The Chant of Savant

Tuesday 15 June 2021

Kweli Wanamjaribu Rais Samia Suluhu Hassan

Japo kazi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ni kulinda mipaka ya nchi ili kuhakikisha kuwa nchi inakuwa salama kiasi cha wananchi kuishi maisha yao kwa amani na usalama kama ambavyo limefanya tangu nchi yetu kuwa huru, kuna haja ya kubadili mwelekeo inapoonekana kuna mambo yanayokwenda ndiyo siyo. Sina wasi wasi wala shaka na Jeshi la Polisi ambalo kazi yake ni kuhakikisha unakuwapo usalama nchini na ufuataji na utekelezaji wa sheria. Hata hivyo, taarifa ya juzi kuwa basi la Scorpion litokalo Shinyanga kwenda Kasulu, Kigoma lilitekwa na majambazi karibu na kambi ya wakimbizi ya Nduta na abiria kuporwa fedha na vitu vyao mbali na kupigwa, limenifanya nifikiri nje ya kasha tena bila kasha (thinking out of the box and without box).

Utekaji kama huu ni sawa na ugaidi. Kwani, husababisha hofu na mashaka hakuna mfano. Ugaidi au terrorism husababisha hofu au terror. Hivyo, kupambana nao huwa ni kazi ya vyombo vyote vya usalama tokana na tishio usababishao kwa jamii na nchi. Kutekwa kwa basi la Scorpion ni ugaidi wa wazi mbali na kuwa uchokozi kwa taifa. Pia ni jaribio kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua hatua. Kwa wanaokumbuka alivyomuonya IGP Simon Sirro, nadhani wakati wa kufanya kweli ni sasa. Kwani, hata kama Sirro hawezi kutabiri kitakachotokea, kwa mujibu wa ahadi ya Rais, Sirro amekalia kuti kavu. Hana haja ya kuendelea kukalia kuti kavu bali kujiwajibisha na kutafuta shughuli nyingine isiyomuongezea presha.

 Kimsingi, unapomchokoza Amiri Jeshi wa Majeshi yetu lazima ulipie kwa gharama yoyote. Majambazi walioteka basi husika wamemchokoza Rais na haswa haswa IGP. IGP, kwa kushindwa kuona hili likija, amemchokoza rais japo si kwa kutaka. Katika uwajibikaji wa umma, ningekuwa Sirro ningepeleka barua ya kujiuzulu kwa Rais mara moja ili kumpa nafasi ya kupambana na kadhia hii vizuri. Nadhani hata Rais anaongojea uamuzi huu wa kizalendo na kiwajibikaji kwa hamu sana ili kumpa nafasi ya kutafuta mtu mwingine atakayepambana na kadhia hii vilivyo.

Kama Sirro ataamua kuwajibika–––jambo ambalo si bora kufanya tu bali haliepukiki kwa sasa–––si kwamba atajijengea heshima na kuaminika tu bali ataonyesha alivyo kiongozi aliyekomaa ambaye yuko tayari kubebe msalaba wake. Rejea Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi alivyojiwabisha hata kwa kosa ambalo hakutenda na kujingea heshima na kukubalika kiasi cha kuwa Rais baada ya kufanya hivyo. Hivyo, Sirro asione aibu kujiwabisha kabla ya kuwajibishwa. Kwani, akiwajibishwa, atapoteza hata heshima ambayo anayo kwa sasa na kusahaulika haraka. Asiogope kuwajibika. Kuna maisha nje ya u-IGP.

Kujiwajibisha kwa Sirro kutatoa changamoto na somo kwa atakayerithi nafasi yake kujua  yanayoweza kumtokea iwapo hatasimamia vizuri ofisi yake. Niseme wazi. Kilichotokea si kosa la Sirro bali changamoto kwake kama kiongozi. Mzee Mwinyi alipojiwajibisha, hakuwa ameshiriki mauaji yaliyosababisha kuchukua hatua hiyo. Kilichomsukuma ni kusutwa na nafsi yake huku akitaka kuweka mfano na rekodi ambayo, hadi tunaandika, havijawahi kuvunjwa. Ni furaha, heshima na ufanisi kiasi gani kuwa katika vitabu vya historia tena kwa namna ya kupendeza.

Kwa upande wa watekaji, tunapaswa kuwa na sheria kali mbali na utaratibu usio na huruma nao. Kwa mfano, kwanini tusiruhusu askari wetu kupiga risasi watu kama hawa au shoot to kill ili liwe somo kwa wengine? Mbali na hiyo, kuna haja ya kuhakikisha kuwa tunakuwa na magari ya doria kwenye barabara zetu kwa saa 24 siku saba kwa wiki ili kubaini jinai na uovu huu kabla ya kufanyika. Isitoshe, kuwepo kwa magari ya kutosha ya daria na upashanaji wa habari kwa wananchi, kutasaidia kujenga mazingira ambayo yatawakatisha tamaa wote wanaofikiria kuteka magari kama njia ya kujipatia kipato au utajiri.  Tutakapokuwa na sheria za shoot to kill, yeyote atakayejiingiza kwenye jinai, atakuwa anafanya uamuzi akijua mwisho wake ni nini.

Khusiana na kuweka majeshi, napendekeza hivi tokana na namna raia wanavyowaheshimu na kuwaogopa. Sidhani kama kutakuwa na magari machache ya jeshi kwenye doria za barabarani, kuna jambazi atathubutu kutaka kuonyeshana ubabe na wanajeshi. Hatuwezi kuacha watu wetu wanateseka wakati ambapo taifa letu halina kitisho toka nje wakati wanajeshi wetu wapo na walishaapa kuilinda nchi hii kulhali. Lazima tuwatumie. Pia uwepo wa jeshi nao utatoa onyo kali kwa majambazi. Kwani, wanajua uimara na ukali wa jeshi letu.

Tumalizie kwa kusisitizia kuwa muda wa IGP Sirro kujiwajibisha umefika huku tukimuomba Amiri Jeshi wetu Rais SSH kutuletea mtu mwenye uwezo na pia kuridhia kutumia JWTZ kuwasaidia Polisi kupambana na utekaji magari na aina nyingine za ujambazi vilivyoanza kujitokeza hivi karibuni. Ni ushauri wa bure tu.

Chanzo: Raia Mwema Leo.


No comments: