabu ya kifo ili ima kutoa onyo, kutenda haki au kukomesha kadhia hizi ambazo ni madonda ndugu yaliyofanya Afrika iwe shamba la bibi na maskini wakati imejaliwa mali na raslimali nyingi kuliko mabara yote duniani. Tukio la hivi karibuni ambapo raia wawili wa China walikamatwa wakishirikiana na mtanzania kutorosha dhahabu yenye thamani ya mamilioni ya fedha lingetokea China, wahusika wangekuwa wanajiandaa kuonja mauti. Kwani, China huwa haina mchezo wala mswalie Mtume linapokuja suala la kulinda mali na raslimali za umma. Japo kuna kampeni nyingi za kimataifa kuondosha adhabu ya kifo kwenye mataifa mengi, hili lisihusiane na wanaohujumu nchi. Hata hizo nchi za magharibi zinazotuhadaa na kutushawishi tuondoshe adhabu ya kifo hutumia adhabu hii hii kuwaondoa wale yasiyowataka kama ilivyokuwa kwenye sakata la kumuondosha madarakani rais wa zamani wa Iraq Saddam Hussein. Pia, kinara wa haki za binadamu duniani, Marekani, ina majimbo ambayo haytaondoa adhabu ya kifo ili kutumika kuwaua wale wasiotakiwa kama vile wanaoishambulia nchi hiyo kigaidi na wengine wa aina hii. Isitoshe, wanufaika wengi wa kuhujumu, kuibia nchi za kiafrika na kutorosha mali na mitaji wengi wao ni wageni toka mabara mengine.
        Katika kupendekeza kutolewa adhabu ya kifo au kifungo cha maisha kwa wanaoibia au kuhujumu taifa ili wasipata fursa ya kufaidi chumo la wizi na hujuma, napendekeza tujifunze toka China nchi ambayo hutoa adhabu ya kifo kwa makosa haya. Je kwanini China waliamua kuwanyonga wanaohujumu au kuibia taifa hili? Mantiki ni rahisi kuwa anayehujumu au kuibia China, anakuwa ameibia watu zaidi bilioni moja wa China. Anakuwa ameibia wachina wote akiwamo yeye mwenyewe. Kwa kufanya hivyo, uhai wa mtu mmoja au wachache ukilinganishwa na uhai wa taifa zima, inakuwa rahisi kujua mzani wa haki utalalia wapi. Inaingia akilini hasa ikizingatiwa kuwa kuna wananchi kama askari, polisi na wengine wanaojitolea maisha ya wananchi na mali zao. Inapotokea watu wachache wakazihujumu, wanawakatisha tamaa watu kama hawa. Tusiruhusu hili kamwe.
         Hivyo, kwa mantiki inayotumiwa na China, anayeibia au kuhujumu Tanzania, anaibia watanzania wote. Hivyo, hapaswi kuonewa huruma au kufaidi haki za binadamu. China walikuwa wajamaa kama sisi. Tulianza nalo kiuchumi. Ajabu ya maajabu, tokana na kuwa makini kwenye usimamizi wa mali na raslimali zao, sasa ni taifa la pili kwa utajiri duniani ambalo linaiendesha mbio dunia kwa namna lilivyofanikiwa. Pamoja na mengine, mojawapo ya sababu za kufanikiwa kwa taifa hili ni ithibati na kutokuwa na simile na wezi na wahujumu. Pamoja na kutokuwa na raslimali nyingi kama Afrika, China bado inatoa misaada kwa Afrika bara ambalo limeibiwa na kuendeshwa kihasara pamoja na kuwa na raslimali lukuki. Tokana na uzembe na ukosefu wa uzalendo kwa watu wetu, tumeendelea kuwa shamba la bibi ambapo raia toka mataifa yote huja kujiibia wakitudanganya kuwa wanawekeza wakati wanachukua. Wawekezaji wote wenye kuonyesha tabia za wizi ni wachukuaji si wawekezaji kitu. Watanzania wanaosaidiana nao kadhalika ni wachukuaji na si wazalendo.
        Kwa Tanzania, nchi iliyojaliwa raslimali lukuki kusonga mbele, lazima iwe na sheria kali mojawapo ikiwa ni kuwanyonga wahujumu na wezi wa mabilioni ya umma. Tumekuwa tukitumia sheria na fikra za kikoloni za kuwanyonga au kuwafunga maisha vibaka wakati mijizi mikubwa ikifungwa miezi michache au kupewa faini. Huu ni muendelezo wa ukoloni ambapo wakoloni walitunga sheria kali dhidi ya makapuku ili wasiwaibie wakati wao wakijitungia sheria rahimu kwa ajili ya kufanikisha wizi. Ni bahati mbaya. Baada ya kupata uhuru uliozaa utegemezi, watawala wetu ima waliliona hili wakaliacha kwa vile walikuwa wamewafukuza wakoloni weupe na wao wakachukua nafasi yao kama wakoloni Weusi au kwa vile walikuwa na lengo na kuwaibia wananchi waliowahadaa wakawaamini madaraka.
Je nini kifanyike kupambana na uhujumu na wizi wa mali za umma?
        Kwanza, kila mtanzania awe macho na watu wote anaohisi wanahujumu au kuibia taifa letu wawe ni watanzania au wageni. Hapa kuna haja ya kuwafundisha na kuwamotisha watanzania kuwa wazalendo. Ili kufanikisha haya, wale watakaofichua uovu kama huu wazawadiwe angalau asilimia kumi ya mali walizosaidia kuokoa.
        Pili, kama taifa, tuwe na mfumo na utaratibu wa kuhoji na kutoa maelezo namna ya watu walivyopata utajiri wao. Kila mtanzania ajaze fomu na kueleza alivyopata mali zake. Kama kuna mali zitakazotiliwa shaka, zitaifishwe kama mhusika atashindwa kutoa ushahidi wa uhalali.
        Tatu, wawekezaji watakaobainika kujiingiza kwenye jinai ya kuhujumu na kuibia umma tuwashughulikie kisheria ikiwemo kufuta leseni na kutaifisha zao kabla ya kuwafikisha mahakamani.
        Nne, mamlaka husika zinapaswa kujibu maswali muhimu kuhusiana na kadhia kama hizi. Je huu mchezo ulianza lini na ni wangapi wanaufanya na taifa limepoteza fedha kiasi gani? Je tunao mfumo wa kupashana habari, kuchunguza, kupeleleza vitendo kama hivi? Je tunazo sheria za kushughulikia jinai kwa uzito unaostahiki kama vile kutunga sheria ambazo adhabu zake zitakuwa mbili tu ima kifo au kufungwa maisha?
        Tano, kujibu maswali hayo hapo juu, mamlaka na taasisi husika zinapaswa kufanya uchunguzi wa kuna kubaini ukubwa wa tatizo ili kuweza kulishughulikia kisayansi, haraka na vilivyo.
Tumalize kwa kuihimiza serikali na watanzania kwa ujumla kuwa makini na mali na raslimali zao. Ili kuwapa motisha kufanya hivi, tupitishe sheria za kuwanyonga au kuwafunga maisha wanaojihusisha na jinai hii huku, kama jamii, tukipanga kuwalinda na kuwazawadia wanaofichua uovu huu.
Chanzo: Raia Mwema Leo.

No comments: