The Chant of Savant

Friday 4 June 2021

Spika Ndugai Tamatisha Mbeleko kwa Wabunge 19

Hii si mara ya kwanza wala ya mwisho kugusia sakata la wabunge 19 waliotimuliwa toka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) al maaruf kama Covid-19. Nasema hivi tokana na mkanganyiko, utata na uzito wa sakata hili ambalo––––kadri siku zinavyozidi kwenda––––linaweza kuwa kashfa ya kitaasisi kama siyo ya kitaifa. Pia, niseme wazi. Sina ugomvi binafsi na Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano Mheshimiwa Job Ndugai ambaye amejitokeza kuwa mtetezi mkubwa wa wabunge tajwa hata kwa kukiuka kanuni na kuonyesha kupendelea wazi wazi huku akiumiza upande mwingine katika mgogoro uliosababisha wabunge husika kufukuzwa kwenye chama chao, na hivyo, kupoteza sifa ya kuwa wabunge. Pia, sina ugomvi dhidi ya wala maslahi binafsi toka kwa wabunge husika. Ugomvi wangu ni kutaka haki itendeke kwa pande zote hasa walipa kodi ambao fedha zao zinatumika kuwalipa watu ambao wako bungeni kinyume cha sheria.
        Kwanza, napendekeza spika achunguzwe hata kama itabidi akae pembeni kama wengine kupisha uchunguzi huu ili kuondoa ubaguzi katika kuwahudumia watanzania bila kujali nyadhifa zao kama Katiba inavyoweka wazi kwenye ibara za 1(2); 13(1& 2); 23 (1) kuwa watanzania wote ni sawa na wasibaguliwe kwa hali yoyote. Kitendo kilichofanywa na Spika kuendelea kuwapendelea kwa kuwakingia kifua kama kiongozi wa mhimili wa dola na umma ni kinyume cha katiba. Ni kitendo cha kibaguzi ambapo haki haijatendwa kwa usawa. Hata pesa inayotumika kuwalipa wabunge husika hata kama ingekuwa ni shilingi kumi tu, kwa vile ni pesa ya umma, lazima tuchunguze kujua uhalali wa wahusika kulipwa.
        Pili, napendekeza Spika apewe karipio na mamlaka husika kwa kuingilia uhuru wa chama kingine huku akionekana wazi kupendelea chama chake jambo pia linakinzana na kiapo chake cha kushika ofisi ya umma. Vyama havishindani kwa kuadhibiana kitaasisi bali kupitia uchaguzi na si vinginevyo. Katiba iko wazi. Kwani, ibara ya 9 (h) inakataza ubaguzi na upendeleo na mambo mengine ya aina hii.
        Tatu, Spika achunguzwe kwa sababu ameamua kwa makusudi matupu akijua ni kinyume cha kiapo na wadhifa wake kujigeuza mahakama. Badala ya kutoa uamuzi usiopendelea, Spika amekaririwa na vyombo vya habari mara nyingi akiwatetea wahusika kana kwamba kuna anayemlipa kwa kazi hii badala ya Uspika. Hata kama yupo anayemlipa kwa hilo, hili ni kinyume na Katiba Ibara ya 
        Nne, Spika anapaswa achunguzwe kutokana na kuidhinisha na kushiki matumizi mabaya ya fedha za umma. Je hawa wabunge waliofukuzwa na chama chao wanamwakilisha nani na wanalipwa kama nani na kwa nini wakati hawatimizi masharti ya kuwa wabunge? Je ni wabunge wa chama gani? Nani anapenda kuendelea kuona fedha yake wakilipwa wabunge popo ambao hawajulikana wamo bungeni kwa kudhaminiwa na chama gani?
        Tano, hakuna jambo ambalo linamuweka pabaya Spika kama kuonyesha upendeleo wa wazi wazi wa kiongozi anayepaswa kutokuwa na upande kwenye mhimili anaoungoza. Je Spika angekuwa jaji–––kwa namna alivyoonyesha upeleo wa wazi–––je haki ingetendeka? Je mtu wa namna hii bado ana sifa na  udhu wa kuendelea kuwa kiongozi wa mhimili mtukufu wa dola kama Bunge tukufu? Je mhusika anajua na kuheshimu kiapo chake ambacho sehemu yake inasema kuwa ‘nitatimiza majukumu yangu bila upendeleo wala huba”? Sidhani kama Spika wetu ambaye licha ya kuwa msomi ni mwanasheria hajui hatari ya anachokifanya. Hata hivyo, inategemea na faida anayopata tokana na kuhatarisha cheo chake. Je hiki anachokifanya ndiyo msimamo wa serikali? Je spika ana maslahi gani binafsi katika kashfa hii? Je hii ndiyo sifa ya kiongozi kuwa kioo cha jamii?
        Sita Spika abanwe aeleze ni nini maslahi yake binafsi au chama chake ili watanzania wajue kinachoendelea hasa ikizingatiwa kuwa chama kinachoonekana kuhujumiwa–––licha ya kuwepo kisheria–––kina wanachama ambao ni watanzania waliojiunga nacho kwa mujibu wa katiba kama haki yao ya kujinga na chama watakacho. Hawa pia ni walipa kodi kama mtanzania yeyote anayepaswa na kutegemea kutendewa haki kisheria. Hata ukiangalia ufanisi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) tangu tupate uhuru, sijui kama kinahitaji kushirikishwa kwenye hujuma tena dhidi ya chama kidogo kisicho na tishio lolote kwake. Hivyo, kama wahusika wanadhani wanakisaidia chama chao, wajue fika wanakiumiza na kukidhalilisha. CCM aihitaji wabunge wasio na uhalali wa kuwa bungeni. Je kama ni hivyo, huyu Spika anachofanya kinamsaidia nani zaidi ya yeye binafsi?  Pia sidhani kama Spika alimwelewa rais Samia Suluhu Hassan aliyesema wazi kuwa atateua watu bila kujali vyama vyao. Badala yake atajali sifa na michango yao. Je hawa wanaopendelewa kuendelea kuwa Bungeni wana sifa kweli? Kama wanazo, kwanini wakubali kupendelewa badala ya kwenda na kumalizana na chama chao kwanza?
        Naomba kuhitimisha nikiwataka wahusike wajipime kabla ya kupimwa, wajichunguze kabla ya kuchunguzwa na wajiwajibishe kabla ya kuwajishwa. Jambo jingine wanaloweza kufanya ni kuachana na huu mradi mchafu kabla ya kulazimishwa kuachana nao kwa aibu. Naomba kuwasilisha hoja na kutoa ushauri wa bure kwa wahusika. Muhimu wahusika wajue kisicho riziki hakiliwi na kufuata Katiba yetu siyo suala la chama, cheo, hiari wala nini bali shurti ya kisheria. Na sheria ni msumeno hukata mbele na nyuma bila kujali anayekatwa kama ni chama tawala au chama pinzani, mdogo au mkubwa Spika au Mbunge na kadhalika.
Chanzo: Raia Mwema Leo.

No comments: