The Chant of Savant

Wednesday 9 June 2021

Wabunge kama Taletale Wasitumie Bunge Kupotosha Umma


Hivi karibuni Mbunge wa  Morogoro Mashariki Hamis Taletale, aliwaacha wengi hoi pale alipokuwa akichangia bungeni. Ikiwa ni mara yake ya kwanza kuchangia bungeni, alianza kwa mguu mbaya. Sijui ni kutokana na uhaba wa elimu. Hata sijui kwanini aliamua kujiaibisha kwa kuja na hoja na utetezi hafifu akitetea jambo la hovyo hata kama linamwingizia fedha na kumfikisha hapo alipo. Badala ya kutetea jimbo lililomuamini na kumchagua mbunge wake ili aliwakilishe, alirejea kwenye biashara yake ya muziki hata usioendana na utamaduni wa kitanzannia. Bila aibu wala kuchelea namna umma unavyoweza kuchukulia mchango wake, Taletale alianza kwa kutetea wimbo wa Alleluia wa Diamond ulikataliwa na COSOTA. Badala ya kueleza ni kwanini wimbo husika ulipigwa marufuku, alianza ngojera za ajabu ajabu ambazo siyo saizi ya mbunge.                        Anashangaa kwanini wimbo tajwa ulikataliwa na COSOTA lakini ukakubaliwa na wamarekani kwenye filamu ya Coming to America waliouchagua kama wimbo bora. Sijui ni kwanini hakujiuliza au kutajaza vigezo walivyotumia wamarekani lau tukalinganisha na vile vilivyotumiwa na COSOTA kuupiga marufuku. Natamani mbunge angekuwa mmojawapo wa wanafunzi wangu nikamfundisha maana na mchango wa pop culture kwa Marekani na namna ilivyotumika kama nyenzo ya ukoloni wa kiuchumi. Pia afahamu kuwa wengi wanaopitisha hizo nyimbo wanaweza kuwa vihiyo wa kawaida kama yeye au wataalam wa saikolojia wanaoajiliwa kueneza utamaduni nyemelezi na koloni wa kimagharibi ili kuharibu tamaduni nyingine kuwa tegemezi kwao. Na hivyo, kutumika kwa faida kiuchumi.
        Kitu kingine ambacho Mbunge alishindwa kufahamu ni rahisi. Utamaduni wa Marekani na Tanzania si sawa tu bali kinyume. Mfano, wakati Tanzania haturuhusu usagaji na ushoga, Marekani unaruhusiwa. Inashangaza kwa mtu anayesikika akisema bungeni “I am from Africa” ili lau aonekane anajua kimombo kama alama ya usomi hajui vitu rahisi kama hivi. Hivi kweli wabunge wa namna hii wanaweza kumsaidia mwananchi kwa mambo magumu wakati wanashindwa mambo rahisi kama haya?
        Mbunge ameshindwa kutoa sababu za kukataliwa kwa wimbo akakimbilia na stori za Coming to America. Badala yake alitoa shutuma zisizo na mashiko wala ushahidi kuwa COSOTA inaendeshwa na watu wasiojua sheria bila kueleza vipi na sheria zipi. Mao Tsetung aliwahi kusema kuwa kama hujafanya utafiti, huna haki ya kuhoji. Hii inamgusa mbunge huyu. Je Amerika wametumia vigezo gani kuchagua huo wimbo wake na kwa sababu gani? Je vigezo vyake ni vipi? Je vinafanana na vile vinavyotakiwa na utamaduni wetu? Wabunge wanapaswa kuwa makini kujua wanachotaka kusema au kufundisha badala ya kuangalia faida ndogo kama fedha wakasahau madhara yatokanayo na fedha hizo.
        Mbunge anakuja na madai ya ajabu kama kuwa na utaalamu wa kuzui mvua isinyeshe bila kutoa ushahidi au kueleza namna anaweza kufanya hivyo. Je huyu ana tofauti gani na waganga njaa wa kienyeji wanaowapa masharti wajinga wengi waliotamalaki nchini hadi wakafikia kuua wenzao kwa imani mbovu za kishirikina ambazo ni chanzo kikubwa cha aibu na lawama kwa taifa? Inakuwaje anajua kufunga lakini si kutengeneza mvua ili kusaidia kuitengeneza kwenye  maeneo yenye uhaba wa mvua? Je huyu ana tofauti gani na matapeli wanaotangaza kuwa wanaweza kufanya miujiza kama vile kufufua na kuponya wafu na wagonjwa wakati ni ujuha, ujinga na upumbavu na utapeli wa kawaida ambao serikali zetu zimeshindwa kuutolea uvuvi na kugeuza nchi zetu kuwa za kishirikina.
        Jambo jingine lililoonyesha uhaba wa ujuzi wa mhusika ni pale anapodai kuwa rais ni mmoja nchini bila kujua chanzo na maana ya neno rais ni kapteni wa meli wa kiislam au kiongozi wa kiislam. Kama ni hivyo basi hata mheshimiwa nchini awe mmoja yaani rais. Baada ya hapo tutaambiwa hata mwenyekiti awe mmoja kwa vile rais ni mwenyekiti wa Chama tawala. Huu ni ujinga wa kupitiliza tena wa kiwango cha lami. Je mawazo kama haya yanawasaidia nini wakazi wa jimbo la Morogoro Mashariki? Je haya ndiyo waliyomtuma kuzungumzia kwa niaba yao bungeni au ni kupoteza fursa kwao na muda wa bunge bure?
Hakuna sehemu ambapo mtajwa aliniacha hoi kama kushauri kuwa BASATA na COSOTA wasiingilie kiki za wasanii bila hata kueleza maana ya kiki ni nini. Anataka tuchukue mfano wa msaini wa marekani aitwaye ‘Six’ ambaye alisema eti  ni kichaa lakini anatengeneza fedha. Yeye anataka fedha hata kama ni za fedheha. Kwa wamarekeni hata kuuza mwili ni biashara inayotolewa kodi. Hivyo, inaabudiwa. Lakini kwa waswahili hili ni tusi na aibu kwa jamii nzima. Hatuwezi kuwa watumwa wa fedha kiasi hiki. Nashauri kuwa wanamuziki na wasanii wasiofuata maadili wafungiwe bila kujali wanaingiza mabilioni kiasi gani. Kwa mawazo ya namna hii, tutafikia hata kuhalalisha ujambazi kwa sababu tu unaingiza fedha.
        Tumalizie kwa kuonya kuwa hata kama kila mtu ana haki ya kuelezea mawazo yake, kama mbunge, hana au akionesha kutokuwa na la kusema, asipoteze muda wa bunge kwa kutetea mambo ya ajabu ajabu kama ilivyo kwenye kadhia iliyojadiliwa kwenye makala hii. Taletale akipata muda ajielimishe na kuomba ushauri kabla ya kutoa upupu unaoweza kumvunjia heshima. Bungeni si mahali pa kutetea mambo ya ajabu. Ni mahali pa kutetea mambo yenye maslahi mapana ya taifa badala ya maslahi finyu binafsi kama ilivyojitokeza kwenye kadhia husika hapa.
Chanzo: Raia Mwema Leo.

No comments: