The Chant of Savant

Monday 21 June 2021

Wizi Ndani ya Wizi, Unaiba Bilioni 309 na kurejesha 26

Taarifa kuwa mtuhumiwa wa kashfa ya Escrow ambapo ulifanyika wizi wa dola 22,198,544 sawa na shilingi bilioni 309 (Mwananchi, Julai 16, 2021) unaodaiwa kufanywa na mmilki wa Independent Power Tanzania Limited (IPTL) Harbinder Seth Singh pamoja na mbia mwenzake James Rugemalira hapo mwaka 2014 amefanya majadiliano na serikali na kuamriwa kulipa shilingi bilioni 26 zinachanganya na kutisha.  Hata hivyo, vyanzo mbali mbali vinaonyesha kuwa fedha iliyoibiwa ni kubwa kuliko iliyoripotiwa na gazeti tajwa hapo juu. Kwani, kwa mujibu wa Shirika la Habari la China, Xinghua (June 20, 2017) fedha iliyoibiwa ni dola za kimarekani miloni 122.  Kwa wanaokumbuka kashfa nzima ya Escrow, ilizamisha kati ya dola za kimarekani  takriban  milioni 250 hadi 800 na hadi sasa hakuna waliowajibishwa ukiachia mbali na hawa wawili wa IPTL. Kwa taifa maskini kama letu, huu ni ukatili kwa watu maskini.

            Habari kuwa Mahakama ya Kisutu imemuamuru Singh kulipa shilingi bilioni 26 ilinistua, kunishangaza na kunisikitisha. Haraka haraka nilikumbuka tashtiti na utabiri wa kitabu cha Pepo ya Mabwege. Nadhani ni wengi waliostuka na wakataostuka kadri habari zinavyozidi kuenea na kutafakariwa. Sina ugomvi na mahakama kama sheria zetu zilizotungwa na mkoloni na kubariki ujambazi mkubwa huku zikipatiliza udokozi zilitumika kufikia hukumu hii. Kama ni sheria na siyo mkono wa mtu, basi inapaswa kujiuliza kama hizi sheria zimetungwa kututumia au watu tuzitumie? Je sheria zinafanya hata bongo zetu ziache kufanya kazi kiasi cha kufanya vitu ambavyo hata machizi hawawezi kufanya? Je namna hii tutakomesha wizi wa fedha za umma? Je nani ananufaika na sheria kama hizi zenye kutuletea umaskini huku zikiwachochea majizi wakubwa kuendelea kutusikinisha? Je hakuna namna ya kukata rufaa hata kwa mtanzania binafsi ili kuepuka kupoteza haya mabilioni ya fedha?

            Ushahidi wa kimazingira unaonyesha kuwa hakuna mtu mwenye akili timamu achilia mbali nchi nzima anayeweza kuibiwa shilingi bilioni 309 akakubali kurejeshwa bilioni 26 hata kama angekuwa ni bilionea wa kwanza duniani au taifa tajiri kuliko yote. Hapa swali la kujiuliza, hii hasara ya shilingi bilioni 283 nani atailipa au inawekwa kwenye kundi gani? Je ni msamaha? Je ni rushwa? Je serikali ilitoa taarifa za uongo kuhusiana na kiasi cha fedha kilichokuwa kimepotea? Je hukumu hii imezingatia ni faida kiasi gani mtuhumiwa alipata kwa kukaa na mabilioni kama haya kwa miaka yote kama angetozwa riba hasa ikizingatiwa kuwa fedha nyingi za serikali hutokana na mikopo tena yenye riba kubwa? Je hili linahitaji uwe mchumi au uwe na PhD kulifahamu? Je hapa nani anamdanganya nani na kwanini? Je umma unachukuliaje uchokozi huu wa wazi wa kimfumo? Je nini kifanyike japo kama taifa tuonyesha tuna akili na tunajili mali za umma mbali na kuonyesha dhamira ya kupambana na ujambazi huu wa wazi? Je hiyo pesa ingejenga barabara, reli, shule au zahanati ngapi? Ingeweza kununua madawa au vitabu na huduma nyingine muhimu kiasi gani? Je huwa hawa wanaoridhia wizi huu wa wazi huwa wanajiuliza maswali rahisi lakini muhimu kama haya? Maswali ni mengi kuliko majibu.

            Kwa wanaokumbuka kashfa nzima ilivyoshughulikiwa, watakubaliana nasi kuwa kulikuwa na watu wakubwa nyuma ya wizi huu. Kwani, pamoja na ukali wake, hata Hayati Dk John Pombe Magufuli alipoambiwa afukue makaburi lau taifa lipate haki, alichelea kukubaliana na ushauri tokana na uzito wa suala lenyewe.  Hata hivyo, kama tutaendelea na uzembe na urushi huu, kuna siku wanyonge tunaohalalisha kuibiwa wataamka na kudai chao kwa namna ambayo haipendezi. Nikiangalia kinachoendelea nchi ya jirani ya Msumbuji ambapo kuna tishio la ugaidi unaofanywa na wananchi walikata tamaa baada ya kuachwa nyuma kimaendeleo, naogopa kusikia habari kama hizi ambazo ni juu ya dhuluma ya wazi kwa wananchi. Je rais anaweza kuingilia na kuwauliza wasaidizi wake mantiki ya kuibiwa fedha nyingi kiasi hicho na kuamua kufuta kesi na kuwaacha watuhumiwa waende kumbua na kutumia fedha zetu? Je hii haitachochea na kutoa motisha kwa wengine kupanga kutuibia wakijua wazi kuna sheria au mazingira ya kuwawezesha kuponyoka au to get away with murder kama wasemavyo waingereza? Je kuna mengi ambayo hatuyajui hadi watuhumiwa wanakiri na kufanya majadiliano na serikali juu ya namna ya kuiibia? Je mtu aliyevunja nyumba anaweza kuruhusiwa kujadiliana na aliyemvunjia nyumba au mbakaji na aliyembaka? Je sheria zetu zimetungwa kumtumikia nani na kumtumia na kumnyonya nani? Inakuwaje kesi ya makosa ya uhujumu uchumi ambayo yana mahakama yake maalumu iamriwe Kisutu?

            Tumalize kwa kushauri na kusema wazi kuwa viongozi wetu wanaposimamia ofisi za serikali na mali za umma, wajue kuna kesho na maisha baada ya kuwa nje ya madaraka. Pia tunashauri rais achunguze sababu zenye kuingia akilini za uamuzi huu ambao hata kama unatokana na sheria mbaya, nao ni mbaya na ni tishio kwa usalama wa taifa letu. Je tuibiwe kiasi gani ndiyo tujue sisi ni shamba la bibi ambapo nyani wanaweza kuingia na kujifanyia uharibifu watakavyo kwa vile bibi hana uwezo wa kupambana nao? Haiwezekani mtu akaiba tembo akatozwa faini ya kulipa kuku au sungura na hii ikaitwa haki. Hii ni kuibaka, kuibemenda, kuichafua, kuidhihaki, kuidhalilisha na kuitukana haki. Kama taifa, tusijiruhusu kufanya hivyo, tutaumiza wengi–––tena wasio na hatia tunaodai kuwatetea ambao watamkumbuka Hayati Magufuli kwa uchungu kwa kuachwa yatima–––nasi tukiwamo.

Chanzo: Raia Mwema leo.



No comments: